The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’

Kitabu cha Paulo Freire, Pedagogy of the Oppressed, kinaweza kutusaidia kulifahamu tatizo linalotukabili kama Watanzania, na namna ya kulitatua.

subscribe to our newsletter!

Kichwa cha habari cha makala haya ni nukuu ya mwanazuoni na mwanaharakati wa Kibrazili, Paulo Freire, kutoka kwenye kitabu chake mashuhuri na ambacho kimeendelea kuchochea mijadala mikali katika sekta ya elimu ulimwenguni kote, Pedagogy of the Oppressed.

Hiki ni kitabu cha kipekee na maridhawa katika nyanja za elimu, uchambuzi yakinifu wa masuala ya kijamii na fikira tunduizi. Freire, aliyezaliwa mwaka 1921 na kufariki mwaka 1997, alikuwa mwanaharakati, mdau wa elimu na mwanafalsafa. 

Maudhui na muktadha wa kitabu ni matokeo ya mazingira magumu ya udikteta yaliyoikumba Brazili kwenye miaka ya 1960, ambapo nchi hiyo ilinuka umasikini wa kupindukia na ukandamizaji wa haki ulirasmishwa. Mambo hayo yalisababisha Freire apelekwe uhamishoni nchini Chile.

Kitabu hiki ni maarufu na kimetafsiriwa katika lugha zaidi ya ishirini na tano. Kwa ujumla, kinapinga sera na miundombinu ya elimu duni zilizopitwa na wakati, zinaendeleza unyonyaji na matabaka na kuwadumaza wananchi. Sera hizo zimeshindwa kuwajengea uwezo na kuwashirikisha wananchi katika kuboresha maisha yao na kuwafanya wajisikie fahari na nchi yao.

Freire anasema kuwa mfumo na sera ya elimu sio neutral, au zisizoegemea upande wowote. Badala yake, zote ni matokeo ya utashi wa kisiasa ambao aidha unamkomboa mwananchi, au kumfanya mtumwa katika nchi yake. 

SOMA ZAIDI: Jitihada Zaidi Zinahitajika Kuongeza Ubora wa Elimu Inayotolewa Tanzania

Tafsiri yake ni kwamba, elimu duni imetolewa kama chombo cha tabaka tawala kubaki madarakani na kuendeleza unyonyaji hasa katika kutuamulia aina ya elimu na sera zake. Kwa upeo wa mwandishi, mageuzi na harakati zote za kuleta utawala bora, haki jamii na demokrasia, na katiba mpya haziwezi kutenganishwa na vuguvugu za kielimu, yaani ukombozi wa fikira na uhuru kamili.

Muktadha wetu

Kitabu hiki ni muhimu sana kwa mazingira yetu sasa, ambapo uhuru wa kujieleza, mawazo mbadala, na haki ya kukusanyika zinapingwa na udikteta wa dola unashamiri. Mwandishi Paulo Freire anatoa mwongozo kwa kufuata pale ambapo tunaona hakuna utashi wa kisiasa katika kuleta mabadiliko. 

Mabadiliko anayoyagusa mwandishi ni katiba mpya, kuongezeka kwa matabaka kati ya walalahoi na walalaheri, na kushuka kwa ubora wa elimu. Mwandishi anapingana na mfumo baguzi wa elimu ambao unaacha vijana wengi nyuma bila kuwapatia ujuzi mbadala, unaochochea ukosefu wa ajira, na kusababisha kuongezeka kwa ugumu wa maisha na umaskini ambao ni mtaji wa kisiasa.

Kitabu kinabainisha kuwa aina ya elimu na mtindo wa ufundishaji, anaoufananisha na mfumo wa kibenki, ambapo walimu “huweka” ujuzi na maarifa kwa wanafunzi, ni mtindo wa kikoloni, ambapo mwalimu pekee anaonekana ndiye mwenye ujuzi na maarifa yote na wanafunzi ni wapokeaji tu wa taarifa, wanakariri tu. Hivyo sio washiriki kamili wa mchakato wa elimu.

Mtindo wa elimu kama huo ulipingwa pia na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania, alipoongea juu ya sera ya elimu ya kujitegemea, ndiyo maana Paulo Freire na Mwalimu Nyerere walikuwa marafiki hadi kutembeleana miaka ya 1971. 

SOMA ZAIDI: Kwa Kung’ang’ania Kiingereza, Rasimu ya Sera ya Elimu Imeshindwa Kuzingatia Maslahi ya Wengi

Kwa mujibu wa Freire, elimu hii haiwezi kumkomboa mnyonge na maskini. Je, elimu yetu ina tofauti na haya anayosema Freire? Mfano, utasikia wanafunzi zaidi ya asilimia 50 “walishindwa” mtihani hivi majuzi. Je, ni kweli walishindwa ama ni namna nyingine ya kuwakandamiza vijana wasio na hatia? 

Na kama kweli walishindwa, je, tunawapa nafasi na elimu gani nyingine mbadala? Na je, tunatengeneza mazingira gani ya kuchochea uvumbuzi, hamu ya kujisomea na ubunifu ndani na nje ya mfumo rasmi wa elimu?

Hakuna uhalisia

Elimu na miundo yake ambayo haiakisi uhalisia wa mwanafunzi, haichochei fikira mpya, ubunifu wala uvumbuzi na mbaya zaidi haivutii watu kuwa walimu, haitufai. 

Mfumo wa elimu unatakiwa kuwa rafiki, wezeshi kwa makundi ya watu hasa wa vipato duni ili wajisikie huru kutambua mifumo ya unyonyaji, na kuzalisha jamii ya haki na usawa. Bila hayo mabadiliko, elimu itaendelea kuwanufaisha watu wachache na kushindwa kutimiza lengo lake la msingi la kumkomboa mwanadamu.

Kazi kubwa ya elimu ni kuwajengea nidhamu wanafunzi na kuwafungua kifikra kiasi cha kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha. Lengo la elimu siyo tu kuzalisha watu wenye vyeti vinavyoonesha wamefaulu kwa viwango vya juu.

SOMA ZAIDI: Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Umuhimu wa tafakuri hii ya Freire katika ufundishaji nchini Tanzania ni mkubwa sana. Kuna mkanganyiko na udhaifu wa makusudi katika mfumo wa elimu yetu: kuanzia sera na falsafa ya elimu, lugha ya kufundishia, mbinu za kufundishia, na uhusiano kati ya mwalimu na mwanafunzi.

Leo tunaongea kuhusu vijana wengi kuhitimu masomo, lakini bado hawana uwezo na ujuzi wa kuajiriwa, maana yake, pamoja na mambo mengine, mfumo wetu wa elimu una ombwe na udhaifu mkubwa. Vijana wengi hawana ujuzi na mbinu za kimaisha, au soft skills kwa kimombo, ambazo zinahitajika katika karne hii.

Hatima ya elimu yetu na maendeleo ya taifa hili yapo mikononi mwetu wananchi. Kazi ya kuboresha elimu na utawala bora ni yetu sote. Nionavyo mimi, bado hatuna hasira ya kutosha katika kufanya mageuzi kwenye sekta ya elimu. 

Kazi ya elimu iwe ni kutufikirisha, kupanua maono, kudadisi dhana na sera zetu ziwe za uchumi, za taasisi ya kifalme kama ya urais, sera za nje na mahusiano na mataifa, muundo wetu wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar na dhana ya uzalendo na taifa la “maadili.” 

Tupinge mfumo wa elimu unaotumezesha propaganda uchwara na mazingira ya ki-imla ambayo yanawekwa na mamlaka. Mazingira hayo yanakandamiza uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari, hasa katika kuleta taarifa za kiuchunguzi, tafiti huru na mawazo mbadala.

SOMA ZAIDI: Wadau Wasisitiza Utekelezaji wa Vitendo Mikakati Elimu Jumuishi

Ninafahamu kuwa Serikalini kuna mpango mkakati wa kuongeza ujuzi na maarifa, na waajiri wanatozwa tozo ya uendelezaji ujuzi kufanikisha mpango huo. Ninaelewa kuwa tozo hii inatakiwa kutumika katika programu mbalimbali za kuendeleza nguvu-kazi kwenye maarifa na ujuzi mpya. Sasa, sijui ufanisi wake upoje mpaka sasa? Tathmini ya mikakati hii ipoje?

Thamani ya lugha

Tuwekeze na kuboresha hata lugha yetu ya Kiswahili. Dira yetu ya taifa itambue nafasi ya Kiswahili katika elimu na maendeleo yetu. Tuwaache watoto wasome na kupata ujuzi kwa lugha wanayoifahamu, huku tukiwafundisha Kiingereza kama lugha nyingine za kigeni, ikiwemo Kichina. Linapokuja suala la lugha, tusilazimishe kumweka punda nyuma ya mkokoteni kisha tukamtaka auvute kwenda mbele, haiwezekani!

Lugha kama Kiingereza inaweza kuwa ni kichaka cha kuficha tatizo la kukosa ujuzi fulani. Ukishakuwa na ujuzi mkubwa katika eneo, au nyanja, fulani, lugha ni kiunzi kidogo sana, japo ni muhimu. 

Wachina wengi wanaokuja Tanzania kufanya miradi huwa na uwezo mdogo wa kutumia lugha ya Kiingereza, lakini kwa sababu wana ujuzi mkubwa katika nyanja zao, lugha haiwakwamishi kutekeleza majukumu yao. Tatizo letu kubwa ni fikira finyu.

Umma unahitaji kuelimishwa na kushawishiwa kufanya maamuzi bora kwa mustakabali mwema wa taifa hili. Propaganda za makusudi kupitia vyombo vya habari ili kuwapumbaza, kuwafubaza, na kuwapotosha Watanzania kwenye masuala nyeti na ya msingi zikomeshwe.

SOMA ZAIDI: Richard Mabala: Je, Kupata Nafasi ya Shule Ni Kupata Nafasi ya Elimu?

Fasihi ni nyenzo nzuri katika kutunza maarifa na utambulisho wetu. Na katika hili, kuna taasisi mbili kubwa hazilisaidii taifa katika makuzi na uendelezaji wa fasihi kama njia ya kuimarisha uhuru wa maoni, nazo ni Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mwalimu Nyerere, katika Azimio la Arusha, alifahamu kuwa kuna mfumo kandamizi na jinamizi, lakini huo mfumo unaishi na kuchanua kwa sababu ya udhaifu wetu. Mfumo upo chini ya tabaka lenye nguvu ya uchumi na kisiasa nchini. 

Tabaka hilo hutumia vyombo vya ushawishi kuwahadaa wananchi na vyombo vya mabavu kuwalazimisha wananchi wafuate matakwa ya mfumo. Ni wajibu wetu kama wananchi kuupinga mfumo huu, na Pedagogy of the Oppressed inaweza kutusaidia kwenye mbinu za kulifanikisha hilo.

Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au X kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts