The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Yaliyowapatanisha, Kuwafarakanisha Serikali, Upinzani 2022

Lipo kwa kuachiwa huru kwa Mbowe na uteuzi wa Faiza kama Mkurugenzi wa ZEC

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Yapo matukio yaliyotokea mwaka huu wa 2022 uliopo ukingoni kuisha ambayo yalizileta pamoja kambi ambazo mara nyingi hutofautiana katika mambo mengi, ile ya upinzani na ile ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Moja ya tukio kubwa lililotokea mwaka huu ni hatua ya Serikali kuyafuta mashitaka iliyokuwa imeyaelekeza dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na washitakiwa wenzake watatu, huku Mwendesha Mashitaka akisema hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Mbowe kusota korokoroni kwa siku takriban 226, akishutumiwa kupanga njama za kufanya ugaidi na utakatishaji haramu, mashitaka ambayo kiongozi huyo wa upinzani ameendelea kuyakana.

Ingawaje wafuasi wa CHADEMA na wadau wengine wa demokrasia nchini Tanzania wana maoni kwamba kesi hiyo haikupaswa kuanzishwa, hatua ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kumuachia huru Mbowe ilipongezwa na watu wengi kutoka kambi zote, ile ya Serikali na upinzani.

SOMA ZAIDI: Kuachiwa kwa Mbowe na Mapungufu ya Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania

Maridhiano ya kisiasa

Jambo jingine ambalo tunaweza kusema limewapatanisha Serikali na upinzani ni kuanzishwa kwa mchakato wa kutafuta maridhiano ya kisiasa kati ya pande hizo mbili, hatua ambayo japo imepokea ukosoaji na ukinzani wa hapa na pale, kwa ujumla imepongezwa na wadau wengi.

Michakato miwili inaendelea hivi sasa ya kutafuta maridhiano kati ya Serikali ya CCM na upinzani. 

Mchakato wa kwanza ni ule uliosimamiwa na Kikosi Kazi, kilichoteuliwa na Rais Samia, kuratibu maoni ya wadau juu ya namna bora ya kuendesha demokrasia ya vyama vingi nchini.

Kikifanya kazi chini ya uenyekiti wa Profesa Rwekaza Mukandala, Kikosi Kazi hicho kilikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia hapo Oktoba 21, 2022, ripoti ambayo imependekeza, pamoja na mambo mengine, kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani.

Mchakato mwengine wa maridhiano ni ule unaoendelea kati ya Serikali, CCM na CHADEMA, ulioasisiwa punde tu baada ya kuachiwa kwa Mbowe kutoka gerezani. 

Mchakato huo ulichochewa zaidi na hatua ya CHADEMA kukigomea Kikosi Kazi cha Samia, ikisema kwamba wajumbe wake hawana mamlaka ya kimaadili ya kuratibu maoni ya wadau kuhusu demokrasia ya vyama vingi hapa nchini.

Tayari vikao kadhaa vimefanyika kati ya Serikali, CCM na CHADEMA vyenye lengo la kutafuta maridhiano kati yao, huku Mbowe akiendelea kuamini kwamba mchakato huo utazaa matunda ambayo siyo tu yatakinufaisha chama hicho bali pia Tanzania kwa ujumla kama nchi.

Kufuatia hatua ya Rais Samia kuanzisha Kikosi Kazi cha kuratibu maoni ya wadau juu ya namna bora ya kuboresha demokrasia ya vyama vingi nchini, Rais Hussein Mwinyi wa Zanzibar naye aliasisi mchakato wake wenye lengo hilohilo kwa upande huo wa Jamhuri ya Muungano.

SOMA ZAIDI: Kikosi Kazi cha Mwinyi Chataka Mamlaka Zaidi kwa Z’bar Ndani ya Muungano

Rais Mwinyi aliunda kikosi kazi hicho chenye watu 11 hapo Oktoba 10, 2022, na kukipa kazi ya kuchambua maoni yaliyotolewa na wadau wa vyama vya siasa, asasi za kiraia pamoja wananchi kwenye mkutano uliofanyika mnamo Oktoba 6, 2022, kujadili hali ya siasa visiwani humo.

Kikiwa chini ya uenyekiti wa Dk Ali Uki, Kikosi Kazi hicho kiliwasilisha mapendekezo yake kwa Rais Mwinyi hapo Novemba 2, 2022, kikipendekeza, pamoja na mambo mengine, matokeo ya urais yapingwe mahakamani, mapendekezo ambayo Mwinyi aliahidi kuyafanyia kazi.

CCM yataka Katiba Mpya

Si hayo tu yaliyowavuta CCM na upinzani na kuwaweka karibu bali hata hatua ya chama hicho tawala kujitokeza hadharani na kuunga mkono madai ya Katiba Mpya ilisaidia sana kupunguza mgawanyiko wa kisiasa nchini Tanzania kwa mwaka 2022.

Akiwasilisha kwa umma wa Watanzania maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM iliyoketi Juni 22, 2022, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka alisema chama hicho kinaona mantiki kwenye madai ya wananchi ya Katiba Mpya. 

“Chama cha Mapinduzi tunasisitiza umuhimu wa uwepo wa Katiba Mpya,” Shaka aliwaambia waandishi wa habari, akiwa jijini Dodoma. “[Hiyo ni] kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa malsahi mapana ya taifa na maendeleo kwa ujumla.”

SOMA ZAIDI: Hatua Tano Muhimu Kufikia Upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania

Msimamo huu wa CCM ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani kama CHADEMA na ACT-Wazalendo, vyama ambavyo vilikuwa vimeibeba ajenda hii kwa muda mrefu vikihitaji Watanzania wapate Katiba Mpya kwa maslahi yao. 

Hivyo, kitendo cha CCM kutoka na kukubali dai hili kuliwaunganisha pamoja kwani ilionekana kuwa hoja la Katiba Mpya ni takwa ambao kila upande linauhitaji nalo. 

Pengine mambo yaliyowapatanisha wapinzani na Serikali yangekuwa mengi zaidi endapo kama kusingekuwa na mambo yaliyowafarakanisha. 

Hii ni kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa kuna mambo yamefanywa na Serikali/CCM na kuungwa mkono na upinzani, kuna mambo mengine yametokea ambayo wapinzani hawafurahishwi nayo.

Katazo la mikutano ya hadhara

Moja kati ya jambo ambalo limefanya upinzani na Serikali kutokuelewana ni hatua ya Serikali kukataa kubatilisha agizo la kufanya mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani lililowekwa na Hayati Rais John Magufuli.

Serikali imeendelea kuhalalisha katazo hilo ambalo wapinzani na wadau wa demokrasia wameliita “haramu” kwa kusema kwamba kunahitajika “kanuni”zitakazokuwa zinaratibu mikutano hiyo, pendekezo ambalo wapinzani wamelikataa, wakisema Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa, 2019, vyote vinaruhusu mikutano hiyo.

Mkwaruzano umekuwa mkali zaidi kutokana na hatua ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kutaka kusimamia utekelezwaji wa marufuku hiyo kwa kuvizuia vyama vya upinzani, hususan CHADEMA na ACT-Wazalendo, kufanya mikutano ya hadhara.

SOMA ZAIDI: Lini Polisi Iliahidi Hadharani Kutekeleza Ushauri Kutoka Chama cha Upinzani?

Mfano wa hivi karibuni zaidi ni hatua ya Jeshi la Polisi kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara kuzuia vyama vya CHADEMA na ACT-Wazalendo kufanya mikutano ya hadhara kwenye mikoa hiyo husika, hatua iliyowakasirisha wafuasi wa vyama hivyo.

Jambo jengine linawahusu wabunge 19 wa Viti Maalum, wakiongozwa na Halima Mdee, ambao CHADEMA imekuwa ikilalamika kwamba wamekuwa wakikingiwa kifua na Bunge na Serikali, licha ya ukweli kuwa wazi kwamba wabunge hao hawapo kihalali ndani ya mhimili huo wa kutunga sheria.

CHADEMA imekuwa ikitaka wabunge hao wafukuzwe bungeni, wakisema taratibu hazikufuatwa katika uteuzi wao kwani Katibu Mkuu wa CHADEMA hakusaini form za uteuzi wao kama taratibu zinavyotaka. Bunge na Serikali, ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hazionekani zikifanyia kazi malalamiko hayo.

Sakata la wabunge hao kwa sasa lipo Mahakama Kuu, Masjala Kuu, baada ya wabunge hao kufungua shauri huko wakipinga uamuzi wa CHADEMA kuwafukuza uanachama.

Uteuzi wa Faina ZEC

Hatua nyengine iliyowafarakanisha upinzani na Serikali, hususan kwa upande wa Zanzibar, ni uamuzi wa Rais Mwinyi kumteua Thabit Idarous Faina kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), hatua iliyokemewa vikali na chama cha ACT-Wazalendo.

Chama hicho ambacho ni mshirika kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK) kimeukosoa uteuzi wa Faina kwa kudai kwamba ni katika usimamizi wake kama Mkurugenzi wa ZEC kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 ndipo ukiukwaji mkubwa wa misingi za uchaguzi wa huru na haki ulipofanyika.

ACT-Wazalendo iliyakataa matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi Mwinyi wa CCM, ikisema kwamba uchaguzi ulijawa na kasoro mbalimbali zilizoufanya ukose hadhi ya kuitwa uchaguzi wa huru na haki, madai ambayo yameungwa mkono na baadhi ya mashirika ya haki za binadamu.

Serikali ya Mwinyi mpaka sasa haijajitokeza hadharani kutetea uamuzi wake huo ambao ACT-Wazalendo imesema unaenda kinyume na dhamira aliyoionesha Rais Mwinyi kwenye kutafuta maridhiano ya kisiasa na kujenga utengamano katika jamii ya Zanzibar.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts