The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wananchi Goba Walilia Dampo Bubu Liendelee Kukaa Kwenye Makazi Yao

Wananchi wanadai taka hizo huzuia mmomonyoko wa ardhi, CAG ashangaa, akitahadharisha athari za kiafya.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. “Umekuja hapa kufanya nini? Umeambiwa hapa kuna changamoto gani? Nani aliyekuelekeza kuwa huku kuna matatizo, nitajie huyo mtu.” Haya yalikuwa ni maswali niliyokutana nayo mara tu baada ya kufika mtaa wa Majengo, uliopo kata ya Goba, jijini Dar es Salaam, nilipofika kwa ajili ya kufuatilia habari hii. 

Maswali hayo yalitoka kwa mama mmoja aliyekuwa amevalia kaptula yenye rangi nyeusi na ndala kuukuu miguuni, akioneshwa kushtushwa na taarifa za mwandishi wa habari kufika kwenye eneo la dampo lililopo nje ya nyumba yake. 

Ilikuwa ni Jumatatu ya Mei 14, 2024, majira ya saa sita mchana nilipofika katika eneo hilo mara baada ya kupata taarifa kuwa sehemu hiyo iliyopo pembezoni mwa Mto Tegeta imegeuzwa kuwa dampo bubu.

Baada ya kujitambulisha vizuri, mama huyo alitulia, akakubali kunisikiliza tukiwa kwenye kivuli, pembezoni mwa nyumba yake pamoja na wananchi wengine. Nikamueleza kuwa suala la lile dampo ndiyo limenifikisha pale, nikimuomba anieleze kuhusiana nalo na akakubali, lakini kwa sharti la kutonukuliwa jina na kutopigwa picha yeye pamoja na nyumba yake. 

Mama huyo alinieleza kuwa eneo lao lipo bondeni, lakini pia pembezoni mwa mto. Hivyo, kadri siku zinavyozidi kwenda, maporomoko ya maji ya mvua yamekuwa yakimega sehemu za ardhi, hali ambayo imekuwa ikipelekea sehemu za nyumba zao kubomoka. 

SOMA ZAIDI: Ujenzi wa Barabara kwa Hisani ya Watu wa Goba Wazua Gumzo Dar

Akanionesha sehemu ya mbele ya dampo iliyokuwa karibu na mto, mama huyo akanieleza kuwa eneo hilo palikuwa na majirani zake wawili ambao nyumba zao na viwanja vyao kwa sasa havipo baada ya ardhi iliyokuwepo hapo kuondolewa na maporomoko ya maji, jambo lililowalazimu wahame. 

Eneo la mto ambapo takataka zinamwagwa

Maporomoko hayo yaliendelea kumega ardhi na nyumba yake pia haikuachwa salama, baadhi ya vyumba vikabomolewa. Mama huyo akanieleza kuwa ikambidi afikirie namna ya kujinusuru na hali hiyo, ndipo ambapo alipata wazo wa kutumia taka zitakazomwagwa nje ya nyumba yake na kandokando ya mto ili kuzuia maji yasiendelee kumega ardhi. 

Ilimlazimu kuanza kutafuta sehemu ambazo taka zitapatikana ili ziweze kwenda kumwagwa pale, kitu ambacho anadai kuwa hakikuwa rahisi kukipata, hata alipokwenda Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuomba ruhusa ya magari ya taka yaelekezwe kumwaga hapo, hakuruhusiwa.

Aliendelea kupambana na akafanikiwa kupata magari ya taka ambayo yalikubali kwenda kumwaga taka katika eneo hilo ambalo si rasmi; taka ambazo anaeleza kuwa zikijishindilia vizuri zinailinda nyumba yake dhidi ya athari za mmomonyoko wa ardhi uliokuwa unaendelea. 

Hali ya eneo hilo haikuwa ya kuridhisha kwa sababu imezungukwa na taka za kila aina, panya wakubwa nao wanaonekana wakizurura hapo. Jambo hilo lilinifanya nimuulize mama huyu kama anaona kuwa suala la kumwagwa taka katika eneo hilo ni sahihi kwa afya zao, na akanieleza kuwa suala la afya halina shida kwa sababu wanatibu taka hizo baada ya kumwagwa. 

Nahitaji gari 20

Josephat Abel ni mmoja kati ya wakazi wa eneo hilo ambaye yeye alikubali kuzungumza na mwandishi na kunukuliwa utambulisho wake. Nyumba yake kwa sasa ipo hatarini kubomoka baada ya mvua zilizonyesha hivi karibuni kubomoa sehemu ya kiwanja chake, hali ambayo inamfanya kuishi kwa mashaka.

SOMA ZAIDI: Wanawake Wanavyotumia Takataka Kujipatia Kipato

Abel anaeleza kuwa ili kuinusuru nyumba yake anahitaji takribani magari 20 ya taka yafike kwenye eneo lake na kumwaga taka, kitu ambacho kwa siku za hivi karibuni kimeshindwa kufanyika baada ya mvua zilizonyesha kuharibu barabara, hivyo kuzuia magari hayo kufika kwenye eneo lake. 

Nyumba zilizoboka katika eneo hilo kutokana na maji ya mto kuzipiga

“Tuliomba uongozi utuletee taka hapa, kama unavyoona palikuwa na mmomonyoko, udongo wenyewe ni wa mchanga,” Abel anasema. “Taka kavu zikishajishikilia chini haziondoki, wala maji yakija hayaondoi. Kwa hiyo, kama wanaweza wakatusaidia kutuletea taka kama mwanzoni, angalau tunaona inaweza ikatusaidia.”

Baadhi ya viongozi wa mitaa iliyopo ndani ya kata ya Goba walinieleza kuwa madampo bubu yaliyoanzishwa kwenye kata hayapo tu kwenye mtaa wa Majengo. Walinieleza kuwa madampo hayo yanayozinusuru na mmomonyo kaya nyingi pia yako kwenye mitaa ya Kinzudi, Kunguru, Muungano na Matosa. 

Viongozi hao ambao hawakuwa tayari majina yao kunukuliwa kwenye habari hii walinieleza kuwa wanakubaliana na uanzishwaji wa madampo hayo kwani umekuwa msaada kwa wananchi, lakini suala hilo haliwezi kupewa kibali cha kufanyika kwa uhalali. 

Waliongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imekuwa ikipinga vikali vitendo vya kuanzishwa kwa madampo hayo kwa sababu eneo rasmi kwa ajili ya kutupa taka ndani ya jiji la Dar es Salaam ni dampo la Pugu Kinyamwezi, lililopo ndani ya Halmashauri ya Ilala. 

CAG ashangazwa

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023, ililitaja eneo la Majengo kuwa na dampo bubu ambalo linakusanya taka mbalimbali za barabarani na kwenye masoko mbalimbali yaliyopo kwenye halmashauri ya manispaa ya Ubungo. 

SOMA ZAIDI: Hali ya Uchafu Mbeya Yazisukuma Mamlaka Kuibuka na Mikakati Mipya

CAG alionesha kutoridhishwa na hali hiyo kwa sababu dampo hilo linachafua mazingira na kuhatarisha afya za kaya zilizopo katika eneo hilo. 

“Wakati wa ziara ya kutembelea eneo hilo, nilibaini magari mawili, moja likiwa mali ya taasisi binafsi na katika hali ya kushangaza lingine lilikuwa mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, likiwa na taka zisizofunikwa karibu na eneo hilo la kuhifadhi taka lisiloidhinishwa tayari kutupa taka.

“Pia, nilibaini kuwa kila gari la kubeba taka limekuwa likitozwa Shilingi 5,000 kwa safari. Fedha hiyo hulipwa kwa mmiliki wa eneo karibu na mto kama ada ya kuhifadhi taka, licha ya kutokuwa na idhini ya kukusanya ada hizo,” alisema CAG Charlse Kichere kwenye ripoti hiyo. 

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *