The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mtaalamu Aonya Matumizi ya Njia za Kienyeji Kubana Uke: ‘Uke Una Ubano Wake wa Asili’

Wanawake wanaonywa kwamba kufanya hivyo kunawaweka kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa sugu, ikiwemo saratani.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Ushauri umetolewa kwa wanawake kuacha kutumia njia za kienyeji kubana uke, huku mtaalamu akibainisha kwamba kufanya hivyo kuna muweka mwanamke kwenye hatari kubwa ya kupata magonjwa mbalimbali, ikiwemo yale ya saratani.

Ushauri huo umetolewa na Dk Ummulkulthum Omar, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, wakati wa mahojiano maalum aliyoyafanya na The Chanzo hivi karibuni.

Kwenye mahojiano hayo, Dk Ummulkulthum alizungumzia tabia zinazoendelea kushika kasi miongoni mwa wanawake ya kutumia mbinu za kienyeji kubana uke, akiwashauri wanawake kuacha tabia hizo huku akisisitiza kwamba uke una ubano wake wa asili.

Yafuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa Dk Ummulkulthum anaanza kuelezea madhara ya kuweka vitu kwenye uke wa mwanamke:

Dk Ummulkulthum Omar: Kwanza, tunatakiwa tufahamu mwili wa binadamu, kila kiungo, kina mazingira yake kinavyofanya kazi. Mwili ili ufanya kazi kuna kitu kinaitwa PH acidit au alkalinity ya ile sehemu yaani, majimaji ambayo yamo katika kile kiungo chenyewe kinachopolekea kazi zifanyike kwa ufanisi zaidi.

Sehemu za uke, kuna PH yake maalum. Sasa unapoweka weka vitu katika uke unaweza kupelekea kubadilisha mazingira ya uke, unapobadilisha yale mazingira ya uke inakuwa unatoa mwanya kwa sababu kawaida kwenye uke kuna normal flora, yaani bakteria ambao siyo wa madhara.

Hawa kawaida tu wanakuwepo kwenye uke kwa ajili ya kuukinga ule uke usipate maambukizi. Sasa unapobadilisha mazingira ya ule uke kwa kuweka kitu kingine, unapoweka kitu kingine, bila shaka mazingira yataathirika.

Kwanza wale normal flora ambao ni walinzi wa ule uke utafanya kuwaondosha. Wakiondoka wale, wale kazi yao nyengine ni kukinga ambao hawahusiki kuja kukaa pale. Kwa hiyo, wale wakiondoka unatoa nafasi kwa bakteria wengine kuja kukaa katika sehemu za uke na baadaye kuleta maambukizi katika uke.

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Aeleza Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Saratani ya Shingo ya Kizazi

Kwenye uke maambukizi yakitokea unaweza kuona nini? Harufu za ajabu zinaanza kutoka chini. Majimaji ambayo si ya kawaida yanatoka kwenye uke. Unaweza kupata muwasho, maumivu wakati wa tendo la ndoa, au saa nyingine hata wengine wakafikia ni hali mambukizi makubwa hata kuweza kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa na ukajikuta mtu kutokijiskia kufanya mapenzi.

Kwa sababu unapokuwa na hali kama hiyo, basi hata ile hamu ya tendo la ndoa inakupungukia kwa sababu kama unakuwa unarudi nyuma harufu mbaya na maumivu, kwa hiyo hata ile hamu ya kufanya tendo la ndoa itapungua. Kwa hiyo, kuna athari ya kuweka vitu katika uke. Tusipoangalia tunaweza kujikuta tunapata matatizo makubwa sana.

The Chanzo: Dk Ummy, wanawake ni warembo, wanapenda mambo mazuri mazuri. Je, kuna athari yoyote inaweza kutokea iwapo wanawake wataweka udi au moshi wake unaingia kwenye sehemu yake ya uke, maana naona hii inafanywa sana?

Dk Ummulkulthum Omar: Kusema la haki sijafanya utafiti kuhusiana na hicho kitu. Lakini kama utakuwa unaweka chochote tunajua, chochote kinaweza kuwa kemikali, kwa sababu ndani ya ule moshi mna nini? Kama kutakuwa na kemikali zikaingia katika kuta za uke, zikaenda zikabadilisha mazingira, basi zinaweza kuleta athari sawasawa kama kuweka kitu ndani ya uke.

