Dar es Salaam – Saa tano asubuhi, jua tayari linawaka katika mtaa wa Mshikamano, Mbezi Louis, jijini hapa. Katikati ya taka zilizochanganyika, Dunstan Mazinge (29) anachambua chupa za plastiki moja baada ya nyingine, akitafuta zile anazoweza kuuza.
“Mimi hizo nyeusi huwa sizichukui, hazina pesa,” anasema.
Mazinge hukusanya zaidi chupa nyepesi (Polyethylene Terephthalate – PET) zisizo na rangi zinazotumika kuhifadhia vinywaji, ambazo anasema ni rahisi kuziuza kwa sababu zina soko la uhakika.
Pia, hukutana na aina nyingine za plastiki, zikiwemo ngumu kama ndoo, madumu ya maji na viti vya plastiki (High-Density Polyethylene -HDPE), ingawa hizi hupatikana mara chache zaidi kuliko chupa za maji.
Baadhi ya plastiki hizi ngumu, kama HDPE, zinaweza kuuzwa kwa bei kubwa zaidi kwa kilo kuliko PET, lakini ni sehemu ndogo ya anachokusanya kwa siku.
Kwake, tofauti kati ya chupa anazoweka kwenye gunia lake na zile anazoacha si rangi pekee, bali ni thamani yake sokoni na kama kuna mnunuzi aliye tayari kuilipia.
Zuberi Shekazi (53) hununua plastiki kutoka kwa waokota taka kama Mazinge na kuuza kwa wanunuzi wakubwa.
“Nikiuza kilo moja ya plastiki isiyo na rangi kwa Sh. 700, ile nyeusi inaweza kuuzwa Sh. 300 tu,” anasema. “Unaweza kuwa na mzigo mkubwa, lakini mwisho wa siku pesa huioni,” anasema Shekazi.

Chama cha Wachakataji wa Plastiki (Association of Plastic Recyclers – APR) kinaeleza kuwa carbon black, rangi inayotumika kwenye baadhi ya plastiki nyeusi, inaweza kufanya plastiki hizo kuwa vigumu kutambua na kutenganisha wakati wa urejelezaji. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa plastiki zote nyeusi haziwezi kuchakatwa.
SOMA ZAIDI: Vijana Wabuni Mfumo wa Kidijitali Kudhibiti Taka Dar es Salaam
Shekazi anasema baadhi ya plastiki hukataliwa na viwanda vya kuchakata kwa sababu ambazo yeye hazijui vizuri. Wakati mwingine humchukua zaidi ya mwezi kukusanya tani moja, kutegemea kiasi cha plastiki kinachopatikana na idadi ya waokota taka wanaoshindania plastiki yenye thamani zaidi.
“Inategemea tu na siku. Sasa hivi tuko wengi tunaofanya kazi hii, na plastiki zenye bei nzuri tunalazimika kuzishindania huko mitaani,” anasema.
Kwa upande wa pili wa mnyororo huo ni viwanda vya kuchakata. Ramadhani Kamote, Meneja wa Cheng Xin Investment Co. Ltd, kiwanda cha kuchakata plastiki, anasema kwa sasa wananunua plastiki za PET kwa Sh. 500 hadi 600 kwa kilo, ingawa kuna vipindi bei hushuka hadi Sh. 200.

“Inategemea na msimu tu, kipindi cha joto plastiki zinakuwa nyingi na bei inaweza kuwa ndogo, na wakati wa baridi chupa zinaweza kuadimika hivyo bei ikapanda,” anasema Kamote.
Kamote anaeleza kuwa kiwanda hicho kinachakata aina mbalimbali za plastiki, zikiwemo nyeusi, na kuuza malighafi kwa wazalishaji wa bidhaa za plastiki ndani na nje ya nchi. Anasema plastiki nyeusi huziuza kwa wateja maalum wanaozihitaji. Anakadiria kuwa kwa mwezi mmoja kiwanda hicho hukusanya takribani tani 150 za aina zote za plastiki.
Bei ya plastiki nyeusi bado ni ndogo kuliko ya zisizo na rangi, kama Shekazi alivyosema. Hata hivyo, plastiki ambazo Mazinge anaziacha haipotei. Inabaki kuwa sehemu ya mkondo wa taka ambao thamani yake ni ndogo kiasi kwamba kuzikusanya hakulipi. Na hiyo ni sehemu ya tatizo kubwa zaidi la taka za plastiki nchini Tanzania.
Gharama za taka za plastiki
Kwa mujibu wa tathmini ya Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) iliyochapishwa mwaka 2021, Tanzania ilizalisha wastani wa tani 315,000 za taka za plastiki mwaka 2018. Asilimia 34 pekee ya taka hizo zilikadiriwa kukusanywa, huku karibu tani 29,000 zikikadiriwa kuishia baharini, kwenye mito na maziwa.
Rashida Awadhi, mkazi na mfanyabiashara wa chakula katika eneo la Kimara Temboni, jijini Dar es Salaam, anasema moja ya madhara makubwa ya taka za plastiki anayoyaona katika eneo lake la kazi ni kuziba kwa miundombinu ya maji machafu.

“Yaani hapa ikifika kipindi cha mvua unajiuliza haya makopo yote yametoka wapi, maana maji yanafurika kila mahali, mitaro inapozibwa na haya makopo. Si tu kwamba yanatuletea kero kwenye biashara zetu, maana hata wateja wakiona hali ya uchafu hawaji,” anasema Awadhi.
SOMA ZAIDI: Mhitimu wa NIT Alivyobadili Changamoto ya Taka Kuwa Fursa Wilayani Mafia
Kwa watumiaji wa fukwe, suala la taka za plastiki nalo limekuwa kero kubwa.
“Unaweza kuja hapa na familia halafu ukakuta kuna uchafu wa kila aina, hasa hizi plastiki, mpaka unajiuliza zinatokea wapi na unaanza kupata wasiwasi kama umeleta watoto sehemu salama kwa afya zao. Hizi plastiki zinaharibu kabisa muonekano wa ufukwe na kukatisha hata hamu ya kuja beach (ufukweni),” anasema Reinhard Kidali, mtumiaji wa ufukwe wa Msasani, maarufu kama Beachmavi.
Kwa Abdi Khalifa, mratibu wa mradi kutoka Human Dignity and Environmental Care Foundation (HUDEFO), asasi ya kiraia inayofanya kazi katika masuala ya mazingira na usimamizi wa taka, tatizo ni kubwa kuliko plastiki ambazo hazina thamani sokoni.

“Tatizo si plastiki tu ambazo hazina thamani sokoni. Tatizo ni pengo kati ya kiasi cha plastiki kinachoingia kwenye matumizi kila mwaka na uwezo wa mfumo wa kukusanya, kuchakata na kuzirudisha kwenye uzalishaji,” anasema.
Kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia (World Bank) chini ya mpango wa PROBLUE, uliochapishwa mwaka 2023, uchafuzi wa plastiki katika maeneo ya pwani ya Dar es Salaam ulisababisha hasara ya kiuchumi ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 10.33 mwaka 2019 – zaidi ya nusu ikitokana na hasara ya sekta ya utalii, na dola milioni 2.2 zikiwa ni makadirio ya gharama za kiafya, zikihusisha vifo 41 vya mapema vilivyokadiriwa kuchangiwa na uchafuzi wa plastiki mwaka huo.
Utafiti huo unaeleza pia kuwa taka za plastiki huchangia kuziba mifereji ya maji na kusababisha mafuriko yanayovuruga shughuli za kiuchumi katika baadhi ya maeneo ya jiji hilo.
Ufuatiliaji wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) uliochapishwa mwaka 2025 kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa udhibiti wa uchafuzi wa taka za plastiki unaonyesha kuwa pengo hilo bado lipo. CAG alibaini kuwa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na serikali za mitaa hazikuwa zimesimamia kikamilifu wajibu wa wazalishaji katika kukusanya taka zinazotokana na bidhaa zao.
Wajibu wa wazalishaji
Wazalishaji hawako nje kabisa ya mfumo huo. Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za mwaka 2022 tayari zinawataka watengenezaji na wasambazaji wa bidhaa zilizomo kwenye chupa za plastiki kuanzisha, kuendesha au kushiriki katika mfumo wa kuchukua tena taka za chupa za plastiki kwa ajili ya kuchakata au kuzitupa kwa njia salama.
Hata hivyo, wajibu huo wa kuchukua taka tena (take-back) una wigo finyu kuliko mfumo wa uwajibikaji wa mtengenezaji baada ya bidhaa kuwa taka (Extended Producer Responsibility – EPR). Chini ya mfumo huu, wazalishaji wangekuwa na wajibu mpana zaidi wa kushughulikia bidhaa zao zinapokuwa taka, ikiwemo kusaidia kugharimia ukusanyaji, urejeshaji au urejelezaji wake.
SOMA ZAIDI: Dodoma Inayokua, Taka Zinavyoongezeka: Mitaa Yakumbana na Changamoto ya Utupaji Taka Holela
Mhandisi Luhuvilo Mwamila, Meneja wa Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, anasema moja ya mapungufu katika mfumo wa sasa ni kutokuwepo kwa utaratibu maalumu wa kufuatilia kwa uwazi kiasi cha plastiki ambacho kila mzalishaji anaingiza sokoni na kiasi kinachokusanywa au kuchakatwa baadaye.
“Mfumo imara zaidi wa uwajibikaji wa wazalishaji unapaswa kuweka wazi kiasi ambacho mzalishaji ameweka sokoni, kiasi anachotakiwa kukusanya, nani analipia ukusanyaji na urejelezaji, na utekelezaji wa wajibu huo unathibitishwaje?” anasema Mwamila.
Kwa waokota taka, suala la nani analipa linahusiana moja kwa moja na kipato chao.
Tina Mfanga wa Mtandao wa Waokota Taka Dar es Salaam (MTAWADA) anasema kwa moja ya mahitaji yao ni kuwepo kwa mfumo wa uhakika wa kuwalipa waokota taka wanaokusanya bidhaa za wazalishaji mitaani.

