The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jinamizi la Ajali za Barabarani Litatumaliza Watanzania. Ni Kweli Serikali Haiwezi Kufanya Kitu?

subscribe to our newsletter!

Jinamizi la ajali za barabarani linaloendelea kuitafuna Tanzania na kuwaacha wananchi wake kwenye misiba, majonzi, na simanzi zisizoisha limenifanya nitakari kwa muda juu ya ni nini haswa huwa kinawasukuma waliokabidhiwa ofisi za umma kufanya maamuzi yanayohusu maisha, uhai, usalama, na ustawi wa wananchi.

Kama wananchi, tumekuwa tukishuhudia ajali nyingi za barabarani zikitokea katika maeneo mbalimbali ya nchi, zikihusisha vifo na majeraha ya maelfu ya watu katika kasi ambayo, nahofia, imefanikiwa kujenga dhana katika mawazo na akili zetu kwamba hiki ni kitu cha kawaida sana, na hivyo hata viwango vya kujali miongoni mwetu vimepungua.

Haishangazi kuona, kwa hiyo, kwa mfano, ajali iliyotokea kule Mbeya Juni 5, 2024, na kupelekea vifo vya watu 16, mpaka kufikia Juni 6, na kuacha majeruhi wengine kadhaa, imechukua nafasi ndogo sana kwenye mijadala ya Watanzania, kwenye majukwaa kama vile mitandao ya kijamii, kama vile hakuna kitu kilichotokea.

Ajali hiyo, ambayo tunaambiwa ilitokana na lori lililogonga gari nyingine mbili baada ya breki zake kufeli, imetokea wiki chache tu baada ya ajali nyingine huko Kilwa, mkoani Lindi, kuuwa watu 13 na kujeruhi wengine kadhaa hapo Aprili 22, 2024, ambayo nayo, kama zilivyo ajali nyingine nyingi baada na kabla yake, kama ile iliyoua watu saba Morogoro Mei 14, imepita kama kivuli, ikiacha watu wakiendelea na mambo yao.

Hatufahamu ni wastani wa watu wangapi wanaporwa uhai au uwezo wao wa kujifanyia mambo yao wenyewe kila siku na ajali za barabarani, na nimejaribu kutafuta takwimu mtandaoni nimekosa, lakini dalili zote zinaonesha kwamba hili ni tatizo kubwa ambalo sitakuwa nikiongeza chumvi hata kidogo nikisema linahitaji utatuzi wa haraka, ikibidi hata litangaziwe hali ya dharura. 

SOMA ZAIDI: Ajali za Barabarani Zinavyoangamiza Vijana Tanzania

Fikiria, kwenye siku 12 tu za Disemba 2023, Tanzania ilipoteza watu 46, wastani wa watu wanne kila siku, kwenye ajali za barabarani. Kwa nini hiyo siyo kashfa ya kitaifa?

Kutokuguswa 

Hii ndiyo inanileta kwenye hoja yangu ya msingi, kwamba je, kama wananchi, tungeshuhudia hali hiihii ya mambo, ukawaida huu unaoashiriwa kutokuguswa kwa ‘viongozi’ wetu endapo kama idadi hiyo ya watu wangekuwa wanafariki kutokana na, kwa mfano, mashambulio ya kigaidi?

Fikiria, kama magaidi wangeua watu 13 Lindi Aprili mwaka huu, na Mei wakaua watu saba Morogoro, na Juni wakaua watu 16. Je, tungebaki kwenye hali kama ya sasa inayoashiria kutokuwepo kwa utashi wa kufanya kitu miongoni mwa wale waliokabidhiwa dhamana ya kulinda maisha na usalama wetu kama raia?

Sababu ipi ya kifo cha mwanadamu, kama naweza kuuliza, inakuwa na uzito wa kuwasukuma waliopewa dhamana ya kulinda maisha, uhai, usalama, na ustawi wa wananchi kuinuka kwenye masofa na viti vyao na kuanza kuchukua hatua stahiki kukabiliana na sababu hiyo? 

Kifo cha aina gani kinahuzunisha zaidi ya kingine na kuweza kuwalazimisha wenye mamlaka kuacha porojo na visingizio vya kila aina na kuanza kulinda kweli roho za wanaowaongoza? Mazingira gani ya kifo ni ya kuogofya zaidi ya mengine?

SOMA ZAIDI: Ajali za Barabarani Zilivyoteketeza Maisha ya Watanzania 2022

Ni kweli Serikali inataka kutuaminisha kwamba hakuna kitu inaweza kufanya kuondokana na jinamizi hili linalowajengea hofu Watanzania kuhusu kutumia usafiri wa barabara – usafiri unaotumiwa na mamilioni ya wananchi wa tabaka la chini na, kwa kiwango fulani, lile la kati? 

Je, Serikali ingekuwa na mkwamo huuhuu wa kuchukua hatua stahiki kama Watanzania wangekuwa wanafariki kwa kiwango hikihiki kutokana na ajali za ndege, aina ya usafiri inayopendwa na maafisa wake?

Marekebisho ya sheria

Kila wakati Serikali inapotakiwa kutoa maelezo juu ya mikakati inayopanga kuchukua kukabiliana na jinamizi la ajali za barabarani, inakuja na maelezo ya juujuu, yaliyokosa mashiko na hamasa, ikiwemo lile walilozoea kutoa kuhusiana na haja ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, ahadi Serikali inayopenda kuitoa lakini imeshindwa kuitekeleza hadi sasa.

Bila ya shaka, mikakati ya kupunguza ajali za barabarani itapaswa kwenda mbele zaidi ya marekebisho ya sheria na kujumuisha mambo kama vile tathmini ya mahusiano yaliyopo kati ya wamiliki wa mabasi na malori ya mikoani na wafanyakazi wao, mahusiano ambayo ushahidi unaonesha ni ya kinyonyaji, na pasi na shaka yoyote ile yatakuwa yanachangia kwenye tatizo.

Mikakati pia inaweza kuhusisha uwajibishwaji wa askari wa usalama barabarani wala rushwa pamoja na udhibiti wa vyombo vya usafiri vinavyoingia barabarani kuhakikisha ubora. Lakini, kwa nini Serikali kila siku inasema itaifanyia marekebisho sheria hiyo na mwisho wa siku hakuna marekebisho yoyote yanafanyika?

SOMA ZAIDI: Mbeya Katikati ya Mtanziko wa Kulinda Maslahi ya Kiuchumi na Kujikinga na Ajali za Barabarani

“Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani wa mwaka 2021 ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo Juni 30, 2021, ikiwa ni baada ya miaka takriban sita ya ushawishi, uchechemuzi na vuguvugu kufanikisha hatua hiyo,” The Chanzo iliripoti Februari 21, 2022. “Hata hivyo, tangu kusomwa kwake, muswada huo ulipotelea kusikojulikana na hivyo hatma yake kutojulikana.”

Kwa nini Serikali, iliyojijengea sifa ya kupitisha sheria mbalimbali bungeni kwa hati ya dharura, licha ya kulalamikiwa na wadau, inahofia sana kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani? 

Je, inawezekana sababu ikawa ni wamiliki wa mabasi na malori ya mikoani, ambao baadhi yao wanajulikana kuwa vigogo na wafadhili wakubwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wanahisi sheria mpya itakinzana na maslahi yao binafsi ya kujitengenezea faida pana zaidi na nono?

Kama hiyo siyo sababu, kisingizio cha kuchelewa kuifanyia marekebisho sheria tajwa, hatua ambayo, kama nilivyosema, haitoshi kukabiliana na jinamizi la ajali za barabarani, lakini ni hatua ambayo angalau wadau wanaofanya kazi kwenye eneo hilo la usalama barabarani wanaamini itasaidia kwa kiwango kikubwa kurekebisha hali ya sasa?

Serikali, pamoja na Bunge, kwa nyakati mbalimbali wamekuwa wakali sana kuhusu waendesha bodaboda nchini na ajali wanazozisababisha ambazo wamekuwa wakizihusisha na uendeshaji wao usiofuata sheria. 

SOMA ZAIDI: Nini Kimekwamisha Mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani Tanzania?

Kwa nini, nauliza, hatuoni Serikali hiyohiyo, na Bunge hilohilo, zikizungumza kwa hisia kali hizohizo kuhusu ajali zinazosababishwa na mabasi ya abiria na malori ya mizigo ya mikoni? Je, sababu inaweza kuwa hakuna kigogo wa CCM au Serikali anamiliki bodaboda na hivyo ni rahisi kuwashambulia bodaboda kila siku na kwa hisia hasi muda mwingine?

Kuacha visingizio

Nadhani ifike wakati Serikali iache kuendeleza visingizio na kuanza kubuni na kutekeleza hatua madhubuti zinazolenga kukomesha ajali za barabarani nchini. Hatuwezi kuendelea kuishi na kufanya mambo yetu kama vile suala la ajali za barabarani ni kama kuchomoza na kuzama kwa jua, kwamba lazima kutokee haijalishi hali iliyopo.

Ni wakati Serikali iangalie kwa jicho la tatu vifo vya Watanzania vinavyotokana na ajali zisizokwisha za barabarani na kujiuliza kama ingeendelea na biashara kama kawaida endapo kama vifo hivyo vingetokana na matukio ya kigaidi au ajali za ndege, na kama jibu ni hapana, ianze kuchukua hatua stahiki sasa.

Sehemu ya kuanzia ni kwa Serikali kutimiza ahadi yake ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani, hatua itakayowezekana tu kwa Serikali kutoa kipaumbele kwa maisha ya Watanzania badala ya maslahi ya kifedha ya wamiliki wa mabasi na malori, pamoja na kushirikiana na wadau wengine kubuni na kutekeleza mikakati mingine imara ya kutokomeza kabisa ajali za barabarani Tanzania. 

Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts