The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mkopo wa Dola Bilioni 2.5 Kutoka Korea Kusini: Je, Tanzania Imeweka Rehani Bahari na Madini Yake?

Uchambuzi wa The Chanzo, uliojikita kwenye aina hiyo ya mikopo, pamoja na nyaraka za makubaliano kati ya Korea Kusini na baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo, madai hayo yanaonekana kuwa mbali na ukweli.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Madai kwamba Tanzania inaweza kuwa imeweka rehani rasilimali zake za bahari na madini ili kukidhi vigezo vya kupata mkopo wa Dola za Kimarekani bilioni 2.5 kutoka Serikali ya Korea Kusini yanaonekana kutokuwa ya kweli, uchambuzi wa utoaji wa aina hiyo ya mikopo uliofanywa na The Chanzo unaonesha.

Madai hayo ni sehemu ya mjadala mkubwa unaoendelea hivi sasa nchini Tanzania, hususan kwenye mitandao ya kijamii, tangu taarifa za kusainiwa kwa makubaliano ya mkopo huo zilizoporipotiwa kwa mara ya kwanza na VOA Swahili hapo Juni 3, 2024.

Kichwa cha habari cha habari hiyo kilisomeka Tanzania Imepokea Mkopo Kutoka Kwa Korea Kusini na Kutoa Sehemu ya Bahari na Madini na kuzua mjadala mpana, uliojumuisha ufafanuzi kutoka kwa Serikali, ulioisababisha VOA Swahili kukibadilisha kichwa chake cha habari na kusomeka Tanzania Imekopa Dola bilioni 2.5 kutoka Korea Kusini.

Lakini pamoja na VOA Swahili kubadili kichwa cha habari cha taarifa yake hiyo, bado mijadala mingi imeendelea katika mitandao ya kijamii, huku baadhi wakionesha kupinga mkataba huo, wakitumia madai yaliyoibuliwa na chombo hicho cha habari, kwamba Tanzania imeweka rehani bahari na madini yake ili kupata mkopo huo, kama sababu za ukinzani wao.

Lakini kwa mujibu wa uchambuzi wa The Chanzo, uliojikita kwenye utolewaji wa aina hiyo ya mikopo, pamoja na nyaraka za makubaliano kati ya Korea Kusini na baadhi ya nchi zingine zilizowahi kupokea mikopo hiyo, madai hayo ya bahari na madini kuwekwa rehani yanaonekana kuwa mbali na ukweli wa mambo.

Siyo nchi pekee

Uchambuzi wa The Chanzo umebaini kwamba Tanzania ni kati ya nchi 59 zinazopata mikopo kutoka Korea Kusini kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea (EDCF)

Kwa mujibu wa Benki ya Exim ya Korea inayosimamia mikopo hiyo, nchi kumi zilizopata mikopo mikubwa zaidi ni pamoja na Vietnam (dola bilioni 2.5), Cambodia (dola bilioni 1.7), Bangladesh (dola bilioni 1.7), Ufilipino (dola Bilioni 1.5), Indonesia (dola bilion 1.087), Misri ( dola bilioni 1.086), Tanzania (dola milioni 974), Uzbekistan (dola milioni 933), Sri Lanka (dola milioni 930) na Myanmar (dola milioni 898).

Mikopo hii ya Serikali ya Korea Kusini ilianzishwa rasmi Juni 1, 1987, ikiwa na lengo la kuliwezesha taifa hilo Asia Mashariki kuongeza mashirikiano na nchi zinazoendelea, lakini pia kujenga uwezo wa Korea Kusini kuuza ujuzi na bidhaa zake nje ya nchi.

Uchambuzi wa The Chanzo umebaini kwamba ili kukidhi masharti ya mikopo hii, ambayo kwa aina yake, na kwa mujibu wa taarifa za Benki ya Exim, ni mikopo nafuu, nchi mkopaji haihitajiki kuweka dhamana ya kitu chochote, ukweli unaoua madai kwamba Tanzania imelazimika kuweka rehani rasilimali zake za bahari na madini kupata mkopo huo.

Hii pia inaweza kuonekana kwenye muundo wa mikataba ya mikopo hii kama ambavyo inaonekana katika tovuti ya mfuko, (unaweza kuupitia mkataba wa mfano  hapa). Pia, riba ya mikopo hiyo iko chini ya riba ya soko. Muda wa kulipa mikopo hii pia ni mrefu zaidi ukilinganisha na aina zingine za mikopo.

SOMA ZAIDI: Gavana Benki Kuu: Ni Muhimu Kuwa Makini Na Mikopo Ya Kibiashara

Kwa mujibu wa Serikali ya Korea, mikopo hii wanaeleza kuwa riba yake ni kati ya asilimia 0.01% mpaka 2.5%. Lakini muda wa mikopo hii ni miaka 40, kukiwa na muda wa fungate wa miaka 15; Unaweza kuangalia taarifa hili kwenye ripoti ya mwaka ya EDCF.

Kuhusu hati ya makubaliano kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini kwenye uchumi wa buluu na madini ya kimkakati, ambayo nayo imekuwa sehemu ya gumzo, huku baadhi ya wachangiaji wakihusisha mazungumzo hayo na mkataba uliotolewa, uchambuzi wa The Chanzo pia umebaini kwamba haya ni masuala mawili tofauti na wala hayahusiani kwani, kama tulivyoonesha hapo juu, mikopo hii haiweki kigezo chochote cha uwepo wa dhamana.

SOMA ZAIDI: Wadau Wataka Mikataba ya Uwekezaji Katika Bandari Iwekwe Wazi

Uchambuzi wa The Chanzo pia unaonesha kwamba ufafanuzi wa Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura, kuhusiana na mkopo huu, unaweza kuwa na mashiko kwani mengi aliyoyaeleza yanawiana na matokeo ya uchambuzi wetu huru tulioufanya kuhusiana na mikopo hii, ikiwemo mapitio ya ripoti ya mwaka ya EDCF.

“Tanzania haijagawa chochote kubadilishana na mkopo nafuu kutoka Korea [Kusini] kama ilivyoandika,” Mavura alisema kwenye ufafanuzi wake aliouchapisha kwenye mtandao wa X, zamani Twitter. “Tanzania inapata mkopo wa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu.”

Kwenye ufafanuzi wake huo, Mavura pia aliuita mkopo huo kuwa ni wenye masharti nafuu, wenye riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate ya miaka 25. “Yaani unaanza kulipa baada ya mwaka wa 26,” alifafanua Mavura. “Hivyo, si kweli kwamba mkopo huo utalipwa kwa miaka mitano.”

Tumeangalia baadhi ya mikataba ya nchi mbalimbali kwa mikopo kama iliyopewa Tanzania, mfano mkataba kati ya EDCF na serikali ya Bangladesh, mkataba unaopatikana wazi (unaweza kuupakua hapa). Hoja za Mavura zinawiana na vigezo vya mkataba kati ya Serikali ya Bangladesh na EDCF, ambao The Chanzo imeuchambua, unaoonesha kwamba muda wa malipo ni miaka 40, muda wa fungate wa miaka 15 na riba yake ni asilimia 0.01. 

Hii ina maana kwamba, kama Tanzania imepewa fungate ya miaka 25 katika mkopo wake huo na EDCF, itakuwa pia imepata masharti mazuri.

Korea Kusini inapata nini?

Baadhi ya wachangiaji kwenye mijadala inayoendelea wamehoji kwamba kama Tanzania inakopeshwa kwa masharti kama hayo, wakopeshaji wake, yaani Korea Kusini, watapata nini kutokana na mikopo ya aina hiyo?

SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

Faida kubwa kwa wakopeshaji wa mikopo ya aina hii, ambao ni pamoja na India na China, ambako Tanzania imekuwa ikichukua mikopo ya aina hii pia, ni kuwa kampuni za nchi husika hutumika kwenye utekelezaji wa kile mikopo hiyo inakusudiwa kufanya. 

Ndiyo maana mikopo hii hutolewa na benki za kuuza na kununua nje, yaani Exim-Korea, Exim-India, Exim-China, na kadhalika. Korea Kusini itafaidika kwa kampuni zake kuweza kufikia masoko mapya, yaani Tanzania. 

Kwa namna hii, nchi hizi zinakuwa zikiamini kuwa baada ya makampuni haya kuingia yanaweza kupata fursa zaidi na kupata uzoefu mpya katika masoko mapya, kama ilivyoonekana kwenye ujenzi wa Daraja la Tanzanite, mradi wa vitambulisho vya taifa na hata mradi mpya unaotegemewa wa upimaji ardhi.

Wadau wanataja changamoto kubwa ya mikopo ya aina hii ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha kuna usawia wa manunuzi ya huduma na bidhaa kutoka katika nchi iliyotoa mikopo na nchi inayopokea mikopo lakini pia ulipaji wa kodi katika miradi husika.

Umuhimu wa uwazi

Baadhi ya wataalamu na wadau wanaofanya kazi kwenye eneo la kuhimiza uwazi kwenye shughuli za Serikali wameieleza The Chanzo kwamba mkanganyiko uliotokea juu ya mkopo huu ungeweza kuepukika kama Tanzania ingekuwa na utaratibu wa kuweka mikataba yake wazi.

SOMA ZAIDI: Ripoti za CAG: Wadau Wahimiza Uwazi Matumizi Fedha za Umma

Semkae Kilonzo, Mkurugenzi Mtendaji kutoka shirika lisilo la kiserikali la Policy Forum, ambalo limekuwa likipigia chapuo uwazi Serikalini, ameiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu kwamba Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza duniani endapo kama itaamua kuchapisha mikataba ya mikopo na kuiweka wazi.

“Hapa ni kusisitiza uwazi wa mikataba, hati za maelewano na matamko,” alisema Kilonzo kwenye mahojiano hayo. “[Kutokuwa wazi] ndiyo sababu inayoleta hali ya kutokuaminiana.”

Kama mikataba ya mikopo kati ya Korea [Kusini] na Tanzania ingekuwa wazi, basi jamii nzima ingeelewa kuwa mikopo hiyo haihusiani na kuweka rehani madini na bahari. Lakini pia, kuna uwezekano mkubwa ikatokea mazingira ya masharti hasi basi wananchi wanaweza kupata fursa ya kuiwajibisha Serikali.

Hoja hii inaungwa mkono na Moses Kimaro, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uwajibikaji anayefanya kazi na taasisi ya Wajibu, ambaye aliiambia The Chanzo kwamba kwenye uwajibikaji na uwazi, suala la uthibitisho wa taarifa kwa jamii ni la muhimu.

“Ili kuondoa hali ya kutoaminiana ni vyema taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vikubwa zikathibitibitishwa ili uwajibikaji uwepo,” alisema Kimaro ambaye taasisi yake inafanya kazi kuhimiza uwazi na uwajibikaji Serikalini, hususan kwenye eneo la manunuzi ya umma.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Ni.taarifa yenye uchambuzi wenye ushaidi.unaothibitisha hoja. La msingi hapa ni faida gani Korea inaipata kwa kutoa mikopo yenye riba za chini hivi. Faida ni kupata fursa za kibiashara na uwekezaji. Je tuna uwezo wa kujadiliana nao ili hizi fursa wanazozipata za biashara na uwekezaji zintunufsisha nasisi? Kwanini hatu negotiate nao kama block la Afrika. Nguvu ya pamoja ni.muhimu katika bargaining

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *