Mwanza. Takriban wananchi saba kutoka vijiji vya Diloda na Golimba, wilayani Hanang, mkoani Manyara wanalazimika kuripoti polisi angalau mara moja kwa mwezi baada ya polisi wilayani humo kuwahusisha na madai ya uhujumu uchumi kutokana na hatua yao ya kukosoa utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Taarifa zilizoifikia The Chanzo zinaeleza kwamba polisi waliwakamata wananchi hao, wote wakiwa ni wanaume, mnamo Machi 11, 2024, katikati ya harakati za wananchi za kudai fidia stahiki kutokana na kuchukuliwa kwa ardhi yao kupisha ujenzi wa bomba hilo la mafuta kutoka nchini Uganda linalokosolewa vikali na baadi ya wananchi na wanaharakati wa mazingira.
Kupitia mahojiano iliyofanya na wananchi takriban kumi walioathiriwa na mradi huo, The Chanzo iligundua kwamba wananchi wana malalamiko mengi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo, kubwa lao likiwa ni lile la kupunjwa kwa malipo wanayostahiki kupatiwa, na kusumbuliwa na polisi wanapoibua madai hayo kwa mamlaka husika.
“Tumepewa kesi ya uhujumu uchumi, na hapa tunalazimika kwenda kuripoti polisi kila baada ya muda fulani,” alisema mmoja wa wananchi hao ambaye The Chanzo imeamua kuficha jina lake kulinda usalama wake. “Hii siyo sawa, simu zetu zimechukuliwa tangu mwezi wa tatu. Ni mbali sana kule, unatumia nauli ya Shilingi 16,000 kwenda. Sasa piga picha, kwa maisha yetu haya, unapata wapi Shilingi 16,000?”
“Tulipoandikishwa maelezo tulitakiwa kuwa tunaripoti kila baada ya siku moja, yaani leo unaenda, inapita siku moja, ndipo unaenda tena,” aliongeza mwananchi huyo. “Tulifanya hivyo, na tuliopata muda wa kwenda ni watu saba pekee. Sasa kuanzia hapo tunaandamwa mpaka leo.
“Tunamshukuru Mungu yule askari ametuhurumia, sasa hivi anatupa muda mrefu kidogo, sasa hivi tumeambiwa turipoti baada ya mwezi mmoja, japo tunatamani jambo hili liishe.”
Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Hanang, Amina Kahando, alikataa kulitolea ufafanuzi suala hili kwa njia ya simu, akimtaka mwandishi afike ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo ya ana kwa ana. Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Almishi Issa Hazali, alisema halifahamu suala hilo kwani yeye ni mpya wilayani hapo, akiahidi kulifuatilia.
Malipo duni
Wananchi kutoka katika vijiji hivyo vya Diloda na Golimba wameiambia The Chanzo kwamba Serikali imekuwa ikiwalipa malipo yasiyoendana na thamani halisi ya ardhi zao wanazopaswa kuziacha kupisha ujenzi wa bomba hilo la mafuta ambalo Uganda na Tanzania wanalitegemea kutengeneza ajira zaidi 30,000.
Wananchi wanaeleza kuwa walilipwa kwa tathmini ya miaka ya nyuma na kupelekea kulipwa Shilingi 300,000 kwa ekari moja, jambo ambalo wanasema siyo sawa hata kidogo.
“Watu hapa wanauziana ekari moja kuanzia Shilingi 500,000 hadi Shilingi milioni moja milioni huko, lakini sisi tumelipwa Shilingi 300,000,” alisema mmoja wa wananchi ambaye The Chanzo imeamua kuficha jina lake kwa sababu za kiusalama. “Ndiyo, tumeshasaini mkataba, lakini Serikali ingeliangalia hilo itusaidie. Kiukweli sisi tupo tayari mradi upite, lakini watuzingatie kwenye hili.”
SOMA ZAIDI: Utata Leseni Ya Uchimbaji Madini Serengeti Kwenye Maeneo ya Wananchi. Afisa Adai Sio Lazima Kuwashirikisha
Mwananchi mwingine alidai kwamba Serikali haikuwaeleza wananchi ukweli wote, akiishutumu kwa kushindwa kuwaeleza wananchi athari hasi za kibnaamu na kimazingira zinazoweza kutokana na ujenzi wa bomba hilo.
“Alikuja Mzungu hapa na Mwafrika mmoja, akaitisha kikao na watu ambao mashamba yao yalipitiwa na mradi,” alisema mwananchi huyo tuliyeamua kutotaja jina lake. “Huyu alitupa faida na hasara za mradi, na baada ya wale watu kuondoka ndipo tulipokea wito na kupewa kesi ya uhujumu uchumi.”
“Sisi tulijua ni watu wa mradi kwa sababu wamekuwa wakija hapa mara nyingi, tulimsikiliza na baadaye tulipoitwa kwa mkuu wa wilaya tuliambiwa kuwa tunafanya vikao na watu ambao hawatambuliki na Serikali,” aliongeza mwananchi huyo. “Sasa sisi tungejuaje hatambuliki? Wao [Serikali] wamfuatilie na wamzuie yeye, siyo sisi; sisi tuliitwa kama tunavyoitwa mara zote, tungejuaje hajatoa taarifa huko?”
Wapinga mradi?
Baraka Machumu ni mwanaharakati wa mazingira anayefanya kazi na GreenFaith, shirika lisilo la Kiserikali lenye makao yake makuu nchini Marekani, ambalo limekuwa mstari wa mbele kupinga ujenzi wa bomba hilo la mafuta kwa sababu za kimazingira.
Kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Machumu, ambaye amekuwa akiwaelimisha wananchi kuhusiana na athari za kimazingira zinazoweza kutokana na bomba hilo la mafuta, alisema kwamba badala ya kuwanufaisha wananchi kama Serikali inavyodai, mradi wa EACOP, unaodaiwa kuajiri takriban Watanzania 5,000, unawatesa wananchi.
SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Ulipaji Fidia Mbeya Wahofiwa Kuchochea Migogoro Kati ya Wananchi
“Walikuwa wamekubaliana kuchukua hatua 30, lakini sasa hivi wamediriki hadi kuchukua hatua nyingine 25, kitu ambacho hayakuwa makubaliano ya awali,” alisema Machumu kuhusu mvutano kati ya wananchi na Serikali. “Hata wanaolipwa hawalipwi inavyostahili, na wale wanaohoji wanabatizwa jina la ‘wapinga mradi.’”
“Itambulike kwamba sisi hatupingi mradi, hakuna kitu kama hicho. Sisi tunachokitafuta ni uwazi wa matokeo mabaya na yasiyofaa yanayotokea na yatakayotokea baada ya mradi huu.
“Sasa hivi pekee, hata mradi haujakamilika, watu wa Katesh na Chongoleani, Tanga, wanateseka, na wanapojaribu kuhoji wananyamazishwa. Sisi tunachokifanya ni kupaza sauti zao pekee dhidi ya uonevu unaofanywa na watu wa EACOP, na siyo kupinga,” alisisitiza Machumu.
Ulipaji fidia
Madai haya yanakuja wakati ambapo Serikali inasema imeshalipa fidia watu wapatao 9,823, kati ya 9,904 waliotambuliwa kuathiriwa na upitishwaji wa bomba hilo la mafuta, huku Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko, ambaye pia ni Waziri wa Nishati, akiliambia Bunge hapo Mei 9, 2024, kwamba Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 34.93 kwa ajili ya zoezi hilo.
Biteko alisema pia Serikali imejenga nyumba 340 kwa ajili ya watu 294 ambao walihamishwa makazi kupisha ujenzi wa bomba hilo la mafuta lenye ukubwa wa kilomita 1,443, na kumilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya kimataifa ya mafuta ya TotalEnergies, Serikali za Tanzania na Uganda, na CNOOC, ambayo ni kampuni ya Kichina.
SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro
Mmoja kati ya wananchi ambao wanatakiwa kuripoti polisi kila mwezi amezisihi mamlaka za nchi kuachana na kesi hiyo kwani inawasababishia usumbufu mkubwa, na kwamba nia yao wao siyo kupinga mradi bali stahiki zinazoendana na ardhi yao.
“Hatuna ubavu wa kupinga mradi sisi,” alisema mwananchi huyo. “Kwa sababu tumeshasaini tayari, hatuna namna, wao wasikilize hoja zetu. Kwa kweli watu wanaishi kwa hofu kwa kile ambacho tumefanyiwa sisi. Kwa kweli hatujui hatima ya sakata hili itakuwa ni lini. Tunaziomba mamlaka husika kuingilia kati na kumaliza kadhia hii.”
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.