Bunge la Tanzania lilipitisha bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi siku ya Mei 14, 2024 ambapo jumla ya bilioni 460.33 zimepangwa kutumika na wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ukilinganisha na bilioni 295.92 zilizotengwa kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 56.
The Chanzo tumefanya uchambuzi wa bajeti hii ambayo imebeba Sekta ya mifugo na uvuvi ambazo kwa mwaka 2022 zilichangia kwa asilimia 8.5 kwenye pato la taifa. Uchambuzi wetu, unatoa alama katika vipengele mbalimbali vya bajeti kwa madaraja matatu A ikionesha inaridhisha, B inaridhisha ingawa ina changamoto na C ina changamoto za msingi.
SOMA ZAIDI: Uchambuzi: Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2024/25 Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Kilimo?
Kipengele cha kwanza tulichoangalia ni eneo la upelekaji fedha iliyotengwa kwenye bajeti. Katika eneo hili, tumeipatia Wizara ya Mifugo na Uvuvi alama B. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mwenendo wa utolewaji fedha ukilinganisha na bajeti ilioyotengwa umekuwa hafifu.
Mfano mwaka wa 2022/23 Wizara ilipelekea asilimia 43 tu ya fedha ilizoziomba, huku mwaka 2021/22 zikipelekwa asilimia 66 na mwaka 2020/21 ambapo Wizara hiyo ilitengenewa kiwango kidogo katika kipindi cha miaka mitatu ilipelekewa fedha kwa asilimia 88. Mwaka wa fedha 2023/24 hadi kufika mwezi Aprili ikiwa imebaki miezi miwili kumaliza mwaka Wizara hii imepelekewa asilimia 50 tu ya fedha.
Hii ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi ikiwa Serikali kweli imedhamiria kuleta mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi ambazo sio tu zina mchango mkubwa kwenye ajira za mamilioni ya watanzania bali pia ni muhimu kwa kujitosheleza kwa chakula na kuingizia nchi fedha za kigeni.
SOMA ZAIDI: Uchambuzi Bajeti Wizara ya Afya Kwa Mwaka 2024/25
Kipengele cha pili tulichokiangalia ni muundo wa taarifa ya bajeti. Katika eneo hili tumeipa alama A kutokana na namna ambavyo taarifa hiyo imevielezea vipaumbele vya Wizara na namna ambavyo wizara imepanga kwenda kuvitekeleza. Uwasilishaji huu wa taarifa unasaidia wananchi kuelewa vipaumbele gani vimepatiwa fedha zaidi wakilinganisha na matamanio yao.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni katika sekta ya mifugo na uvuvi, uimarishaji wa upatikanaji wa mbegu bora za mifugo na samaki, malisho, vyakula, afya ya mifugo na viumbe wa majini, kuimarisha uchumi wa buluu, na kuimarisha programu za Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) kwa uchache.
SOMA ZAIDI: Uchambuzi wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Kwa Mwaka 2024/25
Changamoto ambayo Wizara inapaswa kuboresha katika uwasilishaji wake ni kueleza kiwango cha fedha kilichopangwa kutumika kwa kila kipaumbele badala ya kuonesha kwa baadhi ya vipaumbele tu. Hii itasaidia kuongeza uwazi kwa wananchi kuweza kufuatilia utekelezaji wa vipaumbele hivyo.
Kipengele cha tatu ni mrejesho wa bajeti iliyopita, yaani taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/24. Katika eneo hili, tumeipatia Wizara ya Mifugo na Uvuvi alama A kutokana na namna ambavyo imeweza kutoa mrejesho wa utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vya Wizara na utekelezaji wa taasisi na mamlaka mbalimbali zilizochini yake.
SOMA ZAIDI: Uchambuzi Bajeti ya TAMISEMI 2024/25
Sambamba na mrejesho huo pia taarifa ya wizara imeweza kujumuisha taarifa za kina za hali ya sekta ya mifugo na uvuvi kama vile idadi ya mifugo, uzalishaji na mauzo ya mazao ya mifugo na uvuv lakini pia taarifa za ushiriki wa wadau mbalimbali katika kukuza sekta.
Kwa mujibu wa taarifa hizi, mathalani taarifa ya idadi ya mifugo bado Tanzania inayo safari ndefu inayohitaji Serikali na wadau kujidhatiti katika kuhakikisha kwamba fursa zinazopatikana katika sekta zinaweza kuchangia zaidi katika uchumi na kuinua hali za wananchi.
Mfano, pamoja na Tanzania kuwa na mwambao wa bahari ya Hindi wenye urefu wa kilomita 1,424 bado uvunaji wa samakai upo chini sana ukilinganisha na maeneo ya ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika. Hili ni eneo ambalo Serikali inapaswa kujidhatiti kuhakikisha fursa hii inatumika ipasavyo kupitia mipango yake ikiwemo wa ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa.
Pia katika mifugo bado jitihada kubwa inahitajika katika kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kama maziwa. Mfano kati ya lita bilioni 3.9 za maziwa zilizozalishwa kwa mwaka 2023/24 ni asilimia 2 tu ya maziwa hayo yaliweza kusindikwa huku wakati huo huo nchi ikitumia takribani bilioni 23.4 kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi.
Pia mchango wa ng’ombe wa asili ambao ni takribani asilimia 96 kwenye uzalishaji wa maziwa ni mdogoukilinganisha na ng’ombe wa kisasa wa maziwa. Kwani asilimia 4 ya hao ng’ombe wa kisasa walichangia takribani asilimia 33 ya uzalishaji wa maziwa yote ya ng’ombe.