The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bob Marley: One Love Itufikirishe Umuhimu wa Kuwekeza Kwenye Filamu

Mwaka 1960, Tanzania ilikuwa na majumba 48 ya filamu wakati idadi ya watu ilikuwa milioni tisa tu na sasa tuna majumba tisa wakati idadi yetu ni milioni 63. Inawezekana vipi hii?

subscribe to our newsletter!

Siku ya wapendanao mwaka huu, au Valentine Day kama siku hiyo inavyoitwa, hapo Februari 14, nilipata mapenzi ya nguvu baada ya kualikwa kuitazama filamu inayohusu maisha ya msanii maarufu wa miondoko ya reggae duniani, Bob Marley, iliyopewa jina la Bob Marley: One Love.

Filamu hii iliyoonyeshwa duniani kwa mpigo siku hiyo ya wapendanao inakadiriwa kugharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 70. Kwa muktadha tu, Tanzania: The Royal Tour iligharimu Dola za Marekani milioni mbili tu. Hiyo inakueleza mengi kwenye uwekezaji unaotakiwa kwenye kutengeneza kazi za sanaa zenye kuacha alama.

Siku ya kwanza filamu hii ya Bob Marley: One Love iliporudishwa kwenye majumba ya sinema iliingiza Dola za Marekani milioni 14 kutoka kwenye kiingilio tu, au Box Office kama wasemavyo wenyewe. 

Mpaka kufikia Februari 22, filamu hii ilikuwa imeingiza Dola za Marekani milioni 80.  Filamu hii imezalishwa na Ziggy Marley, mtoto wa hayati Bob Marley, na kutengenezwa na studio za Paramount Pictures, kule Rais Samia Suluhu Hassan alikotembelea mwaka 2022. Filamu ya Bob Marley: One Love ilishutiwa mjini London na kule Jamaica.

Moja ya zawadi ambayo Afrika Mashariki iliwahi kumpatia Robert Nesta Marley wakati wa uhai wake, na Jamaica kwa ujumla, ni tamaduni ya nyimbo za jadi kutoka katika kabila la Nande ambapo mwanamke wa shoka, au legendary mother of abundance kwa kimombo, huchezewa ngoma na watu waliomzunguka ijulikanayo kama Nyabinghi

SOMA ZAIDI: Tafakuri Fupi Kuhusu Filamu ya Tanzania: The Royal Tour

Watumwa waliofika Jamaica enzi hizo waliendeleza utamaduni huu, hasa Rastafarians, kama ulivyotukuzwa na Bob Marley katika wimbo wa Jump Nyabinghi uliotolewa mwaka 1983 ambao msanii huyo aliyeaga dunia hapo Mei 11, 1983, aliuimba na bendi ya The Wailers.

Tunakumbuka simulizi kutoka nchini Zimbabwe kuwa Julius Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania, alipokutana na Bob katika jukwaa siku ya uhuru wa taifa hilo la kusini mwa mwa Afrika, wawili hao hawakuiva kabisa. 

Hata hivyo, baada ya Bob kutumbuiza baadhi ya vibao vyake katika hafla hiyo, kama vile Zimbabwe na Afrika Unite, Mwalimu alikoshwa sana kiasi ya kusimama na kumshangilia Bob.

Ilikuwa ni baada ya Mwalimu kurudi kutoka ziara yake hii ndipo aliamua kutoa heka 1,000 za ardhi kule Kigoma kwa ajili ya Rastafarians na Waafrika waliotaka kurudi kutoka “utumwani” sehemu mbalimbali za dunia. Historia hii ilikuwa kichwani mwangu wakati wote nilipokuwa naitazama Bob Marley: One Love na kutafakari masuala kadhaa.

Maendeleo ya filamu

Moja kati ya masuala haya ni mkazo tunaoweka, kama nchi, kwenye filamu na uhimu wake katika kuweka kumbukumbu zetu kama taifa. Hebu fikiria hii: mwaka 1960 nchi yetu ilikuwa na majumba 48 ya filamu wakati idadi ya watu ilikuwa milioni tisa tu na sasa tuna majumba tisa wakati idadi yetu ni milioni 63. Inawezekana vipi hii?

SOMA ZAIDI: Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?

Kufikia mwaka 1989, wakati sekta ya filamu iliposambaratika, Tanzania ilikuwa na majumba 54 ya filamu, hii ilikuwa idadi kubwa kabisa kuliko nchi zote za Afrika ukiiondoa Afrika Kusini. Kwa sasa, jiji la Nairobi, Kenya peke yake lina majumba mengi ya filamu kuliko Tanzania yote! 

Kwa lugha rahisi unaweza kusema hakuna miundombinu ya filamu Tanzania. Hakuna mfumo wa usambazaji, hakuna shule za mafunzo, wala hakuna sera ya taifa ya filamu. Mwaka 2023, tulizuiwa kufanya mkutano wetu na kuonywa kwa barua na Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kuacha mara moja kuzungumzia sera ya filamu. 

Sera iliyopo ya utamaduni siyo tu haizungumzii kabisa filamu bali haina hata neno filamu ndani yake! Sheria yetu ya udhibiti ya 1976 pia nayo imepitwa na wakati.

“Watu wengi wanafikiri kwamba mungu mkubwa atakuja kutoka mbinguni, kuchukua kila kitu, na kumfanya kila mtu ahisi amelewa,” Bob Marley anaimba kwenye wimbo chake Get Up, Stand Up. “Lakini kama unajua thamani ya maisha, ungetafuta thamani yako hapa duniani, na kuanza kuuona mwanga, na kupigania haki yako.”

SOMA ZAIDI: Je, Serikali Inaifahamu Dhana ya Utamaduni Anuai?

Sisi Watanzania lini tutaanza mchakato wa kutafuta thamani yetu hapa duniani? Je, lini tutatumia watu wenye maarifa kututengenezea mpango mkakati wa kitaifa? Je, lini tutaunda chombo cha maendeleo ya filamu, kwa mfano, kwa sababu kwa sasa hatuna?

Tunafahamu kuwa Bodi ya Filamu iliundwa kudhibiti na siyo kuendeleza filamu. Ipo haja ya kutofautisha vyombo vya maendeleo na vile vya udhibiti, au censorship kama wasemavyo wenyewe. Majirani zetu Wakenya wametuonyesha mfano kwa kuunda Tume ya Filamu ya Kenya (KFC) ambayo ni tofauti na Bodi ya Uainishaji Filamu ya Kenya (KFCB).

Hapa Tanzania tumebarikiwa kuwa na maeneo mazuri ya kutengeneza filamu. Ni wakati sasa wa kutengeneza mpango wa kuyatumia. Tumejaaliwa hadithi nyingi na utamaduni uanuai, ambavyo vyote ni ‘mgodi’ mkubwa unaoweza kuzalisha filamu lukuki kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadaye.

Kwa kumalizia, mnamo mwaka 2022, muigizaji mmoja wa Kitanzania aitwaye Samia Suluhu Hassan alicheza filamu ya Tanzania: The Royal Tour na baada ya hapo, mwaka ulofuata, 2023, ikatangazwa kwamba atacheza filamu nyingine, Kijiji cha Milele, aliyoicheza na muigizaji maarufu wa nchini China, Jin Dong.

Pengine, kutokana na mapenzi yake makubwa aliyonayo kwa filamu, muigizaji huyu ameshagundua changamoto nyingi zinazowakabili wanafilamu wenzake wa hapa Tanzania. Chondechonde, tafadhali, mkimuona mwombeni awe Nyabinghi wetu.

Robert Mwampembwa ni msanii, mwandishi na Mkurugenzi wa Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT). Kwa maoni, anapatikana kupitia ‎robert@ubunifu.co.tz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *