The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Afrika: Tuendelee Kunywa Mtori Nyama Zipo Chini?

Bila wananchi na viongozi wao kuchukua hatua madhubuti kurekebisha hali ya mambo, Afrika itaendelea kubaki nyuma kimaendeleo.

subscribe to our newsletter!

Wanasema kwamba ukidanganywa mara ya kwanza, wewe bado huhesabiki kama mjinga, ila ukidanganywa mara ya pili, na ukadanganyika, basi wewe tunakuita mjinga. Pia, wanasema kwamba ujinga ni wakati wa kwenda tu, na si kurudi. Hapa Afrika, tumeshadanganywa zaidi ya mara mbili, na ujinga hautukabili wakati wa kwenda tu, bali na kurudi pia.

Bwana wee, ndiyo nimeshawaita wajinga, sasa niueni basi, kwani na mimi si nimejiweka humohumo, shida yenu nini? Lakini kabla hamjaniua, nisikilizeni kwanza. Ipo hivi, bara letu hili la Afrika limekuwa kwenye maumivu makubwa ya kimaendeleo miongo hata miongo kwa sababu kadha wa kadha nitakazojaribu kuzieleza.

Hapo awali kulipoibuka vuguvugu la kudai uhuru miaka kama 60, ama 70, iliyopita, nchi zote za bara la Afrika zilipigana vikali na wakoloni wa wakati ule, siyo tu kutaka kutoka kwenye waliyoyaita manyanyaso na mateso ya kutawaliwa, bali pia kutaka kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa kisingizio kwamba wakoloni wale walikuwa wakituzuia kupiga hatua, wakitunyanyasa na kututoa utu wetu.

Aghalabu, viongozi wote wa wakati ule walipambana vikali kuwatoa wakoloni wale, lakini wakisahau kujipanga vyema kujitawala, ama kujua baada ya wakoloni kuondoka nini kitafuata. Hivyo, wakakuta wamefanikiwa kuwaondoa, lakini wakati huohuo wakiwahitaji. 

Kwa kufanya hivyo, wakoloni walewale wakarudi tena kuendelea kututawala kwa mtindo na sura tofauti, wakati huu kwa ukoloni usio wa moja kwa moja bali kwa njia ya vibaraka, sera na miundo walioitaka wao.

SOMA ZAIDI: Afrika Imejipanga Kukabiliana na Taathira za Teknolojia ya Akili Unde?

Tena, kwa bahati mbaya, wengine waliwaondoa kwa kuuza nchi zao bila wao kujua. Mfano huko Afrika ya Magharibi na Kati walipotawaliwa zaidi na Wafaransa, wao waliuza haki nyingi za kiuchumi na kifedha kwa wakoloni wao, tena kimaandishi, ili mradi tu walitaka kusikia maneno kuwa, “Sasa mpo huru” hata kama maneno hayo hayakuwa na maana yoyote katika hali ya kawaida.

Kwa mfano, nilibaki hoi niliposoma kwamba ilikuwa ni lazima kwenye muundo wa benki zao kuu basi kuwe na mwakilishi kutoka Serikali ya Ufaransa. Eti walitakiwa kuwa wameweka asilimia 50 ya akiba ya fedha zao za kigeni kwenye hazina ya Benki Kuu ya Ufaransa na ni lazima kila siku kuwe na mwakilishi anaetoa taarifa huko Ufaransa juu ya mwenendo wa kifedha kwenye hizi nchi. Ajabu kweli kweli yaani!

Hali hii ambayo wanazuoni wameipa jina zuri sana kweli la ukoloni-mamboleo imeendelea kuitesa bara la Afrika jana, leo na kesho. Mathalani, sasa hivi katika bara letu tunasumbuliwa na matatizo mengi, lakini makuu manne kwa haraka haraka nitayabainisha. 

Haya ni matatizo katika daraja la juu kwani, kwa muono wangu, nadhani ndiyo chanzo cha matatizo yote mengine mtu anayoweza kuyataja kama sababu ya mkwamo wa kiuchumi na kimaendeleo barani Afrika na hivyo, nikipata nafasi ya kumshauri Rais wa ‘Stanza,’ nitamwambia aanze na angalau moja kati ya haya.

Vipaumbele fyongo

Kwanza ni vipaumbele visivyo sahihi. Hapa tuna mtiti si mdogo, nadhani kuwa nchi nyingi za Kiafrika hazina mpango mkuu wa kimaendeleo wa maana kwa siku zijazo, au kama upo basi huwa ni kama pambo tu kwa sababu huwa hakuna mwendelezo. 

SOMA ZAIDI: Juhudi za Dhati Zinahitajika Kuifikia Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo

Mataifa mengi ya Afrika yanadhani miundombinu, kwa mfano, ni tafsiri ya moja kwa moja ya maendeleo na ni jambo la kipekee. Kuna miradi mingi inayoendelea katika nchi nyingi za Afrika ambayo, kiukweli ukiitazama, haitafsiri maana halisi ya maendeleo ya watu.

Katika hali hiyo, viongozi wengi wameingizwa mkenge na mawakala wa ubepari kama Benki ya Dunia na nchi kama China kuchukua mikopo mikubwa na ya muda mrefu ili kuifanikisha. Nchi nyingi za Afrika zinatumia mikopo hii kujenga miundombinu mikubwa, zikiajiri kampuni kutoka nchi hizo ambazo zimetolea huduma za mkopo. 

Miradi hiyo inajumuisha barabara, madaraja hadi majengo marefu. Hii ni mikopo kutoka Benki ya Dunia na China. Vipi kuhusu watu? Wengi wanabaki chini ya mstari wa umasikini na viwango vya elimu vinashuka. Miundombinu hiyo ni kama ndovu weupe, ama kimombo huitwa white elephant.

Baba wa Taifa la Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema, “Maendeleo ya kweli ni maendeleo ya watu sio maendeleo ya vitu.”

Utawala mbovu

Jambo la pili, ama tatizo la pili nilionalo ni utawala. Hili liko wazi. Majibu mengi tayari yameashiria hili. Nchi za kipolisi, ufisadi, kuvuruga Katiba, kung’ang’ania madaraka, ukabila, na kadhalika, ndiyo sifa ambazo viongozi wengi wa Afrika walijipea kinga dhidi yake, tena nyingine kikatiba kabisa. 

SOMA ZAIDI: Urusi Inavyotumia Karata ya Ulinzi, Usalama Kukita Mizizi Afrika

Katika nchi nyingi za Kiafrika ni kawaida kuona muhula wa kiuongozi unapoisha, basi rais anashawishi Bunge kubadilisha Katiba ili kuondoa kikomo cha mihula.

Sasa anafikia kikomo cha umri wa miaka, kwa mfano 75, na hatastahili kugombea urais, lakini atashawishi tena Bunge kuondoa ukomo wa umri pia. Hili, au jambo linalokaribia hilo, linatokea katika sehemu nyingi za Afrika. 

Watu huyapenda tu madaraka bila hata kuwaza, au kujua, yawapasayo kufanya wakiwa hapo madarakani. Ni ulevi tu wa ving’ora, kupigiwa magoti, kutoa amri na kunyenyekewa. Ujinga-ujinga tu.

Tatizo la tatu ni kunakili na kubandika, au kwa kimombo wanasema copy and paste, mikakati na sera za maendeleo. Rasmi ama sio rasmi, Afrika haichagui. Viongozi wengi hunakili kila kitu bila kutathmini kama kinafaa na kukidhi haswa mahitaji ya nchi yake ama la. 

Wanakosa itikadi thabiti. Kwa mfano, mwelekeo wa utawala wa nchi nyingi za Kiafrika unaonyesha mchanganyiko wa ujamaa, ubepari na mchanganyiko mwingine.

SOMA ZAIDI: GMO: Suluhisho la Usalama wa Chakula Afrika?

Afrika inataka kuwafurahisha kila mtu. Imfurahishe mhafidhina, imfurahishe mliberari, imfurahishe mjamaa, imfurahishe mbepari, yaani imfurahishe kila mtu na matokeo yake inajikuta haisogei kwa sababu itikadi moja inagongana na nyingine, hasa katika utekelezaji wa sera na mipango. 

Mfano wakati huohuo inataka uchaguzi huru na wa haki ili kukidhi matakwa ya wapebari, ila kiongozi huyohuyo atahakikisha anafanya kila aina ya faulo ili tu asitoke madarakani, hata kama wananchi watamkataa. Unajiuliza hizi pesa zilizotumika kuendeshea huu uchaguzi wa kimagumashi si zingeelekezwa kuchimba visima tu tujue moja.

Afrika inadhani chochote, au kila kitu, ambacho kimefanya kazi mahali pengine kinaweza, na kinapaswa, kufanya kazi Afrika. Kwa hiyo, wakishaenda huko nchi za watu wanabeba na kuleta kwetu kama wamekatwa vichwa. 

Kuna kipindi ‘Stanza’ waliunga masomo yote ya sayansi, wakaunda masomo mawili tu. Sijui hata yule Waziri wa Elimu wa wakati ule aliliokota wapi lile wazo. Lakini kunakili ni jambo moja kubwa na janga lingine la kukosa uendelevu, yaani kiongozi ananakili jambo hili na kabla halijaanza kuzaa matunda, mwingine anakuja, analiondoa, na kubandika lingine alilokwapua huko na yeye!

Uhamaji wa akili

Tatizo la nne na ambalo ni kubwa kwa mawazo yangu ni uhamaji wa akili, ama kwa kimombo huitwa brain drain. Kweli, hii si ajabu. Sayansi ilithibitisha kuwa akili haipimwi kwa rangi. Afrika, kama mabara mengine, inazalisha akili bora pia, zipo. Tatizo sasa ni kuwa Afrika haiwezi kuhifadhi hata asilimia 70 ya akili zao. 

SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Ajenda Kuu ya Wakulima Wadogo Wanawake Barani Afrika

Mathalani, kuna taarifa niliyowahi kusoma inayosema kuwa jimbo la Chicago, nchini Marekani, lina madaktari wengi Waethiopia kuliko wote walioko Ethiopia. Fikiria hilo kwa muda! Hii inaonekana kama tatizo ambalo Afrika italazimika kukabiliana nalo kwa siku nyingi zijazo.

Akili za Kiafrika zilizobora zinahamishwa na kubakiziwa akili zezeta. Ama la, zile zinazobakizwa basi hubakizwa mahsusi kutumika na mabeberu kwa maslahi yao na siyo kuisaidia Afrika. 

Wakati huohuo, nchi za kibeberu hutumia nguvu kubwa kuhakikisha inaharibu mifumo ya kielimu kwa makusudi kwa kutuwekea mitaala wanayojua ama kwa hakika haiwezi kutusaidia kitu zaidi ya kukuza watu sanamu, au roboti, wasiojua kufikiri, kubuni na kuvumbua, bali kukariri wanacholishwa.

Kwa hiyo, kama viongozi wetu na sisi Waafrika wenyewe hatutaamua kubadilika na kuweka mguu chini, basi kutoka kiuchumi tuendelee kunywa mtori nyama tutazikuta chini!


Lello Mmassy ni mwandishi wa kazi mbili bunifu, Mimi na Rais na Chochoro Za Madaraka. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia lellommassy1@gmail.com au X kama @LelloMmassy. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Kaka kwanza kabisa napenda kukupa pongenzi kwa uandishi mzuri kabsa na wa kina ilioufanya juu ya Mambo kadha wa kadha ambayo yamekuwa yakikwamisha maendeleo ya bara letu la Afrika. Pia vile vile nipende kukutia moyo katika kazi zako za uandishi na mwenyezi Mungu akujalie hekima kwa ni site tunaamini ya kuwa ipo siku Afrika yetu itajikwamua kutoka katika mikono mibaya ya mabeberu na itakuja kusimama imara na kuwa sehemu minimum na salama kwa dunia nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts