Dar es Salaam. Maelezo yanayofuata yametolewa kutoka sauti kwenda kwenye maneno kutoka kwenye mahojiano maalum ambayo The Chanzo imefanya na Dk Baruani Mshale, mtaalamu wa masuala ya maliasili na mabadiliko ya tabianchi. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji.
Rai yangu mimi katika ngazi ya kitaifa Tanzania, kwanza ni kuweza kuangazia ni vitu gani ambavyo vinatuepelekea, kama taifa, tunashindwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kiwango kile ambacho tunatakiwa tuweze kukabiliana nacho.
Ukisoma makabrasha ya Serikali, unaona kabisa wameanisha na kuabainisha mbinu tofauti tofauti [za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi], na ni mbinu nzuri sana katika sekta nyingi. Lakini ukija katika suala la utekelezaji, unakuta kwamba utekelezaji una legalega.
Utekelezaji una legalega kwa sababu kwanza hakuna bajeti ya kutosha ambayo inawekwa katika kukabiliana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi na wizara husika.
Lakini pia, sekta muhimu ambazo zinaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi hazipati bajeti ya kutosha ya kuweza kukabiliana nayo. Kwenye sekta ya nishati, sekta ya kilimo, nakadhalika.
SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Ni Nini? Mtaalam Afafanua
Kwa hiyo, rai yangu ya kwanza ni kuweza kuangalia vipaumbele vyetu katika kuweka hizo bajeti.
Lakini vilevile, kuweza kuwa na mfumo wa kitaasisi na hili siyo suala jipya, ni suala ambalo limekuwa likiongelewa Tanzania kwa zaidi ya miaka 15 sasa.
Kwamba namna ambavyo tunakabiliana na masuala ya tabianchi na mazingira kiujumla, imegawanyika gawanyika [na] hatuna uratibu mzuri. Kwa hiyo, lazima tuwe na uratibu mzuri, tuboreshe ukusanyaji wa takwimu zetu [ili] kuweza kujua wapi kutakuwa na athari gani na lini, ili kuweza kuweka mbinu za kukabiliana nazo, yaani zile response actions ambazo zitakuwa zinafanyika kwa wakati.
Lazima tuangazie vilevile masuala ya nani wataathirika zaidi. Na hapa linakuja suala la athari hizi katika mtazamo wa kijinsia na makundi tofauti tofauti.
Mabadiliko ya tabianchi na mbinu ambazo tunazitumia tunaweza tukawa na nia nzuri, lakini unaweza kukuta kwamba zile mbinu bado zinaacha baadhi ya makundi, hasa ya wanawake, nyuma wakati wao ndiyo wanabeba mzigo wa familia inapokuwa imeathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.
SOMA ZAIDI: Nini Hupelekea Mabadiliko ya Tabianchi?
Kwa mfano, ukame na kupungua kwa maeneo ya misitu nakadhalika na kukosekana kwa nishati mbadala ina maana sasa wanawake watatembea umbali mrefu kuweza kutafuta kuni ambazo watazitumia katika matumizi yao pale nyumbani.
Wanawake watahusika katika kulima zaidi japo kuwa wanaume wanahusika lakini wanawake watahusika pia, watakuwa na mzigo mkubwa zaidi, mwanaume atakapotoka kwenda kutafuta ina maana ataacha mwanamke pale na watoto.
Kwa hiyo, masuala ya jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lazima pia yaangalie masuala ya kijinsia, ili kuweza kuhakikisha kwamba hakuna upande ambao unabebeshwa mzigo zaidi.
Hili ni suala ambalo binafsi sijaona likitendewa haki Tanzania. Kwa hiyo, hiyo ni rai yangu kwamba masuala ya kijinsia na mabadiliko ya tabianchi lazima yaangaziwe kwa kina.
Lakini vilevile, mashirikiano baina ya sekta za umma na sekta binafsi [ni lazima yaimarishwe kwenye kukabiliana na hizi athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi].
SOMA ZAIDI: Nini Kinadhihirisha Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania?
Tumesikia hivi karibuni kwamba Benki ya CRDB wamepata ruhusa ya kuweza kupata ile ruzuku kutoka ile Global Climate Facility. Lakini mpaka sasa hivi hatujui kama zile fedha zimeshaweza kuwafikia walengwa, kuweza kuboresha kama ni mifumo ya kilimo cha kisasa, kilimo ambacho kinaendana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa sababu zile fedha ni nyingi sana na zingeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa. Lakini hatujui mpaka sasa hivi zimefikia kiasi gani.
Kwa hiyo, badala ya kuwa tu jukumu la Serikali ya Tanzania, lakini vilevile sekta binafsi inaweza ikawa na jukumu la kusaidia katika kujenga uwezo wa wananchi wetu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuachana na shughuli za kimaisha [au] shughuli za kilimo ambazo zinakuwa tegemezi na zinaathiriwa zaidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Benki nyingine zinaweza zikafanya vitu kama hivyo. Tulisikia kwamba Benki ya NMB, kwa mfano, na wao wana mikakati yao ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
SOMA ZAIDI: Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Huathiri Maisha, Uchumi wa Watanzania
Tungependa kusikia zaidi na Serikali iweze kushirikiana nao. Taasisi nyingine pia ziweze kuangalia jinsi gani ambavyo tunaweza tukasaidia wananchi wetu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa hiyo, suala la kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni suala muhimu sana na liangaliwe na wadau wote na Serikali ihakikishe tuna uratibu mzuri.
Katika ngazi ya kimataifa ninapata uzito kidogo kutoa rai yangu, najiuliza hata kama kuna haja ya kusema rai yangu ni nini kwa wao. Kwa sababu wadau katika ngazi hiyo hakuna wanasichokifahamu, mijadala hii imekuwa ikiendelea, hayo majadiliano yameenda kwa miaka mingi sana, kila kitu wanakifahamu. Lakini bado utekelezaji wake ndiyo unaendelea kuwa tatizo.
Labda rai yangu mimi itakuwa ni moja tu kwamba, kuhakikisha mbinu zote za kuzuia, ama kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, haziwi na athari hasi kwa watu walioko katika nchi ambazo zinaendelea, nchi ambazo ni maskini.
SOMA ZAIDI: Mtaalamu Apangua Hoja za Wanaopinga Uwepo wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi
Kwamba tutaendelea kushiriki, kuhudhuria katika hayo mazungumzo, na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunatetea maslahi yetu vilevile na kuonesha kwamba wao ndiyo wamesababisha tatizo zaidi kuliko sisi na sisi tunaathirika zaidi.
Na hatuwaombi kama msaada lakini ni jukumu lao kutokana na kitu ambacho wamekisababishia kwetu na wafahamu tu kwamba sisi tukiathirika haimanishi kwamba wao wako salama.
Na kama ambavyo tumeona idadi ya wakimbizi wanaotoka nchi za kaskazini mwa Afrika na Afrika magharibi kwenda Ulaya imeongezeka. Tutaambiwa kwamba ni kutokana na migogoro inayotokea katika zile nchi, migogoro ya kisiasa, nakadhalika.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi?
Lakini tunafahamu kabisa kwamba mabadiliko ya tabianchi ni sababu moja wapo ambayo imepelekea watu wengi kuona kwamba hawana matumaini katika nchi zao. Na wanakimbilia katika nchi ambazo wanaona kuna tumaini ndiyo kama nchi za Ulaya nakadhalika.
Kwa hiyo, wasipotusaidia sisi, wasipolipia gharama za sisi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha hali katika nchi zetu, wafahamu kwamba wao pia hawatasalimika.
Kwa sababu watu wetu wataendelea kukimbilia kule na itakuwa ni tatizo kwao. Kwa hiyo, hili ni tatizo kwetu sote na ni jukumu lao kushirikiana na sisi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
SOMA ZAIDI: Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi Kusiathiri Haki Zingine za Wanajamii