Ilikuwa Septemba 28, 1958, wakati wananchi wa Guinea, taifa la Afrika Magharibi, walipoamua kwa karibu asilimia 95 kuukataa ukoloni wa Ufaransa nchini mwao . Aliyeongoza vuguvugu la kudai uhuru alikuwa si mwengine bali Ahmed Sekou Toure. Toure alikuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi shughuli alizozianza alipokuwa nchini Ufaransa. Uamuzi wa Guinea kusema HAPANA uligeuka chachu ya kupigania uhuru kwa mataifa mengi barani Afrika.
Katika hotuba yake ya kihistoria Sekou Toure alitamka: “Ni afadhali kuwa huru katika umasikini kuliko utajiri katika utumwa.” Lilikuwa ni tukio la aina yake mwaka mmoja na nusu tu baada ya uhuru wa Ghana chini ya mwanamapinduzi mwengine wa Kiafrika, Kwame Nkrumah. Ghana, kama tunavyojua, lilikuwa taifa la kwanza kujitawala barani Afrika.
Miaka miwili baadaye Sekou Toure, mfuasi wa nadharia ya Karl Marx ambaye wafuasi wake walipenda kumwita jina la mkato ‘Sekou,’ alikitangaza chama chake Partie Democratique de Guinee (PDG) kuwa chama pekee cha kisiasa na taifa hilo la Afrika Magharibi likawa la chama kimoja. Mwanasiasa huyo aliyeipa pigo Ufaransa akawa maarufu barani Afrika, akishirikiana na Nkrumah kuongoza harakati dhidi ya ukoloni barani humo. Kiongozi huyo wa Ghana anakumbukwa kwa hotuba yake maarufu siku ya kupandishwa bendera ya Ghana huru, pale alitapoamka: “Ghana haitajihesabu kuwa huru wakati kukiwa na ardhi ya Afrika ambayo bado ipo chini ya ukoloni.”
Telli, Katibu Mkuu wa Kwanza wa OAU
Umoja wa nchi huru za Afrika OAU, ulipoundwa Mei 25, 1963 mjini Addis Ababa, tayari nchi kadhaa zilikuwa zimeshaungana na Ghana na Guinea kuwa huru. Aliyechaguliwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja huo, alikuwa msomi, mwanasiasa na mwanadiplomasia mahiri kutoka Guinea, Boubacar Diallo Telli. Kabla ya hapo aliteuliwa mwakilishi wa kwanza wa nchi yake katika Umoja wa Mataifa akiwa pia balozi nchini Marekani. Telli aliiongoza OAU (sasa inajulikana kama Umoja wa Afrika, au AU) kwa vipindi viwili Julai 1964 hadi Juni 1972, akikabiliwa na changamoto kubwa. Aliwahi kuuliza wakati mmoja: “Bila ya OAU Bara la Afrika lingekuwaje ?” Telli alikuwa mshauri wa Sekou na mwanadiplomasia mwenye msimamo, fikra na busara.
Wataalamu wa siasa za Afrika wanaamini mvutano kati ya watu hao wawili ulianza baada ya Telli kushindwa kupata uungwaji mkono alipotaka kugombea kipindi kingine kuwa Katibu Mkuu wa OAU mwaka 1972 ambapo Sekou Toure hakumuunga mkono. Badala yake alimshawishi arudi nyumbani na akamteuwa Waziri wa Sheria. Telli alijihisi mtu pekee mwenye uwezo na sifa za kumrithi Sekou Toure ambaye naye alimuona kuwa tishio kwake na hasa kwasababu ya sifa, heshima na umaarufu aliojijengea kimataifa. Kutokana na hayo uhusiano wao taratibu ukaanza kuwa mbaya baada ya Telli kurejea nyumbani.
Sekou Toure alianza kuchukua hatua kali za kimapinduzi ziliazonza baada ya shambulio lililoongozwa na askari kiasi ya 400 wa kukodiwa wenye asili ya Kireno, mamluki wageni kutoka nchi jirani na Waguinea waliokuwa uhamishoni walipoivamia Guinea Novemba 22, 1970. Hata hivyo, shambulio hilo lilishindwa. Kushindwa huko kulitokana na ushirikiano kati ya vikosi vya ulinzi vya Guinea na wapiganaji wa Chama cha Ukombozi wa Guinea Bissau na Visiwa vya Cape Verde waliokuwa na Makao Makuu na kambi zao nchini Guinea. Kwa pamoja, vikosi hivyo vilipigana bega kwa bega na vikosi vya ulinzi dhidi ya wavamizi na kulikandamiza shambulio hilo. Adui mkubwa wa Guinea haikuwa tu Ufaransa na nchi nyengine za Ulaya bali hata nchi jirani kama vile Cote dìvoire, Senegal na Gabon, ambako Ufaransa ilikuwa na ushawishi mkubwa.
Jaribio la kumpindua Toure la feli
Wavamizi walikuwa na malengo mawili. La kwanza ilikuwa ni kumpindua Sekou Toure na la pili ilikuwa ni kumkamata kiongozi wa PAIGC Amilcar Cabral, rafiki wa karibu wa Sekou Toure. Kuanzia hapo Sekou Toure akawa anawaangalia kwa jicho jengine wale aliokuwa na wasiwasi nao, ingawa hadi wakati huo hakukuwa na dalili ya mvutano na Telli. Mwaka 1976 mambo yakamgeukia. Telli alikamatwa pamoja na mawaziri wengine wawili na maafisa wawili wa jeshi ikidaiwa walihusika na mpango wa kuipindua serikali. Telli alikana na njama yoyote dhidi ya dola.
Madifing Diane, mkuu wa zamani wa usalama na waziri katika utawala wa Sekou Toure, hadi leo ni mmoja wa wale wasiokubaliana na hoja ya kwamba Telli hakuhusika. Diane anasisitiza kwamba kwamba mpinzani Amadou Diallo aliungama wakati akihojiwa na maafisa usalama kwamba Telli alihusika katika mpango wa kutaka kuipindua serikali. Lakini katika kitabu chake La Mort de Diallo Telli (Kifo cha Diallo Telli), mwandishi huyo aliyeachiwa huru 1980 na kukimbilia uhamishoni alisema alilazimika kumtosa Telli kwa sababu ya kuteswa na kusisitiza hakukuwa na mpango wa watu wa jamii ya Fulani dhidi ya utawala. Alidai wakiwa gerezani Telli alimuelewa na kumsamehe.
Telli aliuwawa akiwa mfungwa katika gereza la mateso la Boiro katikati mwa mji mkuu wa Guinea, Conakry, mwaka 1977 baada ya kukiri kuandaa njama za mapinduzi. Hadi leo haijafahamika kwanini OAU ulishindwa kutamka lolote juu ya kukamatwa au kuuwawa kwa katibu mkuu wake wa kwanza. Aliyetwikwa lawama hasa ya kifo chake na wengine wote waliotajwa kuwa wasaliti wa mapinduzi ya Guinea ni Ismail Toure, ndugu wa baba mmoja na Sekou, aliyekuwa na ushawishi mkubwa na tishio pia. Wakosoaji lakini hawaamini kwamba aliyoyatenda hayakuwa na baraka za kaka yake. Ismail aliuwawa wiki chache baada ya mwanajeshi Lansana Conte kutwaa madaraka katika mapinduzi wiki chache baada ya kifo cha Sekou Toure.
Tokea kukamatwa kwa Telli na kuuwawa mwaka 1977 na kufariki dunia kwa Rais Sekou Toure mwaka 1984, mivutano ya jadi ya kikabila kati ya Wafulani na Malinke, kabila la Sekou Toure, zimezidi. Wafulani, ambao ni 40 asilimia ya wakaazi wakiwa kwa sehemu kubwa wenye kudhibiti uchumi, hawakupata kutawala Guinea. Rais wa pili Lansana Conte alitoka kabila dogo la tatu la Susu na Rais wa sasa Alpha Conde, kama Sekou Toure, ni Mmalinke. Hapana shaka kisa cha Telli na wengine waliopotea nchini Guinea ni simanzi , lakini ni matukio yanayofanana na historia za mapinduzi au tawala za kimapinduzi karibu kote duniani. Kuanzia mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789, mapinduzi ya kisoshalisti ya Urusi yalioongozwa na Vladimir Lenin mwaka 1917 na zaidi wakati wa utawala wa Joseph Stalin ambaye leo hata baadhi ya makomred wanamlani. A yaliyotokea Zanzibar kufuatia mapinduzi ya mwaka 1964. Kuna usemi kwamba: “Mapinduzi yanapomaliza wapinzani huwageukia watoto wao.”
Ufuasi wa Toure, Telli bado uko hai
Kwa wafuasi wa wanasiasa hao wakuu wawili, upande wa Sekou bado kiongozi huyo wa zamani ni shujaa na wanamuangalia Telli kama msaliti. Wale wa upande wa pili, wanamuenzi Telli kama mwanasiasa shupavu aliyekuwa na ujasiri wa kumwambia Sekou Toure kile alichokuwa akikifikiria kila palipokuwa na haja ya kufanya hivyo kwa masilahi mapana ya Taifa lake na Afrika kwa ujumla. Afrika inamuangalia kila mmoja wao kwa mtazamo tafauti. Wote wametoa mchango mkubwa katika historia ya Guinea na Afrika. Sekou Toure aliijenga Guinea kisiasa, kijamii na kitamaduni na kutumia kutambuliwa umahiri wa Telli kimataifa kuwa mafanikio ya nchi yake na kiyoo kwa mataifa mengine.
Kuhasimiana wanasiasa hao wawili kunafanana na yaliotokea kwengineko barani Afrika ambapo viongozi wakuu wa nchi walifarakana na wanasiasa wenzao waliokuwa bao bega kwa bega kupigania uhuru wa nchi zao. Mfano ni Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na mwanasiasa aliyekuwa maarufu, waziri wake wa mambo ya nje Oscar Kambona. Nchini Kenya nako, Jomo Kenyatta na Makamu wake wa Rais Jaramogi Oginga Odinga mambo pia yalienda mshikemshike. Zambia Rais Kenneth Kaunda na Waziri wa nje na baadae Makamu wa Rais Simon Kapwepwe vivyo hivyo. Na hata Somalia kati ya Siad Barre na Omar Arteh Ghalib. Ghalib alikuwa miongoni mwa mawaziri wa mambo ya nchi za nje waliosifika katika kanda ya Mashariki mwa Afrika. Wakati Kambona alitoroka nchini, Jaramogi, Kapwepwe na Ghalib walikamtwa na kuwekwa ndani. Sababu kubwa yakukosana wanasiasa hao na wakubwa waliokuwa wakitawala ni tafauti za muelekeo, zikiwemo nadharia, pamoja na kuona umaarufu wao kuwa kitisho kwa mamlaka zao.
Tukirejea ya Guinea, mpaka leo ni jambo lisiloepukika kuizungumza nchi hiyo pasina kulidhukuru jina la Sekou Toure na Diallo Telli. Kitendawili cha masaibu ya watu hao wawili bado hakijatenguliwa. Sambamba na hayo, swali linalobaki miaka 36 baada ya kifo cha Sekou Toure ni je, kiongozi huyo alikuwa dikteta au mlinzi wa uhuru na mapinduzi ya Guinea? Na je, miaka 43 baada ya kuuwawa kwa Diallo Telli, ni kweli mwanadiplomasia huyo alikuwa msaliti?