The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mashirika ya Umma Yanayotengeneza Hasara Yamilikishwe kwa Wafanyakazi Wao

Hii inaweza kuwa njia imara ya kufanikisha lile ambalo Serikali imeshindwa kulifanikisha mpaka sasa: kusimamia uwajibikaji kwenye mashirika haya na kuyafanya yazalishe faida badala ya hasara.

subscribe to our newsletter!

Hadaa moja kubwa ya itikadi, au falsafa, ya uliberali, itikadi ambayo imekuwa ikitawala dunia, na hata Tanzania, tangu kuisha kwa vita baridi, ni kwamba demokrasia ni nzuri lakini ikitekelezwa tu katika nyanja ya kisiasa, na siyo vinginevyo.

Kwamba demokrasia, angalau ile ya kiliberali, yaani hii tuliyonayo hapa Tanzania, ni mfumo mzuri wa kuendesha nchi – uwepo wa vyama vingi vya siasa, chaguzi za mara kwa mara, utawala bora, na kadhalika – lakini hatuwezi kutumia mfumo huo huo kuendesha taasisi, au kampuni, yenye lengo la kutengeneza faida.

Na ‘demokrasia’ hapa ina maana ya mfumo wa kiutawala unaowapa watu, iwe wananchi au wafanyakazi, mamlaka ya kuendesha maisha yao wenyewe kadiri wanavyoona inafaa kwa ustawi wao wenyewe na ule wa vizazi vyao vinavyokuja. Kwa kifupi, ‘demokrasia’ hapa ni mfumo unaowaruhusu watu kujitawala badala ya kutawaliwa.

Ukinzani huu wa kimantiki unaacha maswali mengi sana. Kwa mfano, kama uliberali unaamini uwepo wa uhusiano kati ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi ya nchi fulani, uhusiano ambao hata mimi naamini upo, iweje uhusiano huo usiwepo kati ya kampuni kuendeshwa kidemokrasia na uwezekano wa kampuni hiyo kutengeneza faida zaidi?

Kwa nini demokrasia iwe na manufaa katika ngazi ya kitaifa, kijimbo, kikata na kimtaa, au kijiji, ngazi ambazo kwa hapa kwetu ndiyo tumekuwa tukishiriki kwenye kuchagua wawakilishi, lakini isiwe na manufaa katika sehemu za kazi, sehemu ambazo, kama wafanyakazi, tunatumia muda mwingi zaidi wa maisha yetu?

SOMA ZAIDI: Wafanyakazi Wanaogoma Sahara Media Waeleza Masaibu Yao

Kimsingi, demokrasia ina manufaa makubwa sana endapo kama itatekelezwa katika sehemu za kazi. Magwiji wa masuala ya usimamizi wa kibiashara wanabainisha, pasi na shaka yoyote, kwamba utendaji kazi wa wafanyakazi katika kampuni fulani huongezeka maradufu pale wafanyakazi hao wanapohisi kuwa sehemu ya kampuni husika.

Kuna mengi yanaweza kufanyika kuwapa wafanyakazi hisia hii ya umiliki, moja ikiwa ni kuwaomba maoni na ushauri wao kwenye uendeshaji mzima wa kampuni, pamoja na kuwapatia mrejesho wa kweli, siyo wa kijanjajanja, juu ya mwenendo wa kampuni yao, ikiwemo utengenezaji wa faida na hasara.

Umiliki halisi

Lakini kama kampuni inaweza kufanya vizuri sokoni kwa wafanyakazi wake kuwa na “hisia” ya umiliki, hali itakuwaje kama umiliki utakuwa “halisi” badala ya kuwa wa kihisia tu? Kampuni itakuwa na hali gani kama itaendeshwa kidemokrasia? Kwa lugha nyepesi, kampuni itafanyaje sokoni kama wamiliki wake watakuwa ni wafanyakazi wake?

Jibu rahisi ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kampuni hiyo kufanya vizuri zaidi sokoni ukilinganisha na ile inayomilikiwa na mtu binafsi. Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya kampuni kumilikiwa na wafanyakazi na kampuni hiyo kufanya vizuri zaidi kiuzalishaji na uhai wake.

Wafanyakazi kumiliki kampuni zao wenyewe ni suala linalozidi kupata umaarufu ulimwenguni kote, husuan katika mazingira ambayo uhakika wa kazi unatishiwa na maendeleo makubwa ya kiteknolojia, kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na masikini, na mdororo mkubwa wa ustawi wa wafanyakazi ulimwenguni kote.

SOMA ZAIDI: Haya ni Baadhi ya Madhila Wanayopitia Wafanyakazi wa SBC Tanzania

Nchini Tanzania, wafanyakazi kumiliki kampuni zao siyo jambo linalotiliwa mkazo sana, iwe na watunga sera au hata wachumi na washauri wengine wa maendeleo. Hapa nchini, ni kampuni imilikiwe na dola, yaani Serikali, ambayo haina maana sawa na kumilikiwa na wafanyakazi, au imilikiwe na ‘mwekezaji,’ yaani mtu binafsi mwenye mtaji wa kufanya hivyo.

Katika mazingira ambapo kampuni iliyokuwa ikimilikiwa na Serikali inafanya vibaya sokoni, kwa mfano inashindwa kutoa huduma kama inavyotegemewa, suluhu kubwa inakuwa ni kuibinafsisha hiyo kampuni kwa kumpa ‘mwekezaji.’ Wazo la kuibinafisha kwa wafanyakazi wake linakuwa halipo mezani.

Serikali imekuwa ikifanya hivi mara zote tangu wimbi la ubinafsishaji lianze nchini hapa chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi, ikipata ukinzani hafifu sana kutoka kwa wananchi. Mfano wa hivi karibuni kabisa ni hatua ya Serikali kutaka kumpa ‘mwekezaji’ mradi wa mabasi yaendayo kasi kufuatia malalamiko ya kushindwa kutoa huduma ipasavyo.

Kabla ya hata kuanza kwa wimbi la ubinafsishaji, wazo la wafanyakazi kumiliki kampuni zao halikuwahi kumvutia hata Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, aliyependelea zaidi dola, au Serikali, kumiliki makampuni ya biashara. Hii ni moja kati ya hoja ambazo Walter Rodney, mwanazuoni wa Kiguyana, anabainisha kwenye insha yake ya mwaka 1980 kuhusu ukinzani wa kitabaka nchini Tanzania.

Majaribio

Lakini hii haimaanisha kwamba hakujawahi kuwa na majaribio ya wafanyakazi, au wananchi, kujikusanya wenyewe na kuendesha kampuni zao, au jamii zao, bila ya utegemezi wa ‘mwekezaji’ yoyote. Ingawaje ni kwa kiwango cha chini, Umoja wa Madereva na Makondakta Dar es Salaam—Msata (UMAMADARMS), ni moja ya jitihada za wafanyakazi kumiliki kazi zao bila ya uhitaji wa ‘bosi.’

SOMA ZAIDI: Rostam Aziz Adaiwa Kushikilia Zaidi ya Bilioni Tatu za Mafao ya Wafanyakazi Wake wa Zamani 

Historia ya Jumuiya ya Maendeleo ya Ruvuma, au Ruvuma Development Association (RDA), pia inatoa fundisho la uwezekano wa wananchi kuja pamoja na kujitafutia maendeleo yao wenyewe bila kutegemea wanasiasa au ‘wawekezaji.’ 

Ikianzishwa kwenye miaka 1960, RDA ilikuwa hadithi nzuri ya kile kinaweza kutokea pale wananchi wakiunganisha nguvu zao kutatua changamoto zao, ikafanikiwa sana mpaka kuitisha Serikali iliyoamua kuipiga marufuku hapo mwaka 1969! Historia hii inatufundisha kuhusu kile tunachoweza kufanya katika kutatua changamoto zetu za sasa.

Kwa mfano, katika wakati ambapo mashirika kadhaa yanayomilikiwa na Serikali, kama vile Shirika la Ndege, Shirika la Reli, Shirika la Simu, na mengineyo mengi, yakiripotiwa kutengeneza hasara za mabilioni ya shilingi kila mwaka, licha ya kupatiwa ruzuku na Serikali, tunaweza kufikiria kuyabinafsisha mashirika haya kwa kuyamilikisha kwa wafanyakazi wake?

Mpaka sasa, Serikali, inayohusika na kuyapatia mashirika haya viongozi na menejimenti zao, ikiwa  kama mmiliki wao, imeshindwa kusimamia uwajibikaji kwenye mashirika haya, hali inayompelekea Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuripoti hasara zinazotengenezwa na mashirika haya mwaka hadi mwaka.

Imefikia hatua sasa mpaka Rais Samia Suluhu Hassan amepoteza hamu ya kuzungumzia hasara hizi, akigoma kabisa kutia neno wakati akipokea taarifa hizo kutoka kwa CAG hapo Machi 28, 2024, katika Ikulu ya Chamwino. Kwa Serikali, chaguzi ni mbili tu: Serikali, au dola, iendelee kumiliki mashirika haya, au yapewe ‘mwekezaji.’

Tupanue wigo

Ushauri wangu mimi ni kwamba tupanue wigo wa chaguzi zilizopo kwa kujumuisha ile ya wafanyakazi wa haya mashirika wayamiliki ili wayaendeshe kidemokrasia, ikiwemo kusimamia uwajibikaji wa viongozi na menejimenti zao, jukumu ambalo mpaka sasa Serikali imeshindwa kulitekeleza. 

SOMA ZAIDI: Nini Kimeua Uandishi wa Habari za Wafanyakazi Tanzania?

Kama wafanyakazi watawajibika kuchagua viongozi wa mashirika hayo, viongozi hao watawajibika kwa wafanyakazi, ikiwemo kuondolewa kwenye nafasi za uongozi, hali ambayo itakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kuongezeka kwa ufanisi katika uendeshaji wa mashirika hayo.

Bila shaka, kama Serikali itaamua kutekeleza ushauri huu itapaswa kuunda timu yake ya wataalamu kuutathmini kwa kina na kushauri namna bora ya kuutekeleza. Timu hiyo inaweza kutembelea nchi chache zenye kutekeleza utaratibu huu, kama vile Spain, ambako Shirika la Mondragon limekuwa likipigiwa mfano kama hadithi nzuri ya wafanyakazi kumiliki kampuni zao.

Timu hiyo ya wataalamu pia inaweza kutathmini maeneo ya uhitaji ili utaratibu huo utekelezeke vizuri, ikiwemo elimu kwa wafanyakazi itakayowafanya watambue wajibu wao kama mabosi-wafanyakazi, lakini pia namna bora wanaweza kuendesha operesheni za kampuni chini ya utaratibu huo mpya. 

Mahitaji mengine yanaweza kuwa ya kimtaji ambao Serikali inaweza kuwasaidia wafanyakazi kuupata, ikiwemo kutoka katika taasisi za kifedha zilizopo nchini. Kama Serikali inaweza kutoa ruzuku kwa mashirika yanayotengeneza hasara kila mwaka, itashindwa vipi kufanya hivyo hivyo kwa mashirika yanayomilikiwa na wafanyakazi?

Mashirika haya kumilikiwa na wafanyakazi wao, hata hivyo, haitoi uhakika wa mashirika hayo kufanya vizuri na kuacha kutengeneza hasara; bado yatapaswa kukabiliana na changamoto zilizopo katika soko na mafanikio yao yatatokana na namna yatakavyokabiliana na changamoto hizo.

SOMA ZAIDI: Changamoto na Haki za Wafanyakazi wa Majumbani

Hata hivyo, ushahidi unaonesha kwamba manufaa yanayotokana na wafanyakazi kumiliki kampuni zao, hususan kwenye eneo la maslahi na ustawi wa wafanyakazi, yanayapiku yale yatokanayo na kampuni kumilikiwa na mtu binafsi. 

‘Mwekezaji’ anaweza kuwa tayari kuleta mashine kiwandani inayoweza kupoteza kazi za wafanyakazi kumi au zaidi kama sehemu ya mikakati yake ya kujikusanyia faida zaidi. Wafanyakazi, ambao ni wamiliki, wanaweza kuleta mashine hiyohiyo ili wafanye kazi masaa machache zaidi na kupata muda wa ziada kufanya vitu wanavyovipenda zaidi.

Wazo ni kuipeleka demokrasia katika sehemu ya kazi, wazo ambalo itikadi ya uliberali inalipinga vikali, ikijua kwamba uamuzi huo utachochea anguko la mfumo wa kiuchumi unaotoa kipaumbele kwenye kujilimbikizia faida kwa hasara ya mamilioni wengine, ukiwaacha wafanyakazi, na jamii wanamoishi, kwenye dimbwi kubwa la umasikini.

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Njia za uzalishaji kukabidhiwa kwa wananchi, wafanyakazi wenyewe ni tumaini katika kujenga taifa lenye uchumi imara. Makala nzuri Comrade Tony

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *