The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Tukienda Kufurahia Mbuzi Choma Msalato, Tukumbuke Pia Kuhimiza Uwekezaji Kwenye Afya ya Mifugo

Ugonjwa wa wanyama siyo tu unahatarisha afya na maisha ya Watanzania, bali pia chumi zao zinazotegemea uuzwaji wa mazao ya wanyama hao.

subscribe to our newsletter!

Hivi karibuni nikiwa Dodoma nilialikwa na familia ya rafiki zangu Kwenda kula nyama choma ya mbuzi huko Msalato “Mnadani.” Nimefika minada mingi kutafiti, lakini sikuwahi kufika mnada wa Msalato. 

Baada ya kufika huko, nilielewa kwa nini haikuwahi kunipitikia kwamba Msalato haikuwa mnada kwa tafsiri rasmi ya minada ya mifugo ambako wanauza na kununua wanyama walio hai kama ilivyozoeleka, ila wanyama hununuliwa kutoka minada mengine na vijijini na kuletwa pale kwa ajili ya kuchinjwa na kuuzwa kama mazao ya mifugo.

Tulifika pale majira ya saa moja jioni, njiani nilikua na shauku ya kujua mnada gani huu unafanya kazi usiku huu, si tutakuta nyama nzuri zimeisha? Hapa hapakuwa kama minada mingine niliyokuwa nikiiwaza kichwani mwangu ambapo mida hiyo watu huwa ndo wanamalizia kufungasha!  

Kilichonishangaza ni kwamba nilipofika pale nilikuta umati mkubwa wa watu na magari kiasi kwamba hata sehemu za kupishana ilikuwa hakuna, na maegesho ya ya magari yakiwa ni ya kutafuta. Ikabidi niulize, kwani huu mnada huwa unaanza na kuisha saa ngapi? 

Nikaarifiwa kwamba huanza asubuhi sana, majira ya 12 asubuhi kwa kuchinja na maandalizi, na kuanza kuchoma nyama, halafu kuanzia saa tano watu wanaanza kuwasili, na mnada huanza kuchanganya kuanzia saa kumi. Kwa hiyo, muda tuliofika ndo ilikuwa wenyewe haswa, na watu huisha majira ya saa sita usiku! 

Shauku ya utafiti

Harakaharaka nikapa shauku ya kufanya utafiti, nikianza kuwaza kimahesabu, ikiwemo kujiuliza hawa watu wote niliwakuta mnadani hapo walikuwa wanatoka wapi, na nani anafanya nini?

SOMA ZAIDI: Kutibu Wanyama Wetu Ni Kulinda Afya, Ustawi Wetu Kama Binadamu 

Nikatamani kuelewa mnyororo mzima wa thamani kwa yanayoendelea pale mnadani, na kwa sababu kilichonipeleka pale ni nyama ya mbuzi nikasema nijikite kwenye hilo zao moja kwanza. Nikajulishwa kwamba mnada ule ni mahususi zaidi kwa “mbuzi choma,” japo kuna mazao mengine ya mifugo kama ng’ombe na kuku inayouzwa pia. 

Basi tukafika kwenye banda mojawapo ambalo wenyeji wangu walikua wamepazoea, tukachagua nyama ambayo tumeipenda, kisha tukaelekezwa pa kwenda kukaa. Kutokana na wingi wa watu, inabidi uambatane na mhudumu wa banda husika ili muuzaji ajue ulipokaa ili aweze kuja kukuhudumia kitoweo kitakapokuwa tayari.

Basi nilipokaa tu nikaanza utafiti wangu usio rasmi kuhusu huu mnyororo wa thamani ambao niliumalizia kwa kuwapigia wadau mbalimbali wanaohusika na mnada ule ili nipate taarifa zenye uhalisia zaidi.  

Wadau mbalimbali

Nikajifunza kwamba kuna wadau mbalimbali ambapo kila mmoja ana kazi yake mahususi na inafanyika kwa ufanisi mkubwa. Inakadiriwa kwa wastani wanachinjwa mbuzi wasiopungua 400, ambao ni wastani wa kilo zaidi ya 4,000, kwa siku.

Pale kwenye banda la nyama kuna mmiliki wa banda, wachoma nyama sio chini ya wawili, na wahudumu wa wateja. Meza tulizokalia zilikuwa zinamilikiwa na mtu mwingine ambapo alikua akikodisha Shilingi 1,000 kwa meza na Shilingi 300 kwa kiti kwa siku. Halafu kuna wauza vinywaji baridi na vikali, ugali, chipsi na kachumbari vya kusindikizia nyama.

SOMA ZAIDI: Afya Moja Ni Nini Na Kwa Nini Ujali Kuhusu Ufanisi Wake? 

Baada ya kula kuna wakusanya mabaki ya mifupa na chupa za plastic. Hawa nao wana mnyororo wao; wale wakusanya mifupa wanauza kwa wanaofuga mbwa majumbani kwa wastani wa Shilingi 1,000 au 2,000 kutegemeana na makubaliano, na wale wa chupa wanaenda kuuza kwa kilo kwenye vituo vya ukusanyaji. Kwa hiyo, hakuna kinachotupwa.

Pia, kuna waburudishaji, kama vile wanenguaji na wacheshi, bila kusahau wahubiri injili wenye vipaza sauti. Yaani, kuna mpaka kutoa sadaka ukilielewa neno.

Vilevile, kuna waosha magari ambapo nikaja kujua kwamba magari zaidi ya 500 hupaki hapo. Kwa sisi tulikaa masaa mawili, kwa hiyo, kwa wastani huo kila gari linachangia Shilingi 1,000 kwenye maegesho.  

Kuna wauza mbogamboga na bidhaa za nyumbani ambao si sehemu ya moja kwa moja kwenye mnyororo ila ni wanufaika. Bila kusahau huduma ya maliwato ambapo mtu huchangia Shilingi 500.

Kwa kifupi, kwa masaa mawili tuliyokaa tulihudumiwa na watoa huduma wasiopungua watano. Baada ya utafiti wangu mfupi – bila shaka na kushiba nyama! – nikatafakari jinsi gani mifugo, hasa midogo kama mbuzi, inaweza kuwa na mnyororo uliosukwasukwa namna ile wenye kuajiri na kukutanisha watu wengi kiasi kile.

Wadau walinijulisha inakadiriwa wastani wa watu 10,000 hukusanyika eneo lile kila siku ya Jumamosi ya kila wiki.

Afya ya mifugo

Lakini je, kwa kiasi gani tunajali afya ya mifugo hiyo? Ikitokea ugonjwa, au tishio lolote la kiafya, litakalosababisha mnada ule ufungwe, unakua umezima mnyororo mzima, hivyo kuathiri Uchumi wa mtu mmoja moja, na mapato ya Serikali. 

SOMA ZAIDI: Wananchi Waishio Bonde la Mto Msimbazi Hatarini Kupata Tatizo la Usugu wa Dawa

Lakini pamoja na kwamba matukio ya kufunga minada na maeneo kama hayo ni nadra, mifugo inapougua huko shambani hupunguza uzalishaji. Mfano kuna magonjwa kama sotoka ya mbuzi na kondoo na ugonjwa wa mapafu ambayo husababisha kati ya asilimia 50 hadi 90 ya vifo vya wanyama kwenye zizi kama hatua stahiki zisipochukuliwa kuudhibiti, achilia mbali hasara zitokanazo na kutupa mimba, na kupungua uzito!

Hivyo basi, ili tuendelee kufurahia ulaji wa nyama, huku Watanzania wenzetu wakijipatia kipato, ni muhimu Serikali na wadau wengine kuwekeza kwenye kulinda afya ya mifugo kwa humasisha na kusimamia uchanjaji.

Kwa sasa kuna kampeni ya kitaifa inaendelea ya uchanjaji wa mifugo dhini ya magonjwa ya homa ya mapafu ya ng’ombe, sotoka ya mbuzi na kondoo na kideri  kwa kuku.  Hivyo, ni muhimu kuhamasishana kufanikisha zoezi  hili ili tuweze kufaidi mazao ya mifugo!

Dk Janeth George ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na mtafiti mkereketwa wa uchumi wa afya ya wanyama na binadamu. Pia, huchambua mifumo ya afya. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia jnthgrg10@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×