Balozi wa Tanzania aliyemaliza muda wake wa uwakilishi nchini China baada ya kuahmishiwa London, Uingereza, Mbelwa Kairuki, aliagwa rasmi na Jumuiya ya Watanzania wanoishi katika jimbo la Guangdong nchini China mwanzoni mwa juma hili.
Akihutubia katika hafla hiyo iliyofanyika Septemba 9, 2023, Makamu Mwenyekiti wa Diaspora of Tanzanians in Guangdong (DITAG), Hasheem Shelali, alieleza namna ambavyo Balozi Kairuki alivyoweka jitihada za makusudi kuwaunganisha Watanzania kupitia mwavuli wa DITAG ambapo hapo awali waliishi kwa matabaka.
“Kabla ya uwepo wako nchini China kama Balozi, hatukua na jumuiya iliyo rasmi tunayoiona leo,” Shelali alisema kwenye hafla hiyo.
“Tulichokuwa nacho ni umimi, ubinafsi, na makundi ya kijamii ama maeneo flani,” aliongeza. “Haikuwa rahisi kutuunganisha, lakini kutokana na busara zako, ushawishi wako na ustahimilivu wako, ulituweka pamoja, ukatuunganisha na kutushawishi tuianzishe Jumuiya yetu hii.”
Kwenye hotuba yake ya kwanza alipokutana na Watanzania waishio China katika Hoteli ya Westin Guangzhou Machi 2017, Balozi Kairuki alikaririwa akitamani kuona Watanzania wakitumia uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili kukuza biashara za watu wa pande zote mbili.
Mafanikio makubwa
Miaka sita baadaye, Watanzania wengi waliopo China na waliopo hapa nchini Tanzania wamechangamkia fursa mbalimbali na kupata mafanikio makubwa.
Wana jumuiya ya DITAG walimshukuru Balozi Kairuki hasa kwa namna alivyotoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari, mikutano nchini na wafanyabiashara hasa wakati wa wimbi la UVIKO-19 jambo lililouisha mitaji au kunufaisha wadau mbalimbali.
Kwa kufanya hivyo, mara tu baada ya China kufungua mipaka yake, wanadiaspora walipata hamasa ya kusajili makampuni ya biashara kati ya Tanzania na China, hivyo kuliongezea pato taifa kupitia wanadiaspora.
SOMA ZAIDI: Kwa Kuzipatanisha Saudia na Iran, China Imelamba Dume Kwenye Siasa za Kimataifa
Hii imepelekea biashara kati ya nchi yetu na China kuongezeka maradufu, tofauti na hapo awali ambapo makampuni yaliyokuwa yanauza bidhaa yalikuwa ni machache sana, ambayo pia yalikuwa ni ya Wachina.
Hali ilivyo hivi sasa kampuni zaidi ya 100 za Watanzania zimesajiliwa nchini China kuuza maharage ya soya, ufuta, kahawa, korosho, na mazao ya uvuvi. Haya ni matokeo ya uongozi mahiri wa Balozi Kairuki kupitia usajihishaji wake.
Alama za Kairuki
Kwa msisitizo mkubwa, wana DITAG waliainisha maeneo makubwa manne ambayo Balozi Kairuki ameacha alama ya kukumbukwa.
Maeneo hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa Ofisi za Ubalozi Mdogo jijini Guangzhou, ambapo hapo kabla Watanzania wengi walisafiri mwendo wa saa nane kwa treni kufuata huduma za kibalozi jijini Beijing.
Jambo hili ni mafanikio makubwa kwani Guangzhou ndiyo kitovu cha Biashara nchini China.
Kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za ndege za Shirika la ndege la Air Tanzania ambapo kwa sasa kuna safari tatu kwa juma pia kumetajwa kama alama muhimu kati ya nchi za Tanzania na China, hasa katika uwanda wa biashara, utalii na mwingiliano wa watu.
Wakirejea kipindi cha wimbi la UVIKO-19, usafirishaji wa mizigo uliwezekana kupitia uanzishwaji wa usafiri huu.
SOMA ZAIDI: Tamu, Chungu Za Kuagiza Mzigo Kutoka China Kipindi Cha COVID-19
Upatikanaji wa fursa kwa Watanzania kushiriki maonesho mbalimbali ya kibiashara ni jambo jingine ambalo lilionekana gumu kabla ya uongozi wa Balozi Kairuki.
Mara baada ya ufuatiliaji wake wa karibu, leo hii bidhaa mbalimbali za Tanzania zimefanya vizuri katika masoko ya China kwa kuwa yalionekana kupitia majukwaa mbalimbali. Hii imeleta urahisi katika masoko ya moja kwa moja na hata yale ya mtandaoni kama Ali Baba na JD.COM.
Imani ya kibiashara kati ya Watanzania wafanyabiashara waishio China na wafanyabishara wa hapa nchini ni jambo jingine ambalo limefikiwa kwa ufanisi mkubwa.
Kabla ya hamasa za mara kwa mara za Balozi Kairuki kupitia vyombo vya habari, wafanyabiashara nchini waliamini Wachina kuliko wanadiaspora walioko China, hali iliyopelekea wakati mwingine kudhulumiwa. Hali hiyo sasa imeondoka kupitia hamasa ya hali na mali kupitia Balozi Kairuki.
Hii ilijidhihirika zaidi wakati wa wimbi la UVIKO-19 ambapo, pamoja na mipaka kufungwa, biashara ilifanyika bila hofu wala woga kutokana na imani kubwa iliyojengeka kupitia Balozi Kairuki.
Balozi Kairuki pia amepongezwa kwa kujiwekea utaratibu wa kutembelea kampuni za Watanzania walioko China na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
SOMA ZAIDI: Tembo wa Zawadi Kutoka kwa Nyerere Kwenda kwa Rais wa Ireland Alivyoibua Mzozo wa Kidiplomasia
Jambo hili liliamsha ari ya kazi miongoni mwa kampuni ndogo na kubwa kutokana na kuthaminiwa na kutambuliwa na Serikali yao. Vilevile, ilizijengea kampuni hizo heshima kwa wenyeji.
Akimkaribisha Balozi Kairuki, Konseli Mkuu wa Tanzania Jijini Guangzhou, Khatib Makenga amemshukuru Balozi Kairuki kwa malezi, maelekezo na ushirikiano alioupata wakati wakifanya kazi pamoja.
Makenga ameahidi kuendeleza masuala yote yaliyokuwa kwenye mipango ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa Ofisi za Konseli Kuu, Guangzhou na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan yanafikiwa.
Aidha, Makenga alitumia fursa hiyo kumhakikishia ushirikiano wa kutosha Balozi Mteule wa Tanzania nchini China, Khamis Mussa Omar.
Ahimiza umoja
Kwa upande wake, Balozi Kairuki aliwashukuru wanajumuiya ya DITAG kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha uongozi wake wa Ubalozi nchini China, akisisitiza wanajumuiya kubaki wamoja na wenye mshikamano, huku wakikumbuka kuwekeza nyumbani kwa mustakabali wa kuiletea nchi yetu maendeleo.
Akihitimisha hotuba yake, Balozi Kairuki aliwataka wanajumuiya kumpatia ushirikiano uleule aliokuwa akiupata Balozi Mteule, Omar.
SOMA ZAIDI: Buriani Bernard Membe, Mwanasiasa Sungura, Mwanadiplomasia Nguli
Balozi Kairuki anaondoka Beijing baada ya kuhudumu miaka sita ambapo, pamoja na kukuza uhusiano wa nchi hizo mbili, amesimamia diplomasia ya uchumi kwa umahiri mkubwa.
Biashara na uwekezaji umekuwa kwa kiwango kikubwa. Mathalan, mwaka 2021, nchi ya China ilikuwa mwekezaji mkubwa hapa nchini, ikiwa imewekeza mtaji wa Dola za Marekani, bilioni 7.6.
Mnamo mwaka 2017, biashara kati ya Tanzania na China ilikuwa Dola za Marekani 2.5 bilioni na hadi kufikia mwaka 2021, iliongezeka na kufikia Dola za Marekani 9.6 bilioni.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Jimboni Guangdong, hasa jijini Guangzhou, ilihudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida, Konseli Mkuu wa Tanzania Guangzhou, Khatib Makenga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri pamoja na wanajumuiya wa DITAG.
Abertus Paschal ni mwandishi na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia rabertus@gmail.com au X (Twitter) kama @rutaraka. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi, na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
All the best bro,your doing well, congratulations…My God bless and Keeping you,on positive stand.I love U