The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

Maboresho hayo hayaepukiki kuepusha maboresho ya sheria yanayotarajiwa kukinzana na Katiba.

subscribe to our newsletter!

Tukiwa tayari tuko mwishoni mwa mwaka 2023, sasa ni dhahiri kuwa haiwezekani kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya na kuanza kuitumia Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 au Uchaguzi Mkuu 2025.

Kitaalamu, katika hatua hii tuliyopo, yapo mambo kadhaa tunaweza kuyafanya kama nchi ili kuepuka hali ya taharuki huko tuendako. Moja ni kuuahirisha rasmi mchakato huo ili tuendelee nao baada ya Uchaguzi Mkuu 2025.

Pili ni kuboresha sheria mbalimbali zinazogusa masuala ya uchaguzi ili Uchaguzi Mkuu ujao usifanyike ukiwa na malalamiko yaleyale ya miaka nenda, miaka rudi.

Kama taifa, tunapaswa tufanye juhudi za kuunasua Mchakato wa Katiba Mpya kutoka topeni kichakani, tuuache ukiwa mahali pazuri na peupe.

Kwa bahati mbaya, mchakato huo uliahirishwa vibaya mwaka 2014 pasipo kuweka utaratibu wa kisheria juu ya lini na wapi tutarejea tena kwenye mchakato huo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hii ndiyo ilikuwa sababu kuu ya kutelekezwa kwa mchakato huo rasmi baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.

Kauli za viongozi kuwa Katiba si kipaumbele chao baada ya uchaguzi isingeweza kupata nafasi kama Watanzania tungekumbuka kukubaliana, kwa maandishi, kuhusu ratiba nzima ya namna ya kurejea kwenye mchakato baada ya uchaguzi.

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba Tanzania

Hili lilipaswa lifanyike wakati wa kuahirisha Mchakato wa Katiba Mwaka 2014. Kwa sasa, maoni yangu ni kwamba bado tunaweza kufanya hatua muhimu ya kuahirisha rasmi mchakato huu.

Tunaweza kufanya hivyo kwa kupeleka Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bungeni ambao utahuisha mchakato na kuchora ratiba nzima ya jinsi tutakavyorejesha mchakato huo katika uhai wake sasa na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025.

Sambamba na uhuishaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kutahitajika pia kuhuisha Sheria ya Kura ya Maamuzi ili tuwe na seti kamili ya sheria za mchakato zikieleza nini kitafanyika lini.

Hatua hizi za kuhuisha sheria ni hatua za kufanyika sasa, zikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, ni ukweli kwamba tumekwishajichelewesha sana kiasi kuwa hatutaweza kukamilisha Mchakato wa Katiba Mpya na kuanza kuitumia Katiba hiyo kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwaka 2025.

Ingawa Katiba Mpya si kwa ajili ya uchaguzi pekee, uchaguzi ni sehemu muhimu ya kwa nini Katiba Mpya inahitajika.

Kwa sababu hiyo, ipo haja nyingine ya kuhakikisha kuwa, kama taifa, tunafanya marekebisho ya sheria kadhaa muhimu zinazogusa uchaguzi kabla uchaguzi ujao kufanyika ili kupunguza malalamiko. Kwa uchache, naziona sheria kama sita au saba zenye mahitaji ya kuziboresha.

Tume huru

Kwanza, kuna sheria mpya itapaswa kutungwa ikiitwa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC). Hii itaweza kuweka sawa masuala ya uratibu na usimamizi wa uchaguzi kiasi cha kupunguza malalamiko ya kila uchao kuhusu kukosekana kwa uhuru wa tume.

Watanzania wengi wamekuwa wakishauri tume hii huru iwe ndiyo mratibu na msimamizi wa chaguzi zote nchini: rais, wabunge, madiwani, Serikali za Mitaa, na chaguzi za wawakilishi wa Tanzania katika vyombo vya kikanda kama vile Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Bunge la SADC, na Bunge la Afrika (PAP).

SOMA ZAIDI: ‘Kidole Kimoja Hakivunji Chawa’: Uchaguzi Mkuu wa Nigeria 2023 na Mambo Makuu ya Kujifunza Tanzania

Sheria hii pia itaboresha mfumo wa uandikishaji wapiga kura ili kupunguza malalamiko, hasa ya vijana kuchelewa au kushindwa kabisa kuandikishwa pamoja.

Maboresho pia yatasaidia kuondoa hofu kuwa tume imekuwa ikifanya kazi kwa maelekezo ya Serikali, na hivyo kukipendelea chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Sheria ya pili ambayo inapaswa kuboreshwa ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania.

Sheria hii ndiyo inayoweka mfumo mzima wa uandaaji na usimamizi wa uchaguzi nchini. Kwa bahati mbaya, sheria hii imemegewa kipande kimoja tu cha uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

Nimewasikia Watanzania kwa miaka zaidi ya 30 ya demokrasia hapa nchini kwetu wakitoa wito kuwa sheria hii isiache uchaguzi wowote wa kiserikali nchini.

Kwa sababu hiyo, sheria itapaswa kuweka mfumo mzima wa maandalizi, usimamizi na uratibu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Uchaguzi Mkuu na Uchaguzi wa Watanzania wanaokwenda kutuwakilisha katika mabunge mengineyo nje ya nchi yetu.

SOMA ZAIDI: Mchakato wa Katiba Mpya Tanzania: Yajayo Yanafurahisha

Watanzania wengi wanataka sheria hii iwezeshe matumizi ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa ajili ya chaguzi zote nchini na kwamba uchaguzi wote huo ufanyike katika tarehe moja itakayoteuliwa na Tume ya Uchaguzi mwaka 2025.

Kuna hoja kwamba itakuwaje viongozi wa Serikali za Mitaa wakae madarakani kwa zaidi ya miaka mitano ili kuwahamishia kwenye Uchaguzi Mkuu.

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba hii haitakuwa mara ya kwanza kwa kitu kama hicho kufanyika kwani hata madiwani waliwahi kuwa sehemu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hadi walipohamishiwa Uchaguzi Mkuu ambapo walilazimika kuhudumu kwa miaka sita kusubiri tarehe ya Uchaguzi Mkuu. Hakuna linaloshindikana!

Vyama vya siasa

Sheria nyingine muhimu sana kuiboresha ni Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 ya Sheria za Tanzania. Hii ndiyo inayoweka mfumo mzima wa usajili na uratibu wa vyama vya siasa Nchini – Bara na Zanzibar.

Kwa uchache, sheria hii inatarajiwa kuwa ndiyo inayoweza kunidhamisha vyama na kuvifanya vijiendeshe na kuendeshwa kwa misingi ya haki, usawa, demokrasia na uzalendo.

Kwa sasa, Watanzania wengi wanaona kuwa vyama ni kama mali ya watu binafsi kwa vile vikundi vilivyoanzisha na kusajili vyama hivyo ndivyo vimeshikilia taasisi hizo tangu mwaka 1992.

SOMA ZAIDI: Maswali Muhimu Uchaguzi Mkuu wa Kenya Ukielekea Mahakamani

Vyama vimeshindwa kuweka na kusimamia dhana ya kupokezana vijiti ambayo ni muhimu sana kwa uendelevu wa taasisi yoyote ya kidemokrasia.

Ofisi ya Msajili ya Vyama nayo inalalamikiwa kwa upendeleo na ulegevu katika kusimamia shughuli za vyama, ikiwemo maadili. Vitendo vya ukiukwaji wa sheria, maadili na tunu za taifa vinaonekana kuwa vinatokana na ulegevu wa ofisi hii.

Kwa sababu hiyo na nyingine zinazohusu uboreshaji wa ufanisi wa vyama vya siasa, inashauriwa kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama iwe ni sehemu ya idara za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili tume iwe ndiyo nyumba kuu ya demokrasia ya uchaguzi.

Sambamba na hilo, Ofisi ya Msajili wa Vyama inahusika na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa na inashauriwa kuwa ofisi hiyo kuwa sehemu ya tume kutaleta ufanisi juu ya matumizi ya ruzuku kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uchaguzi wa wanachama kwa usawa, ikiwa ni pamoja na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Rusha na uchaguzi

Ukiacha sheria hizo tatu nzito, kuna ushauri kuwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi pia iboreshwe ili kuiwianisha na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika kukomesha rushwa katika uchaguzi.

Kwa sasa, rushwa ya uchaguzi imekithiri nchini kiasi cha kuzuia uwezekano wa Watanzania wenye sifa za kuchaguliwa kwa kigezo cha kukosa pesa za kulipa na kuhonga watu wakati wa michakato ya uchaguzi.

SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Aidha, baadhi ya watu wanaona kuwa sheria hiyo ya gharama za uchaguzi imekuwa ikijikita kudhibiti rushwa ya baadhi ya vyama tu, huku mapapa ya rushwa katika vyama vikubwa yakiachwa na kulindwa yanapotembeza pesa wakati wa michakato ya uchaguzi.

Kwa kuhamishia Ofisi ya Msajili wa Vyama kuwa sehemu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, usimamizi wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi pia utaboreshwa na kudhibiti zaidi hongo, takrima na aina nyingine za rushwa iliyojificha kwenye maneno na matendo matamu.

Pamoja na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, kuna sheria nyingine mbili za kurekebisha. Kwanza, ni Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Saidizi ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa kutumika vibaya kudhibiti shughuli za mikutano ya vyama vya siasa.

Aidha, sheria hii imelalamikiwa kwa ulegevu wake katika kutoa ulinzi thabiti kwa wanasiasa wanaogombea kiasi cha kupelekea udhalilishaji, mateso na ukatili dhidi ya baadhi ya wagombea, hususani wanawake, huku Jeshi la Polisi likiwepo na kushindwa kuchukua hatua.

Maboresho katika sheria hii yataweka wazi wajibu wa polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi, huku wito ukiwa ni kuisuka vema sheria hiyo ili itenganishe kazi ya polisi na tabia ya wao kutumika kisiasa.

Pamoja nayo, kutahitajika kuhamisha baadhi ya mambo kutoka Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya kuifuta sheria hiyo kwa vile haitatumika tena baada ya uchaguzi wote kuwekwa mikononi mwa Sheria ya Uchaguzi ya Taifa kwa maboresho yanayokuja.

SOMA ZAIDI: Yanayokera Kuhusu Katiba ya 1977 na Haja Yakuwa na Katiba Mpya Sasa

Mwisho, kumekuwa na wito kuwa Sheria ya Elimu ya Taifa itazamwe upya ili kuona uwezekano wa kuipa nguvu ya kubeba vifungu vya uratibu wa elimu ya uraia nchini.

Kwa miaka mingi sasa, elimu ya uraia amekuwa kama mtoto yatima, huku sehemu yake ikiwa mikononi mwa Msajili wa Vyama na sehemu ndogo ikiwa mikononi mwa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutegemeana na maudhui ya elimu ya uraia inayotaka kutolewa.

Wapo ambao wamefikia kushauri kuwa inaweza kuhitajika kutungwa kwa sheria mpya ya elimu ya uraia ili eneo hilo muhimu la elimu liratibiwe vema na kupewa kipaumbele.

Maboresho ya Katiba

Na kwa mabadiliko yote hayo ya sheria, ni wazi kuwa kuna ibara kadha wa kadha za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitakazoguswa.

Hivyo, inashauriwa kuwa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania kwa mara ya 15 hayaepukiki ili kuhakikisha kuwa maboresho ya sheria tajwa za uchaguzi hayapelekei kukinzana kwao na Katiba ya nchi.

Tangu kuandikwa kwake mwaka 1977, Katiba ya Tanzania imefanyiwa marekebisho mara 14. Mabadiliko ya mwisho yalifanyika mwaka 2005 ambayo hadi sasa ni zaidi ya miaka 18 imepita.

Maboresho ya Katiba ndani ya kipindi kirefu hivyo ni jambo la kawaida na la muhimu sana.

SOMA ZAIDI: Nia Ovu ya Wanasiasa Yahatarisha Kuwanyima Watanzania Katiba Mpya

Swali langu kwa sasa ni je, begi la miswada ya Serikali tuliyoahidiwa inaingia bungeni kuanzia Mkutano wa Bunge unatotegemewa kuanza Oktoba 31, 2023, limebeba nini na limeacha nini?

Tusubiri, tuone. Mungu ibariki Tanzania na watu wake wote!

Deus Kibamba ni mtafiti anayefundisha utatuzi wa migogoro na uendeshaji wa mazungumzo ya amani katika Chuo cha Diplomasia. Anapatikana kupitia +255 788 758581 na dkibamba1@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts