Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Soko la Maandazi lililopo kata ya Hananasif, wilaya ya Kinondoni jijini hapa wamezitaka mamlaka za halmashauri ya wilaya hiyo kukamilisha ujenzi wa soko hilo ulioanza mwaka 2015, lakini umeshindwa kukamilika hadi leo hii, kasoro inayochochea changamoto mbalimbali kwao na kwa wananchi pia.
Kwa nyakati tafauti, The Chanzo ililitembelea soko hilo na kuona wafanyabiashara wachache wakiwa wanauza bidhaa humo, huku kukiwa na ukosefu unaonekana kwa haraka wa wateja. Miundombinu pia ya soko hilo hairidhishi, ikiwemo soko kutoezekwa vya kutosha, hali inayowafanya wafanyabiashara kunyeshewa kukiwa na mvua.
“Pamoja na kwamba tupo tunafanya biashara, lakini soko bado [halijakamilika],” Pangalasi Joseph, Mweka Hazina wa soko hilo, ameieleza The Chanzo. “Maji hatuna, umeme hamna na hata wiring chooni kule ya umeme bado haijafanyika, unaona, na kuna cape (kofia) za kuzungushia huko kwa ajili ya mvua bado hawajamaliza vilevile.”
“Kwa hiyo, nilikuwa napenda kutoa ushauri kwa Serikali, kama wanatusikiliza, waje kutusaidia ili kuweza kumalizia soko letu,” Joseph alishauri. “Lakini na wafanyabiashara waweze kuja kwa wingi tuweze kufanya biashara.”
Kwa sababu soko hilo limeshindwa kukamilika, wafanyabiashara wengi wa mtaa wa Bwawani, ambapo soko hilo lipo, wameshindwa kuhamia humo na kuweka biashara zao. Badala yake, wengi wao wamejenga vibanda pembeni ya soko hilo, hali inayolalamikiwa na wale waliopo sokoni kama kitu kinachowakimbizia wateja.
SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni
“Kwanza wanatuzunguka watu wa magengeni, wa binafsi, kila mtu na sehemu yake,” Hassan Abdallah, maarufu kama Mzee Mkwanji, mfanyabiashara sokoni hapo, anasema. “Halafu vilevile, hapa hapajaisha kiukamilifu, na watu wenye vizimba humu hawamo kwa sababu biashara imekuwa ngumu. Unaweza kuchukua kizigo kidogo ukakaa nacho mpaka wiki, mpaka vingine vikaharibika.”
Ujenzi wa soko
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kawawa, Adam Omary, Soko la Maandazi lilikuwa ni soko la kawaida tu, lililokuwa likiendeshwa na wananchi wenyewe, kabla ya Serikali kulichukua eneo hilo na kuahidi kuliendeleza kama sehemu ya mradi wa uendelezaji masoko Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.
Omary anasema kwamba Serikali ilitoa Shilingi milioni 37 kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo. Pia, taarifa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni ambayo The Chanzo ilipatiwa inalitaja soko hilo kama baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo halmashuri imetekeleza kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo Shilingi milioni 40 zinatajwa kutumika kuendeleza mradi huo.

Muonekano wa ndani wa Soko la Maandazi unaoonesha uwepo meza tupu upande wa kushoto na wafanyabishara wachache upande wa kulia. PICHA | HIJA SELEMANI.
“Maazimio yetu makubwa kuhusiana na hili soko, tulichokiazimia soko litakapokamilika kabisa – kwamba huduma zote ziko pale, huduma za maji pamoja na umeme – wafanyabishara wote, wanaofanya biashara za aina ya soko, ambao wako mtaani, wote wanatakiwa waingie pale sokoni, hatutaruhusu mfanyabiashara yeyote yule anayefanya biashara aina ya soko kufanya biashara mtaani,” Omary aliiambia The Chanzo.
“Lazima biashara zote ziende pale sokoni,” alisisitiza kiongozi huyo. “Tunaamini kutokana na idadi ambayo tunayo, vile vizimba ambavyo tunavyo pale, wafanyabishara wataingia pale, na hata kwa wale ambao wanaweza kukosa, bado tuna eneo la mzunguko pale, tunaweza kufanya namna yeyote ilimradi wafanyabishara wote wawepo pale.”
Miundombinu duni
Wafanyabiashara wa pembezoni walioongea na The Chanzo wameeleza kwamba hawana shida kuhamia sokoni hapo endapo kama miundombinu muhimu, ikiwemo umeme, maji na vyoo, imeanzishwa sokoni hapo na inafanya kazi vizuri. Wametaja kukosekana kwa miundombinu hiyo kama sababu kuu za wao kutokwenda hapo.
SOMA ZAIDI: Serikali Mara Yaendelea Kuhamisha Wananchi wa Nyatwali, Huku Ukiukwaji wa Haki za Binadamu Ukiripotiwa
“Hatwendi sokoni kwa sababu soko halijamalizika,” Emmanuel William, mfanyabiashara anayeendesha genge pembeni ya soko, anasema. “Kwa mfano, wangeweka umeme pale, ina maana tungefanya biashara mpaka jioni. Muda wa kufunga sisi hapa [gengeni] ni saa nne, [au] saa tano.”
Anasema hawezi kwenda sokoni ambako biashara zinafungwa saa moja jioni, hali inayowafanya wakose wateja wa jioni, hususan wale wanaotoka makazini. Anaongeza: “Pale wangemaliza soko tu, wakaweka na umeme pale inamaana mahitaji yote watu watakuja kama kawaida.”
Maoni haya ya William, maarufu kama Swai, yanaungwa mkono na wafanyabiashara kadhaa wa magenge ambao The Chanzo imeongea nao, wakitaja kukosekana kwa huduma hizi muhimu kama sababu za wao kutokwenda kwenye soko hilo.
Wafanyabiashara hawa pia wanaungwa mkono na wakazi wa mtaa wa Kawawa, wanaosema ni ngumu kufanya biashara sokoni hapo, huku huduma hizo muhimu zikikosekana.
Mwonekano wa nje wa soko la Maandazi kama ilivyoonekana Agosti 8, 2025. PICHA | HIJA SELEMANI.
“Kuna watu wanatafuta maisha sehemu tofauti tofauti, mbali na wanapoishi, mtu unatoka usiku, unarudi usiku, labda saa tatu, [au] saa nne, utakuta hapa hawa jamaa wameshafunga, wameshaondoka,” Ernest John, mkazi wa mtaa wa Kawawa, anasema.
“Tangu hili soko linaanza kujengwa, mpaka hivi sasa, bado halijatengemaa, yaani kwa kwa matumizi ya kibinadamu bado, bado kabisa hayajatimia.”
SOMA ZAIDI: Wananchi Goba Walilia Dampo Bubu Liendelee Kukaa Kwenye Makazi Yao
Alipoulizwa endapo kama ana matumaini yoyote kwamba ujenzi wa soko hilo utakamilika hivi karibuni kama ambavyo Serikali ya Mtaa ilivyoahidi, Mzee Mkwanji, mfanyabiashara katika soko hilo, alisema hana uhakika na hayupo kwenye nafasi ya kusema kwa uhakika.
“Kwa sababu, soko zamani lilikuwa la wananchi wenyewe wanaendesha, tunaendesha taratibu na kujenga kwa nguvu zetu, na wakati huo watu walikuwa wengi wanafanya biashara,” Mzee Mkwanji alieleza.
“Sasa, wale viongozi, mpaka kuhusu Manispaa wachukue hilo soko, hapo nitakuwa siwezi kukupambanulia, katika hilo shauri mimi sikuwemo, na wala si kiongozi kusema kwamba mjumbe labda, au mwanakamati. Isipokuwa biashara tumeanza muda mrefu, lakini tangu kuanza kujenga, halijakamilika.”
Ripoti ya CAG
Kwenye ripoti yake ya mwaka wa fedha 2023/2024, Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) alihusisha hali ya kukwama kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa masoko inayobuniwa na mamlaka za Serikali za mitaa na kutokuwepo kwa mipangilio thabiti, ushirikishwaji wa wadau, na hatari zinazoweza kutokea.

Soko Maandazi likionekana kutokuwa na wateja, kama ilivyoonekana Agosti 8, 2025. PICHA | HIJA SELEMANI.
Kwenye uchunguzi wake wa halmashauri tatu nchini, ikiwemo ile ya Kinondoni ambayo Soko la Maandazi lipo, CAG aligundua utumiaji duni na ufanisi mdogo wa uendeshaji, hali ambayo alibainisha imesababisha upotevu wa mapato na utoaji duni wa huduma.
SOMA ZAIDI: Ujenzi wa Barabara kwa Hisani ya Watu wa Goba Wazua Gumzo Dar
“Masoko yaliyokamilika bado hayajatumiwa kikamilifu,” anaandika CAG kwenye ripoti yake. “Katika baadhi ya kesi, wafanyabiashara wanaendelea kufanya kazi katika maeneo yasiyo rasmi, huku miundombinu ya soko karibu ikiwa tupu, ikionesha kutolingana kwa maamuzi ya uwekezaji na mahitaji halisi ya biashara.”
Ushiriki wa wadau
Richard Temu ni mratibu wa programu ya uraghbishi inayolenga kuchagiza ushiriki wa wananchi katika kujiletea maendeleo kutoka shirika lisilo la kiserikali la Twaweza.
Kwenye mahojiano na The Chanzo, Temu alisema kwamba changamoto kama hizi zinarekebishika kwa kuwepo na ushirikishwaji wa kweli wa wananchi kwenye ubunifu na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama ile ya ujenzi wa masoko.
Temu alisema kwamba haitoshi tu kwa wataalamu wa Serikali kwenda kuwauliza wananchi wana maoni gani kuhusu mradi fulani. Anashauri kwamba ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe kuwajengea wananchi imani kwamba maoni yao yanahitajika na yatathaminiwa ili wasiongee tu kile wataalamu wanataka kusikia, wamalize, waendelee na shughuli zao.
“Serikali izingatie kabisa kwamba katika miradi hii wananchi pia wana matamanio yao, wana mahitaji yao, na kama lengo la hii miradi ni kuwahudumia wananchi, na pale wananchi wako makundi tofauti na mahitaji yao ni tofauti pia.
“Kwa hiyo, kama wanavyoongelea habari ya kuwasikiliza wadau, kushirikisha wadau, basi lazima waweze kuwachambua wale wadau wako wa aina ngapi, ili kila mdau maoni yake yaweze kuingia na kuchangia katika kuboresha ubunifu wa ule mradi ambao unakwenda kuibuliwa pale,” alishauri Temu.
Hija Selemani ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia hijaselemani9@gmail.com.