The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Waandishi Kujisimamia Haina Maana Sawa na Chombo cha Habari Kumtoa Kafara Mfanyakazi Wake

Kumuwajibisha mwandishi, badala ya chombo chake, baada ya kugundulika kukiuka maadili au sheria za nchi, hakusaidii, kwa namna yoyote ile, kukuza uhuru wa habari Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Jumanne ya Mei 21, 2024, nilipata upendeleo wa kuwa kwenye jopo la watalaamu kujadili hali na mazingira ya uhuru wa habari Tanzania, iliyoandaliwa kama sehemu ya kongamano la kuadhimisha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA).

Nilitumia dakika chache nilizopatiwa na mwendesha mjadala kujibu swali – Uhuru wa habari unaonekanaje haswa? – kwa kubainisha kwamba kwangu mimi binafsi, na kwa uzoefu kutoka nchi nyingine zinazosifika kwa kuwa na uhuru mkubwa wa habari, pamoja na vigezo vya kimataifa, uhuru unamaanisha uwezo na nafasi ya waandishi wa habari kujisimamia wenyewe, badala ya kusimamiwa na Serikali.

Niliwaeleza washiriki, ambao walikuwa ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, kwamba haijalishi dhana ya ‘uhuru wa habari’ inaweza kubishaniwa kiasi gani, Serikali kujipa jukumu la kusimamia maadili ya uandishi wa habari, kama ilivyo hapa kwetu, haiwezi kuendana hata kidogo na kanuni za ‘uhuru wa habari.’

Nilieleza kwamba katika mazingira ambapo Serikali inaweza kufungia gazeti baada ya kuchapisha habari ambayo waziri anadhani ni ya uongo, au ya uchochezi, badala ya kulishitaki gazeti husika katika Baraza la Habari Tanzania (MCT), au hata Mahakamani, kunakinzana moja kwa moja na matamshi ya Serikali kwamba inajali uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wao kufanya kazi zao hapa Tanzania.

Nilisema kwamba hapa nchini kwetu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akishawishika kwamba kuna wakili ameenda kinyume na maadili ya uwakili, haimfutii leseni bali kumshitaki kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili, nikieleza kwamba iko hivyo hivyo pia kwa wauguzi, wakunga na wanataaluma wengine. Nikahoji, kwa nini iwe tofauti kwa waandishi wa habari?

Ufafanuzi

Ni bahati nzuri kwamba Waziri Nape Nnauye, ambaye pia hujitambulisha kama mwandishi wa habari, alichagua kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja nilizoziibua wakati wa mjadala pale alipokuja kwenye mimbari kumkaribisha Majaliwa. Pamoja na mambo mengine, Nape aliahidi kwamba huko ninakopendekeza twende ndiko Serikali inakokwenda, akisema Serikali inafanya kila linalowezekana kuboresha mazingira ya vyombo vya habari nchini.

SOMA ZAIDI: Labda Suluhu ya Serikali Kudharau Maoni ya Wananchi ni Kuacha Kushirikiana Nayo?

Lakini kwenye ufafanuzi wake huo, Nape alizungumza jambo ambalo nahisi tunapaswa kulitahadharisha. Akizungumza kwa kulandana na hoja zangu, Nape alisema kwamba tunakotaka kwenda ni mahala ambapo mwandishi wa habari akikosea, atawajibishwa yeye binafsi badala ya chombo kizima cha habari.

“Kama ambavyo daktari akikosea hatufungi hospitali,” Nape, ambaye pia ni Mbunge wa Mtama (Chama cha Mapinduzi – CCM), alisema kwenye kongamano hilo, “mwanahabari akikosea, atapambana na hali yake, na taaluma yake, wenzake waendelee na kazi. Kwa hiyo, tunaenda huko.” 

Hili ni jambo ambalo lipo ndani ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, 2016, (Kifungu 14(b)) na kutiliwa mkazo kwenye Kanuni za Huduma za Habari, 2017, (Kifungu 22(a) na (b), zinazohusu uwezo wa Bodi ya Ithibati, ambayo wajumbe wake watateuliwa na waziri mwenye dhamana ya habari, kumnyima mwandishi kibali cha kufanya kazi, au press card, na kumtoa kwenye orodha ya waandishi, au roll of journalists, kama atathibitika kukiuka maadili ya uandishi wa habari au sheria za nchi. (Takwa hili la kisheria halijaathiriwa na marekebisho ya hivi karibuni ya Sheria ya Huduma za Habari, 2016).

Sasa labda ukizungumza kama mmiliki, ambao hisia zangu zinanituma kuamini kwamba walisukuma takwa hili liwemo kwenye sheria na kanuni kwani lina maslahi mapana kwao, utaratibu huo kimsingi hauingii akilini hata kidogo ukizingatia namna uandaaji wa habari, au maudhui ya habari, unavyofanyika ndani ya chumba cha habari. 

Kwa wale ambao hawajawahi kupita kwenye chumba cha habari, ni muhimu kufahamu kwamba mchakato wa uzalishaji maudhui ya habari ni mchakato mrefu sana, unaohusisha wadau wengi sana mpaka maudhui kuchapishwa na kuliwa na mlaji lengwa.

SOMA ZAIDI: Bila Uhuru, Vyombo vya Habari Vitaendelea Kubaki Kuwa Midomo ya Serikali

Habari huanza na wazo, ambalo mwandishi anaweza kuja nalo mwenyewe au kupewa na mhariri au hata na chanzo kingine cha habari, kama vile mwananchi. Wazo la habari likipokelewa, mhariri ataenda kuwashirikisha viongozi wengine waandamizi kwenye chumba cha habari, na baada ya kupata idhini ya vikao rasmi, mwandishi anakabidhiwa rasmi kazi ya kuligeuza wazo hilo kuwa habari.

Kwenye mchakato mzima wa kulifanyia kazi wazo fulani, mhariri na chombo husika cha habari, kupitia vikao rasmi ndani ya chumba cha habari, wanakuwa wanafahamu mwandishi anafanya nini kwani huwasiliana na mhariri wake kwenye kila hatua anayochukua. 

Kwa hiyo, kazi inaacha kuwa ya mwandishi wa habari binafsi, na badala yake inakuwa ya chombo kizima cha habari, kampuni nzima.

Uwajibikaji

Sasa niambie, katika mazingira kama hayo, mwandishi wa habari anaachwaje apambane na hali yake, kama Waziri anavyosema, wakati kazi imehusisha mnyororo na mlolongo wa wahusika, kuanzia mwandishi wa habari mwenyewe, mpiga picha, mhariri wake, wahariri wa lugha, wabunifu, viongozi wengine katika chumba cha habari, na wengine wote wanaohusika kuidhinisha maudhui kabla ya kuchapishwa?

Mwandishi wa habari kuachwa apambane na hali yake kunaweza kuwa na faida kwa kampuni kwani haitakuwa sehemu ya kubeba msalaba unaotokana na kutendeka kwa kosa fulani, na wala siyo ngumu kuona kwa nini baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari wanaona hilo ni wazo zuri.

Ni muhimu tufahamu kwamba ni wamiliki hawahawa wanaolalamikiwa kuwafanyisha kazi wafanyakazi wao kwenye mazingira magumu, ikiwemo kulipa mishahara duni, au kutokulipa kabisa mishahara kwa miezi kadhaa, kutaja baadhi tu ya changamoto.

SOMA ZAIDI: Wafanyakazi Wanaogoma Sahara Media Waeleza Masaibu Yao

Mwandishi wa habari kupambana na hali yake pia kunaweza kuwa na maslahi kwa Serikali kwani inapunguza kiwango cha uhasimu ambacho mamlaka za nchi ziko tayari kukabiliana nao.

Serikali inaweza kusita kuichukulia hatua kampuni X kwani mmiliki wake ni kigogo Serikalini au kwenye chama tawala, au ni tajiri ambaye hufadhili shughuli za chama tawala, kama vile kampeni, au hata pengine anaweza kuwa ni mfadhili wa waziri fulani. (Unaweza kusoma hapa nani anamiliki chombo kipi cha habari Tanzania).

Mbali na hapo, mwandishi kupambana na hali yake haichangii chochote kwenye kuimarisha uhuru wa habari. Sana sana, hali hiyo itazidisha hofu na wasiwasi miongoni mwa waandishi wa habari, na hivyo kupelekea kuzorota kwa uwezo wao wa kufanya uandishi wa habari wenye tija na ambao unaweza kuisaidia jamii kusonga mbele.

Mtu anaweza kujenga hoja kwamba mwandishi wa habari anaweza kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari, au sheria za nchi, bila kampuni yake kuwa na taarifa. Inawezekana. 

Lakini inawezekana pia mwandishi kujikuta katika hali hiyo wakati anafanya kazi aliyopewa na mhariri wake. Sheria na kanuni hazielezi ni katika mazingira yapi mwandishi anaweza kutolewa kafara na katika mazingira yepi mwajiri wake atabeba msalaba. 

Serikali inapaswa, kwa kushinikizwa na wadau wote, wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari, wadau wa habari na walaji wa maudhui ya habari, kuboresha uhuru wa habari kwa kuruhusu waandishi wajisimamie wenyewe kupitia vyombo vyao huru, kama vile Baraza la Habari Tanzania (MCT), na siyo na ‘Bodi ya Ithibati’ ambayo waziri ndiyo ataiunda na kusimamiwa na Serikali.

Pia serikali haiwezi kufanikisha hili kwa kuweka mazingira ya chombo cha habari kumtoa kafara mfanyakazi wake na kujidanganya kwamba kufanya hivyo ni kuimarisha uhuru wa habari Tanzania. 

Waandishi pia wasikubali hili kutokea, na wanapaswa kusimama imara kudai mabadiliko ya kisheria na kikanuni kuondoa uwezekano wa ‘mabosi’ wao kuwatoa kafara ili kujikinga na matokeo ya kazi za chombo cha habari husika.


Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *