“Tutasisitiza mapatano kwa njia ya kidiplomasia na nafikiri Ethiopia watarudi na kuona walipokosea, lakini pia tupo tayari kwa ajili ya vita kama Abiy [Ahmed atataka vita.”
Hiyo ni sehemu ya nukuu ya mshauri mwandamizi wa Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mahamud, alipokuwa akifanya mahojiano na jarida la The Guardian kuhusu mgogoro unaoendelea kukua baina ya nchi yake na Ethiopia.
Mvutano huo umeibuka baada ya makubaliano yaliyofanywa mnamo Januari 1, 2024, baina ya Ethiopia na eneo lililojitangaza kujitenga ndani ya Somalia la Somaliland, ambapo Somaliland ilitoa sehemu ya eneo la bandari yake ya Berbera kwa ajili ya kujengwa kambi ya kijeshi ya wanamaji ya Ethiopia.
Kama fadhila, inasemekana kwamba Somaliland itapewa sehemu ya hisa ya uendeshaji kwenye Shirika la Ndege la Ethiopia. Kulingana na Serikali ya Somalia, msukumo mkubwa wa Somaliland kutoa eneo hilo umetokana na uhitaji wa nchi hiyo kutaka kutambuliwa na kuungwa mkono na Ethiopia kama taifa kwa siku za usoni.
Ifahamike kuwa Somaliland ilijitenga na taifa la Somalia mnamo mwaka 1991 na kuanzia kipindi hicho imefanikiwa kujiendesha na kuanzisha mihimili ya Serikali, polisi, jeshi na sarafu yake. Changamoto kubwa inayoikumba nchi hiyo ni kutotambulika kama taifa huru na mataifa mengine, hivyo kupelekea kutengwa kwenye maamuzi, mashirikiano, mikopo na misaada ya kimataifa.
Tamaa ya Ethiopia
Hatua ya kukubaliwa kutambulika na kuungwa mkono na taifa lenye nguvu barani Afrika kama Ethiopia ni mafanikio makubwa kwa nchi hiyo. Ifahamike kuwa baada ya Eritrea, nchi ambayo imepakana na bahari ya Red Sea, kujitenga na Ethiopia mwaka 1993, Ethiopia ikawa ndiyo nchi kubwa duniani isiozungukwa na mkondo wa bahari.
Hali hii imekuwa ikiiathiri nchi hiyo kwenye suala la usalama, usafirishaji, uwekezaji na uchumi. Kwa sasa Ethiopia inanufaika na Eritrea kupitia bandari ndogo za Asab na Massawa ambazo zipo karibu na mfereji wa Bab al-Mandab.
SOMA ZAIDI: Afrika Imejipanga Kukabiliana na Taathira za Teknolojia ya Akili Unde?
Hata hivyo, ushirikiano huu umekuwa siyo wa uhakika hasa kutokana na migogoro isioisha baina ya Serikali hizo mbili pamoja na uwepo wa shinikizo kubwa ndani na nje ya Eritrea ya kuitaka Serikali hiyo kutoruhusu kupitishwa kwa silaha kwenda Ethiopia kupitia bandari hizo.
Kutokana na changamoto hiyo ya kukosa uhuru wa matumizi ya bandari hizo, Ethiopia ikahitaji kupata huduma kupitia bandari ya Djibouti, nchi ambayo ipo pembezoni mwa ghuba ya Aden. Ikumbukwe kuwa Ethiopia ni moja ya nchi barani Afrika iliyo na uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi, ikiripotiwa ukuaji wake kwa muongo uliopita kukua kwa asilimia 9.9 kabla ya vita vyake na Serikali ya Tigray.
Mchango mkubwa wa uchumi huo ulitokana na biashara ambapo asilimia 90 ya bidhaa zake hupitia bandari ya Djibouti. Umuhimu huu wa Djibouti ulipelekea mwaka 2011 mataifa haya mawili, kwa kushirikiana na Serikali ya China, kujenga reli yenye urefu wa kilomita 752.7 ambayo ilipunguza muda wa usafirishaji bidhaa kutoka siku saba mpaka masaa kumi kutoka Bandari ya Djibouti hadi Ethiopia.
Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni Ethiopia ilikopa kiasi cha Dola za Marekani milioni 730 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 150 itakayoiunganisha nchi hiyo na Djibouti ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa nchini mwake.
Ikumbukwe pia mwaka 2012, Ethiopia ilisaini makubaliano ya ujenzi wa reli wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 22 pamoja na nchi ya Sudan Kusini na Kenya kwenye mradi ulioitwa LAPSSET, au Lamu Port-Southern Sudan-Ethiopia Transport.
Mradi huu ulipangwa kuweza kusafirisha bidhaa kutoka bandari ya Lamu mpaka kusini mwa Ethiopia, japokuwa utekelezaji wa makubaliano hayo umekuwa ni wa kusuasua.
Mwaka 2018 pia Ethiopia iliingia makubaliano ya kutumia bandari ya Sudan na Rais wa wakati huo, Omar Hassan al-Bashir, ila isivyo bahati kabla ya utekelezaji wa makubaliano hayo, Rais Bashir alipinduliwa na makubaliano hayo yakafa.
Bandari ya Somaliland
Somaliland inapatikana kusini mwa pwani ya Ghuba ya Aden, eneo ambalo limekuwa muhimu kwa dunia tangu ufunguliwe rasmi mfereji wa Suez mwaka 1869.
SOMA ZAIDI: Juhudi za Dhati Zinahitajika Kuifikia Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo
Eneo la Somaliland la Bab-el-Mandeb limeunganisha Ghuba ya Aden pamoja na bahari ya Red Sea, hivyo kulifanya eneo hili kuwa sehemu pekee yenye njia fupi ya kuunganisha Asia na Ulaya.
Ifahamike pia Asia Magharibi ndiyo kiini cha uzalishaji wa mafuta duniani, kwa kuzingatia ripoti kutoka taasisi ya U.S Energy Information Administration iliyoeleza kuwa kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2023, asilimia 12 ya mafuta yote yaliyouzwa duniani yalipitia njia hiyo, huku asilimia nane ya gas –LNG– iliyouzwa katika nusu hiyo ilipita katika ukanda huo.
Kutoka mwaka 2020-2023, kumekuwepo na ongezeko la wastani wa asilimia 60 ya usafirishwaji wa mafuta kupitia njia hiyo ya bandari ya ukanda wa Somaliland, lakini pia baada ya kuwekewa vikwazo vya biashara, hasa mafuta, kwa nchi ya Urusi na Jumuiya ya Ulaya pamoja na Marekani baada ya Uvamizi wake nchini Ukraine, eneo la Asia limekuwa likitegemewa zaidi na mataifa hayo, hivyo kuzidi kuongeza umuhimu kwenye njia hiyo.
Mataifa kama Saudi Arabia na United Arab Emirates (UAE), ambayo yameendelea kufanya biashara ya mafuta na Urusi, yamekuwa yakitumia njia hiyo kupitisha mafuta ghafi kuingia nchini kwao kwa lengo la matumizi ya uzalishaji wa umeme.
Ripoti ya taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI): The Foreign Millitary Presence in the Horn of Africa imeeleza kuwa jiografia ya maeneo yanayozalisha mafuta na gesi na changamoto za usafirishaji wa bidhaa hiyo kupitia maeneo yenye migogoro, uharamia na vita ndiyo kumepelekea eneo la pembe ya Afrika kuwa ni eneo lenye kambi nyingi za kijeshi za mataifa ya nje.
Baada ya Eritrea kujitenga, nchi ya Ethiopia haikuwahi kuwa na kambi ya jeshi la wanamaji mpaka alipoingia madarakani Waziri Mkuu Abiy Ahmed mwaka 2018 ambapo alitangaza kuwa “kutafufuliwa” kwa jeshi hilo kwa msaada wa nchi ya Ufaransa, na kambi hiyo itaendesha mafunzo ya kijeshi nchini Djibouti.
Sababu kubwa ya kuanzishwa kwa jeshi hilo inasemekana ni kujilinda dhidi ya nchi ya Misri, ambao wamekuwa wakihasimiana juu ya mgogoro wa matumizi ya maji ya Mto Nile kupitia mradi wake wa kufua umeme wa Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD).
SOMA ZAIDI: Urusi Inavyotumia Karata ya Ulinzi, Usalama Kukita Mizizi Afrika
Baada ya mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 na vita vyake dhidi ya Serikali ya Tigray, uchumi wa Ethiopia ulishuka kiasi cha kushindwa kulipa madeni, hatua iliyopelekea Serikali hiyo kuiomba Djibouti kupunguza kodi ya forodha ya bidhaa zake.
Serikali ya Djibouti haikupitisha ombi hilo, na tufahamu kuwa Ethiopia hulipa zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja kila mwaka kama kodi ya forodha ya bidhaa zake kwenye bandari ya Djibouti. Inakadiriwa kama Ethiopia itafanikiwa kukamilisha ujenzi wa bandari Somaliland, itapunguza kwa asilimia 30 ya bidhaa zake zilizokuwa zikilazimika kupita bandari ya Djibouti.
Dunia itarajie nini?
Jumuiya za kimataifa, pamoja na Afrika kwa ujumla, melaani vikali mkataba huu ingawa ni wazi kuwa Somalia itachelewa kufikia hitimisho la kuivamia Somaliland. Hatua kubwa inayoweza kufikiwa ni kuwekewa vikwazo kwa Ethiopia au hata kusimamishwa uanachama kwenye Jumuiya ya Maendeleo Afrika (IGAD) au Umoja wa Afrika (AU).
Ethiopia, kwa kufahamu uzito wa hatua waliyoichukua, ni wazi walikuwa wamejitayarisha kwa haya. Hayatawasumbua kwa muda mrefu, hasa ukizingatia udhaifu wa AU ila pia umuhimu wake kimkakati kwenye eneo ililolishikilia kwa sasa, yaani bandari ya Berbera, kwenye sekta ya biashara na usalama duniani.
Mategemeo mengine makubwa ni kutengwa na nchi jirani kama Djibouti ambayo itatazama kama ni mkakati wa Ethiopia kupunguza utegemezi kwake na kuathiri uchumi wake ambao zaidi ya asilimia 70 ya GDP yake hutegemea pato la bandari.
Nchi za Misri na Eritrea zitatazama hatua hiyo kama muendelezo wa kujidhatiti kwa Serikali ya Ethiopia kijeshi, ikiwa siku za usoni kunaweza kukatokea migogoro au vita. Ifahamike pia Rais aliyepita wa Marekani, Donald Trump, aliwahi kukaririwa akimshauri Rais wa Misri, Abdel Fatah Al-sisi, kuivamia Ethiopia katikati ya mgogoro wa Mto Nile.
SOMA ZAIDI: Je, Wimbi la Pili la Siasa za Kijamaa Amerika Kusini Litadumu?
Kufuatia umuhimu wa kimkakati wa eneo la bandari ya Barbera na Somaliland kwa ujumla katika usafirishaji wa mafuta na gesi, hasa ukizingatia mgogoro unaoendelea sasa katika ghuba ya Aden baina ya nchi ya Marekani na wanamgambo wa Houthi wa Yemen, Ethiopia itahitajika kwenye meza kuu ya maamuzi ili kurahisisha usafirishwaji wa bidhaa hizo.
Kuwepo kwa Ethiopia kwenye meza hiyo kutachochewa pia na ushirika wake na Serikali ya UAE ambayo ni mmiliki wa kampuni ya Dubai Port World inayoendesha zaidi ya bandari 78 duniani. Ni vyema kufahamu kuwa UAE ndiyo ilikuwa msuluhishi wa mgogoro wa Ethiopia na Eritrea, sifa ambayo ilifanya Abiy Ahmed kutunukiwa tuzo ya Nobel.
Ethiopia imesogea katikati ya kiini cha uchumi wa dunia ya biashara kwa sasa, itakuwa rahisi kukosolewa lakini siyo kuondolewa. Afrika inapaswa kujifunza kwenye hili kuwa, palipo na maslahi ya kibiashara ya dunia na mataifa makubwa, kinachotazamwa ni maslahi na si makubaliano ya Waafrika.
Ezra Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917/+255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.