Mara kadhaa ninapokuwa nasikiliza redio za mashirika makubwa ya nchi za magharibi, huwa wakati fulani mtangazaji anawaunganisha na, kwa mfano, mchambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati na kumuhoji kuhusu tukio lililotokea au linaloendelea eneo hilo.
Mtu huyu huwa ana taarifa nyingi kuhusu eneo hilo na hutoa maoni yake kuwa linaloendelea eneo hilo au jambo lililotokea limetokana na kitu fulani kilichowahi kutokea au kilichopo baina ya watu wa eneo hilo.
Huyu si lazima awe anaishi Mashariki ya Kati, bali mtu ambaye amejenga utashi wa siasa za eneo hilo, utamaduni na nafasi yake katika dunia na hivyo kufuatilia habari za eneo hilo na hata kusoma kilichotokea na kinachoendelea kutokea ili awe na ufahamu mpana.
Mwingine ni yule ambaye amesomea siasa za eneo hilo na hivyo anajua sababu za matukio fulani kutokea na wakati mwingine kubashiri yanayoweza kutokea iwapo mambo fulani hayatashughhulikiwa.
Mwingine ni mwalimu wa chuo, mhadhiri au mtu aliyefanya utafiti au anayefanya utafiti wa siasa za eneo hilo na hivyo anaweza kutoa maoni yake kutokana na uzoefu alioupata katika kazi yake.
SOMA ZAIDI: Tumejitahidi AFCON, Lakini Tunajipangaje Upya?
Si rahisi kwa mtu huyu kupigiwa simu na kuombwa maoni yake kuhusu kinachoendelea Ukraine na Urusi, labda kuwe na matukio yanayofanana na hivyo kuombwa kuzungumzia nini kilifanyika wakati tukio kama hilo lilipotokea Mashariki ya Kati.
Na vyombo hivi havifanyi hivyo kwa sababu tu vimeona umuhimu, bali vina sera za ndani zinazoongoza waandaaji vipindi kutafuta watu wanaoaminika katika masuala fulani, ndiyo watoe maoni yao au kuchambua masuala hayo. Je, vyombo vyetu hapa Tanzania vina hizo sera?
Nyenzo za uchambuzi
Uchambuzi ni uwezo wa kutumia nyenzo ambazo mtu anazipata katika nyanja tofauti maishani, kama elimu, ushiriki, ufuatiliaji wa kina kutokana na utashi au kuwa muathirika wa matukio fulani na mengine mengi.
Wale wanaosoma huambiwa kuwa wanapewa nyenzo, au tools of analysis kwa kimombo, kwa ajili ya kuzitumia kupambanua mazingira tofauti ya maisha, yaani hawafundishwi jinsi ya kuishi au kufanya kazi, bali elimu ya maisha.
Hizo nyenzo ndizo wanazozitumia kuchambua mambo mbalimbali yanayotokea katika siasa, majanga ya kijamii kama magonjwa ya mlipuko, mafuriko, vita, michezo, sanaa na mambo mengine mengi ya kimaisha.
SOMA ZAIDI: Usajili Dirisha Dogo Ni Kwa Ajili ya Kuziba Mapengo Tu
Hawa wakipelekwa darasani, hawaendi kufundishwa jinsi ya kuchambua kile wanachoulizwa na vyombo vya habari, bali kujua zaidi kuhusu siasa au matukio ya maeneo wenye uzoefu nayo na mabadiliko ambayo yanaonekana kutokea kwa sababu tayari zile nyenzo wanazo.
Wakati huu ambao Serikali inasema inaangalia uwezekano wa kuanzisha mafunzo kwa ajili ya wachambuzi wa michezo, ni muhimu kutafakari suala hilo. Mitandaoni washaanza kuhoji eti nani atawafundisha hao wachambuzi?
Na baadhi wanatoa maoni kwa kuwataja baadhi ya haohao wachambuzi kuwa ndiyo wawe walimu. Yaani unaona jinsi tatizo lilivyo kubwa; kama Serikali imeona kuwa kuna tatizo, iweje haohao wenye matatizo ndiyo waende kufundisha wengine jinsi ya kuchambua?
Nimetangulia kutoa mifano hiyo ya redio au televisheni kubwa za nchi za magharibi zinavyofanya kuchambua jambo kubwa lililotokea dunia au eneo moja la dunia, zikitumia watu ambao ni wazoefu wa matukio kama hayo au waliosomea au wanaofanya utafiti kuhusu masuala kama hayo au hata baadhi ya viongozi waliowahi kuongoza masuala yanayohusiana na kilichotokea wakati huo.
Hapo unapata uzoefu, mwenendo, mwelekeo, historia na maoni kuhusu tukio hilo linamaanisha nini na watu wategemee nini. Narudia tena kusema, hawa si watalaamu wa kila kitu, bali wa eneo fulani walilojenga utashi wa kujua kinachoendelea au wamesomea.
SOMA ZAIDI: Waamuzi Zanzibar Wametia Doa Kombe la Mapinduzi
Na hawa si waajiriwa, bali huweza kulipwa posho kutokana na redio au televisheni kuchukua muda wao wa kazi nyingine kwa kuwahoji kuhusu kinachoendelea duniani.
Ndiyo maana redio na televisheni za wenzetu zinazorusha matangazo ya moja kwa moja ya mpira wa miguu, hutumia zaidi wachezaji wa zamani kuchambua mechi hizo kutokana na uzoefu wao wa hali ya uwanjani, shinikizo la mashabiki, maelekezo ya makocha, mahusiano ya wachezaji uwanjani na tabia ya baadhi ya makocha.
Hawa hawaingii studio wakiwa sita au watano, labda kama wana uzoefu tofauti, unakinzana au maoni tofauti yenye mrengo mmoja.
Tena hawa hawashindi studio kusubiri kuchambua kila kitu, bali zile dakika zao tisini. Na wala hawaweki kiapo kwamba Manchester United lazima ifungwe na Chelsea, bali hubashiri kutokana na hali waliyoielezea kiuchambuzi.
Ukosefu wa ubobevu
Lakini redio zetu zinafanya tofauti. Kwanza kuna wataalamu wa kila kitu na ambao siku saba za wiki wako tayari kuingia studio kuzungumzia chochote kinachotokea au watakachoulizwa. Kwao kusaka habari zaidi za kilichotokea kwenye mitandao ya kijamii na kwenda kukizungumzia redioni, ndiyo utalaamu wenyewe na si ubobezi katika suala linalojadiliwa.
Imefikia wakati uchambuzi umekuwa wa kuibua habari au kashfa na si wachambuzi kuchambua habari au hiyo kashfa na mazingira yake. Hivi karibuni, kocha wa timu ya taifa alishushiwa tuhuma nzito sana kuhusu uteuzi wa wachezaji kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zinazoendelea nchini Ivory Coast.
SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF
Nilitegemea kasfa kama hiyo iibuliwe na chumba cha habari cha kituo hicho cha redio, ikiwa na ushahidi mwingi halafu wachambuzi waichambue kulingana na uzoefu wao katika masuala ya uteuzi wa timu za taifa, wakitoa mifano mbalimbali ya baadhi ya makocha waliokumbwa na tuhuma kama hizo.
Lakini iliibuliwa na mchambuzi bila ya hata upande wa pili kupewa nafasi ya kujitetea na bila maelezo ya kina na ushahidi. Hapo unajiuliza kuwa hao jamaa walikuwa wanachambua ushiriki wa Tanzania AFCON 2023 au walikuwa wanaibua kashfa ya kilichotokea. Uchambuzi ni nini?
Siku nyingine nilikuwa nasikiliza kipindi kimoja wakati Simba ikielekea kufanya mkutano wake mkuu kwa ajili ya kujadili na kupitisha marekebisho ya katiba. Hawa jamaa walikuwa studio wakijadili muundo mpya wa umiliki bila ya kujua vizuri wahusika ni kina nani katika muundo huo na kila mmoja ana wajibu wa kufanya nini kukamilisha mfumo mpya wa umiliki wa klabu.
Sioni ajabu kwa baadhi ya mashabiki na wanachama wa Simba kutoelewa kinachoendelea hadi sasa, kama ni sehemu ya waskilizaji wa vipindi vya namna hii.
Wapo wanaomlaumu mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la Soka (TFF) kutokana na kufanya vibaya kwa timu ya taifa ya soka bila ya kujua majukumu yake ni yapi. Huzungumza kana kwamba wanajua kwa undani uhusika wake kwenye timu ya taifa, kumbe ni tofauti kabisa.
SOMA ZAIDI: Simba Iongeze Muda wa Maoni Marekebisho ya Katiba
Na wapo ambao wamesomea ualimu wa mpira wa miguu na kuhamishia redioni elimu ile ya mifumo wa mpira kiasi cha kuonekana wanazungumzia dhana ambazo hazionekani kwa macho ya kawaida badala ya kujikita katika kile kinachoonekana na wengi. Inakuwa kama wanatoa taarifa za kiufundi za mechi kumbe wanazungumza na waskilizaji wa kawaida.
Huyu huonekana kama anataka kuonyesha uelewa wake wa mifumo ya mpira kumbe alitakiwa azungumze lugha rahisi inayoeleweka na waskilizaji wa redio na si jopo la ufundi linalojadili mwenendo wa soka la nchi.
Yuko mchambuzi ambaye anakwenda studio kwa sababu yuko zamu na si kwamba amebobea katika eneo fulani. Siku hiyo atachambua chochote. Kama ana ufahamu mdogo kuhusu tukio hilo kubwa la siku hiyo, mambo yataburuzwa kulingana na upeo wake na si kuwapa wasikilizaji au watazamaji ufahamu mkubwa zaidi wa kilichotokea.
Tatizo litakuwa kwako wewe ambaye utajaribu kumpigia simu kumuelewesha kwamba alitakiwa azingatie masuala fulani ambayo ni muhimu kila suala hilo linapoangaliwa. Wenye akili huchukulia ushauri kuwa ushauri, lakini wapumbavu huchukulia ushauri kuwa ni matusi. Jibu utakalolipata litakusaidia kumuelewa yule uliyemshauri.
Tunafundisha nini?
Kwa hiyo, katika mazingira kama hayo, ni lazima kuwe na matatizo katika uchambuzi wa michezo kwa sababu unafanyika kwa mtindo wa bora liende na si kwa nia ya kuwaelewesha zaidi wasikilizaji au watazamaji kuhusu kilichotokea.
SOMA ZAIDI: Kila la Heri Maandalizi ya Stars AFCON 2023
Hawa utawapeleka chuoni ili uwafundishe nini? Elimu waliyopata hadi wamefikia kiwango cha kupewa dhamana ya kutangaza moja kwa moja redioni, haikuwapa nyenzo za kuwawezesha kujua mambo gani ya kuzingatia katika uchambuzi?
Muda walioishi hadi sasa haujawafanya wajenge utashi katika mambo machache na hivyo kuwa na uwezo wa kuyazungumzia kwa mapana na marefu? Uwezo wa kuzungumzia kila kitu wanautoa wapi?
Kama ungeniuliza kuhusu mafunzo kwa wachambuzi, ningesema hayahitajiki bali vyombo vya habari vinahitaji kuwa na mwongozo binafsi wa kitaalamu wa kuweza kuendesha programu zao, kutafuta watu sahihi wanaoweza kujua maudhui yanajengwa na nini na uteuzi sahihi wa watu wanaoweza kuwa wanawachambulia matukio mbalimbali yanayotokea nchini na duniani kwa ujumla.
Si kila mtu anaweza kuwa mchambuzi na si kila mchambuzi anaweza kuchambua lolote. Si kila mchezaji wa zamani anaweza kuchambua mpira, na si kila kocha anaweza kuchambua mechi.
Na hivyo si kila mwandishi wa habari za michezo anaweza kuwa mchambuzi. Binafsi nimeziambia redio siwezi kuchambua mechi bali matukio ya maendeleo ya michezo. Kuna mengi ya kuzingatia ili neno “wachambuzi” lisiwe kera kama linavyozungumziwa sasa mitandaoni.
SOMA ZAIDI: Michezo ni Muhimu Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa Mafanikio
Badala ya kujikita kutafuta jinsi ya kutoa mafunzo kwa wachambuzi, ni muhimu Serikali ikaweka msisitizo kwa vyombo vya habari kujitengenezea utaratibu mzuri wa kutoa maudhui yake ili visiruhusu kila mtu ambaye ni rafiki wa mmiliki, kuwa mtangazaji na mchambuzi.
Serikali haitaweza kufundisha kila kitu. Vitu vingine mtu anavipata kutokana na elimu na uzoefu wake katika maisha na jinsi anavyoweza kuitumia kupambanua mambo. Kadri anavyojikita katika eneo fulani ndivyo anavyobobea na kuanza kuaminika.
Nadhani kuna sehemu ambayo haijakaa sawa na ambayo Serikali imeiona. Hivyo, irekebishwe kwenye vyombo vya habari na si kufikiria suala kubwa kama la mafunzo ya utoaji maoni binafsi.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.