Ufafanuzi Mdogo Kuhusu Kikokotoo Kipya cha Asilimia 33

Siyo kweli kwamba kikokotoo hicho kinapunguza mafao kwa mnufaika.
Thomas Ndipo Mwakibuja14 March 202344 min

Kumekuwepo na hofu kubwa miongoni mwa wafanyakazi tangu kikokotoo kipya katika mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kianze kutumika hapo Julai 1, 2022. Kikotoo hicho ni matokeo ya makubaliano ya pamoja kati ya Serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Moja kati ya malalamiko makubwa kuhusiana na kikokotoo hicho ni madai kwamba Serikali imeamua kupunguza malipo kwa wastaafu, huku wakosoaji wakitaja kushuka kwa malipo ya kiinua mgongo kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 33 kama ushahidi wa malalamiko yao hayo.

Licha ya kikokotoo hicho kufanya kazi kwa takriban mwaka mmoja sasa, bado malalamiko yameendelea kuwepo miongoni mwa wafanyakazi na wastaafu, hali iliyoisukuma TUCTA kujitokeza hadharani hivi karibuni na kuitaka Serikali itoe elimu zaidi kuhusiana na suala hilo nyeti.

Akizungumza mjini Morogoro hapo Machi 9, 2023, Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya alisema kwamba moja kati ya makubaliano yao na Serikali ni kwamba Serikali ihakikishe inatoa elimu ya kutosha kwa wafanyakazi ili waelewe kikokotoo hiki kipya ni nini.

Mimi siyo mtu wa Serikali lakini nikiwa kama mtaalam wa masuala ya hifadhi ya jamii nimehisi kuwiwa kutoa mchango wangu ikiwa ni sehemu ya kusaidia juhudi hizi za kuelimisha umma kuhusiana na jambo hili muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi, wastaafu, na taifa kwa ujumla.

Usalama wa kifedha

Ni muhimu kwanza tukafahamu kwamba mfumo wa hifadhi ya jamii, ambao hufadhiliwa na wanachama wa mfuko husika kwa njia ya michango ya kila mwezi, hulenga kuhakikisha kuwa wanachama wanapata huduma za kijamii kama vile afya, elimu, pensheni, na huduma nyingine za kijamii.

Mbali na malengo hayo, hifadhi ya jamii pia huhakikisha usalama wa kifedha kwa wanachama wake pindi mwanachama apatapo janga lolote litakalosababisha yeye kupoteza kipato, ikiwemo kustaafu, ulemavu, kufiwa, uzazi, na kukosa ajira.

Kwenye fao la pensheni, mfuko hutumia zana maalum kuhesabu kiasi cha pensheni ambacho mwanachama atapokea baada ya kustaafu. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Inachukua Muda Mwingi Kwa Watu Kupata Mafao Yao Kutoka NSSF, PSSSF?

Zana hii huzingatia mambo mbalimbali kama vile muda wa kuchangia, kiwango cha michango ya kila mwezi, kiwango cha riba kinachopatikana, na muda wa malipo ya pensheni. 

Kwa kutumia taarifa hizi, zana hii inaweza kutoa makadirio ya kiasi cha pensheni ambacho mwanachama atapokea baada ya kustaafu. Hii zana ndiyo huitwa kikokotoo.

Ulipaji

Kwenye malipo ya pensheni, mnufaika hulipwa kwa awamu mbili: awamu ya kwanza inaitwa mkupuo, au kiinua mgongo, na awamu ya pili ndiyo wengi tunaifahamu inaitwa pensheni ya mwezi ambapo mnufaika hupokea malipo ya pensheni kila mwezi.

Nataka niseme hapa kwamba siyo kweli kwamba kiwango cha pensheni kimepanda au kimeshuka kwa mnufaika tangu Serikali itangaze matumizi ya kikotoo kipya hapo Julai 2022. 

Kilichobadilika baada ya kutangazwa kwa kikotoo hicho ni njia za kukokotoa haya malipo katika awamu zote mbili za malipo, yaani kiinua mgongo na malipo ya kila mwezi.

Zamani kabla ya hiki kikokotoo kipya cha asilimia 33, mnufaika wa pensheni alikuwa analipwa asilimia 25 katika malipo ya mkupuo, yaani malipo ya awamu ya kwanza, kwa kutumia kanuni ya CP = (1/580*N*APE) *12.5*25%) na malipo ya awamu ya pili akilipwa asilimia 75 kwa kutumia kanuni ya MC = (1/580 * N*APE)*75%*1/12).

Kilichobadilika ni kwamba sasa hivi mnufaika wa pensheni atakuwa analipwa kiinua mgongo, yaani malipo ya awali, asilimia 33 kutoka asilimia 25 na malipo ya kila mwezi atakuwa analipwa asilimia 67 kutoka asilimia 75.

Kwa hiyo, tunaweza kuona hapa kwamba kilichoongezeka ni malipo ya awali huku malipo ya kila mwezi yakipungua. Lakini malipo kwa ujumla yako vilevile, yaani asilimia 100 (33 + 67 = 100) kama inavyoonekana hapo juu.

Mnufaika alipwe pesa zote?

Kwa mtazamo wangu, faida moja wapo ya kikokotoo hiki kipya ni kwamba mnufaika wa pensheni atalipwa kiinua mgongo kikubwa tofauti na zamani, na hivyo kumfanya kuwa na uwezo mkubwa wa kuwekeza na kufanya mambo yake mengine baada ya kustaafu.

Nafahamu baadhi ya madai ambayo yamekuwa yakitolewa na wafanyakazi, wastaafu, na wadau wengine wakishinikiza walipwe pesa zao zote baada ya kustaafu. 

Hata hivyo, nasikitika kuhitimisha kwamba jambo hili ni gumu kulitekeleza kwani siyo tu lipo nje ya sheria na miongozo ya hifadhi ya jamii Tanzania bali pia ni kwenda kinyume na dhana nzima ya hifadhi ya jamii.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Ni Muhimu Kufungamanisha Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii?

Duniani kote, pia, hakuna sehemu ambako utaratibu kama huo unatumika.

Nihitimishe safu hii kwa kukumbusha kwamba lengo kubwa la pensheni ya kustaafu/uzee ni kukulinda/kumlinda mnufaika wa pensheni kwenye kipindi chote cha uzee mpaka pale atakapo kufa.

Zipo hasara nyingi za kiuhifadhi wa jamii endapo kama wanufaika watalipwa malipo yao yote kwa asilimia 100, kwa ujumla, pale anapo staafu. 

Hizi ni hasara zinazogusa pande zote, mfuko husika na mnufaika pia!

Thomas Ndipo Mwakibuja ana shahada ya sayansi kwenye hifadhi ya jamii kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Kwa maoni, anapatikana kupitia thomasmwakibuja@gmail.com au +255 767 879 281. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Thomas Ndipo Mwakibuja

4 comments

 • Magambo

  8 May 2023 at 8:38 PM

  Kwani ni sababu Gani za msingi zilizosababisha kubadilisha kikokotoo na kuacha Cha zamani Ili Hali hakuna mnufaika aliyelalamika? Pia hakuna sababu za msingi zaidi yamunufaa yenu binafsi baadae ya kuona mmemaliza hela kwenye majumba yasiyouzika na hamna kitu.Turudishieni kikokotoo Cha zamani msijitetee kujifanya mnajua kukokotoa wakati mlifeli hesabu.

  Reply

 • Charles L.stanslaus

  21 June 2023 at 9:40 AM

  Bwana Thomas Mwakibuja, ufafanuzi wako ni mzuri, ila kama mwana-mahesabu sijajua kwenye kanuni zote ulizotuwekea kwenye maelezo hazieleweki kwa sababu; kuna variables hujazisema zina maanisha nini katika kanuni zote mbili za kikokotoo cha mkupua (kiinua mgongo na kile cha pensheni ya kila mwezi)! Kwa sisi wastaafu tunataka tujua tutatoka mzigo kiasi gani? Ahsante.

  Reply

 • Veneranda

  27 August 2023 at 4:14 PM

  ingeleta maana kama mngefafanua maana ya hizo formula mfano hizo herufi zinasimama badala ya nini?

  Reply

 • Paschal

  29 August 2023 at 6:40 PM

  Umeeleza vizuri sana ila hizo fomla zako hazijaeleweka ni vema ukaeleza maana ya izo symbo uchanganuz wa kanuni.

  Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

{{ category }}{{ date }}

{{ title }}

{{ category }}{{ date }}

{{ title }}

{{ category }}{{ date }}

{{ title }}

{{ category }}{{ date }}

{{ title }}

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2023 © All Rights Reserved