The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kufungiwa kwa JamiiForums: Hatufanyi Hii Kazi kwa Sababu ni Rahisi, Bali kwa Sababu ni Muhimu

Ndiyo maana mshikamano, na kufanya kazi kwa pamoja, ni muhimu kwenye juhudi zetu za kupigania taifa tunalolitaka.

subscribe to our newsletter!

Nimeyachukua maneno niliyoyatumia kwenye kichwa cha habari cha makala haya kutoka kwenye moja ya vipindi vya YouTube vinavyozalishwa na mchumi na mchambuzi wa Kiingereza, Gary Stevenson, anayeendesha kampeni dhidi ya hatari ya kukua kwa pengo kati ya walionacho na wasionacho nchini humo na barani Ulaya kwa ujumla.

Stevenson alirekodi video hiyo akionekana kuwa na hasira za wazi dhidi ya watu wanaodhani utekelezaji wa mawazo yake, ikiwemo lile la kutoza kodi zaidi utajiri badala ya kazi, ni rahisi sana, kiasi ya kumwambia, wanapokutana naye mtaani, kwa nini asiingie tu kwenye siasa na kwenda kutekeleza mawazo hayo?

Stevenson, mwandishi wa kitabu mashuhuri cha The Trading Game: A Confession, anaoneshwa kushangazwa na kufadhaishwa na kile anachokiita kiwango kikubwa cha ujinga na utoto kinachooneshwa na watu wanaomwambia kauli hizi, akisisitiza kwamba kama kutakuwa na suluhu yoyote dhidi ya tatizo analolipigia kelele, basi haitatoka kwake kama mtu binafsi, bali itakuwa ni zao la watu wengi kufanya kazi kwa pamoja.

“Hakuna sehemu nimewahi kusema kwamba kuwatoza kodi mabilionea itakuwa ni kazi rahisi,” Stevenson, ambaye uchambuzi wake wa masuala ya kiuchumi ni ule ambao hata watu wa kawaida wanaweza kuuelewa, anasema. “Hatufanyi hiki tunachofanya kwa sababu ni rahisi; tunafanya kwa sababu ni muhimu.”

Nilishindwa kujizuia kukumbuka maneno haya ya mchumi huyo anayezua gumzo kubwa hivi sasa nchini Uingereza na kwengineko baada ya kusoma taarifa ya Serikali kulifungia jukwaa la JamiiForums kwa siku 90 kwa kile ilichodaiwa, pamoja na mambo mengine, kuwa ni kuchapisha maudhui yanayoenda kinyume na “maadili ya Kitanzania.”

SOMA ZAIDI: TCRA Yaifungia Jamii Forums Kwa Siku 90. Yatangaza Kuzuia Upatikanaji wa Jukwaa la Jamii Forums Tanzania 

Nimetafakari endapo kama watu wetu waliokabidhiwa dhamana ya uongozi wa nchi wanajipa muda wa kufikiria kabla ya kuchukua maamuzi wanayochukua, hususan kwa kuzingatia athari hasi ambazo maamuzi hayo, mengi yakiwa ya kiholela, yanaweza kusababisha.

Athari za muda mrefu

Mimi binafsi nimehuzunishwa kwa sababu najua maamuzi kama haya yana athari za muda mrefu kwenye maendeleo ya tasnia ya habari Tanzania, ambayo tayari inakabiliwa na changamoto lukuki zinazotuzuia wananchi kunufaika nayo ipasavyo. 

Uamuzi huu wa Jumamosi ya Septemba 6, 2025, wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa JamiiForums naufananisha na ule wa kumpiga mateke mtu ambaye tayari yuko chini amelala.

Nasema hivi kwa sababu, tasnia ya habari ni moja kati ya tasnia yenye uwezo mdogo sana wa kubakisha wafanyakazi kwenye maeneo yao ya kazi kwa muda mrefu. Pia, uandishi wa habari hapa Tanzania ni moja kati ya tasnia yenye uhaba mkubwa wa watu wenye uwezo, umahiri, vipaji na ari ya kufanya kazi.

Hii inatokana na ukweli kwamba watu wengi wenye sifa hizo hawadumu kwenye tasnia, wanaingia leo, wanakaa kwa miezi au miaka michache, halafu wanaondoka kutafuta kazi kwenye maeneo mengine, iwe ni uafisa habari kwenye taasisi za umma au binafsi, au kazi zingine zinazohusiana na kile walichokisomea na kubobea nacho.

SOMA ZAIDI: Waandishi Kujisimamia Haina Maana Sawa na Chombo cha Habari Kumtoa Kafara Mfanyakazi Wake

Watu hawabaki kwenye tasnia ya habari kwa sababu mbalimbali, ikiwemo asili ya kazi yenyewe, ikiwa ni kazi yenye uhitaji wa nguvu na muda mwingi wa mwandishi, mazingira magumu ya kufanya kazi yanayoambatana na ujira na maslahi mengine duni yasiyoendena na uhalisia wa maisha.

Lakini ukweli mwingine mchungu ni kwamba watu hawabaki kwenye tasnia ya habari kwa sababu, nadhani, hii ni tasnia ambayo mtu hategemewi kudhihirisha uwezo, umahiri, kipaji, na ubunifu wa hali ya juu wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku, na akifanya hivyo, anafanya kwa hatari yake mwenyewe, au mwajiri wake. 

Wakati ni sifa hizi hizi ndiyo zingekuwa msingi wa kupandishwa vyeo na kuboreshewa maslahi mengine endapo kama ungekuwa kwenye kada nyingine tofauti na uandishi wa habari.

Adhabu

Utamshawishi vipi mtu mwenye uwezo, umahiri na talanta za kipekee kwamba tasnia ya habari ndiyo nzuri kwake wakati kitendo cha kuandika tu kile ambacho kipo hadharani tayari kinapelekea chombo chake cha habari kufungiwa kwa siku 90?

Nani atathubutu kuja na ubunifu kwenye vyumba vya habari wakati mara ya mwisho gazeti la The Citizen wamefanya hivyo ilipelekea kampuni yake mama, Mwananchi Communications Ltd, kusitishiwa leseni zake zote nne za uzalishaji maudhui kwa siku 30? 

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru, Vyombo vya Habari Vitaendelea Kubaki Kuwa Midomo ya Serikali

Na hapo bado hatujataja hatari za waandishi kukamatwa kiholela na polisi na kuwekwa ndani, au, mbaya zaidi, hata kupotea katika mazingira ya kutatanisha na usipatikane tena, ukiiacha familia yako njia panda, ikishindwa kujua iweke matanga, au iendelee kuvuta subira kwamba siku moja utarudi.

Kama hivyo ndivyo hali ilivyo, nani anaweza kuwa na uthubutu wa kufanya uwekezaji mkubwa na wa maana kwenye uandishi wa habari za maslahi ya umma Tanzania – badala ya ule wa michezo, filamu, na aina zingine za burudani, ambazo ni sehemu salama za kuzalisha faida bila kukwaruzana na wenye mamlaka?

Na kwa sababu wimbo wa taifa sasa hivi ni kutengeneza mazingira wezeshi ya uwekezaji, wenye mamlaka wanaiangalia tasnia ya habari kama moja wapo ya sekta nyeti ambazo uwekezaji kwake siyo tu unaweza kuchangia kwenye kukuza pato la taifa, bali pia kutatua tatizo kubwa la ajira miongoni mwa vijana?

Kwa ufupi, sekta ya habari kama inavyoratibiwa na kusimamiwa hivi sasa inaifanya isivutie kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu wenye uwezo, na hata kwa wale waliopo kwenye vyumba vya habari tayari ambao kila kukicha wanatuma maombi ya kazi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi na hata Serikalini ili waondokane na kadhia waliyopo.

Siyo habari nzuri

Hii si habari nzuri kwa jamii na umma kwa ujumla, huku malalamiko ya kukosekana kwa uwezo na umahiri kwenye namna vyombo vya habari vinafanya kazi zao yakiwa tayari yanasikika mara kwa mara. Jamii, katika hali inayoeleweka kabisa, inahisi mategemeo yao kwa waandishi wa habari na vyombo vyao vya habari hayatimizwi, au yanatimizwa kwa hali isiyoridhisha.

SOMA ZAIDI: ‘Mhariri Msalabani’ Inatueleza Nini Kuhusu Historia ya Uhuru wa Habari Tanzania? 

Na hii ni bahati mbaya sana, kwani uwezo duni wa vyombo vya habari kwenye kufanya kazi zake, hususan ile ya kuchochea uwajibikaji wa umma, unawaweka wananchi kwenye nafasi dhaifu ya kushiriki kwenye uendeshaji na uamuzi wa masuala ya nchi yao.

Kama kuna taarifa ambazo chombo cha habari kinasita kukupatia kwa kuhofia kufungiwa ina maana unabaki gizani, huku mikono yako ikifungwa, na usiweze kuchukua hatua yoyote kurekebisha hali hiyo ya mambo isiyoridhisha.  

Hali ikiendelea kuwa hivyo, mantiki ya nchi kuwa Jamhuri inapotea, na lengo la kujenga taifa la kidemokrasia, linaloshamiri kwa kutegemea uzalishwaji wa mawazo anui, linabaki kuwa ndoto ya alinacha.

Na ndiyo hapa sasa ningependa kukumbushia umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja kufikia hatma ambayo sote tunataka kuifikia kama taifa. Kama anavyosema Stevenson, kama kutakuwa na mabadiliko yoyote kwenye namna mambo yalivyo hivi sasa, basi hayatatokana na juhudi za mtu mmoja, bali sote kwa pamoja.

Tuendelee kupigania jamii tunayoitaka, tukishikana mikono, huku tukikumbushana kwamba hatufanyi lolote tunalofanya kuelekea lengo hilo kuu kwa sababu ni rahisi. Bali, tunafanya yote hayo kwa sababu tunajua kuna ugumu mkubwa, lakini umuhimu wake unatupa nguvu na ari ya kusonga mbele.

Aluta continua!
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×