Fao la Urithi ni moja kati ya mafao yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania, PSSSF na NSSF, kwa wategemezi wa mwanachama aliyefariki dunia akiwa kazini. Lengo kuu la fao hili ni kuhakikisha kuwa wategemezi wa marehemu wanaendelea kupata msaada wa kifedha baada ya kifo cha mpendwa wao aliyekuwa mwanachama wa mfuko.
Kwa mujibu wa sheria, wategemezi wanaostahili kulipwa ni mjane au mjane wa marehemu, watoto wa marehemu walio chini ya umri wa miaka 18, au chini ya miaka 21 ikiwa wanaendelea na elimu, na wazazi, au ndugu, wa marehemu waliopitishwa na mahakama iwapo hakuna mjane, au mgane, wala watoto wa marehemu.
Malipo ya fao la urithi hulipwa kwa asilimia ya mafao ambayo marehemu angepokea. Kisheria, mjane, au mgane, hulipwa asilimia 40 ya mafao ya marehemu, na ikiwa wapo zaidi ya mmoja, hugawana hiyo asilimia kwa usawa.
Mtoto, au watoto, hulipwa asilimia 60 ya mafao, ambapo ikiwa ni zaidi ya mmoja, hugawana kwa usawa. Ikiwa yupo mjane, au mgane, peke yake, au mtoto pekee, hulipwa asilimia 100 ya mafao hayo.
Muda wa kulipwa kwa fao la urithi unategemea hali ya mwanachama aliyefariki. Kwa mwanachama aliyefariki bila kutimiza miaka 15, au miezi 180, ya uchangiaji, wategemezi hulipwa kiasi cha mkupuo, au Special Lump Sum kwa kimombo, kulingana na michango ya marehemu.
SOMA ZAIDI: Fao la Kukosa Ajira ni Nini, na Nani Anastahili Kulipata?
Kwa mwanachama aliyefariki akiwa amekamilisha miezi 180 au zaidi, wategemezi hulipwa Kiinua Mgongo, au Commuted Pension Gratuity, na pensheni ya kila mwezi.
Mjane, au mgane, mwenye miaka 45 au zaidi hulipwa pensheni ya kila mwezi hadi atakapofariki au kuoa, ama kuolewa, tena. Kwa mjane, au mgane, ambaye hajatimiza miaka 45 na ana watoto chini ya miaka 15, naye pia hulipwa pensheni ya kila mwezi. Watoto wa marehemu hulipwa pensheni ya kila mwezi hadi kufikia miaka 18 kama hawasomi, au hadi kufikia miaka 21 kama wanaendelea na elimu.
Fomula ya ukokotoaji
Kikokotoo cha malipo ya fao la urithi kwa mwanachama aliyefariki akiwa amechangia zaidi ya miaka 15, au miezi 180, hufanyika kwa kutumia fomula maalum.
Kwa mifuko ya PSPF na LAPF, kiinua mgongo hukokotolewa kwa kutumia fomula: 1/580 x miezi ya uchangiaji katika mfuko x wastani wa mishahara bora ya miaka mitatu ndani ya miaka 10 kabla ya kustaafu/kufariki x 0.40 x 12.5.
Hapa, 1/580 ni kikokotoo limbikizi, 0.40 ni asilimia 40, na 12.5 ni makadirio ya miaka 12.5 ya kuishi baada ya kustaafu.
SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo Kuhusu Kikokotoo Kipya cha Asilimia 33
Pensheni ya kila mwezi hukokotolewa kwa fomula: 1/580 x miezi ya uchangiaji x wastani wa mishahara bora ya miaka mitatu x 0.60 x 1/12, ambapo 0.60 ni asilimia 60 na 1/12 ni wastani wa kitakacho lipwa kila mwezi.
Kwa mwanachama aliyefariki na alikuwa akichangia mfuko wa PPF/NSSF au GEPF, wategemezi wake watalipwa asilimia 35 kwenye malipo ya mkupuo na asilimia 65 kwenye malipo ya kila mwezi.
Kama alichangia mifuko miwili, PSSSF na NSSF, wategemezi watalipwa na mifuko yote kwa kikokotoo cha ujumuishiaji wa michango, au totalization formula. Ikiwa alichangia miezi 180, wategemezi watalipwa pensheni ya kila mwezi kutoka kwa mifuko yote miwili.
Mafao mapya
Kuanzia Januari 1, 2025, mifuko ya hifadhi ya jamii imeanzisha mafao mawili mapya kwa wategemezi wa mstaafu aliyefariki dunia: pensheni ya mkupuo ya miezi 36 na msaada wa mazishi.
Pensheni ya mkupuo ya miezi 36 hulipwa kwa wategemezi wa mstaafu aliyekuwa akilipwa pensheni ya kila mwezi, ikiwa ni mjane, au mgane, au watoto walio chini ya miaka 18 au 21 ikiwa wanaendelea na masomo.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Inachukua Muda Mwingi Kwa Watu Kupata Mafao Yao Kutoka NSSF, PSSSF?
Malipo yake ni sawa na pensheni ya kila mwezi ya marehemu mara 36. Kwa mfano, ikiwa marehemu alipokea Shilingi 1,000,000 kwa mwezi, familia italipwa Shilingi 36,000,000.
Fao la msaada wa mazishi linalipwa baada ya kupokea taarifa ya kifo cha mstaafu aliyekuwa akilipwa pensheni. Fao hili linatakiwa kuombwa ndani ya siku 30 tangu kifo, na kiasi chake ni Shilingi 500,000 kwa familia ya mstaafu.
Thomas Ndipo Mwakibuja ni mtaalamu wa hifadhi ya jamii. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia thomasmwakibuja@gmail.com au +255 767 879 281.