The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tanzania Inahitaji Dira Moja ya Taifa, Ilani Tofauti za Vyama vya Siasa

Ilani za vyama vya siasa wakati wa uchaguzi zibaki kama mikakati tu ya muda mfupi ya kutekeleza mipango ya muda mrefu ya maendeleo na dira ya taifa.

subscribe to our newsletter!

Katika makala iliyopita nilieleza umuhimu wa nchi kuwa na dira, au falsafa, ya maendeleo inayoeleweka kwa umma ili kuwezesha uratibu wa mipango, mikakati na sera katika mwelekeo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii utakaopelekea kujenga jamii mpya inayotazamiwa na umma, au ideal society kwa kimombo.

Moja ya mrejesho nilioupata kutoka kwa mmoja wa wasomaji kwa njia ya barua pepe ulikuwa ni swali liloulizwa: Je, tunawezaje kuwa na dira, au falasafa, ya maendeleo katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ilihali kila chama kina mwelekeo wake wa kiitikadi?

Sasa vyama vingi, kama tutaelewa msingi wake vizuri kama taifa, haviwezi kuzuia uwepo wa dira moja ya taifa ya maendeleo ambayo ni muhimu katika mchakato mzima wa maendeleo na kuhakikisha kunakuwepo na mwendelezo kati ya vipindi tofauti vya uongozi, hata kama tutakuwa tunabadilisha vyama katika kila baada ya miaka mitano ya uchaguzi. 

Ilani za vyama vya siasa wakati wa uchaguzi zitabaki kama mikakati tu ya muda mfupi ya kutekeleza mipango ya muda mrefu ya maendeleo na dira ya taifa, yaani vyama vya siasa vitofautiane mtizamo wa namna ya utekelezaji lakini si katika dira yenyewe. 

Hii inawezekana tu kama tutakuwa na mfumo wa vyama vingi halisi na si wa kiini macho, ambapo hakuna chama kimoja kinahodhi dola na mifumo yake, na kila mwananchi, au kikundi cha wananchi, bila kujali kutoka kundi gani la kisiasa, au kijamii, wanashirikishwa kujiamulia mambo yao bila kubuguziwa, au kuingiliwa kutoka nje.

Utamaduni wa vyama vingi

Kinadharia, vyama vya siasa ni vyombo vinavyoundwa na wananchi wenye maslahi na mwelekeo wa kisiasa unaoshabihiana juu ya hatma ya taifa lao. Hivyo basi, katika vyama vingi vya siasa inatazamiwa kila chama kuja na mapendekezo yake kulingana na mwelekeo wake wa kisiasa juu ya namna bora ya kuendesha Serikali na kuyafikia matarajio ya umma kwa ujumla.

SOMA ZAIDI: Michezo ni Muhimu Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Mafanikio

Ndiyo maana unapofika wakati wa uchaguzi kila chama cha siasa huja na ilani ya uchaguzi zinazoelezea programu ya chama husika juu ya namna kitakavyoendesha Serikali katika kipindi maalumu kilichowekwa Kikatiba.

Sasa, nchi yetu Tanzania ilirejea kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 baada ya kufutwa na Katiba ya mpito ya mwaka 1965. Licha ya mabadiliko madogo ya Kikatiba na kisheria yaliyowezesha kurejea kwa mfumo vyama vingi hiyo 1992, bado tuna mfumo wa vyama vingi wenye chama kimoja kinachoendelea kuhodhi dola kimfumo, yaani Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa hiyo, pamoja na ahueni iliyoletwa na mfumo wa kisiasa wa vyama vingi, bado imekuwa ngumu sana kuenenda na utamaduni wa mfumo huo. Ndiyo maana ile inayoitwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025, japokuwa iliandikwa miaka saba baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, haikuwa na ushiriki mpana wa wadau muhimu wa kisiasa na wananchi kupelekea moja ya sababu ya ilani za vyama vya siasa tofauti na CCM kutoakisi dira hiyo katika chaguzi zilizofuata baada ya 1992.

Kutokana na uhodhi wa chama-dola uliopo nchini ni rahisi sana kwa vyama vya siasa tofauti na CCM kuona kwamba jambo lolote linalokuja kwa jina la Serikali, au taifa, kuonekana kama ni jambo linaluhusu CCM pekee.

Sasa hii ni kinyume na utamaduni wa vyama vingi, na haujaanza kuhojiwa leo. Profesa Chachage S. Chachage, moja kati ya wanazuoni wanaoheshimika nchini, katika moja ya makala zake magazetini miaka ya mwanzo baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi aliwahi kuhoji kwamba, “Vyama vingi tunavipenda, lakini utamaduni wake tunauweza?” 

SOMA ZAIDI: Haya Ndiyo Yaliyofanya Dira ya Taifa ya 2025 Isifanikiwe Kikamilifu. Mchakato wa Dira ya 2050 Waanza

Kwa maoni yangu, tumeshindwa kuuishi utamaduni wa vyama vingi kuanzia kwenye kuweka misingi imara ya Kikatiba na kisheria na hata katika mitizamo ya wananchi wa makundi yote ya kisiasa na kijamii kwamba kila chama au wananchi wana haki sawa ya kushiriki katika shughuli za kisiasa  bila kujali mitizamo yao.

Tunahitaji dira moja

Sasa kama kweli tumedhamiria kujenga taifa ambalo lina maendeleo endelevu ya kweli, linaloweza kudumisha utengamano wake na uhuru, ni muhimu sana kuheshimu utamaduni huo wa vyama vingi kuanzia kwenye mifumo yetu ya kisheria na kimtazamo.

Lakini pia wananchi kupitia makundi yao mbalimbali ya kimslahi, kama vile vyama vya wafanyakazi, wakulima, vyama vya siasa, jumuiya za kijamii na kadhalika, ni muhimu sana wakashirikishwa kwelikweli na si kwa wale waliopewa dhamana ya kurataibu masuala ya kitaifa kufanya mambo ili mradi waonekane wametimiza wajibu.

Kama yatafanyika mambo makubwa hayo mawili, ni rahisi sana watu na makundi mbalimbali ya kimslahi kuwa na imani na michakato ya kitaifa kama uundwaji wa dira ya maendeleo. Kama watu watakuwa na imani nayo ndivyo itakavyowezesha hata vyama vya siasa kuja na ilani za uchaguzi ambazo zinaeleza mikakati ya muda mfupi ya kufanikisha mipango ya muda mrefu ya maendeleo na dira ya taifa kwa ujumla.

Kwa kuwa maendeleo kama mchakato wa mapambano yanayoendelea, ni muhimu sana kwa taifa kujizatiti katika dira na mipango ya maendeleo yenye mwendelezo ambao haukatishwi katishwi kwa ujumla na vipindi vya miaka mitano mitano ya uchaguzi kutegemea na nani anachukua hatamu ya uongozi.

SOMA ZAIDI: Falsafa ya Maendeleo Inayoeleweka kwa Umma ni Msingi Imara wa Ukombozi wa Taifa

Ni rahisi kupoteza mwelekeo kama hakutakuwa na dira, au falsafa, ya maendeleo ya taifa ambayo itakuwa juu ya mitizamo ya kisiasa ya vyama vyetu. Kwa hiyo, chama kinachoshika Serikali baada ya uchaguzi kupitia ilani yake ndiyo kiunde mpango wa maendeleo ya miaka mitano ambao utatekelezwa na Serikali.

Joel Ntile ni mwanamajumui wa Afrika na mchambuzi wa masuala ya kijamii-uchumi. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia barua pepe yake ntilejoel@protonmail.com au kupitia Twitter @JoelNtile. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *