Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Dk Ida Hadjivayanis, Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili, SOAS University of London katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Umoja wa Mataifa, New York, Marekani mnamo Julai 7, 2023.
Ninayo furaha kubwa kuwa nanyi leo hapa New York, UNESCO, ili kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani. Ningependa kuanza kwa kusema kwamba ni fahari kubwa sana kwetu kwamba lugha ya Kiswahili imetambulika kama lugha muhimu ya Kiafrika duniani.
Dhamira ya mazungumzo haya ni kuonyesha nafasi na jukumu la Kiswahili kama lugha ya umoja inayozungumzwa nchi kadha wa kadha barani Afrika na duniani, hasa katika muktadha wa ulimwengu wa leo wa kidijitali.
Kwa kuutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika zama za kidijitali, tunaimarisha uwezo wake wa kukuza mwingiliano wa tamaduni, ubadilishanaji wa maarifa, na maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa wazungumzaji wa Kiswahili duniani kote.
Ninataka kuanza mazungumzo haya kwa kuwakumbusha kwamba, jinsi Kiswahili kinavyokua na kusambaa hivi sasa si bahati nasibu. Yaani, si kwamba Kiswahili kimepata bahati ya kukua na ukuaji huu umetokea tu – hivi hivi, – hapana. Ukweli ni kwamba hatima ya Kiswahili ilikuwa ni lazima iwe lugha kubwa duniani.
Hii ni kwa sababu, Kiswahili si njia ya mawasiliano tu bali ni mfumo mzima wa mawazo, itikadi, falsafa na tamaduni ambazo zimekuwa zikikua kwa karne nyingi. Kiswahili kilienea kutokana na biashara na kushirikiana kwa jamii tofauti; biashara zilizohusisha nchi zinazoguswa na Bahari ya Hindi kuanzia mwambao wake kuelekea bara zima la Afrika Mashariki na Kati, sehemu za ughaibuni kama Uajemi, nchi za Kiarabu, Bara Hindi, Australia na hata Uchina.
Hivi sasa Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na takriban zaidi ya watu milioni 200 walioko sehemu tofauti duniani kote, lakini hasa barani Afrika. Tunafahamu kwamba chanzo chake ni nchi ambazo sasa zinajulikana kama Tanzania, Kenya, Uganda, DRC na nchi zinazopakana na maeneo haya kama kusini ya Somalia, Rwanda, Burundi na Msumbiji.
Tumesikia kwamba nchi nyingi zimeanza kufundisha Kiswahili shuleni ikiwa ni kama lugha ya Kiafrika inayoleta ukombozi wa kimtazamo– kwa mfano, Afrika ya Kusini, Sudani ya Kusini na Botswana. Na hivi majuzi zimeongezeka nchi za Urusi na Colombia ambazo zitaanza kufundisha Kiswahili shuleni kuanzia Septemba mwaka huu [wa 2023].
Majukwaa ya kujifunza lugha, kwa mfano Duo Lingo, imetoa taarifa kwamba masomo yake ya Kiswahili yamekua kwa asilimia 22 mwaka uliopita na hivi sasa kuna wanafunzi 512,000. Asilimia kubwa ya wanafunzi hawa wapo Marekani.
SOMA ZAIDI: Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria
Kwa mawazo yangu, kushehena kihistoria na kitamaduni kwa lugha hii kutazidi kukua na ni muhimu kwetu kuutambua na kuusherehekea ukuaji huo na pia kuheshimu uwezo wa lugha hii kutuunganisha sote tunaotumia Kiswahili ili tuwe kitu kimoja.
Kiswahili katika zama hizi kinaweza kuendelea kukuza uelewano na ushirikiano kati ya watu wenye asili na mitazamo tofauti kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa karne kadhaa. Jambo la kuzingatia ni kwamba, tukubali lugha inapokua lazima ibadilike, ikumbatie tamaduni mpya na iende na wakati.
Wiki iliyopita nilialikwa kuzungumza katika makumbusho ya Sanaa za Kisasa ya Louisiana yaliyopo Denmark. Nilipokuwa pale, washiriki ambao ni Kabage Karanja na Stella Mutegi kutoka Cave Bureau Nairobi, walitambulisha neno Binadamucene kuwa na maana ya neno la kizungu – Anthropocene.
Neno hili liliundwa mwaka 2000 na lina maana ya zama za binadamu – wakimaanisha zama ambazo mazingira yamebadilishwa na hata kuharibiwa kutokana na vitendo vya binadamu duniani. Kwa nchi za magharibi, hususan Uingereza, zama hizi zilianza wakati wa mapinduzi ya viwanda. Kwa bara la Afrika, wanazuoni wanadai kwamba zilianza wakati wa kuingia kwa Mkoloni Afrika.
Ni kipindi hiki wakati mazingira yalipobadilishwa hasa kwa kuanzishwa kwa miundombinu kama vile barabara, reli na bandari. Wakati huu ukulima ukawa wa kibiashara na siyo wa kukidhi mahitaji ya jamii kama vile chakula cha kulisha koo. Na ni wakati huu ambapo Kiswahili kilibadili hati zake kutoka zile za Kiarabu na kuenda hizi tunazozitumia sasa, za Kilatini.
Neno Binadamucene limechanganya Kizungu na Kiswahili, wanasarufi wanaweza kuliona kama upotoshaji, wengine labda wangependelea neno litoholewe na kuitwa Antroposini au Binadamusini – na wengine labda wangependa neno ambalo litafahamisha dhana hii – mfano ‘zama za binadamu’ litumike. Kwangu mimi, ninahisi muhimu kuliko yote ni kwamba dhana mpya ambayo ni ya kisasa imeingizwa katika wigo wa dunia ya Kiswahili.
Hakuna Kiswahili kimoja
Sipo hapa kuamua neno hili litafsiriwe vipi kwa Kiswahili – hiyo ni kazi ya BAKITA na BAKIZA pamoja na mabaraza mengine ya lugha. Nipo hapa kuwakumbusha tu kwamba hakuna Kiswahili kimoja. Hakuna njia moja ya kusema Kiswahili. Kuna lahaja nyingi na kumekuwa na lahaja tofauti tangu awali, na sasa kuna njia nyingi za kusema Kiswahili.
SOMA ZAIDI: Wadau wa Elimu Wahoji Ukimya wa Dira ya Taifa Katika Kutambua Nafasi ya Kiswahili Kwenye Elimu
Bila shaka watu wa mwambao wanajulikana kuwa ‘wenye Kiswahili’ na sasa lugha hii imesambaa kwa marefu na mapana. Kusambaa huku ni ishara ya Kiswahili kuwa lugha hai. Kwa hivyo, Kiswahili ni shina lenye matawi kemkem. Tuwe na umoja wa watu wanaotumia na kukikubali Kiswahili katika uwingi wake.
Ninasema hivi kwa sababu, tofauti za jinsi lugha inavyosemwa zitazidi kukua. Kiswahili kinazidi kuvuka mipaka yake ya kihistoria – sasa kipo Uchina, Urusi na hata Colombia; basi tutegemee ukuaji mkubwa sana.
Bila shaka Serikali za Afrika Mashariki zitapeleka walimu huko ili kufundisha lugha fasaha, lakini kama vile ilivyokuwa kwa Kiingereza ambapo kuna Global English – Kiingereza cha Ulimwengu – ambacho kina tofauti kama Kiingereza cha Marekani, Nigeria, Bara Hindi na kwengineko.
Ninahisi kwamba ni dhahiri jinsi Kiswahili kinavyozidi kupanuka, kutajitokeza Kiswahili cha maeneo tofauti duniani na tunapozungumzia lugha ya umoja, hasa katika muktadha wa kidijitali ni muhimu kwetu kukubali uwepo wa lugha hii katika namna tofauti, yaani kuna kuzungumza kwa Kiswahili kwa njia tofauti.
Kwa mawazo yangu, kukubali jambo hili ni moja kati ya mikakati na mipango itakayokiwezesha Kiswahili kuendelea kukua na kuwa na nafasi kamilifu kama lugha muhimu katika mawasiliano, uvumbuzi, na ujuzi wa kidijitali. Na sasa tunaona jinsi tofauti za lugha hii linavyofanyiwa utafiti na wanaisimu wabobezi ili kuelewa athari zake.
Kwa mfano, mradi wa Hannah Gibson, Lutz Marten na Thomas Jelpke unatafiti lahaja na njia za kuzungumza Kiswahili Kenya na Tanzania na pia Uganda na DRC. Jambo hilo halimaanishi kwamba Kiswahili sanifu kinapunguziwa hadhi yake. Hapana asilan!
Njia kuu ya kuwezesha lugha kuendelea katika nyakati za kidijitali ni uwepo wa lahaja sanifu, uwepo wa maandishi kamilifu yanayotumiwa, yanayofundishwa na kueleweka na wote, yaani uwepo wa usanifu wa lugha. Lugha ambazo hazina lahaja sanifu zimeshindwa kuwa na nafasi katika zama hizi.
SOMA ZAIDI: Hatua Zilizobaki Ili Kiswahili Kiwe Lugha ya Kufundishia Tanzania
Kuna mifano mingi ya lugha hizo barani Afrika. Kwa hivyo, kutokana na Kiswahili kuwa na lahaja yake sanifu, lugha hii imeweza kutumiwa na kutumika katika majukwaa tofauti kama Google na mengineyo. Hili ni jambo muhimu sana.
Umuhimu wa Kiswahili sanifu hauna kifani. Zamani kulikuwa na dhana waliyokuwanayo wengi ya kuona Kiswahili kama lugha iliyozama katika mfumo wa maneno na maumbo ya kikongwe au ya kihistoria. Yaani, ilionekana kuwa lugha inayofaa kwa kuandika mashairi na utenzi tu. Hii si kweli asilan.
Kiswahili hivi sasa kinakidhi utaalamu tofauti na pia kinakidhi sayansi na kiteknolojia. Kwa kweli Kiswahili kinakuwa daraja au kiungo cha jamii mbalimbali na kuwezesha ushirikishwaji wa wote katika ulimwengu huu wa kidijitali.
Hata hivyo, ingawa katika kipindi cha muongo mmoja huu uliopita, bara zima la Afrika limekumbwa na ukuaji mkubwa wa teknolojia za kidijitali na muunganisho wa intaneti uliobadilisha njia za watu kuwasiliana, kupata taarifa na kufanya biashara katika bara zima, bado kuna tofauti kubwa za kidijitali.
Tumeona kwamba teknolojia ya simu za mkononi imeunda mazingira ya kidijitali ya Kiafrika. Kumeongezeka simu mahiri za bei nafuu na upatikanaji wa mitandao ya simu. Pia, sehemu kubwa ya watu wamepata ufikiaji wa mtandao kwa mara ya kwanza.
Viwango vya kupenya kwa simu za mkononi vimeongezeka, na kuwawezesha watu kupata huduma za mtandaoni, na kushiriki katika uchumi wa kidijitali.
Mgawanyiko wa kidijitali
Hata hivyo, kuna umuhimu wa kukiri kwamba bado kuna mgawanyiko wa kidijitali usiyo na usawa katika bara la Afrika. Kuna tofauti katika upatikanaji wa mtandao, ujuzi wa kidijitali, na miundombinu ya kiteknolojia kati ya maeneo ya mijini na vijijini, na pia katika nchi mbalimbali.
Juhudi zinafanywa ili kuziba mapengo haya kupitia mipango inayokuza mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, kupanua muunganisho, na kuwekeza katika miundombinu ya kiteknolojia. Katika mazingira haya ya kidijitali yanayoendelea kwa kasi kubwa, nafasi ya lugha imekithiri ile ya kuwa njia ya mawasiliano na imekuwa lango lililojaa fursa, maarifa, na uwezeshaji.
SOMA ZAIDI: Kutweza Kiswahili ni Ishara ya Kujidharau, Kutojiamini
Kila siku tunashuhudia mapinduzi ya kidjitali kutokana na ukuaji mkubwa wa teknolojia na kupanuka kwa mitandao. Mojawapo ya faida kuu za kukumbatia Kiswahili katika enzi ya kidijitali ni uwezekano mkubwa wa ukuaji wa uchumi. Ulimwengu wa kidijitali una fursa zisizo na kikomo za biashara, huduma za mtandaoni na ujasiriamali wa kidijitali.
Kwa kutumia uwezo wa Kiswahili, tunaweza kuunda mfumo wa kiikolojia wa kidijitali uliostawi. Pia, tunaweza kueneza matumizi ya Kiswahili katika majukwaa yaliyojaa fursa mpya za kiuchumi ambazo zitavutia uwekezaji.
Kwa upande wa Kiswahili, tumeona juhudi hizi zikichukua sura ya utafutaji wa misamiati. Kwa mfano, maneno yamekuwa yakitafsiriwa na kufikiriwa kwa kina ili yaendane na maendeleo ya kisasa ya kidijitali na kiteknolojia.
Maneno kama ‘kushirikisha’ na ‘kusambaza’ sasa yameshika tama. Lakini hivi karibuni kumekuwa na mradi wa kuziba mwanya wa ‘utenganisho wa kidijitali’ uliofanywa na Nanjala Nabola na mwishoni yalipatikana maneno takriban 50 ikiwa ni pamoja na “deep fakes” (Ughushi Mbizi), “trolling” (Ukeraji Mtandaoni).
Zaidi ya hayo, enzi ya kidijitali zinatupa fursa ya kuhifadhi na kuendeleza utamaduni na urithi wa Waswahili. Hapa ninafikiria, kwa mfano, kuhifadhiwa kidijitali kwa nyaraka na miswada iliyopo kwenye makumbusho na vyuo tofauti duniani.
Kwa mfano, chuo changu cha SOAS University of London, kimeweza kuhifadhi kidijidali utenzi, mashairi na barua kongwe zilizoandikwa karne kadhaa zilizopita na hivyo kuweza kusomwa na wote kutoka popote duniani. Kiswahili ni katika lugha chache za Kiafrika zenye historia ya kuandikwa.
SOMA ZAIDI: Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi
Mswada mkongwe zaidi tulionao hadi hivi sasa ni tafsiri ya utenzi uliofanywa huko Pate na Sheikh Aidarus bin Uthaima mwaka 1650. Utenzi huo uliandikwa Misri karne ya 13 na unaitwa Hamziya. Kutokana na juhudi za kidijitali, leo sote tunaweza kuusoma utenzi huu mtandaoni.
Hata hivyo, bado zipo nyaraka nyingi sana ambazo hatujaweza kuzihifadhi kidijitali. Kufanya hivyo kutatuwezesha kuelewa historia yetu kwa kina zaidi na kutawezesha utafiti muhimu sana wa kitaaluma kuhusu dunia ya Waswahili – dunia ambayo imeandikwa na wavumbuzi wa zamani wanaozungumzia ustaarabu wa miji adhimu kama Kilwa, Lamu na Zanzibar.
Wito wangu leo ni kwa sisi kufikiria jinsi ya kuhifadhi nyaraka hizi ambazo ni muhimu kwa historia yetu.
Pia, kwa kupitia majukwaa tofauti mtandaoni tunaweza kushirikisha muziki wa Kiswahili, fasihi yetu, sanaa na ngano ili kukuza ushawishi wa sanaa na kuhakikisha kwamba vizazi vijavyo vinaendelea kukumbatia na kuenzi mila na desturi zetu. Elimu itafaidika sana kutokana na kukumbatia Kiswahili katika enzi hizi.
Upatikanaji wa rasilimali bora za elimu katika Kiswahili utawawezesha watu binafsi na jamii kujivunia na kuuthamini ulimwengu wa Kiswahili. Kwa kutumia majukwaa ya kidijitali tunaweza kukuza ujuzi wa kusoma na kuandika, na kutoa fursa muhimu za kujifunza kwa wale ambao labda wameachwa nyuma.
Umuhimu wa tafsiri
Siwezi kuwa hapa nisizungumzie umuhimu wa tafsiri katika zama hizi. Tafsiri kwa Kiswahili na pia kutoka Kiswahili kuenda kwenye lugha nyingine kama vile Kiingereza nakadhalika.
Ningependa kutoa mfano wa Tuzo ya Fasihi ya Mwalimu Nyerere iliyoanzishwa na Wizara ya Elimu Tanzania, ikiongozwa na Profesa Adolf Mkenda pamoja na Dk Lela Mussa. Tuzo hii inawezeshwa na teknolojia kwani miswada hutumwa kupitia mitandao tofauti, ushindi hutangazwa kwa kupitia mitandao, na waandishi hufarijika kwa kuona kazi zao zikichapishwa na kusambazwa nchini kote.
Kazi ya tuzo ni kuziba pengo la kudorora kwa uandishi na usomi wa Kiswahili. Na hapa ndipo tafsiri imepewa nafasi adhimu ya kuwa njia muhimu inayoingiza maandiko mapya katika fasihi ya Kiswahili kutoka kwenye tamaduni, itikadi na falsafa zilizoandikwa kwa lugha nyingine.
Mfano mzuri ni tafisri yangu mwenyewe ya kazi ya Abdulrazak Gurnah ambaye alishinda Tuzo ya Nobel ya mwaka 2021. Mimi nilitafsiri Paradise kwa Kiswahili na kuiita Peponi. Hivi sasa Peponi ni kazi pekee ya Gurnah katika lugha ya Kiafrika. Ni muhimu kuona kwamba lugha ya kwanza ya Kiafrika kumpokea Gurnah ni Kiswahili.
SOMA ZAIDI: Ida Hadjivayanis Aichambua ‘Peponi’ Ya Abdulrazak Gurnah
Bila shaka Abdulrazak Gurnah amekuwa na mashabiki kemkem Afrika ya Mashariki kwa miongo mingi sasa, lakini kuwepo kwa kazi yake katika lugha ya Kiswahili kumeongeza wigo wa wale watakaomsoma na kufahamu ayasemayo gwiji huyu na pia kutatoa chachu kwa wale watakaopata hamu ya kutafsiri kazi nyingine.
Kwa kumalizia, ningependa kusema kwamba, kuibua uwezo wa Kiswahili katika zama za kidijitali kunahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa wadau mbalimbali – Serikali, taasisi za elimu, kampuni za kiteknolojia, waundaji maudhui, na jamii inayozungumza Kiswahili.
Wote hawa wanatakiwa waungane ili kuendeleza na kukuza mipango ya kidijitali inayolenga Kiswahili. Hii inaweza kujumuisha kuunda programu za kujifunza lugha, kutafsiri na kutoa huduma maarufu mtandaoni kwa Kiswahili.
Tukumbuke tu kwamba, kukikumbatia Kiswahili katika enzi ya kidijitali siyo tu suala la kuhifadhi lugha; ni fursa ya kuwawezesha watu, kuimarisha jamii, na kuendesha ukuaji wa uchumi.
Tumeutambua uwezo mkubwa wa Kiswahili, sasa tushirikiane kwa pamoja, katika tofauti zetu, ili kuhakikisha kwamba lugha hii inachukua nafasi yake ipasavyo katika mapinduzi ya kidijitali. Kwa pamoja, tunaweza kutengeneza mustakabali mwema kwa wote wanaoithamini lugha hii adhimu.
Asanteni!
Dk Ida Hadjivayanis anapatikana kupitia ih11@soas.ac.uk au Twitter kama @IdaHadjivayanis. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.