Kwa hii itategemea na ile kemikali zilizomo katika ule moshi na namna zitakavyoathiri katika kuta za ule uke wako. Kama zinataleta athari ya kubadilisha mazingira ya PH, kwa hiyo, inaweza kuleta athari.

The Chanzo: Kumekuwepo na wimbi la watu kuwashawishi wanawake [au] mabinti kutumia vipipi ili kwa ajili ya kubana uke, kitaaalamu hasa Dk Ummy hiyo inafanya kazi kweli?

Dk Ummulkulthum Omar: Yaani kusema la haki kila zama zinavyokwenda watu wana mambo mengi kabisa yanaibuka. Lakini uke una ubano wake wa asili na kusema ukweli  mwanamke kila inapokuwa anapopata mabadiliko kutoka hatua moja kwenda nyingine, kwa mfano, anapoanza kuzaa, bila shaka kutakuwa na mabadiliko katika sehemu zake za uke, ndiyo kitu kinachopelekea watu kuanza kufikiri kufanya vitu tofauti ili kurudisha  ule mvuto wa asili.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Wajawazito Wanakuwa na Tabia Zisizo za Kawaida?

Lakini mvuto wa asili haurudi kwa kuweka kemikali, au kuweka vitu. Kwa hiyo, ni vitu ambavyo watu wanafanya mtaani tu, lakini kisayansi havina nafasi kwa vyote vinapelekea mabadiliko katika mazingira ya uke.

The Chanzo: Na je, kuna ukweli kwamba unapotumia vitu hivi kuweka ukeni kunaweza kusababisha kupata saratani ya shingo ya kizazi?

Dk Ummulkulthum Omar: Kwa sababu kama tulivyosema inapelekea kuongezeka kwa maambukizi, maambukizi yanaweza kuwa bakteria, maambukizi yanaweza kuwa ni virusi, kuna virusi vinaitwa human papillomavirus, kuna aina fulani ya human papilloma, wako wengi sana, ila kuna aina fulani ambao wakiingia katika shingo ya kizazi wanaweza kupelekea mabadiliko katika shingo ya kizazi na ikibadilika ile hali halisi ya shingo ya kizazi baadaye ikabadilika kufanyika saratasi ya kizazi. Kuna ukweli kwamba unapotia tia vitu [kwenye uke], kuna uwezekano wa kupata saratani ya kizazi.

The Chanzo: Kuna hii njia pia ambayo kwenye mitandao ya kijamii inazungumziwa sana kutoa harufu au kunuka harufu kwenye sehemu za siri. Wanasema unaweza kuchukua maji ya moto ukaweka kwenye beseni ukaweka baking power halafu ukakalia mara tatu ile harufu ikate, kitaaluma haswa hii ikoje?

Dk Ummulkulthum Omar: Yaani sisi madaktari hatuwezi kuzungumza kile kitu kama hakuna utafiti wa kuthibitisha kuhusu hicho kitu. Kwa hiyo, kama ni maneno tu ya mtaani mtu kafanya kaona mabadiliko, pengine kaona mabadiliko ni kwa sasa hivi, ila baadaye hicho kitu kitafanya ndo kitu muhimu sana.

Sasa hivi unaweza kujikuta umepata faida uke umebana lakini mbeleni kuna athari unaweza kuja kuzipata. Kwa hiyo, si busara mtu kuiga kafanya leo mtu kapata matokeao mazuri.

SOMA ZAIDI: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?

Kwa sababu kama utatizama hivi vitu mara nyingi watu wanafanya kwenye umri mdogo [kwenye] miaka 20 [au] 30. Lakini tunapozungumzia hizi saratani mara nyingi, sisemi mara zote, nasema neno mara nyingi, zinakuja miaka ya 40 [au] 50. Kwa hiyo, utakutana na mbeleni. Sasa hivi utaona unajisadia kumbe pengine unajijengea mazingira mabaya mbeleni.

The Chanzo: Kuna njia gani ambazo ni rahisi zaidi mwanamke anaweza kuzitumia na uke wake ukabana?

Dk Ummulkulthum Omar: Unajua kuna kitu kinaitwa usafi katika viungo vya kike. Usafi ndiyo kila kitu. Kuuweka uke wako katika hali ya usafi. Kuna mambo [wanawake] wanatakiwa wayafanye ili kuhakikisha kwamba uke wao unabakia katika mazingira salama.

Kwanza, kuhakikisha chini unapokwenda haja ndogo ukishamaliza hakikisha unajisafisha kwa kitaula au tishu, kunakuwa kukavu, yaani usivae nguo yako ya ndani hali ya kuwa kuna majimaji chini baada ya kujisaidia.

Hii itapelekea harufu mbaya na kutokwa tokwa na taka katika uke. Ya pili sisi wanawake tuna siku tofauti katika maisha yetu. Katika siku ambazo mwanamke anaelekea katika hedhi kuhakikisha usafi wa hali ya juu kwa sababu chini kunapokuwa kunatoka ile hedhi ni moja katika ya sababu inayoplekea bakteria kupanda juu kwa wingi na ikapelekea maambukizi kama usipokuwa makini.

Mtu anapokuwa katika siku zake kwa siku awe anabadilisha pedi kila baada ya masaa manne mpaka sita kama damu haitoki nyingi. Lakini kama damu inatoka nyingi  masaa matatu mpaka manne amebadilisha ile pedi yake ambayo amevaa hata kama utakwenda chooni kujisaidia usirudie ileile, [vyema kuvaa] nyengine.

Unapomaliza kushiriki [tendo la ndoa], pale maumbile yanakuwa yapo wazi, ni kunyanyuka kwenda kujisafisha baada ya kushiriki tendo la ndoa kwa sababu ukikaa unatoa nafasi ya haya maambukizi katika sehemu za uke.

SOMA ZAIDI: Huduma za Afya ya Akili Ziingizwe Kwenye Huduma za Mama na Mtoto

Lakini la nne ni kuacha kutumia-, sababu katika kuosha uke, kuna watu labda wakienda chooni lazima akoshe uke wake kwa sabuni, unapotumia sababu unalainisha [mazingira ya uke] na unatoa nafasi kwa bakteria ambao si wa kwenye uke wakavamie ile sehemu na wakapeleke maambukizi.

Uke unaoshwa kwa maji mengi ya kuchuruzika, baadaye unakausha na unavaa nguo yako. Lakini kuna watu wanatabia kila akienda kujisafisha lazima aingize kidole ndani na wengi hata wanafundishwa wanapoolewa kile ni kitu ambacho siyo kizuri, kinapelekea michubuko katika uke, lakini pia wale bakteria waliopo kulinda katika uke unawasumbua na kuwaondosha. Kwa hiyo, ile michubuko na kuondosha  wale bakteria.

Lakini ya sita kuna matangazo mengi watu utaona vitu vya kusafishia uke sabuni sijui ma-lotion. Jamani, mtu usitumie kitu ambacho hakijathibitishwa na kabla hujatumia hakikisha unapata ushauri kutoka kwa mtu sahihi.

Lakini watu wanatakiwa wasivae nguo za kubana sana katika uke kwa sababu nguo ya kubana inaongeza joto, kumbuka huku chini pia kuna joto lake la asili na unapovaa nguo nyingi za kubana sana kuongeza joto sasa joto na nyevu ya uke hayo ni mazingira kwa ajili ya bakteria kuwepo kwa wingi.

Na ya saba ni kujua namna halisi ya kujisafisha. Kwa hiyo, kama utajisafisha bila ya kuwa na mpangilio maalumu, kwa hiyo unatakiwa uhakikishe mtu akijisafisha ni kutoka mbele kwenda nyuma.

Pia, kutodharau mabadiliko yanayotokea katika uke. Unapoona kuna majimaji ambayo si ya kawaida kwenye uke au yana uwasho japo kuwa ya mbali harufu, japo kuwa ya mbali, lakini si ya kawaida ambayo umeizoea, unatakiwa utafute ushauri wa daktari ili akuanzishie tiba mapema na mwisho kabisa kutokujibu mtu mwenyewe njia sahihi unapopata shida za uke muone daktari wa mambo ya kike atakuangalia, atakufanyia vipimo, ikihitajika na kukushauri njia sahihi ya kujitibu.

The Chanzo: Dk Ummulkulthum, nakushukuru sana kuzungumza na The Chanzo na nikutakie majukumu mema, nikushukuru sana kwa fursa hii

Dk Ummulkulthum Omar: Asante, nashkuru sana!

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *