The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Mkwamo wa Kisiasa Nchini: Wakati wa Kujenga Muungano wa Kitaifa Dhidi ya Ukandamizaji ni Sasa

Historia inaonesha kwamba hakuna mfumo kandamizi unaoanguka kwa sababu ya malalamiko yaliyotawanyika ya wale wanaokandamizwa.

subscribe to our newsletter!

Tanzania inapitia kipindi kigumu cha mkwamo wa kisiasa unaotokana na kuvurugwa mfululizo kwa chaguzi za kisiasa, kukithiri kwa matukio ya utekaji, kupotea na kuuawa kwa raia bila uwajibikaji na kuongezeka kwa siasa kandamizi dhidi ya makundi mbalimbali ya kijamii. 

Kuanzia vyama vya upinzani, AZAKI, taasisi za dini, wanafunzi hadi wafanyakazi na wakulima, karibu kila kundi limewahi kuguswa na ukandamizaji kwa namna yake. Hata hivyo, changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza ni kukosekana kwa mshikamano wa pamoja wa kisiasa na kijamii, ambapo kila kundi linaonekana kupambana kivyake dhidi ya ukandamizaji, dhulma na unyonyaji. 

Kongamano la Kitaifa kuhusu mwelekeo na hatima ya taifa lililoandaliwa na ACT Wazalendo, Jumamosi, Mei 16, 2026 katika Hoteli ya Serena limefungua upya mjadala muhimu kuhusu mkwamo wa kisiasa uliopo nchini. Mjadala huo ulijikita kusukuma madai ya ukweli, haki na uwajibikaji kufuatia matukio ya mauaji ya wananchi yaliyotokea Oktoba 29, 2025, pamoja na hali ya kuendelea kwa siasa kandamizi na kudhoofika kwa misingi ya demokrasia nchini. 

Katika kuchokoza mjadala huu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo alitoa uchambuzi na msimamo wa ACT Wazalendo kuhusu taarifa ya ripoti ya Jaji Chande iliyoangazia matukio ya mauaji, hali ya siasa kandamizi kuanzia mwaka 1995 hadi sasa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na taifa ili kujikwamua kutoka katika mazingira ya ukandamizaji.

Jukwaa hili lilikuwa muhimu kwa kuleta makundi haya pamoja katika mazingira ambayo kila Kundi limekuwa likipambana peke yake, likilie peke yake na wakati mwingine likiamini kuwa tatizo ni lake pekee.

Vyama vya siasa vya upinzani wa kweli hasa ACT Wazalendo na CHADEMA vinakabiliwa na mazingira magumu ya kisiasa, lakini bado havijafanikiwa kujenga mshikamano wa kudumu wa pamoja. Kila chama kinaonekana kupambana kivyake, kutoa matamko kivyake na kuendesha mapambano yake kivyake. 

Wakati mwingine kushambuliana sio kwa dhimiri bali kutofautiana mbinu ya kukabiliana na ukandamizaji. Hivyo, badala ya kujenga nguvu ya pamoja dhidi ya mfumo kandamizi, mara nyingi ushindani wa ndani unakuwa mkubwa kuliko mshikamano.

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Kwa Kuiachia Siasa kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, CCM Inaumba Zimwi Litakalokuja Kuitafuna Yenyewe

AZAKI nazo zimekuwa zikikabiliwa na mazingira ya hofu, masharti magumu ya uendeshaji na wakati mwingine kutazamwa kwa jicho la kisiasa. Lakini hata ndani ya sekta hiyo, sauti zimekuwa zikitawanyika. Kila taasisi inapochukua hatua kuhusu haki za binadamu, uwajibikaji au demokrasia, mara nyingi hufanya hivyo kwa upweke wake bila jukwaa pana la kitaifa la mshikamano wa kiraia.

Taasisi za kidini nazo zimepitia wakati mgumu. Pale viongozi wa dini wanapokemea ukandamizwaji wa haki, ukosefu wa umoja au matumizi mabaya ya mamlaka, mara nyingi hukutana na mashambulizi ya kisiasa au tahadhari na vitisho. Lakini hata ndani ya taasisi hizo, hakuna msimamo wa pamoja wenye nguvu unaounganisha sauti za haki kitaifa. Kila dhehebu au dini huzungumza kivyake. Kila kiongozi hulia au kujipanga kivyake.

Vyuo vikuu, ambavyo kihistoria vilikuwa chimbuko la fikra za mabadiliko ya kijamii, navyo vinaonesha dalili za kudhoofika kwa mshikamano wa wanafunzi na wanataaluma. Hakuna tena nguvu ya pamoja ya wanafunzi au wanataaluma kama ilivyowahi kuwepo katika vipindi mbalimbali vya historia ya taifa hili. Leo mwanafunzi anayekandamizwa chuoni hujikuta mpweke. Hakuna mwamko mpana wa kitaifa wa wanafunzi au wanataaluma unaoweza kusimama kwa pamoja dhidi ya dhuluma zinazowakabili.

Vyama vya wafanyakazi navyo vimeendelea kupoteza nguvu ya kisiasa na kijamii. Vyama hivi sasa vimekuwa kama tawi la Serikali katika kudhibiti wafanyakazi. Havina sauti wala uwezo wa kuwafanya wafanyakazi kujiona kama nguvu ya pamoja.

Wakulima, ambao ndio wengi katika taifa hili, wanaendelea kupitia changamoto za masoko, pembejeo na sera zisizo rafiki, lakini hawana jukwaa kubwa la kitaifa la kusukuma maslahi yao kwa nguvu ya pamoja.

Kwa kifupi, kila kundi limeguswa na mfumo wa ukandamizaji, lakini kila kundi bado linaamini kuwa linapambana peke yake.

Hii ndiyo hali ambayo Vladmir Lenin alipokuwa anaeleza mapambano ya kitabaka alilieleza kuwa makundi yenye matatizo yanayofanana lakini ambayo bado hayajajitambua kama nguvu ya pamoja ya mabadiliko. 

Makundi yapo, maumivu yapo, hasira zipo, lakini mshikamano wa kisiasa bado haujajengeka kikamilifu.

Katika mazingira kama haya, mfumo kandamizi huwa na nguvu zaidi kwa sababu waliokandamizwa wamegawanyika. Kila kundi linapolia kivyake, dola huwa rahisi kulidhibiti kundi hilo moja moja. 

Leo wanafunzi, kesho waandishi wa habari, kesho kutwa wanasiasa wa upinzani, halafu viongozi wa dini, lakini kwa kuwa hakuna jukwaa la pamoja, kila tukio linaonekana kama tatizo la kundi fulani badala ya tatizo la kitaifa.

SOMA ZAIDI: Wasanii wa Tanzania na Matukio ya Okt. 29: Je, Tatizo ni Ukimya wa Wasanii au Sanaa ya Ukimya kwa Maumivu ya Jamii?

Ndiyo maana mjadala ulioanzishwa katika kongamano la kitaifa la Dar es Salaam ni muhimu kuendelezwa. Taifa haliwezi kutoka katika mkwamo huu ikiwa makundi yote yataendelea kubaki katika visiwa vyao vya mapambano.

Hatua inayofuata inapaswa kuwa ujenzi wa jukwaa pana la pamoja la walioguswa na siasa kandamizi nchini kwa kimombo tungeliita jukwaa hilo United Front. Hii haimaanishi kufuta tofauti za kiitikadi au kisekta, bali kutambua kwamba kuna ajenda za msingi zinazogusa kila kundi.

Agenda hizo ni: Kudai ukweli na haki kwa waathirika wa Oktoba 29, 2025; uchunguzi huru na wa kuaminika wa matukio ya mauaji, utekaji na kupotea kwa wananchi; uwajibikaji wa vyombo vya dol ana wahusika wote; ulinzi wa haki za binadamu; mageuzi ya kisiasa kupitia Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi; na mwisho ni kurejesha uhuru wa kisiasa na kiraia nchini.

Makundi haya yanahitaji kutoka katika hatua ya kusema peke yake kwenda katika hatua ya kuzungumza kwa pamoja.

Vyama vya siasa vya upinzani vinahitaji kujifunza kwamba ushindani wa kisiasa haupaswi kuua mshikamano wa kidemokrasia. Taasisi za kidini zinahitaji kujenga sauti ya pamoja ya maadili ya taifa. Wanafunzi na wanataaluma wanahitaji kurejesha nguvu ya umoja wa kitaifa. AZAKI zinahitaji kujenga harakati pana zaidi badala ya kufanya kazi kwa kutawanyika. Wafanyakazi, wakulima na progressive forces nyingine wanahitaji kuona kuwa mapambano yao yana mzizi mmoja.

Hii ndiyo hatua ambayo Vladimir Lenin aliiona kama safari ya kutoka tabaka lililo ndani yake lenyewe hadi tabaka linalojitambuahatua ambapo  waliokandamizwa wanajitambua kuwa nguvu ya pamoja ya kisiasa yenye ajenda ya pamoja ya mabadiliko.

Historia inaonesha kwamba hakuna mfumo kandamizi unaoanguka kwa sababu ya malalamiko yaliyotawanyika. Mabadiliko huanza pale ambapo makundi mbalimbali yanajenga mshikamano, yanaunganisha madai yao, na kuweka mbele ajenda ya pamoja ya kitaifa.

Kwa sasa, Tanzania inaonekana kuwa katika njia panda. Tuna chaguo moja tu aidha ni kuendelea na hali ya sasa ambapo kila kundi litaendelea kulalamika peke yake huku nguvu za kidemokrasia zikiendelea kudhoofika taratibu na kubaki kwenye mkwamo. Ama kutaka mabadiliko kwa kujenga mwamko mpya wa kitaifa unaounganisha walioguswa na ukandamizaji katika jukwaa la pamoja la mapambano ya kidemokrasia.

Swali muhimu kwa sasa si kama ukandamizaji upo kwa sababu karibu kila kundi tayari limeugusa kwa namna yake. Hoja ni kama makundi haya yataendelea kubaki katika upweke wa malalamiko, au kama yataamua kujenga mshikamano mpya wa kitaifa wenye uwezo wa kuisukuma nchi kutoka katika mkwamo wa kisiasa kuelekea maridhiano, haki na demokrasia jumuishi.

ACT Wazalendo imeonesha njia ya kuleta wadau pamoja, njia ambayo haipaswi kupuuzwa, kubezwa. Watawala hawatotaka kuona wanyonge tunaungana. Tusikubali. Inatosha. Tushikamane. Tushirikiane kuanzia shambani, migodini, kwenye siasa za vyama, madhabauni, gerezani na uraiani. Udhalimu utashindwa, uhuru utarejea. 

Idrisa Kweweta ni mtafiti na mchambuzi wa sera, siasa na masuala ya kijamii, na Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia Idrisakweweta34@gmail.comau X kama @idrisa_kweweta. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.comkwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×