Zanzibar. Wanafunzi katika Kituo cha Tucheze, Tujifunze cha Fukuchani wamekuwa wakisoma chini ya miti kwa kukosa madarasa kwa muda wa miaka 13 sasa, hali iliyolalamikiwa na wakazi wa kijiji hicho wanaohofia kwamba ustawi na hatma ya watoto wao inaweza kuwa mashakani kama mamlaka husika hazitaingilia kati.
Vituo vya Tucheze, Tujifunze, au kwa kifupi kama TuTu, ni vituo vilivyoanzishwa na Serikali ya Zanzibar katika maeneo mbalimbali ya sehemu hiyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwawezesha wazazi kuwapatia watoto wao elimu ya maandalizi karibu na pale wanapoishi.
The Chanzo ilifika katika kituo hicho kilichopo kijiji cha Fukuchani, shehia ya Kigongoni, wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini, Unguja, mnamo Juni 11, 2023, na kushuhudia watoto hao wenye umri kati ya miaka mitatu na mitano wakiwa wamekaa kwenye mabusati tayari kwa ajili ya kuanza masomo.
Leo ndiyo masomo yanaanza baada ya watoto wanaosoma hapa, jumla wakiwa ni 55, kukaa nyumbani kipindi chote cha masika kwani mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha ziliwazuia watoto hao kushiriki kwenye masomo kutokana na kukosa miundombinu muhimu ya kujifunzia kama vile vyumba vya madarasa na madawati.
Fatima Haruna Haji ni moja kati ya walimu watano walioajiriwa na Serikali kufundisha katika kituo hicho tangu mwaka 2013, miaka mitatu tu tangu kuanza kwake, aliyeiambia The Chanzo kwamba hali ya ukosefu wa vyumba vya madarasa kituoni hapo inawakwaza siyo tu watoto bali hata wao kama walimu kwani inapunguza ari na uwezo wao wa kufanya kazi kama wanavyopaswa.
“Hapa kusoma ni kiangazi ila masika ni kubaki nyumbani au kwenda kujibanza kwenye kituo cha afya [kilichopo karibu na kituo hicho],” Fatima alisema. “Watoto ni wadogo. Hawawezi kutembea umbali mrefu, ndiyo maana tumejenga hapo tulipofikia bado hatujapata usaidizi.”
Kutembea umbali mrefu
Kuanzishwa kwa kituo hicho kijijini hapo kulikuja baada ya watoto kuonekana kutembea umbali wa zaidi ya kilomita saba kwenda shule ya maandalizi iliyokuwa karibu na kijiji hicho, wakikabiliana na changamoto kadhaa zilizoisukuma jamii ya Fukuchani kujichukulia hatua ya kuanzisha kituo hicho.
Wanafunzi na walimu wa Kituo cha Tucheze, Tujifunze (TuTu) kilichopo Fukuchani wakiwa chini ya miti kwa ajili ya kuanza kusoma. PICHA | NAJJAT OMAR
Simulizi za wanajamii hiyo zinaonesha kwamba baadhi ya changamoto hizo ni kama vile watoto wakike kubakwa wakiwa njiani kutokana na kuwepo kwa pori kubwa baina ya kijiji cha Fukuchani na Shule ya Msingi Kigongoni ambayo watoto hao walikuwa wakienda hapo awali.
SOMA ZAIDI: Haya ni Lazima Yazingatiwe Ili Upangaji, Upanguaji Safu Katika Sekta ya Elimu Zanzibar Uweze Kuzaa Matunda
Wanakijiji wa Fukuchani hawaridhishwi na hali ya watoto wao kusomea chini ya miti, hali iliyowapelekea kuanza ujenzi wa madarasa ili hatimaye watoto hao wasome kwenye mazingira salama na tulivu, lakini ujenzi huo umeshindwa kukamilika kutokana na wazazi na walezi kushindwa kuumaliza peke yao.
“Jengo letu hili limesimama kwa muda kwa sababu watoto hawa tunaona wanatembea masafa marefu, sasa walimu tumejitolea ili tujenge jengo hili ili watoto wetu hawa wapate huduma hapahapa wasiende masafa ya mbali,” alisema Fatima. “Lakini tunaomba Serikali itutazame kwa jicho la huruma, hili jengo letu likamilike ili watoto wetu wasome hapahapa.”
Boma la nyumba ya vyumba viwili ambalo wanajamii wa Fukuchani wameshindwa kumalizia ujenzi wake wakitaka Serikali iwasaidie. PICHA | NAJJAT OMAR
The Chanzo ilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, endapo kama ana taarifa yoyote kuhusiana na kero hiyo ya wananchi hao ambapo alikiri kutambua uwepo wake, akisema mchakato wa kuitatua uko mbioni.
“Viongozi wa shehia walileta taarifa ya uwepo wa shule hiyo ya wanafunzi wanaosoma chini ya mti kwa Afisa Elimu Mkoa na sisi tumelifikisha wizarani,” alisema Mahmoud, akimaanisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar. “Hivyo, tuna matumaini Serikali italichukulia hatua na ujenzi ule utakamalika.”
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi, Abdalla Abasi Wadi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliiambia The Chanzo kwamba hakuwa na taarifa ya kero hiyo inayowakumba wananchi wake, akiahidi kulifuatilia suala hilo kuona utatuzi wake unafanyika haraka iwezekanavyo.
SOMA ZAIDI: Inachoweza Kufanya Zanzibar Kuhakikisha Watoto Wanaorudishwa Skuli Hawarudi Mitaani
“Tayari pesa za Mfuko wa Jimbo zimeshaingia na kwa sasa nimekusikia wewe [kuhusu hiyo kero],” alisema Wadi ambaye pia ni msimamizi wa Mfuko wa Jimbo la Nungwi. “Nitakwenda kuona na kumega kiasi kidogo cha fedha kumalazia jengo hilo ili watoto wasome kwenye madarasa. Hiyo ni ahadi yangu kwako.”
Wanafunzi hao ni miongoni mwa wanafunzi 3,559 wanaosoma kwenye vituo 69 vya TuTu vinavyoendeshwa na Serikali katika wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini, kisiwani Unguja. Kuna vituo kama hivyo 269 Zanzibar nzima, vyenye jumla ya watoto 18,748.
Taarifa za watoto wa Fukuchani kusomea chini ya miti zinakuja wakati ambapo Serikali ilitenga jumla ya Shilingi bilioni 91.5 kwenye mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kuendeleza elimu ya maandalizi na msingi Zanzibar.
Jumla ya shule 29, zikiwemo shule 22 za maandalizi na shule saba za msingi zinazojumuisha shule mbili za elimu mjumuisho Unguja na Pemba, zilijengwa kwa kutumia fedha hizo, Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumzi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 inaonesha.
Changamoto kubwa
Kesi hii, hata hivyo, ni kielelezo cha changamoto kubwa ya uhaba wa vyumba vya madarasa ambayo Zanzibar inaendelea kupambana nayo katika jitihada zake za kuhakikisha kwamba lengo nambari nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu, linalohusiana na upatikanaji wa elimu bora kwa wote, linatimizwa.
Pengine hakuna sehemu inayodhihirisha ukubwa wa tatizo hili visiwani hapa kama katika Shule ya Msingi Kinuni iliyopo wilaya ya Magharibi B, mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja.
Shule hii yenye wanafunzi 3,453 wa maandalizi na msingi ina vyumba 23 tu vya madarasa, huku ikiwa na walimu 47 tu. Kwa wastani, kila chumba huchukua wanafunzi 150, hali inayosababisha msongamano mkubwa na usumbufu mkubwa katika ufundishaji na ujifunzaji.
Katika jitihada zao za kutatua kero hii, walimu wameamua kutoa madawati kwenye madarasa hayo ili kutengeneza nafasi zaidi.
SOMA ZAIDI: Tumejifunza Nini Kutoka Mkutano wa Pili wa Urathi wa Maalim Seif?
The Chanzo ilitembelea shule hiyo hapo Agosti 1, 2023, ambapo ilifika kwenye Darasa la Pili B, mkondo wa asubuhi, nakukuta jumla ya wanafunzi 160 wakiwa wamekaa kwenye darasa hilo, wanawake 80 wakiwa upande wa kushoto na wanaume 80 wakiwa upande wa kulia, huku kila mstari ukionekana kuwa na watoto saba hadi tisa.
Wanafunzi wa Darasa la Pili B, Mkondo wa Asubuhi, wa Shule ya Msingi Kinuni wakiwa darasani kwa ajili ya masomo. PICHA | NAJJAT OMAR
The Chanzo iliona darasa lililojaa wanafunzi, huku wengine wakiwa wamekaa karibu na mlango wa chumba hicho. Muda huu ni kipindi cha somo la Kiswahili ambapo leo wanafunzi wanafundishwa kuchanganya silabi na konsonati. Unaweza kuona baadhi ya watoto wakiwa wanapigana, huku wengine wakiwa wanasinzia.
Inatuathiri
Halima Ali Yussuf ni Mwalimu wa Darasa la Pili B, Mkondo wa Asubuhi na pia ni Mkuu wa Seksheni 1 ambayo inasimamia madarasa tisa ya awali, ikiwemo Darasa la Kwanza, Pili na Tatu katika shule hii ambaye anakiri uwepo wa changamoto kubwa ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo kutokana na msongamano mkubwa wa wanafunzi.
“Kuna athari za moja kwa moja kwenye suala la kujifunza na kusoma kwa watoto kwa sababu uhaba wa vyumba vya madarasa unaathiri usomaji, kuandika, elimu jumuishi na ufahamu,” alisema Halima. “Kwanza watoto ni wengi, na wengine hawasikii kwa sababu wako nyuma sana. Sasa unakuta wakati wewe unasomesha, wengine wanapigana na wengine hata hawaandiki.”
Halima ameiomba Serikali kuingilia kati, akisema hali hiyo inawaathiri wanafunzi na walimu ambao wanalazimika kutumia sauti kubwa kuhakikisha wanafunzi wote wanasikia, hali anayosema inaweza kuwa na madhara ya kiafya kwa walimu hapo baadaye.
Eshe Haji Ramadhani ni Meneja wa Miradi ya Elimu kutoka Milele Zanzibar Foundation, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na elimu Zanzibar, aliyeimbia The Chanzo kwamba ipo haja kwa Serikali kuboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji Zanzibar kwa lengo la kukuza kizazi kilichoelimika.
SOMA ZAIDI: Kitila Mkumbo Aichambua Rasimu ya Sera ya Elimu, Ataka Iboreshwe
“Kwenye suala la ubora wa elimu, mtoto anahitajika kupata ule umakini wa mwalimu ili apate kujengwa kwenye msingi mzuri wa kusoma na kujifunza,” Eshe, ambaye shirika lake pia hujihusisha na ujenzi wa shule, alisema. “Sasa, [wanafunzi] wakiwa wengi kitu hicho hakipatikani na kinaweza kuleta athari kwenye masomo ya wanafunzi.”
Khamis Yusuf Bakari ni Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi na Samani kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ambaye ameiambia The Chanzo kwamba Serikali inafahamu changamoto za uhaba wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule visiwani humo na tayari imeanza utekelezaji wa kuzitatua.
Kwa mujibu wa Bakari, kwa sasa kuna uhaba wa vyumba vya madarasa zaidi ya 5,000 Unguja na Pemba, akifafanua kwamba hivi sasa Serikali inajenga madarasa 1,000 katika sehemu mbalimbali za visiwa hivyo viwili vikubwa vinavyounda Zanzibar.
“Mipango ya Serikali ni kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 5,000 hadi kufikia 2025 ili kuondoa kabisa suala la kuwepo kwa mikondo miwili [katika shule],” alisema Bakari. “Tumeanza ujenzi huo na mpaka sasa tumeshajenga vyumba vya madarasa zaidi ya 500 kwenye shule za msingi na sekondari nchi nzima.”
Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.