Tunaposikia mwanamke ana ulemavu, uwe ni ulemavu wa viungo vinavyoonekana au visivyoonekana, picha inayokuja kwa wanajamii wengi ni ile ya mzigo, inayoambatana na maswali kama vile, nani atamuoa? Nani atamtunza? Mwanamke huyu anaonekana hawezi kufanya chochote cha kuijenga jamii yake; yeye ni wa kufanyiwa tu.
Wanajamii wengine wanathubutu kumweka ndani tangu akiwa mdogo ili asionekane na kuleta aibu ‘kwa familia.’ Mwanamke mwenye ulemavu anaonekana kama hawezi kukua kiuchumi, wala kijamii kwani anaonekana mwenye kasoro ambazo zinamweka nje ya kundi la wanaostahili kuitwa wanawake.
Kwani kuwa mwanamke ni nini? Kuna picha maarufu ambayo huonekana kwenye mitandao ya kijamii mara kwa mara – mwanamke amebeba kuni kichwani, amemshika mtoto mkononi, mkono mwingine umeshika kikapu chenye vyakula na mgongoni amembeba mwanaume!
Huyo ndiye mwanamke ambaye jamii inaona anastahili kuwa mwanamke – wa kwanza kuamka ili kuitumikia familia yake na wa mwisho kwenda kulala. Mtu asiye na mahitaji ya kwake binafsi, na kama anayo, basi ayashughulikie mwenyewe bila kuomba msaada wowote.
Huyo ndiye mwanamke ambaye jamii zetu zinaona anastahili cheo cha kuwa mwanamke. Je, mwanamke mwenye ulemavu anatosha kwenye viatu hivyo kwa viwango vyetu?
Mwanamke ni uzuri
Halafu kuna jambo jingine ambalo huwa haliongelewi sana ingawaje lina sehemu yake. Tukubali, tukatae lakini uzuri ni sehemu kubwa ya kuwa mwanamke. Mwanamke anaonekana ana wajibu wa kuwa msafi, kupendeza, kunukia, kuvutia na kuwa mzuri. Nisieleweke vibaya, hakuna ubaya wowote katika kuwa msafi na kujipenda.
SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’
Ninachosema ni kwamba, mwanamke asiyejali uzuri, au asiyefikia viwango vya uzuri vilivyowekwa na wanajamii, anaonekana kuwa si mwanamke kamili. Utasikia, ‘ah, amekaa kama mwanaume hivi – hana mvuto.’
Sasa katika hili, kuna wazo ambalo halijadiliwi kiuwazi ingawa lipo – je, mwanamke mlemavu anaweza kuwa mzuri? Kwa harakaharaka tunaweza kuuliza ni swali la aina gani hilo. Na tunaweza hata kujibu ‘ndiyo’ lakini mioyoni tunafahamu kwamba wengi wetu hatuoni hivyo.
Ndiyo maana tukisikia kuwa mwanamke mlemavu ana mchumba, tunashangaa – yaani amekosa mwanamke! Au mtu mwengine anaweza kusema, “jamani yaani ni mlemavu lakini ana sura nzuri,” akimaanisha kuwa uzuri na ulemavu havistahili kukaa kapu moja. Ulemavu unaendana na ubaya na ubaya unaendana na kukataliwa.
Na kisha tukisikia mwanamke mlemavu ana watoto na ameweza kujenga familia, ndiyo kabisa, tutahoji: amewezaje? Ana mvuto gani? Mbona mwili wake haumruhusu? Itakuwa siyo watoto wake, nakadhalika.
Zipo kesi ambapo mwanamke mwenye ulemavu anabakwa, kwa sababu anaonekana hana mamlaka yoyote na mwili wake. Na tena, wapo ambao wamewanyang’anya wanawake wenye ulemavu watoto wao, au kuwafunga vizazi bila wao kujua ili wasiweze kupata watoto kwani wanaonekana hawana haki hiyo.
Madada poa
Hukumu ni nyingi pia kwa wanawake wanaojihusisha na biashara ya ngono. Tunapomwona mwanamke amesimama usiku barabarani, au tunapofahamu kuwa Dada Nanihii hiyo ndiyo shughuli anayofanya, tunawahukumu harakaharaka bila kujali ni nini kilipelekea mwanamke yule kuwa katika mazingira yale.
SOMA ZAIDI: Wanawake Machinga Complex Dodoma Wafurahia Uwepo wa Vyumba vya Kunyonyeshea, Malezi: ‘Ni Ukombozi’
Cha kushangaza zaidi ni kwamba, hakuna mtu atakayemhukumu mwanaume akijua kwamba anajihusisha kingono na mwanamke anayefanya biashara ya ngono. Mizani hailingani. Lakini, hiyo siyo hoja yangu ya msingi kwa sasa.
Nafikiri ni muhimu kutambua kuwa nyuma ya kila mwanamke anayejihusisha na biashara ya ngono, kuna hadithi ambayo hatuijui. Stella (siyo jina lake halisi) ni mwanamke mwenye ualbino.
Yeye anasimulia jinsi alipokuwa na miaka 13 tu aliozeshwa kwa mwanamme aliyemzidi miaka 30. Wazazi wake walifariki akiwa na miaka sita tu. Maisha ya Stella yalijaa unyanyasaji wa kingono na hata akajiingiza katika biashara ya ngono.
Simulizi ya Stella siyo ya kipekee. Kwa sehemu kubwa, wanawake hao wamejikuta katika mazingira ambayo kwa wakati huo, kwa hali ya kiuchumi, kihisia na kiakili waliyokuwa nayo, hawakuona njia mbadala ila kujihusisha na biashara hiyo.
Wengine wametokea katika mazingira ya unyanyasaji wa kingono katika familia tangu utotoni. Ulimwengu wao umejengwa na jumbe zinazowaonesha kuwa hawana thamani na hakuna njia nyingine ya kuishi isipokuwa hiyo.
SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria
Sisemi kwamba huu ni uhalisia kwa wanawake wote duniani kote walio katika mazingira hayo, lakini nasema kuwa kila mwanamke aliye katika mazingira hayo ana jambo lililompelekea kufika pale.
Jamii inachangia
Na kwa kiwango kikubwa, ni lazima jamii ijitathmini kuwa ina mchango gani katika hilo. Kwani jamii iliyo na afya, iliyo na upendo, iliyo na mifumo mizuri ya uhifadhi na ukuzi, hujenga watu wa aina hiyo pia.
Lakini bila kujali waliingiaje, wanachofanya si tofauti sana na wanawake wengine. Shairi langu la Changudoa, lililopo kwenye kitabu changu Jinsi Ya Kurudi Nyumbani, na ambalo lilishindwa Tuzo ya Ebrahim Hussein mwaka 2014 linahoji, umejiuliza sana swali hili: kwa nini usafiri mbali mpaka Uchina kuleta mzigo wakati wewe mwenyewe unauzika?
Unawapita machangudoa waliosimama barabarani usiku wakiwa wamejiachia, midomo yako inawatukana, unawaambia hukumu ya jehanamu inawawangojea. Lakini moyo wako unawaonea gere kwa ujasiri wao.
Angalau wao hawaogopi macho ya watu na maneno wasemayo. Wewe je? Ni lini hukupanua miguu yako ili upendwe? Ni lini hukulala kifuani pa mume wa mtu ili usikie moyo wake ukisema u wa thamani? Ni lini hukuacha kuwa na ATM kwa wakati mmoja?
SOMA ZAIDI: Wanawake Wawili Wauwawa Kikatili Zanzibar. Familia, Wanaharakati Wataka Uwajibikaji
Inasikitisha kwamba kwa kuwahukumu wanawake hawa, jamii inaruhusu udhalimu wanaotendewa na wasimamizi wa sheria wasio waadilifu ambao wanawabaka na kuwadhalilisha.
Je, kuwabaka ni sawa kwa sababu hatukubaliani na shughuli wanayofanya? La hasha! Na tena, wanawake hawa wanaendelea kubaguliwa katika kupata huduma ya afya, jambo linalozidi kuhatarisha maisha yao na jamii kiujumla.
Pia, tofauti na inavyoaminika, wao katika umoja wao, huvamia mitandao ya ‘human trafficking’ inayowaingiza watoto kwenye biashara ya ngono baada ya kuwachukua makwao kwa ahadi ya kuwapatia kazi na kuwaokoa watoto hao.
Inawezekana tusione uhusiano wowote kati ya makundi haya mawili kwa harakaharaka lakini ukweli ni kwamba, wanawake hawa wote wanajengwa au kubomolewa na jamii inayowazunguka.
Iwapo kuna ongezeko la wanawake walemavu ambao wameachwa nyuma katika shughuli za kimaendeleo, basi jamii lazima ijichunguze. Imehusika vipi kuwajenga au kuwabomoa?
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
Pia, iwapo kuna ongezeko la wanawake wanaojishughulisha na biashara ya ngono, basi jamii pia lazima ijiangalie. Nini kimewasababisha wanawake hawa kuwa katika mazingira yale? Na sasa, nini kifanyike?
Jamii siyo hakimu
Jamii siyo hakimu, bali ni sehemu ya hali ilivyo kama ilivyo na ina mchango mkubwa katika hilo. Kabla ya kunyoosha kidole kwa wengine ni lazima tujitathmini sisi wenyewe kwanza.
Na ni muhimu kwa jamii kutambua uzoefu, matamanio, mitazamo na mahusiano ya kijamii miongoni mwa wanawake na wasichana wenye ulemavu na wanawake na wasichana wanaofanya biashara ya ngono; na kuwahimiza kutumia uzoefu huu kuimarisha sauti na ushiriki wao kwenye harakati za ukombozi wa wanawake.
Japokuwa kumekuwa na kupaza sauti kwa miaka mingi, bado kuna mengi ambayo tunaweza kufanya ili ulimwengu wetu uwe jumuishi. Dunia ilivyo sasa, haijampa mwenye ulemavu kipaumbele na haswa huku kwetu Afrika. Miradi inaposanifiwa, inamkumbuka mtu aliye na ulemavu?
Barabara zinapojengwa, mbona hatuoni nafasi ya wanaokwenda kwa miguu pamoja na walio na magari maalumu ya walemavu? Ziko wapi alama za kuwasaidia walio na ulemavu wa masikio? Majengo mbalimbali, kama vile ya hospitali, sehemu za ibada, masoko, magereza, shule, nakadhalika, hayafai kwa matumizi ya watu wenye ulemavu.
SOMA ZAIDI: Vavagaa: Jukwaa la Kifeminia Linalolenga Kuondoa Dhana Zilizopitwa na Wakati
Maeneo haya bado hayana ujumuishi kwani mengi hayakumfikiria mtu mwenye ulemavu yalipokuwa yakijengwa. Ni jambo moja kusema hatuwabagui wenye ulemavu na ni jambo jingine kudhihirisha hilo katika uhalisia.
Serikali inayo wajibu wa kulitathmini jambo hili kwa umakini, na kuweka sera na miongozo madhubuti ambayo itajenga uelewa wa jamii kuhusu watu wenye ulemavu na pia itawahamasisha wanajamii kujenga jamii ambayo inawathamini watu wenye ulemavu na wengine kwenye makundi maalumu.
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.