Tunahitaji kuipitia upya mitaala yetu ya elimu ya msingi na sekondari kwa lengo la kuibadilisha ili iakisi mahitaji halisi ya jamii husika, na hivyo kuwapatia wanafunzi nyenzo zitakazowawezesha kuyafahamu vizuri mazingira yao kwa lengo la kuyakabili vyema na hivyo kuboresha maisha yao, jamii inayowazunguka, na nchi yao kwa ujumla.
Tunahitaji kuondokana na mitaala inayoiangalia Tanzania kama jamii moja yenye matatizo yanayofanana na kuanza kuukabili ukweli kwamba jamii zetu ni anuwai kwa kiwango kikubwa sana, zikiwa na watu wenye asili, utamaduni, na matatizo tofauti.
Kuna mambo yanatuunganisha kama Watanzania, na kuna mambo yanatutofautisha, na hivyo kuutajirisha utambulisho wetu.
Mitaala yetu, hata hii iliyofanyiwa maboresho, haiakisi ukweli huu na tumeendelea kuwapotezea muda watoto wengi kwa kuwafundisha mambo yasiyoendana na uhalisia wa jamii zao, na hivyo kuathiri jitihada zao, na zile za kitaifa, za kujikomboa kiuchumi, kiutamaduni na kijamii.
Bado kama nchi tumeendelea kung’ang’ania kutengeneza mitaala ya ‘Tanzania’ kwa gharama ya kuwanyima wanafunzi uwezo wa kuyafahamu vizuri zaidi mazingira yaliyowazunguka, na hivyo kupunguza uwezo wao wa kuyabadilisha kwa faida zao binafsi na zile za wanajamii wenzao.
SOMA ZAIDI: Uchambuzi wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Kwa Mwaka 2024/25
Hakuna ubaya kuwa na masomo yanayohusu nchi, lakini ni lazima mitaala itengenezwe kuakisi mahitaji halisi ya jamii husika.
Utalii
Kwa mfano, mimi nimezaliwa na kukulia kwenye jamii ambayo shughuli kubwa za kiuchumi ni uvuvi na utalii.
Hizi ni shughuli za kiuchumi zinazomeza vijana wengi wanaoshindwa kuendelea na masomo kijijini kwetu, ambao ni wengi sana, na ungetegemea mitaala ya elimu ya msingi na sekondari kwenye shule za jamii hiyo ingetengenezwa kuakisi ukweli huu.
Hata hivyo, inasikitisha kuona kwamba mitaala ya elimu ya msingi na sekondari ya Zanzibar, ambayo jamii zake zinafanana sana kwa kutegemea uvuvi na utalii kama shughuli kubwa za kiuchumi, inashindwa kumuandaa mwanafunzi kuvuna fursa zinazotokana na shughuli hizi.
Matokeo yake mwanafunzi anatumia miaka takribani kumi ya maisha yake – msingi na sekondari – na akitoka shule ni kama vile hajasoma kabisa, ukitoa uwezo wake wa kuhesabu, kusoma na kuandika!
SOMA ZAIDI: Je, ‘English Mediums’ za Serikali Zinakinzana na Sera ya Elimu Bila Ada?
Siku zote nimekuwa nikijiuliza, kwa nini masomo kama vile ya ukarimu, au hospitality kwa kimombo, na uongozi wa hoteli, au hotel management, yasiwe sehemu ya mitaala ya elimu ya msingi na sekondari, ukizingatia ukweli kwamba utalii ndiyo injini ya uchumi wa Zanzibar?
Kwa nini tusubiri mtoto atumie miaka kumi shuleni, na baada ya kushindwa kuendelea na masomo, kwa sababu mbalimbali, ndiyo tunampeleka asome astashahada au stashahada ya ukarimu au uongozi wa hoteli?
Hii ni kutojitendea haki kabisa, na nadhani ifike wakati tujiulize kwa nini haswa tunatoa elimu kama siyo kwa lengo la kukabiliana na mahitaji halisi ya jamii zetu.
Hii inafanyika katika jamii ambayo Serikali kila kukicha inawapigia kelele vijana kuchangamkia fursa zinazotokana na utalii ambazo mara nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kuchukuliwa na wageni.
Kama kweli tunaamini utalii unatoa nafasi ya kumkomboa kijana wa Kizanzibari, kwa nini tusimjengee huo uwezo wa kuzichangamkia fursa hizi mapema tu anapoanza mchakato wa elimu?
SOMA ZAIDI: Kitila Mkumbo Aichambua Rasimu ya Sera ya Elimu, Ataka Iboreshwe
Fikiria kama mtoto anatambulishwa kwenye masomo haya anapoingia tu shule ya maandalizi na kuongezewa maarifa kadiri anavyoendelea na masomo mpaka anafikia sekondari?
Kwa miaka kumi atakayoitumia kwenye elimu ya msingi na sekondari, mtoto huyu atakuwa amewiva kwenye suala la utalii na kuwa tayari kuchangamkia fursa zinazotokana na sekta hiyo. Linganisha hiyo na mwaka mmoja au miwili atakayotumia kwenye elimu yake ya astashahada na stashahada, mtawalia!
Tubadilike
Lazima tubadilike, hatuwezi kuendelea hivi kamwe. Vivyo hivyo kwenye sekta ya uvuvi. Unaandaaje mitaala yako ya elimu kumuwezesha mwanafunzi kwamba baada ya kuhitimisha miaka kumi ya elimu ya lazima anakuwa tayari kujihusisha na sekta hiyo katika ngazi ambazo ni kubwa na zenye maana zaidi ya kuwa mvuvi au mchuuzi wa samaki tu?
Zanzibar hivi sasa inapiga kelele sana kuhusu uchumi wa buluu na fursa zinazoweza kuvunwa kutoka kwenye sekta hiyo.
Lakini badala ya kuwawezesha vijana kwa mafunzo ya wiki moja na yasiyo na mwendelezo, kwa nini mafunzo hayo yasiingizwe kwenye mitaala ili wakati mwanafunzi anahitimu elimu yake ya sekondari anakuwa amejengewa uwezo wa kutosha wa kijasiriamali utakaomuwezesha kuvuna fursa kutoka kwenye sekta hiyo?
SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?
Na wakati hapa nimetumia sana mifano ya Kizanzibari, hayohayo yanaweza kusemwa kuhusu Tanzania Bara.
Kuna jamii zimebarikiwa kuwa na madini, kwa nini shule za jamii hiyo zisiwe na mitaala yenye masomo yanayoweza kuwawezesha wanafunzi kuchangamkia fursa hizi pindi tu wanapomaliza elimu yao ya lazima? Vivyo hivyo kwa jamii zilizozungukwa na hifadhi za taifa, maziwa, na aina nyingine za utajiri.
Pengine hatua ya kwanza ya kuwezesha kwa hili kutokea ni kwa Serikali kutoa mwongozo wa namna mitaala inavyopaswa kutungwa na kutekelezwa na kutoa uhuru kwa shule na jamii inayoizunguka kuja na mitaala inayoakisi mahitaji halisi ya jamii husika.
Kimsingi, wazazi, kama wadau muhimu kwenye mchakato mzima wa elimu, wanapaswa kuwa na uwezo wa kushawishi ni aina gani ya elimu watoto wao wanapata, na hilo linafanyika kwa kiwango kidogo sana hivi sasa.
Nihitimishe kwa kusema kwamba ni kweli tunahitaji maboresho ya mitaala, lakini isiwe kwa lengo la kuwafanya wahitimu waajirike tu baada ya kuhitimu masomo yao. Kwanza, siyo kazi ya walipakodi kumtengenezea mwajiri waajiri wanaokidhi sifa anazozitaka!
Tuboreshe mitaala yetu kukidhi matakwa halisi ya jamii zetu kama sehemu ya jitihada za pamoja za kubadilisha jamii hizo kwa faida ya wanajamii wote, na kuacha kuwapotezea watoto wetu muda kwa kuwafundisha mambo yasiyowasaidia kwa namna yoyote ile.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Habari,
Mimi sijaelewa bado unavyosema, jamii zote zilizo karibu na madini, uvuvi, n.k zitengenezewe mtaala wa kuendana na jamii hizo, sasa kam ndo hivyo, nchi itakuwa na mitaala mingapi?,
Kwa maoni yangu labda ungeongelea gap la kielimu Tanzania. Kuna elimu ya walionacho na wasionacho.. hapa ndiyo shida ilipoanzia.. kufanya elimu kuwa biashara, chimbuko la english mediums nchini ndo imefanya shule nyingi za msingi kuwa na Elimu ambayo haifanani. Kwa hiyo, shida ya elimu Tanzania sio mtaala, bado nchi kama nchi haijaelewa kutoa hili gap la shule za walionacho na wasionacho..