The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Namna Bora Zaidi ya Kuwathamini Watoto Wetu ni Kusikiliza Mawazo Yao

Wataalamu wa makuzi ya watoto hueleza kuwa watoto wanaosikilizwa hujengeka na kuwa watu wazima wanaoheshimu mawazo ya wengine na kutoa mawazo yao kwa kujiamini na kujithamini.

subscribe to our newsletter!

Mara nyingi, tumekuwa tusisitiza umuhimu wa kusikiliza mawazo, matarajio na malengo ya watoto wetu. Ukiachilia mbali kwamba wazazi hudhani watoto hawawezi kuwa na mawazo chanya na yanayofikika, pia hufikiri kuwa kumsikiliza mtoto na kuyapa kipaumbele matarajio yake ni kumdekeza, au kumvimbisha kichwa na kumpa kiburi, jambo ambalo si sahihi.

Ili tuweze kuwajenga watoto wanaojiamini na kuelewa muelekeo wa maisha yao ya baadaye, lazima kwanza tuweze kuthamini matarajio yao na kuwathibitishia kadri wanavyokua kwamba vyovyote vinavyowasibu moja kwa moja vinatusibu wazazi pia na kwamba wanachokiwaza juu ya maisha yao ni jambo la maana kama tunavyowaza wazazi.

Kulea mtoto, hasa katika dunia ya sasa, kuna changamoto nyingi, na watoto wetu wanakabiliwa na mazingira hatarishi kila siku. Tunaposhindwa kuwasikiliza watoto na kuwajengea dhana kuwa siku zote wakiuliza maswali wanakua wanatusumbua, watoto watashindwa kutushirikisha hata pale wanapokuwa na shida, au wanapohitaji utatuzi na ushauri wetu wa haraka. Tujiulieze, tusipowasikiliza watoto wetu, nani atawasikiliza?

Kama mtu mzima tunapomsemesha mtu mzima mwenzetu na haonyeshi kujali wala kutilia maanani yale tunayomwambia huwa tunajisikia vibaya, na pengine tutaacha kumueleza kile tulichokusudia. 

Vivyo hivyo, watoto hujisikia vibaya pale wazazi wasipowasikiliza mara kwa mara, na baada ya muda, wanaacha kuwashirikisha wazazi hata pale wanapofanyiwa mambo mabaya na kujikuta katika mazingira hatarishi. 

SOMA ZAIDI: Baba Simama, Shiriki Kikamilifu Katika Malezi, Makuzi ya Mtoto Wako

Lakini pia hatari nyingine ya kuacha kukushirikisha ni kufanya maamuzi yasiyo sahihi pale usipopata fursa ya kusikiliza mawazo na matarajio yao awali kabla hayajaleta matokeo hasi kwenye maisha yao.

Tukiwasikiliza watoto tunawajulisha kuwa tunawathamini na tunajali mawazo yao. Wataalamu wa malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wanaeleza kuwa, wazazi wakiwasikiliza watoto hujenga mahusiano ya karibu sana na kuwafanya wawe wazi kuanzia wakiwa wadogo na hata wakiwa watu wazima. 

Pia, wazazi tunatakiwa kuyatambua matarajio ya watoto na kuyapa kipaumbele kwa kuwashauri na kuwapatia miongozo bora ili kuwawezesha kufikia malengo yao, jambo ambalo pia huongeza ukaribu na watoto katika kubadilishana mawazo na kuwa pamoja.

Kuna mifumo ya malezi ambayo haijengi, mifumo ya kuwalazimisha watoto kufanya maamuzi ambayo pengine siyo mapendeleo yao katika mambo mbalimbali, ikiwemo masomo, michezo, fani, taaluma na mengine kadha wa kadha. 

Kwa mfano, mtoto anaweza akawa anafaulu masomo ya sanaa kwa kiwango cha juu na masomo ya sayansi kwa kiwango cha chini sana, lakini mzazi anamgombeza na kusema kwa nini hufaulu hesabu na baiolojia kama wengine? Kwani waliofaulu wana vichwa viwili? 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini ni Muhimu kwa Wazazi Kuwashirikisha Watoto Kwenye Kupika?

Siku nyingine ukirudi na matokeo ya hivi utanitambua! Sipotezi ada yangu ili ufaulu Uraia na Kiswahili, nataka uwe daktari au muhandisi baadaye. Au utakuta mtoto anaadhibiwa kwa sababu anapenda kucheza mpira, kukimbia riadha, au kuchora na kuambiwa anafanya mambo ya kipuuzi na kupoteza muda pasipo kufanya jambo la msingi.

Hata kama tuna matarajio maalum kwa watoto wetu, tujaribu kuonyesha ushirikiano katika kuwasaidia, kuwaeleza mitazamo yetu juu ya maisha yao ina faida gani kwao ili waelewe na waweze kuamua kufanya mabadiliko. 

Unaweza kumuonesha mtoto ushirikiano katika yale anayoyapenda na kufanya vizuri, huku ukimshauri na kumuongoza kuweka bidii katika yale ya mtazamo wako bila kumhukumu, kumuadhibu na kumfokea ili kumsaidia asipoteze muelekeo kwenye mambo yote. 

Kumbuka pia masomo wanayofaulu watoto ndipo uwezo wao ulipo, na hakuna taaluma isiyokuwa na manufaa, bali ni namna gani tutakavyoiendeleza na kuwekeza katika taaluma husika huweza kuzaa matokeo hasi au chanya.

Kumbuka kuwa, tunaposema watoto wapewe kipaumbele juu ya matarajio yao binafsi, hatumaanishi matarajio ya mzazi juu ya mtoto ni mabaya au hayana maana. Hapana, mawazo ya mzazi yana umuhimu mkubwa pia, ila suala la msingi ni kumshirikisha mtoto katika kufanya maamuzi yanayogusa maslahi yake kama mtoto.

SOMA ZAIDI: Usafi ni Muhimu Sana Katika Makuzi ya Watoto Wetu, Tuuzingatie

Majukumu ni mengi ila tujitahidi kutenga muda wa kuongea na watoto wetu. Tuwasikilize kwa umakini pale wanapokuwa wanaongea na tutumie lugha rahisi kuwaelewesha kwa ufasaha pale wanapozungumza jambo ambalo haliko sahihi. 

Wataalamu wa makuzi ya watoto hueleza kuwa watoto wanaosikilizwa hujengeka na kuwa watu wazima wanaoheshimu mawazo ya wengine na kutoa mawazo yao kwa kujiamini na kujithamini.

Endapo tutajenga tabia ya kuwasikiliza watoto, tutawaepusha na mengi katika jamii na kuepuka yale majuto ya ‘Ningejua.’ Waswahili husema, Majuto ni mjukuu. Ila kwa nini tujute wakati tunaweza kuwaepusha Watoto wetu na mabaya mengi kwa kuwasikiliza na kuwafanya wawe rafiki zetu wa karibu? 

Ukimsikiliza mtoto, unamthamini na kumlinda pia. Tunatakiwa kujenga heshima, upendo na uaminifu baina yetu na watoto wetu na si kutengeneza woga unaozaa nidhamu ya woga.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *