Jamani, nilifikiri kwamba nikificha makengeza yangu, hatimaye watu watasahau. Nilikuwa nimejikita kumaliza riwaya, na asikuambie mtu, riwaya ni dikteta, inadai usalimu amri mbele yake na kuacha shughuli zote nyingine hadi umalize. Ndiyo maana nimetoweka, riwaya haitaki kuniacha.
Basi kumbe sivyo. Kuna yule jamaa mbabembabe anayeitwa Musa Lendo, ambaye alikuwa ananisumbua tangu zamani. Hana simile, hana ustaarabu, ni ubabeubabe tu. Basi, baada ya muda wote huu, akanifuata kwa mara nyingine, tena kwa mbwembwe kwelikweli.
Kama kawaida yake, haridhiki kuwaburuza watu tu, hata milango ni adui yake. Hapiga hodi, apiga teke badala yake na kuingia kama vile mtekaji au ICE wa Marekani. Akanikuta naangalia kipakatalishi changu, nikitafakari jinsi ya kumaliza riwaya.
“Bila shaka unaandika uhaini kama kawaida yako.”
“Hapana, naandika riwa …”
“Nyamaza. Enzi zako zimekwisha.”
“Una maana gani?”
“Si ulikuwa unalilia demokrasia na haki za binadamu kama mabwana zako za Ulaya. Sasa unawaona?”
“Nawaona kitu gani?”
“Watawala Bwana. Watawala ni watawala tu, na nyinyi wote ni wakutawaliwa na kuliwa tu.”
Kwa kweli nilikasirika.
“Sasa wewe unakuja hapa na kelele zako, unavunja mlango wangu na amani yangu. Nikueleweje?”
“Mimi ni mtawala Bwana. Naweza kufanya lolote nipendalo na huwezi kunizuia. Angalia huko kwa mabwana zako.”
“Sina mabwana miye.”
“Unao. Eti haki za binadamu, eti demokrasia. Huoni wamekutupa? Siku hizi ni haki za mabavu, mengine upumbavu tu.”
Akanisukuma kwa nguvu nikae kwenye kiti changu bila kutaka.
“Kaa chini nikueleweshe. Tuko katika enzi za mabavukrasia.”
Akaanza kuimba, huku akikanyagakanyaga sakafu na buti zake hadi nyumba ikatingishika.
Nawapenda watawala,
Hawana halahala,
Nyie nyote falafala.
“Si umeona yanayotokea? Nyinyi mnalalamika eti jukwaa lenu limefungwa kwa miezi mitatu. Mabwana zako, wanatamka tu, waziwazi, hawampendi fulani, kipindi chake kinafutwa papohapo. Wanadai wanatetea uhuru wa kusema. Wameonesha kwamba njia ya kutetea uhuru wa kusema ni kuwaziba mdomo wengine wanaosema vingine.
SOMA ZAIDI: Kama Tanzania Ingekuwa Timu ya Mpira Unayoshabikia, Bado Ungeipongeza Hata Kama Inakosea?
“Wenye uhuru wa kusema ni wao, wakisema wao. Tena wakisema wao, wanaweza kusema chochote, kumbagua yeyote, kumtisha yeyote, kusema uongo wowote pia, hata kupendekeza kuua wasio na makazi, ili mradi ni wao. Lakini ole wake akisema asiye mtawala. Ataona cha mtema kuni hadi ateme meno. Kunyamazishwa, kusingiziwa, kutekwa, kupotezwa, kushitakiwa ili mradi uhuru wake wa kusema usiingilie uhuru wao.
“Kweli Bwana, angalia mabwana zako. Si unadai hawa ni walimu wetu wa demokrasia. Wakiweza kufanya wao, kwa nini sisi tusifanye? Uhuru wa kusema hutegemea nani anasema.”
Akaanza kuimba tena:
Nawapenda watawala,
Na raha za kutawala,
Kutumia nguvu ya dola,
Na nguvu ya dala,
Dhidi ya mafala.
Akaninyanyua kwa nguvu.
“Naam, kuwa mtawala ni raha sana. Mtawala hana hata haja na kamusi, maana anaweza kugeuza neno lolote kuwa na maana anayoitaka. Zamani neno gaidi lilieleweka vizuri. Alikuwa na silaha, au vitu vingine, na alijua jinsi ya kutumia hizi kuwaangamiza wengine, hasa wananchi wa kawaida.
SOMA ZAIDI: Watawala Tanzania Wana cha Kujifunza Kwenye Kisa cha Mfalme Henry II wa Uingereza na Askofu Thomas Becket
“Lakini siku hizi, wamegeuza kamusi chini juu. Hata kutamka jina la nchi ni ugaidi. Huko kwa mabwana zako wa zamani wanaojidai watetezi wa uhuru leo mtu akitamka neno Palestina ni kosa la jinai, hivyo wazee wa miaka themanini, watu kwenye viti mwendo, wachungaji kanisani, wote wasio na silaha na wengine bila hata uwezo wa kutumia silaha wamekamatwa kwa sababu watawala wanatawala maneno pia.
“Na kama hawa walimu wetu wa utawala bora wanaweza kufanya hivyo, sisi ni nani kukataa? Ndiyo maana kwetu ni marufuku kutaja jina la nchi iliyopinduliwa na kizazi kipya. Hata neno uhaini tunaweza kulitafsiri tunavyopenda vivyohivyo.
Lakini huu ni mfano mdogo tu. Watawala wanaweza kubariki uvamizi wa nchi nyingine. Wenzao wanaua maelfu ya watoto eti wana haki ya kulinda nchi yao kwa kuweka mpaka mpya wa makaburi ya watoto? Unaweza kufanya mauaji ya kimbari na bado kudai kwamba ni wewe unayeumia na kuwaita wasiokubali wabaguzi wahedi.
Naam. Watawala wanapenda sana matumizi ya bunduki, wakitumia wao lakini, ikitumika dhidi yao, au dhidi ya wenzao, au hata kubebwa tu kujihami, wanalaani kufa na kupona. Na wana uwezo wa kugeuza nyekundu iwe buluu na buluu iwe nyekundu.
Wauaji wote wa ndani, walioua kanisani, au shuleni, au hata chekechea wametoka kwenye kundi lao, au chama chao, au rangi yao, lakini kwa kuwa hawana haja ya kamusi, wanadai wauaji wote ni wa kundi lingine au rangi nyingine. Tena wanadai hivihivi bila hata aibu na kufunga mdomo wa wanaosema vingine.
SOMA ZAIDI: Kuna Uchaguzi, Uteuzi na Uchafuzi. Hapa Tanzania Tuna Nini?
Naam, ukiwa mtawala hata Mungu anaonekana kukubali. Wanaenda kanisani kila wiki kusikiliza ufafanuzi wa mtu ambaye alikataa ubaguzi, ukandamizaji, unyonyaji, aliyekuwa tayari kufa ili kubadilisha dunia watu wapendane, lakini haiwagusi watawala.
Wanatoka kanisani na kuendelea na ukandamizaji wao. Wanaona Mungu kweli alisikiliza maombi yao waruhusiwe kufanya hivyo. Na mtu aliyehubiri chuki, ubaguzi wa wazi, aliyeunga mkono mauaji, wanategemea kumtangaza kama mtakatifu. Kweli watawala wana ushawishi wa ajabu sana. Hadi Mungu ananyamaza.
Musa Lendo akacheka kwa nguvu. Hapo nilijiaribu kusema, lakini akanitishia.
Funga lidomo lako. Sijamaliza. Nyinyi mnajidai na huu uchaguzi eti demokrasia. Hujui siku hizi sisi watawala tunafurahia sana uchaguzi maana siku hizi watu wanaweza kupiga kura bila kuchagua. Ona mabwana zako.
Mara wabadilishe mipaka ya majimbo kwa faida yao, mara watishie wasimamizi wa kura, mara wajaze kura feki, mara wawekeane vipingamizi utadhani wanacheza mchezo wa rede. Ndiyo. Siasa si mchezo. Mpirani, eti mmekataa ushindi wa mezani, lakini kwa sisi watawala, ushindi wa mezani ndio mtindo wa kisiasa, oops, mtindo wa kisasa.
Akarudia wimbo wake tena.
Nawapenda watawala,
Na raha za utawala,
Kutumia nguvu ya dola,
Na nguvu ya dala,
Dhidi ya mafala.
SOMA ZAIDI: Kama Sera ya Matibabu Bure Haitekelezeki, Basi Serikali Iache Kudanganya Wananchi
Naam. Mwenye dola ndiye mwenye dala zisizoisha. Anatawala habari, ana uwezo wa kuua mamilioni ya miti kwa ajili ya mabango kila mahali, ana magari lukuki kiasi kwamba anaweza kuwagawia hata wapinzani wasio na nguvu, sawa na kumpa mwenye uzito mdogo mto wa kuweka chini ya fulana yake ili aonekane mpinzani wa uzito wa juu.
Alitaka kuanza kuimba tena lakini nililazimisha kuingilia kati.
“Lakini Musa Lendo unachothibitisha ni kwamba watawala kote duniani si wapenzi wa demokrasia. Lakini demokrasia haitoki juu daima, inatoka chini. Uhuru hizi zilipiganiwa na makundi mbalimbali, wafanyakazi, vyama vya weledi, wanawake, vyombo vya habari, na kadhalila. Na ukiangalia unakosema wewe, hawa wa chini wanaendelea kupigania uhuru wao kufa na kupona. Ndiyo demokrasia.”
Hapa Musa Lendo akacheka tena kwa nguvu.
“Pumbaf. Endelea na mawazo yako ya kijinga. Hata Baba wa Taifa alikiri kwamba Serikali vyombo vyake ni vya ukandamizaji. Na tutavitumia upende usipende.”
Akaondoka na kubamiza mlango tena kama kawaida yake. Sikuwa hata na hamu ya kuendelea na riwaya yangu. Kwa nini wapo watu kama Musa Lendo wakati tunajua nchi yetu ni nchi ya demokrasia? Kwani lazima tufuate mfano mbaya wa mabeberu?
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.