Dar es Salaam. Ni majira ya saa nane za mchana na chini ya jua linalowaka kwa hasira unaweza kuona watu wakiingia na kutoka katika Soko la Mwananyamala, moja kati ya masoko makubwa yaliyopo katika wilaya ya Kinondoni jijini hapa, huku mizunguko yao ikisindikizwa na harufu mchanganyiko wa bidhaa mbalimbali zinazopatikana sokoni humo.
Miongoni mwa watu wengi wanaofanya shughuli zao sokoni humu yumo Asma Rajab ambaye kazi yake ya mamalishe huhakikisha wafanyabiashara hapa – angalau wale wanaomudu – hawashindi na njaa. Lakini Asma, 30, hayuko peke yake sokoni hapa. Yuko na mtoto wake wa miaka minne aitwaye Khairat Hussein.
Kwenye mazungumzo yake na The Chanzo, dada huyo wa makamo ambaye siyo mrefu wala mfupi, alisema kwamba amelazimika kuja na mtoto wake sokoni hapo kwani hana mtu wa kumuachia nyumbani na yeye hawezi kubaki nyumbani kwani maisha ni magumu.
“Inakulazimu kuja naye kutokana na mazingira ya nyumbani, [kwamba] huna mtu wa kumuachia,” anasema Asma, mama wa watoto wawili. “Mtoto mwenyewe hajafikisha umri wa kwenda shule, au saa nyingine kashafikisha, lakini kutokana na hali ya kimaisha hela huna.”
Asma, hata hivyo, siyo mwanamke pekee aliyelazimika kulea mtoto wake katika eneo la sokoni.
Katika uchunguzi kwenye masoko mbalimbali jijini Dar es Salaam, The Chanzo imebaini uwepo wa wanawake kadhaa wanaolazimishwa na hali duni za kimaisha kulea watoto wao masokoni.
Mosi Hamisi anauza matunda katika Soko la Bakhresa, Manzese jijini hapa ambaye amesema kwamba analazimika kuja na mtoto wake mwenye umri wa miaka minne kwa sababu hali yake ya kiuchumi haimruhusu kubaki nyumbani.
“Kuwa naye sokoni siyo kwamba napenda, lakini nalazimika kwa sababu nyumbani sina mtu wa kubaki na mtoto na inanibidi mimi nitoke kwenda kutafuta kama mama,” Mosi, 38, alisema. “Sina mtu wa kunisaidia mahitaji endelevu kwa sababu uchumi unahitaji msaidiane baba na mama.”
“Kukaa myumbani na mtoto kwa muda mrefu kwa mazingira tunayoyaishi sasa hivi haiwezekani,” anaeleza mfanyabiashara mwingine sokoni hapo Najma Siraji, 24, anayefanya biashara ya ndizi.
“Kwa hiyo, mtu huwezi kukaa na mtoto miezi sita, kumi au mwaka,” anaongeza. “Kwa hiyo, ile hali ya changamoto ya maisha inakufanya kutoka nyumbani kuja kutafuta Sh100 [au] 200.”
Mazingira yasiyo rafiki
Hata hivyo, akina mama hawa wamelalamikia hali ya kukosekana kwa miundombinu rafiki masokoni ambayo ingewawezesha kufanya biashara zao na kulea watoto wao kwa pamoja, hali waliyosema inawaathiri sana.
Uchunguzi uliofanywa na The Chanzo ulibaini kwamba kwenye masoko yote matatu iliyoyatembelea – Mwananyamala, Tandale na Manzese-Bakhresa – hakukua na sehemu iliyotengwa kwa ajili ya shughuli kama vile kunyonyeshea au kulaza watoto.
SOMA ZAIDI: Mfumuko wa Bei Unavyohatarisha Biashara za Wanawake Masokoni
The Chanzo pia iliona akina mama wanalazimika kutumia vyoo vya wakubwa kupeleka watoto wao kwa ajili ya haja mbalimbali, hali ambayo wazazi wenyewe wamekiri kwamba inatishia afya za watoto wao.
Watoto pia walionekana wakiwa wamelazwa kwenye mabanda ya biashara ya wazazi wao ambapo siyo tu hali ya usafi wa kimazingira inaonekana kuhatarisha afya zao bali pia kelele kubwa zilizokuwa zinasikika ziliwafanya watoto hao washindwe kupumzika vizuri.
Najma Siraji ni mama wa watoto wawili ambaye analazimika kumlea mtoto wake mwenye umri wa miezi mitatu katika soko la Manzese-Bakhresa.
Kwenye mazungumzo na The Chanzo, Najma alikiri soko hilo kukosa miundombinu rafiki kwa ajili ya malezi ya mtoto wake.
“Changamoto ambayo nakutana nayo ni kwamba mvua ikinyesha siwezi kubaki hapa sokoni na kuendelea na biashara zangu,” Najma alisema. “Nikiona tu dalili za mvua zimeanza lazima nikimbie nyumbani kwa ajili ya mtoto.”
Kwa upande wake, Asma, mamantilie katika Soko la Mwananyamala, anasema changamoto kubwa ni kwamba hakuna sehemu maalum iliyotengwa kwa ajili ya watoto kucheza au kulala sokoni hapo.
“Mtoto kama huyu ameshazoea kujiachia, muda wote anacheza tu na ukiangalia hapa sehemu ya kupika, moto, majiko, vyakula na wateja inakuwa ni mtihani,” alilamika Asma.
SOMA ZAIDI: Sekta Isiyo Rasmi Yadaiwa Kutokuwa Rafiki Kwa Wanawake wa Kitanzania
“Kuna muda anahitaji kupumzika [au] kulala, unamlaza wapi? Hamna sehemu ya kumlaza. Kuna muda anasikia haja, anataka kujisaidia, anaweza akaona hata aibu ya kuongea, ukashangaa kashajisaidia. Inakuwa ni changamoto.
“Kuna muda inakulazimu umpeleke kwenye choo cha watu wazima. Na unajua kabisa ni choo cha soko, kwa hiyo hata mtu ajitahidi vipi, mtu anayesimamia choo kufanya usafi hawezi kufanya kila saa.
“Kwa upande wa kumuandalia chakula, mazingira ya kazi na mazingira ya nyumbani ni tofauti. Ukiwa mazingira ya nyumbani unaweza mtu ukamuandalia kila kitu, mazingira yakawa vizuri. Lakini unapokuwa kazini inakuwa ni changamoto vitu hivyo kuviandaa,” alisema Asma.
Changamoto hizi wanawake hawa huziibua kwenye jumuiya zao masokoni kitu kilichothibitishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Soko la Mwananyamala Paulina Reuben aliyekiri kwamba miundombinu sokoni hapo siyo rafiki kwa malezi ya watoto.
“Kwanza mazingira ya sokoni ya hapa naona si mazuri lakini kutokana na shida walizokuwa nazo wanakuja nao tu [watoto wao], wafanyaje?” anasema Paulina kwenye mahojiano na The Chanzo. “Mimi nadhani kuna haja ya kuiboresha miundombinu ya soko ili kukidhi mahitaji ya akina mama hawa.”
Maboresho hayo, hata hivyo, yamekuwa magumu kufanyika, hususan ukizingatia ukweli kwamba viongozi wengi wa masoko ni wanaume ambao badala ya kuchukua jitihada za kuboresha miundombinu wamekuwa wakiona njia nzuri ni kuwazuia akina mama hao kuja masokoni.
Said Athumani ni Makamu Mwenyekiti wa Soko la Mwananyamala aliyeiambia The Chanzo kwamba wao kama uongozi walijaribu kuwazuia wanawake hao kujihusisha na malezi sokoni hapo lakini juhudi hizo ziligonga mwamba.
SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni
“Tulijaribu kuwazuia wanawake wenye watoto kuja kufanya biashara masokoni lakini ilishindikana,” alisema Athumani ambaye alishindwa kueleza mkakati wa kufanyia kazi malalamiko ya akina mama hao. “Wakina mama waliandamana na vilevile walitulaani, walitulaani sana sana.”
Alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo ya wanawake, Katibu Msaidizi wa Soko la Tandale Michael Raphael alisema: “Suala la akina mama kuja na watoto kwenye maeneo haya ya biashara kwa hapa sokoni kwa kweli na sisi hatulifurahii. Lakini kila tulipojaribu kuwauliza wanashindwa hawana watu wa kuwaachia hasa ukizingatia vipato vyao ni vya chini.”
Watoto hatarini
The Chanzo iliwauliza wataalamu wa masuala ya malezi na afya za watoto kama kuna hatari zozote zinazoweza kuwapata watoto wanaolelewa katika mazingira ya masokoni ambapo walibainisha kwamba athari zipo na ni nyingi.
Kiiya Kiiya ni Mkurugenzi Mtendaji wa C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalohusika na ulinzi na malezi ya mtoto, ambaye alisema kwamba soko haliwezi kuwa sehemu nzuri ya kulelea na kukuzia mtoto.
“Malezi ya watoto yanahitaji mazingira rafiki ya watoto kukua na kujifunza, watoto wanahitaji kujifunza kwa kushika, kuuliza maswali na kucheza. Na sokoni hakuna kabisa mazingira hayo,” alifafanua Kiiya.
Evans Rwamuhuru ni Meneja wa Programu kutoka Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) aliiambia The Chanzo kwamba watoto wanaolelewa katika mazingira ya soko wapo katika hatari kubwa ya kukosa haki zao za msingi, ikiwemo haki ya ulinzi.
“Haki ya ulinzi inakuwa ni ngumu kwa sababu yupo kwenye mazingira ambayo si rahisi kuyadhibiti,” anabainisha Rwamuhuru. “Kwa hiyo, unakuta huyu mtoto anakuwa kwenye hatari ya kukosa ile haki yake ya kulindwa. Kwa hiyo, unakuta watoto hao wanakuwa kwenye hatari ya kupitia ajira za utotoni.”
SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?
Dk Pius Muzzazzi ni daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambaye amebainisha kwamba mazingira ya sokoni si mazingira salama kwa ustawi wa afya ya mtoto, akitaja hatari kadhaa za kiafya zinazoweza kumkabili katika mazingira hayo.
Hatari hizi ni pamoja na kupata magonjwa kama mzio, homa ya mapafu na magonjwa mengine mengi ya mlipuko, kama vile kifua kikuu na mengineyo.
“Lakini pia kuna magonjwa ya afya ya akili,” Dk Muzzazzi, ambaye pia kwa sasa anahudumu kama Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), alisema.
“Unajua yale ni mazingira ambayo yana kelele, watu wanaongea maneno yoyote yale wanayoyataka, saa nyingine kuna fujo zinatokea, kwa hiyo huyu mtoto anakuwa akiona mazingira hayo anakosa muda wa kucheza na watoto wenzake, kukaa nyumbani.
“Kwa hiyo, hii inawaathiri sana kisaikolojia na hivyo kuwapelekea kupata tunasema stress, au msongo wa mawazo,” alifafanua mtaalamu huyo.
Sehemu tu ya tatizo kubwa
Jane Magigita ni Mkurugenzi Mtendaji wa Equality for Growth, shirika lisilo la kiserikali ambalo limekuwa likifanya kazi kwa miaka mingi na wanawake wanaofanya shughuli zao za kujipatia kipato masokoni.
Kwenye mahojiano na The Chanzo, Magigita alisema kwamba kukosekana kwa maeneo ya kulelea watoto masokoni kunadhihirisha ukweli kwamba masoko mengi nchini hayakujengwa, na wala hayaendeshwi, kwa kuzingatia ujinsia.
SOMA ZAIDI: Fatma Taufiq: Wanawake Tunahitaji Ukombozi wa Kiuchumi
Magigita alizikosoa sheria ndogo, kanuni na miongozo ya uendeshaji masoko kujikita zaidi kwenye ukusanyaji wa ushuru badala ya kuhakikisha kwamba wanawake wanakuwa na nafasi sawa kwenye masoko ya kufanya biashara zao.
“Kama taasisi ambayo tunashughulika kwenye hilo eneo, tunatoa wito kwa halmashauri husika katika miji na majiji nchini, kuona umuhimu wa kujenga vituo vya kulelea watoto, hasa kwenye maeneo ya wazi ya biashara,” Magigita alisema.
“Hali ilivyo sasa imeonekana kwamba wanawake wana mzigo mkubwa wa ulezi na inawapunguzia nguvu wanawake kuwa wazalishaji katika miji,” aliongeza.
Akizungumza na The Chanzo, Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Ubungo Zainabu Masilamba amekiri kwamba masokoni siyo sehemu sahihi ya kulelea watoto, akiwashauri akina mama wapeleke watoto wao kwenye vituo vya kulelea watoto vya gharama nafuu.
“Kama halmashauri, bado hatuna muongozo unaoruhusu kuweka vituo vya kulelea watoto ndani ya soko,” Masilamba alisema. “Kwa hiyo, kwa sasa, njia rahisi ni kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kulelea watoto vilivyo karibu na masoko husika.”
Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com.