Ni rahisi sana kusahau tulikotoka. Ikiwa tutakuwa jamii isiyopenda kutafuta kujua waliotutangulia waliwaza nini, walisema nini, waliona nini, tutajikuta tumesahau chimbuko letu kama watu. Tutabaki tu kusema ‘Enzi za Mwalimu …’
Haswa kwenye ulimwengu wa sasa ambao mambo yanakwenda kwa kasi sana, huku mabadiliko ya kiteknolojia yakiathiri uchumi, na hali ya kijamii kiujumla kiasi kwamba ni rahisi kudhani kwamba misingi ya maendeleo yetu iliyowekwa na waliotutangulia si ya muhimu tena.
Nasema hivyo nikimaanisha kwamba, ni rahisi kudhani kwamba fikra fulani hazituhusu tena kwa sababu zama zimebadilika.
Amani
Binadamu na Maendeleo ni kitabu kinachobeba hotuba 11 alizohotubia Julius Nyerere kati ya mwaka 1968 na 1973 akiwa Rais wa kwanza wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Nitazungumzia hotuba nne tu katika makala hii. Hotuba ya kwanza kunakiliwa ni ‘Mwaka Mpya wa Amani.’
Akihutubia mabalozi hapa Tanzania siku ya Mwaka Mpya mwaka 1968, Nyerere anazungumza kwa namna ambayo ni kama vile anaongea nao leo. Yaani, ungechukua hotuba hiyo na kusema kwamba ilikuwa ya mwaka 2024, hakuna ambaye angepinga.
SOMA ZAIDI: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima
Bila shaka ulikuwa ni utaratibu aliokuwa amejiwekea, kuzungumza na mabalozi katika hafla fupi na kuukaribisha mwaka mpya kwa pamoja. Maana makavazi ya mtandaoni yanaonesha kuwa alikuwa na hotuba nyingine katika mazingira yanayofanana mnamo mwaka 1980.
Katika hotuba hiyo, Mwalimu, kama kiongozi huyo anavyojulikana, anasisitiza kuwa amani na haki za binadamu zinaenda pamoja. “Amani na haki ya binadamu ni vitu viwili vinavyoambatana. Kwa hiyo, katika jitihada za mataifa za kutafuta amani, lazima tujitumbukize vile vile katika jitihada za mataifa za kutafuta haki.” (uk. 2).
Mwalimu anasisitiza kwamba walio huru wanao wajibu wa kuwasaidia wale ambao wamefungwa. “Hatuwezi kupumzika hapo tulipo kwa sababu tu baadhi yetu tuna raha na hali ya kuridhika. Sisi tulio huru, na kupata uwezo wa kuendeleza mataifa yetu, hatuna haki ya kudai wale wanaoonewa, waliotumbukizwa katika shida za kubaguliwa, wanaokufa njaa, na wanaoteswa, waikubali tu hali hiyo. Tukitoa madai hayo, sisi wenyewe tutakuwa ndio tunaowatesa na kuwaonea.”
Tujiulize, leo hii hakuna aliye katika hali hii anayehitaji msaada wetu? Tutafakari na kujiuliza, nini nafasi yetu.
Hitimisho la hotuba yake inaonesha dira na msimamo wa Tanzania: “Sisi Watanzania tutaendelea na juhudi zetu za kuitekeleza imani hiyo mnamo mwaka 1968, na katika hilo tunatarajia ushirikiano kutoka kwenu na kutoka kwa watu mnaowawakilisha.”
Elimu
Katika ‘Faida ya Elimu katika Nchi,’ Mwalimu anamlinganisha mwanafunzi wa chuo kikuu na trekta. Alisema hayo akiwa anazungumza kwenye Chuo Kikuu cha Liberia jijini Monrovia, mnamo Februari 29, 1968.
SOMA ZAIDI: Zainab Burhani Anavyouchora Mchango Chanya wa Baba Katika Malezi ya Watoto Kwenye ‘Mali ya Maskini’
“Tunatumia fedha kutafuta faida kwenye akili ya mwanadamu, kama vilevile tunavyotumia fedha kununua trekta… tukinunua trekta tunalitarajia kufanya kazi kubwa zaidi kuliko kazi ya mtu na jembe lake la mkono, vilevile tunatarajia mwanafunzi tuliyemsomesha chuo kikuu kutusaidia kiasi kikubwa zaidi katika kazi za maendeleo yetu kuliko yule ambaye hakupata bahati hiyo.”
Mwalimu anaongelea dhana ya kusoma kwa ajili ya manufaa ya umma. Elimu inakuwa ni mtaji wa maisha mazuri na maendeleo ya jamii nzima. Zamani kulikuwa na utani kwamba mtu mmoja alikuwa anakwenda shule na kusomeshwa kwa fedha za kijiji, wakiwa na matumaini kwamba angerudi hapo kijijini ili kuboresha maisha yao.
Leo hii, watu hawasomeshwi na kijiji kama zamani. Wengi wanaona kwamba hata hiyo elimu ya darasani haiwasaidii sana maana ajira hakuna. Hata hivyo, elimu ina manufaa mengi zaidi kuliko ajira pekee.
Mimi naamini kwamba katika kupata ufahamu, kukutana na watu, kupanua uelewa kuhusu mambo mbalimbali, mtu anajengwa ili awe mwanajamii bora zaidi. Na kama Mwalimu alivyosema, akimnukuu Bwana Yesu katika Biblia, “Kila aliyepewa mengi, kwake yatatakiwa mengi.”
Mwalimu anasema kuwa Waafrika wapo katika nafasi nzuri sana kuliko walio katika nchi zilizoendelea. Bado tuna nafasi kubwa ya kufanya mambo yawe bora zaidi – kujenga makazi bora, kuwa na elimu bora, huduma bora za jamii, miundombinu, na kadhalika.
SOMA ZAIDI: ‘Mapenzi Bora’ ya Shaaban Robert Inavyochambua Maana Pana ya Dhana ‘Mapenzi’
Hivyo, hakuna haja ya kujenga matabaka, lakini kila mmoja katika nafasi yake anapaswa kuona umuhimu wake na kufanya kazi kwa moyo au mtazamo huo. Mwalimu anasema: “Sisi wenyewe lazima tuwe sehemu ya taifa hilo tunalotaka kulibadili.” (uk. 9)
Anasema, “Maendeleo ya kweli ni maendeleo ya watu.” Tena anasisitiza ushiriki wa watu katika maendeleo hayo. Walio na elimu wasiwadharau wasiyo nayo, wala wasikae mbali wakiendesha mambo kwa kutoa maagizo tu ilhali hawajui nini haswa kinaendelea kwenye jamii. Ni lazima kuwe na ukaribu kati ya viongozi na wananchi, ndio msimamo wake.
Kuwasemea watu
Akiwa Uganda, Mwalimu alizungumza kwenye mkutano wa chama cha Uganda People’s Congress mnamo Juni 7, 1968, wakati huo Milton Obote alikuwa Rais. ‘Lazima Chama Kiwasemee Watu,’ ndiyo jina la hotuba hiyo.
“Wakati wa kutafuta maendeleo, [Serikali] zinaweza zikasahau kwamba watu wanaweza kuwa na mambo fulani ya maana kwao ambayo hawako tayari kuyaacha kwa sababu ya maendeleo ya vitu.”
Anaendelea kusema kuwa nia njema haitoshi, utekelezaji unaeleweka? Mwalimu alikiona Chama kama daraja la kuielemisha jamii kuhusu mipango na nia ya Serikali, lakini pia kuyaleta maoni ya wananchi kwa Serikali. Kwa mtazamo wake, hii ilikuwa kazi ngumu sana kuliko hata kupigania uhuru kwani sasa walikuwa wanajenga nchi.
SOMA ZAIDI: Tusome ‘Kielezo cha Fasili’ Tujue Jinsi ya Kusoma
Nafurahi kusoma mawazo ya Nyerere. Kama Rais wa kwanza wa nchi yetu, aliyekuwa na ndoto ya kuiona si tu Tanzania bali Afrika iliyo na mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijami, nafurahia kuona alikuwa kiongozi wa namna gani ninaposoma mawazo yake.
Pamoja na makosa ambayo anaweza kukosolewa kwayo, kwani hakuna binadamu asiye na kosa, bado ni dhahiri kuwa moyo wake ulikuwa unaipenda nchi yake kwa dhati. Natumai kuwa wataibuka Nyerere wengine wengi kwenye kizazi chetu, ambao wataendeleza mawazo yake kwa kujenga juu ya msingi aliouweka.
Kazi
Ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya Azimio la Arusha, Mwalimu alifungua kiwanda cha nguo Julai 6, 1968, eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam. Alikisifia kiwanda hicho kuwa cha kwanza Afrika Mashariki kuwa na uwezo wa kutia urembo kwenye nguo za pamba.
Katika hotuba yake ya ‘Malengo ya Kazi,’ Mwalimu anawaagiza wafanyakazi wa kiwanda hicho kufanya kazi kwa weledi, kufika kazini kwa wakati na kuwa “Lazima waiangalie mitambo iliyomo, maana mitambo hiyo ni mali yetu.” Kila mmoja aelewe shabaha ya kiwanda ni nini, na maendeleo wanayoenda kuyaleta.
Kulikuwa na matumaini katika hotuba yake kuwa sasa mambo yanakwenda kubadilika. Sawa, Wachina wametujengea kiwanda lakini sasa pamba yetu haitakwenda nje kutengeneza nguo nasi tuletewe tu. Sasa na sisi tunakuwa wazalishaji.
SOMA ZAIDI: ‘Sanaa ya Ushairi’ Inavyomdhihirisha Shaaban Robert Kama Mshairi Mbobevu
“Kabla ya mwaka huu kwisha tutakuwa tunasokota pamba, tunatengeneza kanga, vitenge, na nguo za aina nyingine kutokana na kiasi chochote cha pamba kitakachotosha kuwavika watu wote wa Tanzania.” (uk. 23).
Lakini, tunajua haikuwa hivyo. Leo miaka 56 baadaye, bado tuna matatizo yaleyale. Tunaposoma na kusikiliza mawazo yake kama kiongozi wa nchi, tunayo nafasi ya kujifunza alipokosea, lakini pia kuendeleza alipopatia na kujenga kutokea hapo alipoishia.
Mimi ninaamini kwamba katika siku za usoni tutaiona Tanzania ambayo Nyerere aliitamani sana. Hata hivyo, viongozi pamoja na wananchi wanao wajibu wa kuiweka nchi yao kwanza.
Kila mmoja, akiona kwamba yuko hapa kujijenga, kumjenga mwenzake na kuijenga nchi yake. Kama alivyosema Mwalimu, maendeleo ya kweli ni maendeleo ya watu. Hivyo, maendeleo ni watu. Nami naongezea, watu wenyewe ndiyo sisi.
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.