The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

ZBC, HabariLeo Waongeze Umakini Matumizi ya Kiswahili Fasaha, Sanifu

Jambo linalosikitisha zaidi kwenye makosa ya Kiswahili yanayofanywa na wanahabari ni kwamba makosa hayo hufanywa na vyombo vya habari vya Tanzania, nchi inayojinasibu zaidi na Kiswahili sanifu na fasaha.

subscribe to our newsletter!

Tunasisitiza kuwa tasnia ya habari ni shughuli rasmi na kwa asilimia kubwa inategemea lugha kama mtaji wake. Sauti na maandishi ya wanahabari husambaa kwingi na kwa muda mfupi mno kutokana na maendeleo ya tekinolojia. 

Hivyo, ni wajibu wetu wanahabari kuzingatia matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha ili taarifa tunazoziandika na kuzisema zitoe ujumbe uliyokusudiwa. Halikadhalika kuitunza, kuihifadhi na kuiendeleza lugha yetu na utamaduni wake kwa usahihi, usanifu na ufasaha unaokubalika kijamii na kitaaluma.

Kwa kuanzia, tutazame taarifa hii, ambayo ilichapishwa na kunakiliwa na vyombo mbalimbali vya habari likiwemo Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na gazeti la HabariLeo na kusambazwa katika mitandao ya kijamii ya vyombo hivyo. 

Taarifa hii ilinukuu maneno ya Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi akifafanua kuhusu kadhia ya mawaziri kujiuzulu, Februari 1, 2024. Hapa ninanukuu taarifa hiyo kama ilivyoandikwa bila kuihariri:

Sababu nyingine ya waziri kujiuzulu ni pale ambapo serikali inaamua jambo na wewe ukubaliani nalo, unatoka unajiuzulu kwasababu ukubaliani na maamuzi yaliyotolewa na serikali lakini kuna jambo moja lazima tukumbushane wakati unawajibika kwa njia yoyote ile ya kwanza au ya pili ni lazima uwe mkweli na ukweli naozungumzia hapa ni kama kuna mgongano wa maslahi utangaze,

Kama tumezuia kitu na wewe una biashara hiyo tangaza, sema ukweli, sema ukweli hapa kuna mgongano wa kimaslahi mimi ni muagizaji wa kitu fulani na ninyi mmezuia, lazima tuwe wa kweli sasa hivi ukitoka halafu ukaenda kuwaamisha watu kinyume chake si sahihi.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Matumizi ya Kiswahili Sanifu, Fasaha Katika Tasnia ya Habari?

Nilipoisoma taarifa hii ilinibidi niitafute video hii ili kuona kama kweli mzungumzaji aliyenukuliwa alitamka kama ilivyoandikwa. Nilithibitisha kuwa mwandishi alifanya makosa ambayo hayakuwamo katika matamshi ya mzungumzaji, ambalo lenyewe ni kosa kubwa. Taarifa hii ina makosa mengi ambayo yasingelitarajiwa katu kufanywa na vyombo vya habari, hususani vikubwa kama hivi.

Makosa ya kiuandishi

Kwanza, kuna makosa ya upunguzaji au uachaji wa viambishi. Katika neno ukubaliani, mwandishi ametumia kiambishi cha nafsi ya II umoja yakinifu (u-) katika kitenzi kinachoashiria ukanushi. Kiambishi kilichostahili kutumiwa hapa ni hu-, ambacho ni kiambishi cha nafasi ya II umoja cha ukanushi.

Kadhalika, katika neno naozungumzia, mwandishi amepunguza kiambishi cha nafsi ya I umoja (ni-) mwanzoni mwa kitenzi. Kisha akaamua kuanza na kiambishi cha njeo (na- wakati uliopo). 

Vilevile, neno hili lingekuwa sahihi zaidi kama kingetumika kiambishi cha o-rejesho (u-) ambacho hujificha katika utamkaji, kinachorejelea nomino ‘ukweli’ kabla ya mzizi wa neno. 

Hii ni kutokana na neno hilo kuambikwa kiambishi tamati kijenzi (i- kauli ya kutendea) kabla ya kiambishi tamati maana (a-). Kwa hivyo, neno hilo lilitakiwa kuandikwa ninaouzungumzia.

SOMA ZAIDI: Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Makosa mingine ni ya kuacha fonimu /y/ katika neno ninyi na silabi -ni- katika neno kuwaamisha. Nadhani hili limetokana na umakini mdogo wa mwandishi au mhariri. 

Maneno haya yalitakiwa kuwa nyinyi na kuwaaminisha. Aidha, limejitokeza kosa la kutenganisha maneno katika wa kweli. Kiambishi (wa-) kinachoashiria wingi kimebadilika na kuwa (neno – kihusishi) kutokana na kutenganishwa na neno ‘kweli’. Usahihi wake ni wakweli.

Pamoja na makosa hayo, usomapo taarifa hii utagundua kuwa alama za uandishi, hasa za kituo kidogo na kikubwa, hazikuzingatiwa kabisa. Hii inaashiria kuwa mwandishi hakuzingatia kasi ya msemaji katika utamkaji wake, au tambo. 

Tambo hujumuisha uongezekaji au upunguaji wa msukumo wa hewa katika matamshi. Huhusisha pia kasi ya utamkaji; utuaji mfupi au mrefu na namna ya utuaji.

SOMA ZAIDI: Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania

Kuzingatia tambo kunaweza kumsaidia msikilizaji kutambua pahala pa kuweka alama za kuuliza, mshangao, kituo kikubwa, kituo kidogo na alama nyingine za uandishi, pale anapokusudia kunukuu kimaandishi yale aliyoyasikiliza. 

Hapa inadhihirika kuwa mwandishi hakusikiliza bali alisikia. Kutozingatia alama za uandishi kunaweza ama kupotosha, kutofahamika au kutatanisha maana katika taarifa, kama inavyothibitika katika taarifa hiyo.

Makosa ya kiutangazaji

Katika kipindi cha Rada cha ZBC nilichokiangalia Februari 4, 2024, mtangazaji alionekana kufanya makosa mengi ya Kiswahili sanifu na fasaha. Miongoni mwa makosa hayo ni matumizi yasiyo sahihi ya viunganishi. 

Kwa mfano alisema: “…halkadhalika pia kuepuka muingiliano…” Viunganishi halkadhalika na pia kwa muktadha huu, vinafanya kazi moja. Hivyo, ilipaswa kutumiwa kimoja tu kati ya hivyo.

Kosa jengine ni la msamiati. Mtangazaji alisikika akisema: “….kwa hafla tiba inakuwa haijajulikana.” Msamiati hafla una maana ya sherehe au mkusanyiko wa watu wengi ili kukamilisha jambo maalumu. 

SOMA ZAIDI: Matokeo Kidato Cha Nne 2023: Somo La Kiswahili Laendelea Kuongoza Kwa Ufaulu

Kwa mfano, hafla ya kuapisha viongozi, hafla ya maagano ya kuhitimu masomo, hafla ya kuadhimisha siku kuu maalumu, hafla ya makabidhiano, nakadhalika. Mtangazaji alitakiwa kutumia msamiati ghafla.

Makosa kama haya hujitokeza sana katika sauti na maandishi ya wanahabari. Haya ni makosa ya kutopambanua misamiati inayofanana kimaumbo lakini huwa na maana na matumizi tafauti. Kwa mfano, misamiati wasilisha na wakilisha; baada na badala; feza na fedha; thibiti na dhibiti, nakadhalika.

Katika kipindi hicho hicho, mtangazaji alisikika akifanya makosa ya mara kwa mara ya kuchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza. Hii ni baadhi ya mifano:

“…hata ukienda…kwenye ile garden pale”

“…hawaoneshi kama na wao wana-act hiyo hali?”

“Tupate break kidogo, kisha tutarejea.”

