The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uhusiano wa Kenya na Tanzania: Kwa Nini Utani ni Muhimu Katika Kujenga Ujirani Mwema?

Ukiondoa utani na mzaha, kusema ukweli Tanzania na Kenya ni zaidi ya majirani, wakitegemeana sana kwenye masuala ya uchumi na biashara na hata utamaduni.

subscribe to our newsletter!

Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia utani na kauli za mzaha baina ya Kenya na Tanzania – nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki. Utani huu umekuwa ukidhihirika zaidi kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba nchi hizi zimekua na historia ya utani na kauli za mzaha, kejeli na hata uchochezi kwa miaka mingi.

Hivi karibuni utakua umesikia kauli iliyoelekezwa kwa Tanzania isemayo, Jirani hana stima, hana dola, hana sukari, ana Kiswahili tu kutoka kwa Wakenya. Hapo awali, kulikua na kauli isemayo, Jirani hana unga, hana stima, anaongea Kiingereza kwenye giza ambayo iliaminika imetoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. 

Kwa kweli hakuna ushahidi kama Rais Samia aliwahi kweli kutoa kauli kama hiyo. Hiyo, hata hivyo, haikuwazuia Wakenya kutumia kauli hiyo kama moja wapo ya njia kushambulia sera za Rais William Ruto. Madai haya yalichochewa zaidi pale msanii Ney wa Mitego wa Tanzania alipotoa wimbo uitwao Wapi Huko ambao Wakenya walitafsiri kama unawalenga wao.

Juzi tu wakati Rais Ruto akihutubia mkutano wa viongozi wa juu wa Serikali mjini Naivasha, umeme, ama kwa jinsi Wakenya wanavyouita, stima, ulikatika. Siyo mara moja, bali mara mbili. Vyombo vya habari vya Tanzania viliripoti kwa uzandiki na kwa namna ya kuwananga Wakenya. 

Siyo kwamba vyombo vya habari vya Tanzania havitambui ugumu wa mgao wa umeme unaondelea nchini mwao wenyewe, bali vilifanya makusudi, vikichochea utani dhidi ya majirani zao, Wakenya. Kama nilivyotangualia kusema hapo awali, nchi hizi mbili zimekua na historia ya utani tangu zipate uhuru wao kwenye miaka ya 1960.

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Kenya Umekwisha. Tanzania Imejifunza Nini?

Katika sanaa kama vile maigizo, ushairi, tamthilia na hata riwaya, utani ni sehemu ya ubunifu unaoimarisha simulizi na fasihi kwa ujumla. Katika fasihi ya anthrolopolojia na utafiti wake, utani unafasiri utambulisho kama vile wa kikabila, wa rangi, wa kitamaduni, na hata wa lugha.

Utani pia umekuwa ukitumika kuchagiza uhusiano mwema, ujirani, udugu na hata kuimarisha umoja wa kitaifa hasa kwenye muktadha wa nchi zilizokuwa na mataifa au makabila mengi.

Historia ya taharuki

Kwa muda mrefu sasa, Kenya imejinasibu kama nchi yenye maendeleo kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki. Mara baada ya kujipatia uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1963 Kenya, tofauti na jirani zake, ilifuata mfumo wa kibepari na kuimarisha uhusiano wake na nchi za Magharibi. 

Tanzania, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, iliamua kufuata sera ya Ujamaa ambayo ilitilia mkazo utaifishaji na kujitegemea. Ukiondoa mfumo wa kiuchumi, sera ya Ujamaa ilijikita sana kwenye utu wa binadamu tofauti na sera ya kibepari. 

Kenya, chini ya Rais Jomo Kenyatta, ilijiimarisha kichumi na kuna minong’ono kwamba Mwalimu Nyerere aliwahi kuwaambia Watanzania kwamba wakitaka kuona nchi iliyoendelea, siyo lazima waende London, Uingereza bali wafike tu hapo Nairobi, mji mkuu wa Kenya. 

SOMA ZAIDI: Theresia Dismas: Mwanamichezo wa Kwanza Kuipatia Tanzania Medali ya Kimataifa

Kwa wakati ule, Nairobi ilikua fahari ya Afrika Mashariki na pengine Afrika Mashariki na kati. Kwa upande wake, Tanzania ilisifika kama nchi mfano kwani ilijenga taifa lenye umoja na mshikamano. Ila kulikua na uhasama wa chini chini baina ya nchi hizi mbili. 

Kuna uvumi kwamba Mwalimu Nyerere aliwahi kuizodoa Kenya kwa kusema ni nchi ya wala watu, au man-eat-man society kama wanavyosema kwa kimombo, kutokana na mfumo wake wa kibepari. Naye Rais Kenyatta alijibu kwa kuiita Tanzania nchi ya watu wasiokula chochote, au man-eat-nothing country!

Mivutano na vita baridi ilisababisha kuvunjika kwa Jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Mwaka huo huo, Tanzania ilitangaza kufunga mipaka yake na Kenya.

Licha ya kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili kwenye miaka ya 1990, ushindani na kauli za kubezana zilizidi. Hata pale Jumuiya ya Afrika Mashariki ya pili ilipozinduliwa upya, Tanzania, hasa kwa macho ya Wakenya, ilionekana kama kikwazo katika ujenzi wa umoja wa kikanda. 

Historia hii ya taharuki na kutiliana mashaka ilionekana kwenye utawala wa Rais Benjamin Mkapa na Rais Daniel Moi, Rais Jakaya Kikwete na Rais Moi, Kikwete na Rais Mwai Kibaki na kwa Rais John Magufuli na mwenzake Uhuru Kenyatta. 

SOMA ZAIDI: Uchaguzi Tanzania 2024 Na 2025: Tuna Nini Cha Kujifunza Kwa Majirani?

Itakumbukwa mwaka 2013, Kenya, Uganda na Rwanda ziliungana kwenye mradi wa miundombinu katika kile walichokiita muungano wa walio tayari, au coalition of the willing na kuiacha Tanzania pamoja na Burundi. Wakati wa utawala wa Rais Magufuli, uhasama ulizidi pale alipoagiza kuchomwa kwa vifaranga vya kuku kutoka Kenya mwaka 2017. 

Kilichofuata ni malumbano ya nani zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Wakenya, kwa upande wao, waliwaponda Watanzania kwa kitendo hicho, wakianzisha kampeni kwenye mtandao wa kijamii wa X, zamani Twitter, ya #SomeoneTellTanzania na kuwazodoa Watanzania kwamba hawajui Kiingereza.

Utani mpya

Lakini katika siku za hivi karibuni, utani baina ya Kenya na Tanzania umechukua sura mpya na ya tofauti kidogo. Katika mkutano mmoja jijini Dar es Salaam, Rais Samia alimtania mwezake wa Kenya, Ruto, kwa jinsi Wakenya wanavyozungumza Kiswahili ambacho ni tofauti na Tanzania. 

Naye mwandishi mashuhuri wa Kenya, Larry Madowo, ambaye alikua mshereheshaji katika hafla hiyo, alichagiza utani huo kwa kudokeza kwamba Wakenya wanazungumza na Watanzania kwa Kiswahili kibaya na Watanzania wanajibu kwa Kiingereza kibaya. Mkutano mzima uliangua kicheko, katika hali ambayo wengi wanakubali kwamba ni kiashiria muhimu cha kuimarisha uhusiano mwema baina ya nchi na nchi.

Ukiondoa utani na mzaha, kusema ukweli Tanzania na Kenya ni zaidi ya majirani. Mataifa haya mawili yanategemeana sana kwenye masuala mbalimbali, ikiwemo uchumi na biashara, na utamaduni. Mabadiliko haya ya utani usioumiza yanategemewa yataimarisha sana uhusiano baina ya nchi hizi mbili. 

SOMA ZAIDI: Watanzania na Kilio cha Samaki Kwenye Maji Katika Kiswahili

Sehemu kubwa ya utani huu unatokana na uzungumzwaji wa Kiswahili katika nchi hizi mbili. Kuna kuelewana kwa kiasi kikubwa baina ya Kenya na Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kama utani huu mpya utaendelea, basi uhusiano huo nao utaimarika. 

Nicodemus Minde ana Shahada ya Uzamivu kwenye mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani – Afrika, Nairobi, Kenya. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia nminde96@gmail.com au X kama @decolanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ninakuunga mkono na makala yako kuhusu mahusiano kati ya Tanzania na Kenya ambazo zinaongoza Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *