Dar es Salaam. Wananchi takriban 10,000 kutoka mitaa ya Nzasa, Kimwani na Nyeburu, kata ya Zingiziwa, wilayani Ilala, mkoani hapa wanasubiria kwa hamu utekelezwaji wa ahadi ya Serikali ya kuwarejeshea ardhi yao, wakiamini hatua hiyo itakomesha takriban miaka kumi ya mateso yanayotokana na mvutano uliopo kati yao na Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi.
Mnamo Septemba 10, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliwaambia wananchi wa maeneo hayo kwamba kabla ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 27, 2024, Serikali itakuwa imemaliza mvutano huo ambao umekuwa ukiambatana na uharibifu wa mazao, pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu pale maafisa wa uhifadhi wanapojaribu kuwazuia wananchi kutumia ardhi hiyo.
Mpogolo aliihakikishia The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba mgogoro huo ambao unaendelea kuathiri usalama na ustawi wa wananchi hao lazima upatiwe ufumbuzi, akisema hayo ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwa mawaziri wa kisekta. Hatua hiyo itawafurahisha wananchi wengi, akiwemo Ikungasya Musokwa, ambaye amepitia madhila mengi kutokana na mvutano huo.
Kwenye mahojiano na The Chanzo, Musokwa, 64, alisimulia mkasa uliowahi kumkuta alipokwenda kwenye shamba lake lililopo kwenye ardhi ambayo Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi inashikilia ni eneo lake. Ilikuwa ni Mei 16, 2024, pale yeye na mtoto wake wa kiume walipokwenda kwenye shamba lao hilo kwa ajili ya kusafisha.
“Tukawa tumeingia kusafisha [shamba], ghafla lilikuja gari lililokuwa na askari wa maliasili, lilikuwa na watu nane, wakatuzingira,” Musokwa alisimulia. “Walinipiga vibaya mno, hata nilipojaribu kujitetea wakasema kama umeruhusiwa [kuja, kwamba] tatizo limeisha, tupe barua, nikasema siwezi kukupa barua kwa sababu hata wakati wakusema tusimame kulima hamkunipa barua.”
“Wakasema wewe ni muhalifu kama wahalifu wengine, walinipiga kipigo cha mbwa mwitu, [wakisema] kwamba ni afadhali ufe, huna thamani kuliko kuharibu misitu yetu.”
SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro
“Walinipiga mno, ilikuwa ni ngumu kwangu mpaka nikapoteza fahamu, nikazimia,” aliendelea kusimulia Musokwa. “Wakanipeleka mpaka kituo cha polisi Chanika, pale kituoni nilikaa nikapata ufahamu, nikawaambia jamani nina maumivu makali, naomba mnipeleke hospitali nikapate matibabu, kwa sababu hali yangu ni mbaya, wakasema hakuna mtu wa kukupeleka, utajua mwenyewe.”
Mathew Ntilicha, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), inayosimamia Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, ameiambia The Chanzo kwamba hafahamu uwepo wa mgogoro huo wala malalamiko hayo ya wananchi.
“Kwa sababu sisi msitu wetu umehifadhiwa kwa mujibu wa sheria, nyaraka zetu zote zipo, hata ukienda Wizara ya Ardhi utazipata nyaraka za eneo letu,” aliongeza afisa huyo mwandamizi wa TFS.
Kiini cha mgogoro
Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi inapatikana umbali wa kilomita 12 kusini-magharibi mwa jiji la Dar es Salaam. Ikijulikana kwa jina maarufu kama Mapafu ya Dar es Salaam, hifadhi hiyo ina ukubwa wa hekta 12,015, na ni moja kati ya vivutio vikubwa vya utalii jijini humo.
Kiini cha mgogoro kinatajwa kuwa ni uamuzi wa TFS, mamlaka ya kiserikali iliyopewa dhamana ya kutunza na kuhifadhi rasilimali za misitu nchini, kutanua hifadhi hiyo, iliyoanzishwa Septemba 24, 1954, na Serikali ya mkoloni, kwa kuchukua mita 800 za ardhi ambayo wananchi walikuwa wakiitumia kwa shughuli za makazi na kilimo, kwenye miaka ya 1990.
Ramani inayoonesha Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi. Rangi ya njano inaonesha eneo la mita 900 ambalo hifadhi iliiachia, na kijani inaonesha eneo la mita 800 ambalo Hifadhi inadaiwa kuvamia maeneo ya wananchi.
Tangu wakati huo, wananchi walioathiriwa na hatua hiyo wamekuwa wakipambania urejeshwaji wa ardhi yao hiyo, na kuipelekea Serikali kukiri, hapo Mei 26, 2012, kwamba wakati wa uwekaji mipaka ya Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi, upimaji uliingia ndani ya maeneo ya wananchi kwa takribani mita 800, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la Uhuru la siku tajwa.
Lakini licha ya kukiri huko kwa Serikali, Hifadhi ya Msitu wa Pugu Kazimzumbwi imeendelea kuikalia ardhi hiyo, hali inayowasababishiwa wananchi usumbufu na kadhia mbalimbali, kubwa zao zikiwa ni uharibifu wa mazao pamoja na ukiukwaji mwingine wa haki za msingi za binadamu.
“Juzi, Agosti 26, 2024, [askari wa] maliasili walikuja pale [shambani kwangu], wameng’oa mihogo yangu yote, wamekata ndizi na mipapai,” anasema Salumu Faraji, mkulima na mkazi wa Nyeburu.
“Mpaka sasa hivi sisi wananchi wa Chanika tuna wakati mgumu sana,” aliendelea kulalamika mwananchi huyo, huku akilia. “Hata kipande cha muhogo tunakiona sijui kama kitu gani katika maisha yetu. Tunamuomba mama Samia atusikilize wapiga kura wake, tuna wakati mgumu sana.”
Betty Kivela ni mmoja kati ya watu ambao walinunua kiwanja kwenye eneo hilo na kujenga nyumba. Kevela anadai kuwa mwaka 2011 askari wa maliasili walivamia kwenye eneo lake na kuvunja nyumba yake, kisha wakachukua magodoro, kuku, pamoja na ng’ombe aliokuwa akifuga.
‘Sina mahali pa kukaa’
“Mimi sina mahali pa kukaa sasa hivi na watoto wangu, tunapanga tu, tunapata adha, tunashindwa kuishi,” alieleza mama huyo. “Nilikuwa ni mfanyakazi wa Serikali, nilivyostaafu tu, nikaenda nikanunua kule, nikajenga, [lakini] sasa hivi [nimekuwa] ni mpangaji.”
Betty Kivela, mmoja kati ya waathirika wa mvutano unaoendelea kati ya wananchi na mamlaka za uhifadhi, akizungumza na The Chanzo kuhusu kadhia anazokabiliana nazo. IBRAHIM MGAZA.
“Naomba kumuuliza mama Samia, yeye ni mwanamke mwenzangu, na kazi nimefanya Serikalini, nimetumikia miaka yote mpaka nimestaafu, [lakini] mpaka sasa hivi nahangaika, sina mahali pa kukaa, nifanye nini?” alihoji Betty.
Said Seif ni mzee mwenye umri wa miaka 102, anayedai kwamba alianza kumiliki ardhi kwenye eneo hilo lenye mgogoro tangu mwaka 1943 hata kabla ya Serikali ya kikoloni haijatenga eneo la hifadhi, na anasikitika kufanywa “mkimbizi wa ndani” na Serikali yake mwenyewe.
“Hatujaliwi na viongozi, viongozi wote wanaotawala wanatawala wao tu kwa fikra zao, lakini sisi tunaonewa,” alilalama Seif. “Mimi nasema hivyo kwa sababu nimekwishazeeka na kule kwetu mpaka sasa hivi wajukuu zangu, au watoto wangu, hawana mahali pa kuishi, tunahangaika.”
“Aliyetafuta uhuru alituruhusu turudi kwenye vijiji vyetu tulikoishi zamani, lakini wanaokula uhuru hawa kupata wanapata wao sisi tunapunjika,” aliongeza. “Sisi tunanyanyaswa na watu wanaopewa vyeo. Mama Samia anatoa vyeo, [anawaambia] malizeni maswali, wao wakija huku wanasema ‘mbuzi kaangukia kwa muuza supu.’”
Mnamo Januari 13, 2023, aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, akiambatana na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Nickson Simon, mbunge wa jimbo la Ukonga, Jerry Silaa, pamoja na viongozi wengine walifika kata ya Zingiziwa na kufanya kikao na wananchi wa eneo hilo kwa lengo la kutoa suluhu ya mgogoro huo ambao bado ulikuwa ukifukuta.
Kwenye mkutano huo, Makalla, ambaye kwa sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alieleza kuwa Baraza la Mawaziri limekubaliana kuwa kata ya Zingiziwa iwe ndani wa wilaya ya Ilala iliyopo jijini Dar es Salaam, azimio ambalo lilimaanisha kwamba eneo la mita 800 lililopokwa litakuwa limerejeshwa tena.
Lakini mpaka wakati wa kuchapisha habari hii, hakuna mabadiliko yaliyokuwa yametokea, si kutokana na agizo hili, wala lile la Mpogolo, aliyewaahidi wananchi kuweza kurudi kwenye maeneo yao kabla ya Novemba 27. Wananchi wanasema bado hawawezi kurudi kwenye maeneo hayo, na wameiomba Serikali ianze kutimiza ahadi zake.
Mageuzi
Hii siyo kesi pekee inayohusisha migogoro kati ya TFS, na mamlaka zingine za uhifadhi nchini, na wananchi wanaoishi pembezoni ya hifadhi hizo.
Migogoro hii imekuwa mingi sana nchini Tanzania, ikihusishwa na ukatili na ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu, hali iliyoisukuma Tume ya Rais ya Haki Jinai kuhitimisha kwamba inaweza kuwa inatokana na sura za kijeshi ambazo Serikali imeamua kuzima mamlaka hizi.
“Taasisi ambazo zinatekeleza majukumu ya haki jinai, au zinazotoa huduma kwa wananchi zenye taswira ya kijeshi, [ikiwemo] Jeshi Usu la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu, zirejee katika majukumu yake ya awali ya utoaji wa huduma kwa wananchi,” ilisema sehemu ya mapendekezo ya tume hiyo.
“Mafunzo kwa Askari wa Uhifadhi wa Misitu na Wanyamapori yatolewe na Jeshi la Polisi kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.”
Kwa upande wake, Cathbert Tomitho, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiArdhi, shirika lisilo la Kiserikali linalopigania ulinzi wa ardhi na haki za wananchi nchini, anadhani kwamba suluhu ya migogoro hiyo ni kwa mamlaka za uhifadhi kutii matakwa ya kisheria pale zinapoamua kupanua maeneo ya uhifadhi.
“Ukiangalia migogoro yote, ukiwa ni pamoja na huo [wa Zingiziwa], kinachokosekana ni uelewa wa sheria miongoni mwa wale watekelezaji, maana hawaijui ile sheria kwa sababu haifundishwi,” alidokeza Tomitho.
“Kwa mfano, hilo la upimaji wa maeneo, mpango wa matumizi bora ya ardhi, katika vijiji takribani 12,300, havifiki vijiji 5,000 ambavyo vimefanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi,” aliongeza mdau huyo. “Sasa, unategemea vipi migogoro iondoke wakati mpango wa matumizi ya ardhi haujafanyika?”
Ibrahim Mgaza ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia ibrahimmgaza39@gmail.com.