…nature yake…”

“…pengine masuala ya tradition…”

Kwa sentesi ya kwanza, licha ya kosa la kutumia Kiingereza na Kiswahili, pia kuna kosa la kimuundo. Maneno ile na pale kwa muktadha wa sentesi hii yanafanya kazi kama vioneshi vinavyosisitiza kielezi cha pahala. 

SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis: Kumfasiri Gurnah, Mshindi wa Nobel, kwa Kiswahili

Kimuundo ilitakiwa kutumia neno moja tu kati ya hayo. Yaani, ‘hata ukienda kwenye ile bustani’ au ‘…pale kwenye bustani.’ Maneno ya Kiingereza yaliyotumika yalitakiwa yawe ya Kiswahili – bustani; wanaigiza; mapumziko; maumbile na utamaduni.

Katika kipindi cha Mchezo Supa cha ITV cha Februari 4, 2024, mtangazaji alisema, “Tunawapendeni wote wawili.” Sentesi hii ina makosa ya matumizi yasiyokuwa sahihi ya viambishi, au makosa ya kisarufi. 

Kanuni ya utangazaji ni kutumia viambishi vya nafsi ya II pale mtangazaji anapozungumza na wasikilizaji au watazamaji wake. Hapa matangazaji ametumia nafsi ya III wingi.

Halikadhalika katika kitenzi penda kilichotumiwa hapa, awali kimeambikwa kiambishi (wa-) cha nafsi ya III wingi – wao (tunawapend-), kisha mwishoni kimetumia kiambishi tamati kijenzi (ni-) ambacho huashiria nafsi ya II wingi – nyinyi (tunawapendeni). 

Hili ni kosa kubwa kisarufi. Hakuna upatanisho sahihi wa viambishi. Usahihi wake ilitakiwa kuwa Tunakupendeni nyote wawili.

Katika kipindi hicho hicho, mtangazaji mwengine alisema: “Hiyo ni shuhuda ambayo anaitoa.” Msamiati uliyostahiki ni ushushuda unaotokana na neno shahidi na kuzaa maneno mengi –shuhudia, ushuhuda, ushahidi, shahada

SOMA ZAIDI: Watanzania na Kilio cha Samaki Kwenye Maji Katika Kiswahili

Tunapotumia maneno ushahidi au ushuhuda tutayaweka katika ngeli ya U. Siyo I – ZI kama alivyokusudia mtangazaji. Hivyo, alitakiwa kusema Huo ni ushuhuda ambao anautoa.

Tujisahihishe

Nadhani tunaona namna vyombo vyetu vya habari vinavyobeza na kudharau matumizi sahihi ya Kiswahili sanifu na fasaha. Jambo la kusikitisha zaidi, makosa haya machache yaliyojadiliwa hapa yote yanatoka katika vyombo vya habari vya Tanzania, nchi inayojinasibu zaidi na Kiswahili sanifu na fasha. 

Nadhari yangu inanisaili pasi na majibu, ikiwa ni kweli hiki ndicho Kiswahili tunachoufunza ulimwengu; hiki ndicho Kiswahili tunachokiendeleza na kukisambaza duniani kote. Bila ya shaka, chombo kinaelekea kupoteza rada.

Makala hizi ni chachu ya kuamsha hatua faafu za kulikomboa dau letu katikati ya pepo zenye mawimbi makali na dharba nzito. Asaa tukaipata bandari angali jua halijachwa. 

Nakutakia kila la kheri mpenzi msomaji, na nakuaga hadi Jumanne ya wiki ijayo katika mfululizo wa makala za safu hii, zinazochambua makosa ya Kiswahili sanifu na fasaha yanayofanywa na vyombo mbalimbali vya habari. Usisite kuniandikia endapo utakutana na Kiswahili usichojua ni sanifu na fasaha au la!

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. “Kiambishi klichostahili kutumiwa hapa ni……..” Hebu na hili neno stahili lichunguze je linatumika inavyostahiki?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts