The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Morocco: Chachu ya Soka la Afrika, Duniani

Ni kutokana na uwekezaji mkubwa taifa hilo la Afrika Magharibi linafanya kwenye sekta ya michezo.

subscribe to our newsletter!

Nimebahatika kutembelea maeneo mengi nchini Morocco katika ziara zangu za kikazi na kushangazwa sana na maendeleo makubwa katika nyanja za michezo kiasi ambacho naweza kusema miaka si mingi ijayo, Morocco inaweza kuliingiza bara la Afrika katika ushindi wa mchezo wa soka kidunia.

Tayari, dunia imeanza kushuhudia kupanda kwa kiwango cha soka la wanaume na wanawake barani Afrika kupitia michuano mbalimbali ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka ya hivi karibuni.

Katika nchi kadhaa za Afrika, kumeibuka wachezaji mmoja mmoja wanaotingisha dunia katika uga wa soka, huku wakichukuliwa kwenda kucheza soka la Ulaya na kwingineko kutokana na ubora wa viwango vya soka wanaouonesha.

Sijawahi kuwa mwandishi wala mchambuzi wa soka lakini eneo langu la kitaaluma ni eneo lenye mawanda mapana ambamo mpira ni sehemu muhimu sana katika mahusiano ya kisiasa na kimataifa.

Walio na kumbukumbu watakumbuka kuwa ukombozi wa bara la Afrika ulichangiwa sana na harakati za kutumia mpira, hasa soka kama mbinu ya uhamasishaji.

Ni katika mazingira hayo, nimeona kuwa siwezi kuacha mambo kadhaa niliyojifunza katika safari yangu ya Morocco yapotee bure eti kwa kuwa mimi si mchambuzi wa soka.

Nilitembelea Morocco katika muda ambao ni muhimu sana kihistoria. Kwanza, timu ya taifa ya Morocco imetoka kuitoa Afrika kimasomaso pale ilipoyoyoma na kufikia nusu fainali za Kombe la Dunia linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) tangu kuanza kwake mwaka 1930.

Hivi ni watu wangapi tunajua kuwa tangu michuano hiyo ianze miaka 93 iliyopita, hakuna timu ya Afrika iliwahi kufikia hatua ya nusu fainali ambayo Morocco ilifikia?

SOMA ZAIDI: Ni Kwa Kiwango Gani Waafrika Wanaweza Kujitatulia Matatizo Yao Wenyewe?

Ushindi mkubwa kuliko zote ambazo nchi za Afrika iliwahi kufikia kwenye michuano ya FIFA ni kuingia hatua ya robo fainali ambayo Cameroon, Ghana na Senegal ziliwahi kupata katika miaka tofauti tofauti.

Kwa mfano, Senegal iliwahi kuingia katika hatua ya robo fainali mwaka 2002 na hatua ya makundi mwaka 2018. Kwa upande wake, Cameroon iliwahi zaidi kuanza kufikia hatua ya makundi na baadaye robo fainali mwaka 1990.

Ghana imekuwa na bahati zaidi kwa kuingia robo fainali za FIFA mara mbili mfululizo, mwaka 2006 na 2010.

Kwa watu wengi, ilikuwa ni kama bahati ya mtende kwa Morocco kuchomoza kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022, ikitoboa kuingia makundi, robo fainali na hatimaye nusu fainali, ikiweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kupata mafanikio hayo.

Siyo bahati

Hata hivyo, kwa aliyewahi kutembelea Morocco kama mimi atakubaliana na mimi kuwa haikuwa bahati kwa nchi hiyo ya kifalme kufikia ushindi huo.

Labda itafaa niseme kuwa mafanikio ya Morocco ni matunda ya uwekezaji wa nchi hiyo katika michezo mbalimbali, ikiwemo soka la wanaume na wanawake.

Ukifika Casablanca, utashangazwa na hamasa ya wananchi katika mpira wa miguu lakini ukizidi kwenda mikoani, hamasa ndiyo kwanza inaongezeka.

Kwa mfano, nilitembelea miji yote mikubwa ya Morocco ikiwemo Rabat, Agadir, Tangier, Fez na Marrakech na kubaini kuwa kila mji wenye hadhi ya mkoa una uwanja wa kimataifa wa mpira wa miguu unaokidhi viwango vya FIFA.

Viwanja hivyo vyote vina uwezo wa kuingiza watazamaji kati ya 40,000 na 46,000 kwa wakati mmoja, huku vikiwa na huduma mbalimbali ndani yake kwa ajili ya mazoezi na burudani.

Pia, kuna vyumba vya malazi, mabwawa ya kuogelea, vyumba maalum vya kuondoa uchovu, huduma za matibabu na mazagazaga kibao ambayo kwa mujibu wa mameneja wa viwanja hivyo yanapatikana Morocco na viwanja vingine vichache sana barani Ulaya na Marekani.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Sawa Kwa Wasahrawi Kudai Kujitawala?

Katika chumba kimoja nilichojionea, wachezaji waliocheza mechi nyingi mno kwa wiki wanaingizwa humo kwenye baridi inayofikia nyuzi joto 100 nyuma ya 0 kiasi ambacho ndani ya dakika tatu tu mchezaji anatoka akiwa mpya tayari kukabiliana na mechi nyingine ya tatu ndani ya wiki hiyo.

Uwekezaji wa kifedha

Kuhusu uwekezaji wa kifedha na kibajeti, Morocco pia haina mshindani. Kwa miaka 13 tangu mwaka 2010, Morocco imewekeza katika kujenga na kuboresha viwanja vyake, huku ikiwekeza katika kutambua na kujenga vipaji wa wachezaji watoto na vijana wa kike na wakiume katika viwango vya kufurahisha.

Mfano mdogo tu ni kuwa katika kila mji wenye hadhi ya mkoa, kuna uwanja wa kisasa, timu ya soka la wanaume na la wanawake na timu za chipukizi wa chini ya miaka 17 (U-17) na chini ya miaka 23 (U-23).

Hawa wanakuwa wamepitia kwenye vyuo vya mafunzo ya soka wakiwa wadogo na kuelewa kanuni za awali za mpira.

Aidha, kampuni moja makini inayoitwa SONARGES inaratibu na kuendesha viwanja vyote nchini Morocco.

Pia, lipo Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) ambalo linaratibu shughuli zote za michezo na kuwa kiungo kati ya nchi hiyo na FIFA likiongozwa na rais wake ambaye ndiye mwakilishi wa Morocco katika baraza la FIFA.

Nilizungumza na Msemaji wa Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF), Omar Khyari na akaelezea mkakati uliokamilika wa ujenzi wa kituo chenye hadhi ya kijiji cha michezo kilichojengwa kwa gharama ya dirham milioni 630 za Morocco (takribani Shilingi bilioni 145 za Kitanzania).

Hapo pana eneo lililojengwa kila ukijuacho kuhusu michezo katika eneo lenye hekta 29.3 na ambalo lilizinduliwa na Mfalme wa Morocco Mohammed VI mwaka 2019.

SOMA ZAIDI: Shangwe la ‘Mlete Mzungu’ Lina Harufu ya Ubaguzi wa Rangi

Hapo pana vyumba vya wachezaji na makocha kwa timu za daraja A vipatavyo 66 na Suite 4 kwa ajili ya Makocha; vyumba 150 kwa ajili ya timu za taifa za U-23 na vyumba 45 vyenye vitanda 80 kwa ajili ya timu za U-17.

Makipa pekee wamejengewa vyumba vyao maalum 54 vyenye jumla ya vitanda 98.  Hapa pia pana viwanja vinne vya nyasi asili na vingine vitatu vya nyasi bandia. Kwa ujumla, nilishangazwa na maendeleo haya makubwa!

Ukichukua kijiji hiki, ongeza viwanja vya kisasa katika miji yote niliyotembelea ya Casablanca, Rabat, Agadir, Marrakech, Tangier, Ifrane, Meknes na Fez, unaweza kugundua kuwa Morocco iko vizuri sana kimichezo.

Huduma bora za kijamii

Lakini niligundua pia michezo haiwezi kung’ara pasipo huduma nyingine za kijamii na miundombinu kuwa katika viwango vya kimataifa.

Katika hilo, nilijionea viwanja vya ndege ambavyo vina ubora unaolingana na viwanja vya Uingereza katika miji sita kati ya miji mikubwa ya Morocco niliyoitembelea.

Aidha, Shirika la Ndege la Morocco lina ndege kubwa na za kisasa za kutosha kuruka moja kwa moja kwenda maeneo maarufu duniani kama uwanja wa JF Kennedy (Marekani); Doha (Qatar) na miji mikuu iliyo mingi ya Ulaya.

Pia, kuna uwekezaji katika hoteli za kimataifa katika miji hiyo yote huku maduka, mpangilio wa miji na kilimo cha umwagiliaji vikinishangaza kuliko vyote.

Hivi kweli, nchi ya jangwa kama Morocco inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kiasi cha kutegemewa na soko la Ulaya kwa asilimia zaidi ya 50?

Nilijionea mashamba yalivyotunzwa na kuwekewa miundombinu ya kuhakikisha kuwa kilimo kinachofanyika siyo cha kumtegemea Mungu ashushe mvua bali ni uhakika wa umwagiliaji.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Afrika ni Bara Huru?

Katika mazungumzo yangu na mtu wa Wizara ya Kilimo, nilijulishwa kuwa Morocco ndiyo kinara wa uzalishaji wa mbolea za chumvi chumvi Afrika nzima.

Katika safari yangu ya mwisho kutoka mji wa Fez kurejea Casablanca, nilikutana na malori takribani mia moja kwa uchache yakiwa yamebeba mbolea katika ujazo wa mifuko maalum ya kilo 1,200.

Nilitamani niondoke na fuko moja kwa ajili ya mahindi yangu na migomba shambani kwangu Miswe, Bagamoyo!

Kiukweli, haitanishangaza hata kidogo endapo rekodi ya Morocco katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia ambayo itafanyika Marekani, Canada na Mexico mwaka 2026 itazidi kupaa.

Tayari nchi ya Morocco inajifua na timu nyingi za Afrika katika michuano ya Klabu za FIFA 2022 ambapo nilishuhudia mechi mbili kali sana kati ya Wydad ya Morocco na Al-Hilal ya Saudia.

Pamoja na kufungwa katika mechi hiyo, Morocco waliitoa jasho kali Saudia huku mashabiki wapatao 45,000 wakifanya vimbwanga vikali katika uwanja wa Marrakech. Ilikuwa ni jioni ya furaha sana Morocco!

Vilevile, baada ya kushindwa kushiriki CHAN mwaka huu 2023 jijini Algiers akiwa bingwa mtetezi, kuna maandalizi yanayoendelea kwa ajii ya michuano ijayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika ambayo itafanyika 2025 huku Morocco yenyewe ikiwa imeomba kuwa mwenyeji wake.

Kutokana na miundombinu mizuri na ya kisasa iliyonayo, Morocco pia inaendelea kupokea timu mbalimbali zinazokuja kwa ajili ya mazoezi kutoka kila pande za dunia ikiwemo Real Madrid ambayo nikiwa naendelea na ziara ilifika kufanya mazoezi yake kwenye kituo cha kimataifa cha michezo.

Watanzania, tunajifunza nini kutokana na maendeleo ya soka nchini Morocco?

Mungu ibariki Afrika na watu wake wake!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts