The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fao la Kukosa Ajira ni Nini, na Nani Anastahili Kulipata?

Fao la kukosa ajira ni muhimu sana kwani hutoa msaada wa kifedha kwa kipindi cha mpito baada ya kupoteza ajira bila kuathiri michango ya mwanachama.

subscribe to our newsletter!

Fao la Kukosa Ajira ni msaada wa kifedha unaotolewa kwa mwanachama wa mfuko wa pensheni aliyepoteza ajira kwa sababu zisizo za hiari, kama vile kufukuzwa kazi, kuisha kwa mkataba, au sababu nyingine za halali. Hata hivyo, fao hili halitolewi kwa mtu aliyeacha kazi kwa hiari, kwani kufanya hivyo humfanya apoteze sifa za kupata fao hili.

Mtu anayestahili fao hili anatakiwa, kwanza, kuwa chini ya umri wa miaka 55. Ikiwa umepoteza kazi na umri wako ni zaidi ya miaka 55, basi italazimika ulipwe fao la uzee, au old age pension kwa kimombo.

Pili, fao hili la kukosa ajira hulipwa kwa mwanachama aliyechangia kwenye mfuko chini ya miezi 180. Ikiwa umechangia zaidi ya miezi 180, na uko chini ya miaka 55, ukapoteza ajira, basi utalipwa pensheni iliyocheleweshwa au differed pension kwa kimombo.

Tatu, ili kukidhi vigezo vya kupata fao hili la kukosa ajira, ajira inatakiwa kuwa imekoma kwa sababu zisizo za hiari kama vile kufukuzwa kazi, mkataba kuisha, au kupunguzwa kazini.

Fao la kukosa ajira hulipwa kwa awamu mbili. Kwa aliyechangia zaidi ya miezi 18, malipo ya awamu ya kwanza, atalipwa asilimia 33.3 ya mshahara wake wa mwisho kwa kipindi cha miezi sita. 

SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo Kuhusu Kikokotoo Kipya cha Asilimia 33

Baada ya malipo ya kwanza, mtu huyu atakuwa na kipindi cha miezi 18, au miaka miwili, cha kutafuta ajira, akipata ajira, ataendelea kuchangia katika mfuko pale ulipoishia, na ikitokea amekosa ajira ndani ya kipindi hiki, ataruhusiwa kuchukua kiasi kilichobaki kwenye mfuko.

Kwa aliyechangia chini ya miezi 18, atalipwa nusu ya kiasi alichochangia kwenye mfuko. Baada ya malipo, atakuwa na kipindi cha miezi 18, au miaka miwili, cha kutafuta ajira. Akipata ajira, ataendelea kuchangia pale alipoishia, na akikosa ajira ndani ya kipindi hiki, ataruhusiwa kuchukua kiasi kilichobaki kwenye mfuko.

Pia, malipo ya fao la kukosa ajira yanatofautina kwa mtu mwenye ujuzi, au skilled, na mtu asiye na ujuzi, au unskilled. Kwa mtu asiye na ujuzi, yeye hulipwa kiasi chote alichochangia kwenye mfuko na mwenye ujuzi yeye hulipwa kwa kufuata maelekezo niliyoyaweka hapo juu. 

Hii ni kwa sababu ni ngumu kwa mtu asiye na ujuzi kupata ajira kwa urahisi ukilinganisha na mtu mwenye ujuzi.

Mfumo wa malipo kwa awamu una lengo la kuhakikisha mwanachama anaendelea kuwa na sifa za kupata pensheni ya uzee. Kama kiasi chote kingetolewa mara moja, kuna hatari ya mwanachama kufika umri wa kustaafu bila kufikia michango ya miezi 180 inayotakiwa kwa ajili ya pensheni ya uzee.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Inachukua Muda Mwingi Kwa Watu Kupata Mafao Yao Kutoka NSSF, PSSSF?

Hivyo, malipo kwa awamu yanasaidia kulinda michango iliyopo ili mwanachama awe na nafasi ya kufanikisha sifa za pensheni ya uzee.

Fao la kukosa ajira ni muhimu sana kwani hutoa msaada wa kifedha kwa kipindi cha mpito baada ya kupoteza ajira. 

Utolewaji wa fao hili pia hakupunguzi michango ya awali kwenye mfuko. Kwa mfano, kama ulikuwa na michango 20, ukalipwa fao la kukosa ajira, lakini hukuchukua kiasi chote, ukipata ajira mpya, utaanza kuchangia kuanzia mchango wa 21 na kuendelea.

Mwisho, ni muhimu kukumbuka kwamba fao hili la kukosa ajira ni haki ya mwanachama aliyepoteza ajira kwa sababu halali zilizopo kwenye sheria. Mchakato wa kudai fao hili unahitaji nyaraka zinazothibitisha hali ya kuachishwa kazi kama barua ya kusitishwa kwa ajira.

Thomas Mwakibuja ni mtaalamu wa hifadhi ya jamii. Kwa maoni, anapatikana kupitia thomasmwakibuja@gmail.com au +255 767 879 281. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts