Mwanza. Zaidi ya vijana 100 wa Programu ya Kuwezesha Ushiriki wa Vijana Katika Kilimo Biashara (BBT- YIA) wanadaiwa kuondoka katika kambi ya Chinangali, Dodoma, ambako vijana hao wamekusanywa, wakidai hakuna mwelekeo kambini hapo, huku wakiishutumu Serikali kwa kushindwa kwake kutimiza ahadi ilizotangaza awali.
Kwa mujibu wa taarifa ilizozifikia The Chanzo, mpaka kufikia jioni ya Machi 19, 2024, vijana waliokuwepo kambini hapo ni kati ya 120 na 128 kutoka vijana 268 ambao Serikali imekuwa ikidai kuwepo Chinangali kushiriki kwenye programu hiyo inayokusudiwa kuongeza ajira za vijana milioni tatu na kuongeza ukuaji wa kilimo nchini hadi kufikia asilimia kumi ifikapo mwaka 2030.
“Watu tulioko pale [kambini] mpaka sasa hivi tunafika 134, kati ya watu 268 tuliotakiwa kuripoti, lakini walioripoti ni 261,” alisema mmoja wa viongozi wa vijana hao ambaye The Chanzo imeamua kutotaja jina lake kulinda usalama wake. “Watu wengine waliobaki hawako kwenye kituo, hawako kwenye kituo kwa sababu pale hakuna kinachoeleweka.”
“Wengine wanakuja, wanakaa siku mbili, wanachungulia, wanaondoka, wale wenye uwezo wa kifedha,” aliongeza kijana huyo. “Kwa siku mbili hizi, [Machi 18 na 19], watu wengi wameondoka, tumebaki watu kama 120 hivi. Lakini muda mwingi tunacheza hapo 120 hadi 130. Wengi wamekimbia hali iliyoko pale [kambini].”
Mmoja kati ya vijana walioondoka kambini hapo ameiambia The Chanzo: “Mimi binafsi nimeondoka, kuna mambo yangu nimekuja kufuatilia. Unajua kipindi kile watu wengi tuliondoka kwa sababu hapakuwa panaeleweka hapo ila nitarudi muda si mrefu. Pale kambini kusema ukweli panaboa. Sasa ukae pale ufanye shughuli gani, sasa ukalime shamba la ushirika ambalo hujui hata utavuna nini?”
SOMA ZAIDI: Vijana wa Mradi wa BBT Wadai Kutelekezwa na Serikali: ‘Tunaishi Katika Mateso na Mashaka’
The Chanzo ilimuuliza Vumilia Zinkankuba, Mratibu wa Programu ya BBT, endapo kama taarifa za vijana kuondoka kambini hapo zina ukweli wowote, ambapo aliomba apewe kwanza chanzo cha taarifa hiyo ndiyo ajibu kama ni za kweli au la.
The Chanzo, hata hivyo, iligoma kufichua watoa taarifa wake kwani kufanya hivyo siyo tu kungewaweka hatarini bali pia ni kwenda kinyume na maadili ya uandishi wa habari yanayosisitiza umuhimu wa kuwaficha watoa taarifa.
Mazuri ya Serikali
Taarifa za vijana hao kuondoka kambini Chinangali zinakuja takribani wiki moja baada ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuelezea mazuri mengi ambayo Serikali inafanya kwa vijana hao, kama nia ya Rais Samia Suluhu Hassan kutatua changamoto zinazowakabili vjana wa Kitanzania, hususan zile zinazohusiana na ajira.
Akizungumza katika hafla ya kusherehekea miaka mitatu ya Rais Samia hapo Machi 16, 2024, katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Bashe, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM), alisema kwamba Serikali imekusudia kuwajengea mazingira mazuri ya uzalishaji vijana wote wanaoshiriki katika programu hiyo ya BBT.
“[Serikali] imejenga nyumba ambazo vijana wanakaa; kwa kuwa tumewapaleka [vijana] shambani ili wakashiriki kuandaa maandalizi ya mashamba yao, Serikali inawapatia posho,” Bashe, ambaye amekuwa akiitetea sana programu hiyo, alisema. “Serikali inawalipia [vijana] chakula Shilingi 240,000 kwa mwezi na hela ya matumizi Shilingi 150,000. Pesa hizi wanapewa bure na Serikali.”
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
Katika hotuba yake hiyo, Bashe pia aligusia madai yaliyoibuliwa na baadhi ya wanufaika wa programu hiyo kwamba Serikali inawatelekeza, akisema hizo ni siasa, akiwasihi viongozi wa wizara yake kuzipuuza na waendelee na kazi, akiwaomba kufanya siasa wamuachie yeye kwani kazi hiyo anaiweza vizuri kama mwanasiasa.
“Utasikia mara ooh vijana wa BBT wametelekezwa, wafanywa nini, wamefanywa nini,” Bashe alisema. “Nataka niwaulizeni tu Watanzania, kijana aliyejengewa nyumba, amepewa kitanda, analipiwa umeme na Serikali, analipiwa maji na Serikali, amepewa bima ya afya, anapata posho ya [Shilingi] 390,000 kwa mwezi, anajengewa miundombinu ya umwagiliaji na amepewa barua kwamba unamilikishwa ekari tano za ardhi bure zenye miundombinu ya umwagiliaji, ametelekezwa huyo?”
“Na nimewaambia wale vijana waziwazi, yule anayetaka kufanya siasa, aondoke, awaache vijana waliojitoa waendelee kufanya hili jambo,” Bashe aliongeza. “Hatuwezi kuharibu jambo ambalo linaenda kutatua tatizo la ajira kwa vijana na [mnunuzi] yupo tayari [kununua mazao yatakayozalishwa].”
Madai mtambuka
Lakini mmoja kati ya vijana walioondoka kambini hapo aliiambia The Chanzo kwamba Serikali itakuwa inafanya makosa kupima ukarimu wake kwa kile inachowafanyia vijana bila kuzingatia malengo waliyokuwa nayo vijana hao wakati wanajiunga na programu hiyo na ustawi wao na ule wa familia zao.
“Sababu kubwa [inayopelekea vijana kuondoka] ni ukamilishwaji wa miundombinu,” alisema kijana mmoja ambaye tumeamua kutoweka jina lake hadharani kulinda usalama wake.
SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Waziri Bashe Juu ya Mradi wa ‘Ujenzi wa Kesho Njema’
“Kwa sababu mtu unaona zile ekari tano hazijakamilika, halafu, ndiyo unapata pesa [Shilingi] 150,000, unapata chakula, unalipiwa sawa, lakini kuna maisha mengine, familia zinamtegemea [huyu kijana], na mambo mengine yanatakiwa yaendelee,” aliongeza kijana huyo. “Kwa hiyo, mtu unaona ni bora ukapige vitu vingine mtaani ili kusifeli sana kwingine, nadhani hiyo ndiyo sababu kuu [ya kuondoka].”
Madai haya ya miundombinu na ekari tano za ardhi ndiyo yalikuwa msingi wa habari tuliyoripoti hapo Machi 5, 2024, ikihusu madai ya wanufaika wa programu hiyo hapo kambini Chinangali “kutelekezwa” na “kuishi kwa mateso.”
Habari hiyo ilebeba vilio vya vijana hao ambao waliishuku Serikali kwenda kinyume na ahadi zake za awali zilizowashawishi kujiunga na programu hiyo. Kwa mfano, Serikali iliwaahidi kuwagawia ekari tano kwa kila mmoja pamoja na kuanzisha miundombinu ya umwagiliaji. Badala yake, vijana wote 268 wanalazimika kulima shamba la ushirika linalokadiriwa kuwa na ekari zisizozidi 200.
Wanufaika pia wamelalamikia vigezo na masharti ya umiliki wa ardhi na uendelezaji ambavyo wameviita kama vya “kinyonyaji” na ambavyo vinaenda kinyume na misimamo na ahadi za awali za Serikali.
Vijana waliopo kambini hapo wameiambia The Chanzo kwamba tangu ichapishe habari kuhusu vilio vyao, baadhi ya mabadiliko yametokea kambini hapo, wakiamini kwamba kama sauti zao zitaendelea kupazwa basi kuna matumaini mambo yakaenda vizuri kambini hapo.
SOMA ZAIDI: Bajeti Wizara ya Kilimo Inaakisi Umuhimu wa Kilimo Tanzania?
Kwa mfano, Machi 15, 2024, siku kumi baada ya The Chanzo kuchapisha habari yake, vijana kambini hapo wanasema walianza kupokea hela ya kujikimu, ambacho kilikuwa ni kilio chao cha siku nyingi na ambacho Serikali ilikuwa ikichelewa kukitatua.
Habari hiyo pia ilimuibua Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja, aliyetembelea kambini hapo Machi 15 na kukutana na vijana, ambapo alisikiliza vilio vyao na kuwaahidi kuvichukua na kuvifanyia kazi, chanzo chetu kimesema. Mayanja pia aliwasihi vijana kutumia njia rasmi za kuwasilisha malalamiko, akishauri dhidi ya kutumia vyombo vya habari.
“The Chanzo mmetusadia kupaza sauti zetu, na ile makala imeleta matokeo chanya sana,” alieleza mmoja wa vijana hao kwa furaha. “Baada ya habari hii kuchapishwa, tumeona yale matamko ya kejeli na dharau hayapo tena kwa sasa.”
Kupotosha?
Katika hotuba yake ya Machi 16 hapo Mlimani City, Bashe aliwataka wanasiasa kuacha “kuwapotosha watoto wa kimasikini,” akisema wakati wao “wanavuna posho” kwa kuingia tu Bungeni, vijana wengi nchini hawana fursa zinazoweza kuwakikishia maisha yao ya baadaye.
Ingawaje Bashe hakutaja jina la mwanasiasa yoyote, The Chanzo inafahamu kwamba Halima Mdee, Mbunge wa Viti Maalumu, amekuwa mstari wa mbele kwenye kukosoa namna programu ya BBT inavyoendeshwa, akiwa ndani ya Bunge na hata nje kwa kutumia mitandao ya kijamii.
SOMA ZAIDI: Simulizi ya Kijana wa Mjini Aliyetaka Kupata Utajiri wa Haraka Kupitia Kilimo
Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Mdee alimsihi Bashe aeleze ni nini amekwisha kukifanya mpaka sasa katika kutekeleza bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2023/2024 iliyopitishwa na Bunge mwaka 2023 ya Shilingi bilioni 970.78, ambayo ni sawa na ongezeko la asilima 29.24 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2022/2023, Shilingi bilioni 751.1.
“Kama [Bashe] alikuwa na matarajio makubwa, na hakujua ukubwa wa anachokiahidi, akiri, na aseme wazi watu wajue,” Mdee aliiambia The Chanzo. “Sasa, kama kuwahudumia vijana 268 tu imekuwa kazi, hizo ajira milioni tatu alizoziahidi kufikia 2025 zitatoka wapi?”
Juhudi za kumpata Waziri Bashe kufafanua baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wadau hazikuzaa matunda kwani simu yake haipokelewi kila inapopigwa, na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakuwa amejibu mpaka tunachapisha habari hii.
“Bashe ni kaka na rafiki yangu, napenda mafanikio yake kama kijana, ndiyo maana ninasema,” Mdee alisema.
“Hivyo, asichukulie kama jambo binafsi,” aliongeza Mdee. “Kama kweli ana nia njema na hii BBT, awe makini pia na wanaomshauri, na awe na jicho la ziada. Wanaokukosoa ni wazuri kuliko wanaokupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, lakini kama anadhani yuko sawa asilimia 100 katika utekelezaji wa BBT, ni sawa pia.”
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.
4 responses
Asante kwa taarifa iliyoandikwa kwa weledi mkubwa. Mimi nina matumaini makubwa SANA na hii program ya bbt. Naiombea kila kukicha ifanikiwe.
Mimi ni mmoja kati ya watu waliokuwa na mashamba ya zabibu hapo kwenye huo mradi.
Tumeondolewa kwa nguvu bila fidia yeyote kupisha huo mradi, hadi hivi sasa hakuna fidia yeyote ambayo tumelipwa, na hakuna taarifa yeyote inayo eleweka kuhusu kadhia yetu hii.
Tunahangaika huku kusababisha usumbufu mkubwana hatujui hatima yetu. Je ni haki na ni sawa?
Waandishi wa habari tafadhri tusaidieni kupaza sauti.
Pesa nyingi sana za serikali zinapotelea kwenye matumizi ya magari ya kifahari mafuta na Safari zisizo za tija mwenge makonda na na kuzunguka viongozi wakubwa mikoani wakati wapo viongozi huko mikoani
Mpaka kizaxi hiki Cha wizi kife au kiondoke besha ni mfanyibiashara hana uelewa wa kilimo hajua hajawahi shika jembe
Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ametamka sahihi kabisa! Vijana wasiitaka kufuata masharti na taratibu za kuwemo katika mradi wa BBT waondoke mara moja, hawafai na ni hatari kwa mustakabali wa mradi wenyewe. Hawa vijana wanadhani kila kitu kinatoka “mbinguni” na kuwaangukia kama mana! Tufike mahali tuwe wakweli, wapi uliona Serikali inafanya kama ilivyofanya Serikali ya Tanzania kwa vijana (hapa Afrika)? Ni Burundi tu ndiyo wameiga mfano wa Tanzania na vijana tena wadomi kule wanachapa kazi siyo kamawaida. Hawa wenzetu wanaelekezwa cha kufanya wanaingiza siasa katika kazi! Laiti ningekuwa karibu na mradi huu ningewanyosha na tija ingeonekana.
Gaston Modest Kaziri,
MTENDAJI MKUU,
DEVCOM.