Dar es Salaam. ‘Hatuwezi kuondoa umaskini kama hatuwezi kuwaondoa wakulima wadogo kwenye umaskini,’ hii ni sehemu ya nukuu yenye maana kubwa ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliyoisema Mei 21, 2025, wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/2026.
Bashe alikuwa akiliomba Bunge liidhinishe Shilingi trilioni 1.24 kama bajeti ya wizara hiyo muhimu sana hapa nchini, ambapo asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo kwa ajili ya kuendesha maisha yao.
Sekta ya kilimo imekuwa ikikua vyema miaka ya hivi karibuni, ambapo ukuaji wake umeongezeka kutoka asilimia 2.6 mwaka 2021, hadi asilimia 4.2 mwaka 2023, na unatarajiwa kufikia asilimia tano mwaka huu.
Lakini pia, mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi kutoka Tanzania yalifikia Dola za Kimarekani bilioni 3.54 katika mwaka 2023/24, kutoka Dola bilioni 2.3 mwaka 2022/23.
Mei 22, 2025, Bunge lilipitisha bajeti ya Shilingi trilioni 1.242 kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/2026, kiwango hiki kinaendana na bajeti iliyopitishwa mwaka 2024/25, ambapo Bunge lilipitisha bajeti ya Shilingi trilioni 1.249 pia.
Hali hii inakuwa ni tofauti na miaka minne iliyopita kabla ya mwaka huu, ambapo bajeti ya wizara hii muhimu ilikuwa ikiongezeka kila mwaka. Kwa mwaka 2021/2022 wizara hii ilipewa bajeti ya Shilingi bilioni 294, kwa mwaka 2022/2023 wizara hii ilipewa bajeti ya Shilingi bilioni 751.1 na kwa mwaka 2023/2024 wizara hii ilipitishiwa bajeti ya Shilingi bilioni 970.78.
SOMA ZAIDI: Uchambuzi: Bajeti ya Wizara ya Kilimo 2024/25 Inaakisi Umuhimu wa Sekta ya Kilimo?
Suala la bajeti ya mwaka huu kutoongezeka limetuachia maswali kwamba je, tumefikia sehemu nzuri ya kuwaondoa wakulima wadogo kwenye umaskini, kiasi kwamba haihitajiki kuongeza pesa nyingine zaidi kwa ajili ya kulihudumia kundi hili kubwa?
Na pia suala hili limetoa tahadhari kwa bajeti ijayo kwamba ni kitu gani kitatokea? Pengine inaweza kupungua kabisa, lakini hilo ni suala ambalo tutalijadili mwakani bajeti itakapowasilishwa bungeni.
Kitu kingine kilichotutia wasiwasi kwenye bajeti hii ni kuendelea kushuka kwa fedha zilizoidhinishwa na kutolewa kwa wizara hii kwenye bajeti za miaka mitatu mfululizo iliyopita.
Kwa mwaka 2022/2023 fedha zilizoidhinishwa zilikuwa ni asilimia 64 ya bajeti yote. Kwa mwaka 2023/2024 mpaka kufikia mwezi Aprili, fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na kupokelewa zilikuwa ni asilimia 54 ya bajeti iliyopanga.
Hali imeendelea kuwa mbaya kwani kwa mwaka 2024/2025 hadi mwezi Aprili, yaani miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha kumalizika, Wizara ya Kilimo ilikuwa imepokea asilimia 53.19 ya fedha zote ambazo ilipanga kutumia kwa mwaka huo.
Mwenendo huu wa kushuka unatia shaka zaidi na kuacha maswali kwamba je, Serikali ina nia ya dhati ya kuwaondoa wakulima wadogo kwenye umaskini kama fedha inazopanga kuwapeleka haipeleki kwa kiasi kikubwa.
Ruzuku kwenye pembejeo na zana za kilimo
Kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2025/2026, wizara hiyo imepanga kutoa huduma za zana za kilimo, ambapo wakulima watapewa huduma hiyo kwa bei ya ruzuku.
Ili kutekeleza mpango huo, wizara hiyo imeeleza kwamba itaanzisha vituo 1,000 vya kutoa huduma hiyo, itanunua matrekta 10,000 na zana zote za msingi za kufanyia kazi mashambani, ‘power tiller’ 10,000 na mashine za kuvunia na kukaushia.
SOMA ZAIDI: Bajeti Wizara ya Kilimo Inaakisi Umuhimu wa Kilimo Tanzania?
Wizara imeendelea kueleza kwamba itatoa mafunzo kwa waendesha mitambo ya kilimo kwa kushirikiana na wadau wengine kama Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), wasimamizi na watoa huduma 500.
Vilevile, wizara hiyo imesema kuwa ili kufanikisha suala hili itaanzisha kituo kimoja cha kitaifa ambacho kitakuwa na zana zote za msingi kwa ajili ya kusafisha na kusawazisha mashamba, uchimbaji wa visima na mabwawa na kutoa mafunzo.
Mradi huu ambao umebainishwa kuwa utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu unaweza kutoa picha ya kumgusa mkulima mdogo kama utafanikiwa kuanza kutekelezwa kuanzia kwenye bajeti ya mwaka huu.
Hii ni kwa sababu wakulima wadogo wanakabiliwa na changamoto za matumizi ya dhana duni za kilimo. Hivyo, endapo mpango wa kutoa ruzuku kwenye zana hizo utafanikiwa huenda ukatoa naafuu kwa wakulima hao na kuwawezesha kuwainua kichumi.
Umwagiliaji
Asilimia 30.7 ya bajeti yote ya Wizara ya Kilimo ya mwaka huu inatarajiwa kuelekea kwenye Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Tume hiyo imeomba kuidhinishiwa Shilingi 382,138,408,000. Kati ya fedha hizo Shilingi 308,721,961,000 ni fedha za maendeleo na
Shilingi 73,416,447,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Huu ni muendelezo wa wizara hii kuwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kutoa fursa kubwa zaidi kwa wakulima kulima kwa majira yote, hasa kipindi cha kiangazi ambapo mvua huwa hazipo kabisa na maeneo yanayopokea kiasi kidogo cha mvua.
Kwa mwaka huu wizara imepanga kuwa fedha hizo za kuinua kilimo cha umwagiliaji zitatumika kutekeleza miradi 768 kati ya 780 iliyoanza kutekelezwa mwaka 2022/2023, 2023/2024 na 2024/2025.
Kazi kuu zilizopangwa ni ujenzi wa skimu mpya 60 zitakazomwagilia jumla ya hekta 147,433.46 pamoja na ukarabati wa skimu 41 zenye hekta 72,175. Ujenzi wa mabwawa 19 yenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 326,449,973 utaendelea sambamba na kuanza ujenzi wa mabwawa mengine 28 yenye ujazo wa mita 487,361,277. Pia, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mabwawa 65 utaendelezwa.
Wizara imepanga kujenga skimu katika mabonde 14 ya kimkakati na kukamilisha usanifu wa kina katika mabonde mengine nane. Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu 429 utafanyika, na ujenzi au ukarabati utaanza kwa skimu 98 ambazo tayari zimekamilishiwa usanifu. Miradi hii inalenga kuongeza tija katika kilimo kupitia matumizi bora ya maji.
Mpango kazi wa kukamilisha mpango wa kukiinua kilimo cha umwagiliaji kupitia maandishi unaonekana kunyoka vyema. Suala ambalo linaweza kutia ukakakasi ni kuwa ili kukamilisha haya yote je, Serikali itapeleka fedha zote hizi kama ilivyopangwa kwa mwaka huu?
BBT
Mwaka 2025/26, kupitia programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), Wizara ya Kilimo imetenga fedha na kuweka mipango mahsusi ya kuwawezesha vijana na wanawake katika sekta ya kilimo.
Wizara kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetenga dola za Marekani milioni 35 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana na wanawake.
Aidha, kiasi cha Shilingi bilioni 17 kimetengwa kwenye dirisha la ‘guarantee scheme’, ambacho kitasaidia kutoa mikopo yenye jumla ya thamani ya Shilingi bilioni 51 kwa riba isiyozidi asilimia saba.
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
Kwa mwaka huo, wizara itatambua na kutwaa hekta 80,000 katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kilimo-biashara. Uwekezaji utaanza katika shamba la Mapogolo huko Chunya, mkoani Mbeya kwenye ekari 20,000 kati ya 57,000 zilizopo, ambapo kutajengwa visima, mabwawa, nyumba za vijana na ghala.
Kwenye mpango huu wa BBT wizara imepanga pia kuchimba visima 500 vya umwagiliaji vitakavyomwagilia eneo lenye ukubwa wa hekta 30,393.39 katika halmashauri 178 nchini na kunufaisha wakulima 58,903.
Hii ni mipango mizuri pia ambayo inalenga kuwawezesha wanawake na vijana waliopo kwenye mnyororo wa sekta ya kilimo. Hata hivyo, haya yote ayanweza kufanikiwa pia kama changamoto ambazo The Chanzo iliziripoti mwaka jana kwenye mradi wa BBT Dodoma zitakuwa zimetatuliwa na kuzuia zisitokee kwenye miradi mingine.