The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CCM Inatarajia Kujifunza Nini Hasa Kutoka BJP ya India?

Uhusiano baina ya vyama vya CCM na BJP ni jambo linalohitaji tafakuri na mawazo ya kina.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Februari 1, 2023, The Chanzo iliripoti kwamba ujumbe wa watu watano kutoka chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi (CCM), ulitembelea India ambako ulikutana na viongozi wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata Party (BJP). 

Msafara huo ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara) Abdulrahman Kinana ulialikwa na chama hicho cha BJP kwa madhumuni ya kuanzisha “uhusiano wa kirafiki” baina ya vyama hivyo viwili.

Tunaambiwa Mheshimiwa Kinana aliishukuru sana BJP kwa kuandaa ziara hiyo na akasema kwamba CCM “ina mengi ya kujifunza kutoka BJP, hasa jinsi ya kuwasiliana na kuwatumikia wananchi,” kwa mujibu ya ripoti hiyo ya The Chanzo.

BJP yenyewe ilisema mualiko huo ulibuniwa na chama hicho ili kuutangazia ulimwengu  kuhusu maono na sera zake pamoja na utamaduni wake wa kisiasa. Tunaambiwa CCM na BJP zilikubaliana kuendeleza mahusiano baina yao na nchi zao.

Baada ya kusoma habari ile, hata hivyo, nilijiuliza hivi CCM inategemea kujifunza nini hasa kutoka BJP? Ni maono yepi, utamaduni upi na sera zipi ambazo CCM, kama chama, kinategemea kujifunza kutoka BJP? 

Ni kweli kuwa nchi yetu imekuwa na uhusiano wa karibu sana na India tangu enzi za Waziri Mkuu wake wa kwanza Jawaharlal Nehru na Rais wetu wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere. 

Enzi hizo viongozi hawa na wengineo kama Kwame Nkrumah wa Ghana na Gamal Abdel Nasser wa Misri walivuma kutokana na mshikamano wa nchi zisizoegemea upande wa NATO wala WARSAW, yaani siyo Magharibi wala Mashariki.

Lakini leo hii India siyo tena ile ya Nehru wala ya Mahatma Gandhi. Chama tawala cha BJP leo kimewageuzia kibao viongozi hao waanzilishi. Chama hicho kimegeuka na kuwa siyo tu chama cha mrengo wa kulia bali kimekuwa na maono ya kikabila na kidini.  

Chimbuko la BJP

Ili kuelewa undani wa suala hili kiundani ni vizuri tukaangalia chimbuko la BJP na jinsi chama hicho kinavyotawala India ya leo. Ni vizuri kuelewa maono, utamaduni na sera za BJP ambayo CCM inataka kujifunza kutoka kwake.

BJP ilianza kutawala India mnamo mwaka 2014 baada ya kukiangusha chama cha Congress, au Indian National Congress, kama chama hicho kinavyojulikana kwa kimombo. 

Asili ya BJP ni muungano wa Wahindu uitwao Rashtriya Swayamsevak Sangh (RSS) uliozaliwa mnamo mwaka 1925 ukiongozwa na itikadi ya Hindutva. Itikadi hii ya kidini inaamini kuwa Wahindu ni wazawa na wenyeji wa taifa la India, ikiwatenga Waislamu, Wakristo na wengineo.

SOMA ZAIDI: Watanzania Kili Paul, Neema Wapongezwa na Waziri Mkuu wa India kwa Uwezo Wao wa Kuimba Nyimbo za Kihindi

Kwa hiyo, lengo la RSS ni kuunda taifa la Wahindu, au Hindu Rashtra, bila ya kujali kuwa kwa muda wa karne nyingi India imekuwa inakaliwa na watu wenye dini, kabila na tamaduni tofauti. Chini ya sera hii, RSS imekuwa tayari hata kutumia nguvu.

Ndipo kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, RSS ilikuwa na uhusiano wa karibu na mafashisti wa Ulaya waliokuwa wakitawala Ujerumani na Italy, yaani Adolf Hitler na Benito Mussolini.

Mnamo mwaka 1931, kiongozi mkuu wa RSS, Balakrishna Shivram Moonje, alifanya ziara ya Italy ambako alikutana na Mussolini na kuona jinsi dikteta huyo anavyotoa mafunzo ya kijeshi kwa wafuasi wake. 

Moonje aliporudi India akaanzisha chuo kama hicho ili kuwatayarisha vijana wa RSS kupigania Hindutva. Matawi yakafunguliwa nchini India na vijana wa Kihindu wanaokadiriwa kufikia 600,000 wakapatiwa mafunzo. Leo hii wanaendesha mafunzo kwa mamilioni ya vijana wa Kihindu.

Mmoja wa vijana waliopitia mafunzo hayo ni Narendra Modi ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa jimbo la Gujarat kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2014 na Waziri Mkuu wa India kuanzia 2014 hadi leo.

RSS ina jumuiya zake kwa ajili ya vijana, wanawake, wanafunzi, wakulima, wafanyakazi, wasomi na kadhalika. Hata BJP yenyewe ni jumuiya ya RSS. 

Jumuiya hizi, kwa pamoja, zinajiita familia ya RSS, au Sangh Parivar, ambayo ina matawi siyo tu India bali hata Uingereza, Marekani, Australia, Kenya, Liberia, Nepal na kwengineko duniani. 

SOMA ZAIDI: Siasa za CCM Zilivyoibua Msisimko 2022

Mnamo Septemba 2018, Sangh Parivar iliendesha semina ya kimataifa jijini Chicago, Marekani na wajumbe zaidi ya 2,000 walihudhuria kutoka nchi 60. 

Baada ya maelezo hayo hapo juu, ni vizuri pia tukaangalia jinsi BJP inavyotekeleza sera na maono ya RSS nchini India. Tutaangalia mifano michache tu, kwani kuna mengi yanayofanyika nchini India.

Vita ya Wahindu dhidi ya Waislamu

Mnamo Disemba 6, 1992, kwa mfano, Msikiti wa Kiislamu uitwao Babri Masjid katika jimbo la Uttar Pradesh ulibomolewa na wanaharakati wa RSS, kinyume na uamuzi wa Mahakama Kuu ya India. 

Wahindu walidai kuwa Msikiti huo ilibidi uvunjwe na badala yake lijengwe hekalu la mungu wao Rama. BJP iliunga mkono madai hayo na msikiti huo ukabomolewa kwa nguvu za watu wapatao 150, 000. Polisi hawakuingilia kati.

Baada ya hapo, machafuko yalienea kote nchini India na inakisiwa watu 2,000 walipoteza maisha. 

Uchunguzi wa kimahakama ulifanyika na watu 32 walifunguliwa mashtaka. Kesi ikaendelea hadi Septemba 2020 na hatimaye Mahakama ikawaachia huru kwa sababu ubomoaji huo “haukuongozwa na mtu yeyote.”

Baada ya kubomolewa kwa Msikiti wa Babri, machafuko makubwa yaliibuka katika jimbo la Gujarat mnamo 2002, wakati huo Modi akiwa Waziri Kiongozi wa jimbo hilo. 

Mengi yamesemwa lakini hivi majuzi BBC ilitoa filamu inayoangazia mchango wa Modi kwenye machafuko hayo iliyopewa jina la India: The Modi Question.

SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Wanasiasa Vijana wa CCM Kuhusu Rais Magufuli

Kwenye filamu hiyo ambayo Serikali imeizuia isipatikane nchini India, BBC inadai kwamba Modi alipaswa azuie machafuko ya Gujarat lakini hakufanya hivyo na polisi nao wakakaa kimya. 

Katika machafuko hayo, kundi la Wahindu 11 walimbaka mwanamke wa Kiislamu wa miaka 19 aitwae Bilkis Banu

Wakawaua wanafamilia wake 14, akiwemo kitoto kichanga cha siku moja. Binti wa Bilkis wa miaka mitatu walimuua kwa kumpiga mawe kichwani. Bilkis alizimia na wakamuachia, wakifikiri amekufa.

Wauaji hao 11 walihukumiwa vifungo vya maisha kwa ubakaji na mauaji. Lakini mnamo Agosti 15, 2022, waliachiliwa huru na wakatoka gerezani kwa shamra shamra. Wafuasi wa BJP waliwalaki kwa mashada ya maua. 

Hii ni baada ya Serikali ya Modi kutoa “msamaha maalum” usiotambulika kisheria.

Waendesha mashtaka na Mahakama walisema ni uvunjifu wa sheria kuwaachia. Pia, raia zaidi ya 6,000, wakiwemo wanaharakati na wasomi waliandika risala ya pamoja wakitaka Mahakama ya Kuu kabisa, au Supreme Court, kuingilia kati na kufuta “msamaha” huo. Hata hivyo, hakuna hatua iliyochukuliwa mpaka sasa.

Mnamo Disemba 2019, Serikali ya BJP ilifanya mabadilio katika Sheria ya Uraia (CAA) ambayo imekwenda kinyume na Katiba ya nchi. 

Sheria hiyo mpya inasema wakimbizi na wahamiaji kutoka nchi za jirani wasio Waislamu watasajiliwa na kupewa uraia lakini Waislamu hawatasajiliwa.

Yaani, CAA inawabagua Waislamu ingawa Katiba ya India inasema wazi katika utangulizi wake kuwa India ni nchi ya kisekula, yaani haitambagua raia wake yeyote kwa misingi ya dini yake.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wengineo wamesema CAA ni sheria ya kibaguzi kwa sababu mamilioni ya Waislamu watakosa uraia na wataishia kuwekwa kambini au kufukuzwa nchini.

Sheria nyingine inayofanana na CAA ni ile ya NRC ambayo inakusudia kuanzisha uhakiki wa uraia. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kila mtu anatakiwa ajiorodheshe kwa kuonyesha cheti cha kuzaliwa. 

SOMA ZAIDI: Miaka 45 ya CCM: Mapungufu Makuu ya Chama Hicho Tawala Tanzania

Sasa kuna Waislamu wengi waliohamia jimbo la Assam kutoka jimbo la Bengal tangu enzi za ukoloni wakati majimbo hayo yalipokuwa sehemu ya India. 

Matokeo ya NRC, kwa hiyo, ni kuwa Waislamu takriban milioni mbili wenye asili ya Bengal wanaoishi katika jimbo la Assam wamenyimwa uraia na kwa hivyo wanakosa haki za kiraia.

Mnamo Disemba 2021 pia, uliitishwa mkutano ulioitwa Dharma Sansad, au Bunge la Kihindu, katika mji wa Haridwar. Mada yake kuu ilikuwa “Mustakabali wa Uhindu katika India yenye Uislamu: Matatizo na Suluhisho.”

Wazungumzaji walitoa mfano wa nchi ya Myanmar wakisema ili kuulinda Uhindu ni lazima Wahindu watumie silaha dhidi ya Waislamu. 

Katibu Mkuu wa jumuiya ya Wahindu, au Hindu Mahasabha, alinukuliwa akitamka: “Tukitaka kuwamaliza Waislamu, ni lazima tuwe tayari kuwaua.”

Wakiristo hawako salama

Hali siyo mbaya kwa Waislamu waliopo India tu. Wakristo wapatao milioni 28 walio India nao pia hawako salama. 

Asasi ya Kikristo iitwayo United Christian Forum (UCF), inayo waunganisha wanajamii hao, imekuwa ikitoa wito kwa viongozi wa India waingilie kati na kuzuia mashambilizi dhidi ya Wakiristo. 

Kwenye tamko lao la Juni 13, 2022, UCF ilisema kwamba mashambulizi dhidi ya wanachama yamekuwa yakiongezeka nchini India kuanzia 2014. 

Walitoa mfano mmoja wa mwanamke Mkristo mwenye umri wa miaka 65 na mwanawe walioitwa na wazee wa kijiji na wakatakiwa waukane Ukristo na kujiunga na Uhindu. Walipokataa kufanya hivyo, wakapigwa mpaka ikabidi wakimbizwe hospitali.

Halafu kuna mchungaji wa Kiprotestanti aliyekuwa anaongoza ibada kanisani. Wahuni wakaingia, wakamburuza nje na kumpiga.  Polisi, badala ya kuwakamata washambuliaji, wakamkamata mchungaji na kumfungulia mashtaka! 

John Dayal, mwanahabari wa Kikatoliki na mwanaharakati wa haki za binadamu amesema: “Waislamu na Wakristo huwa wanashambuliwa na Wahindu wenye siasa kali kote nchini India, na polisi nao wako upande wa Wahindu.”

Tafakuri inahitajika

Huu ndiyo utawala wa BJP, chama kinachotaka kuifundisha CCM jinsi ya “kuwasiliana na wananchi.” 

Tayari wanaeneza ulimwenguni maono yao na sera yao ya Hindutva. Huko Uingereza na Marekani jamii za Kihindu na Kislamu zimenyukana kutokana na jitihada za BJP na RSS kueneza huko sera yao.

SOMA ZAIDI: Jenerali Ulimwengu: CCM Imepoteza Muelekeo

Hii ndiyo BJP inayotawala India wakati Serikali yake haina hata Muislamu mmoja katika Baraza lake la Mawaziri. Kati ya wabunge wake 400, hakuna Muislamu hata mmoja.

Hii ndiyo BJP ambayo Serikali zake majimboni zimetunga sheria za kukataza ndoa baina ya Mwislamu na Mhindu. Kuna mifano ya polisi kuingilia kati na wanandoa wasiotii “sheria” hii hupigwa hadharani.

Tukija kwenye vyombo vya habari, tunaona kuwa BJP na RSS wanadhibiti runinga, magazeti na blogu takriban 400 ili kueneza propaganda zao. Si ajabu kuona kurasa za Twitter au Facebook zikiwahamasisha Wahindu “kuwamaliza” Waislamu. 

Kwa mujibu wa UNESCO, wanahabari 30 nchini India wameuliwa kati ya 2015 na 2022. 

Si ajabu asasi ya kimataifa iitwayo Reporters Without Borders (RSF), katika utafiti wake kuhusu uhuru wa habari, imeiweka India katika nafasi ya 150 kati ya nchi 180 ulimwenguni. Kabla ya hapo, India ilikuwa ya 142 sasa imeporomoka hadi 150.

 Asasi nyingine ya kimataifa iitwayo Genocide Watch nayo imetoa ripoti kuhusu India, ikitahadharisha kuwa yanayofanyika nchini humo yanaashiria mauaji ya kimbari. 

Genocide Watch inasema kwamba chuki dhidi ya Waislamu si jambo la kupuuzwa nchini India, kwani sasa imegeuka na kuwa itikadi inayoungwa mkono na vyombo vya dola.

Ni katika mazingira haya ndipo tunapaswa tujiulize, CCM, na Tanzania kwa ujumla, inategemea kujifunza nini kutoka BJP ya nchini India? 

Uhusiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umekuwepo kwa miaka mingi. Hata hivyo, uhusiano baina ya vyama vya CCM na BJP ni jambo linalohitaji tafakuri na mawazo ya kina!

Nizar Visram ni mchambuzi wa siku nyingi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia +255 673 004 559 au nizar1941@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *