Kwa kawaida, nyumba imara hutokana na msingi imara; nyumba ambayo imejengwa juu ya msingi dhaifu inaweza kuharibika na hatimaye kubomoka kirahisi kwa kuwa haiwezi kustahimili misukosuko.
Na ndiyo maana inahimizwa kuwa programu za watoto, na baadaye vijana, ni muhimu kwa michezo yote ili kujenga timu bora, au wanamichezo bora wa baadaye.
Katika soka, hakuna nchi ambayo imewahi kutwaa Kombe la Dunia bila ya kuwa na programu za watoto. Hata Hispania ambayo inasifika kwa kujenga klabu kubwa zenye hadhi ya dunia, yaani Barcelona na Real Madrid, haikuwahi kutwaa Kombe la Dunia hadi ilipoanzisha programu za watoto.
Barcelona na Real Madrid zilitawala soka la Ulaya kwa muda mrefu, lakini nchi hiyo haikuweza kufanikiwa kimataifa hadi ilipoelekeza nguvu kwenye soka la watoto lililozaa nyota kama Iniesta, Sergio Ramos, Gerard Pique na wengine waliokuja kutwaa Kombe la Dunia.
Ngumi za ridhaa
Lakini si rahisi kukuta mchezo wa ngumi ukianzia kwa watoto. Mara nyingi mchezo huu huanzia katika ngazi ya vijana ambao, kwa kawaida, huanzia katika ngumi za ridhaa kabla ya kujiunga na ngumi za kulipwa.
SOMA ZAIDI: Wimbi la Wachezaji Kuvunja Mikataba Lidhibitiwe
Ndivyo ilivyo kwa mabondia wote wanaotamba duniani. Si Muhamad Ali, Michael Tyson wala Antonio Joshua walioanzia kwenye ngumi za kulipwa. Wote walifanya vizuri kwenye ngumi za ridhaa kabla ya mapromota kuwaona na kuwaingiza kwenye ngumi za kulipwa.
Wengi wao walichukuliwa baada ya kufanya vizuri katika Michezo ya Olimpiki, ambayo ni mikubwa duniani. Baada ya hapo, bondia anakuwa ameshaustua ulimwengu kuhusu uwezo wake na hivyo mapromota kumkimbilia kutaka aingie kwenye timu zao.
Hata awali, wakati ngumi za kulipwa zinaingia nchini, ngumi za ridhaa zilikuwa juu, zikiwa na mabondia kama vile Emmanuel Mlundwa, Gerard Isaac na Clement Chacha, ambaye ni mmoja wa waasisi wa ngumi za kulipwa, na baadaye mabondia kama Rashid Matumla na ndugu zake waliozipaisha ngumi za kulipwa.
Ni muhimu ngumi kuanzia katika ridhaa kwa kuwa huko ndiko ambako kijana hujifunza mambo ya msingi kwenye mchezo huo, mbinu na kupata uzoefu.
Asipopitia huko, ni vigumu kwake kuibuka na kuwa bora kwa kuwa atakuwa amekosa mambo ya msingi kabla ya kujiunga na ngumi za kulipwa ambazo kupoteza pambano moja kuna maana kubwa tofauti na ridhaa.
SOMA ZAIDI: Kwa Kufundisha Watoto Hujuma, Tunajenga Taifa la Aina Gani?
Inashauriwa kuwa ni muhimu bondia akashiriki angalau mapambano kumi hadi 20 kabla ya kujiunga na ngumi za kulipwa. Huko anaweza kushinda mapambano hayo yote na anaweza kupoteza baadhi, lakini asiathirike sana kimchezo kwa kuwa hiyo haiwezi kumzuia kupata mapambano mengine ya ridhaa.
Na kadri anavyopata mapambano ndivyo anavyojifunza zaidi makosa yaliyomfanya apoteze mapambano yaliyopita na kuyarekebisha na pia kuimarisha pale ambapo anaona anafanya vizuri.
Ndani ya ngumi za ridhaa bondia anakuwa na muda mchache wa kuutumia kuweza kupata pointi, au kushinda kwa kumzuia mpinzani kuendelea na pambano. Raundi za ngumi za ridhaa ni chache na hivyo humbana bondia kufanya kila awezalo ndani ya muda mfupi na hivyo kujengeka kuwa bondia bora kabisa.
Lakini hali haionekani kuwa hivyo katika miaka hii. Zile enzi za kwenda Anatouglo, au DDC Kariakoo, Relwe Gerezani au Uwanja wa Ndani wa Taifa kushuhudia mapambano ya ngumi za ridhaa kama Klabu Bingwa ya Taifa na Mashindano ya Mikoa sasa zimepotea.
Hazipo tena
Zile enzi za kwenda kuwashuhudia miamba ya taifa kama Titus Simba, Lucas Msomba, Mlundwa, Willy Isangura, Nassor Michael, Chacha, Benjamin Mwangata na Anthony Mwang’onda hazipo tena.
SOMA ZAIDI: Yanga Imefanyiwa Ukatili, CAF Ifanyie Kazi V.A.R
Tutapata wapi mabondia wazuri wa kulipwa kama msingi wenyewe, yaani ngumi za ridhaa, haupo?
Ndio, kuna mwamko mkubwa wa ngumi za kulipwa kwa kuwa kampuni kama Azam Media inafanya kazi kubwa ya kuendeleza ngumi kutokana na uwekezaji wake katika mchezo huo. Na unaweza kusema ni kama Azam Media, pamoja na wadau wachache, imefufua mchezo huo maarufu katika mitaa yetu huku ‘Uswahilini.’
Lakini juhudi za Azam Media na hao wadau wachache zinaongezwa nguvu vipi ikiwa msingi wa mchezo huo unadidimia?
Nafahamu kuwa kulikuwa na jitihada za kufufua uongozi wa ngumi za ridhaa kwa kuanzisha Shirikisho la Ngumi za Wazi (za Ridhaa), lakini hakuna dalili nzuri kwamba ngumi hizo zinarejea kwa nguvu kama ilivyokuwa awali.
Bado vijana wengi wanakimbilia kwenye ngumi za kulipwa kwa matarajio kuwa wanaweza kujitengenezea maisha kwa muda mfupi, kumbe wanakosa mambo ya msingi katika mchezo huo na hivyo kutopanda viwango kama inavyotakiwa.
SOMA ZAIDI: TFF Ifanye Uamuzi Mapema Kocha wa Taifa Stars
Na hata ukiangalia baadhi ya mapambano, unaona dhahiri jinsi vijana hao wanavyokosa mbinu za msingi katika upiganaji na matokeo yake wanarusha makonde kama wanaua nyoka. Ile ladha ya ngumi yenyewe inapotea na kinachobakia ni kushabikia bondia kwa sababu tu ya mambo yake tofauti na mchezo.
Ni muhimu kwa wahusika kuweka juhudi katika kuurudisha mchezo wa ngumi za ridhaa kwa kuwaelimisha viongozi wa klabu za ngumi za kulipwa kutowaharakishia vijana kwenye ngumi za kulipwa na kuwahimiza kuanzia ngumi za ridhaa.
Kama Shirikisho la Ngumi za Wazi litafanya kazi sambamba na ngumi za kulipwa kuna uwezekano wa ngumi za ridhaa kurejesha makali yake na baadaye kuzalisha mabondia bora wa ngumi za kulipwa.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.