“Lakini pia ni muhimu sana wazalishaji wawe na vituo vya kuchakata bidhaa wanazozalisha, ili kile wanachoweka sokoni kiweze kuchakatwa,” anasema Mfanga.
Mfano mmoja wa namna wazalishaji wanavyoweza kugharimia ukusanyaji tayari upo katika soko la PET.
PETpro, mpango wa hiari wa wazalishaji ulioanzishwa mwaka 2022, umekuwa ukiendesha mpango wa majaribio wa kukusanya chupa za PET zenye rangi. Utafiti wa HUDEFO kuhusu mfumo wa EPR na usimamizi wa taka za plastiki nchini Tanzania unaeleza kuwa kupitia mpango huo, wakusanyaji walipewa fedha za kununua chupa hizo na kuzisafirisha hadi vituo vya urejelezaji.
Nicholaus Ambwene, ambaye ni mratibu wa PETpro, anasema wajibu hauishii pale chupa inapouzwa.
“Ni wajibu wa wazalishaji kukusanya na kurejeleza chupa za PET baada ya matumizi,” anasema.
SOMA ZAIDI: Serikali Yatahadharisha Kuhusu Mlipuko wa Magonjwa ya Msimu wa Mvua
Anaongeza kuwa wazalishaji wengine wanapaswa kuonyesha wajibu wao wa kimazingira kupitia mifumo ya uwajibikaji wa wazalishaji kama PETpro, akisema mfumo wa EPR unaweza pia kushughulikia wazalishaji wanaonufaika na soko bila kubeba wajibu unaolingana. PETpro ni mpango wa hiari, si mfumo wa lazima wa EPR.
Tathmini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) ya mwaka 2026, iliyotumia taarifa zilizotolewa na PETpro, inaeleza kuwa PETpro ilikusanya tani 21,000 za chupa za PET zenye rangi kati ya Februari na Machi 2025. Inaeleza pia kuwa kati ya mwaka 2022 na 2025 ilikusanya tani 45,000 za chupa zisizo na rangi, na tani 32,000 zilirejelewa, bila kujumuisha zilizokuwa bado kiwandani wakati taarifa zilipokusanywa. Mwandishi wa tathmini hiyo anasema haikuwa sehemu ya kazi yake kuthibitisha taarifa zote zilizotolewa.
Tathmini hiyo pia inaonyesha kuwa wanachama wanane wa PETpro (Nyanza Bottling, Coca Cola Kwanza, Bonite Bottlers, SBC Pepsi, Sayona Drinks, Cool Blue, A-One Products & Bottles Ltd – MeTL, na SilAfrica Ltd) kwa pamoja walikadiriwa kuwakilisha takribani asilimia 80 – 85 ya soko la chupa za PET za vinywaji nchini Tanzania mwaka 2025.
Hata hivyo, kuwa na sehemu kubwa ya soko hakumaanishi mzalishaji anakusanya taka nyingi zinazotokana na bidhaa zake.
Utafiti mwingine wa Julai 2026, uliofanywa na wataalamu kutoka taasisi ya utafiti ya Norway (NORCE) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ulichapishwa katika jarida la Environmental Science and Pollution Research. Utafiti huo uliangalia taka zenye alama za wazalishaji zilizokusanywa katika maeneo 69 kandokando ya mwambao wa Tanzania wa Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Watafiti walibaini kuwa wazalishaji watatu (Jambo Group of Companies, Bakhresa Food Products Ltd na MeTL Group) walihusishwa na asilimia 52.9 ya taka za plastiki zenye alama za wazalishaji. Kwa ujumla, wazalishaji 29 walihusishwa na asilimia 95.1 ya taka hizo.
Kwa Khalifa, swali ni kama kiwango cha urejelezaji kinaendana na kiasi cha plastiki kinachoingizwa sokoni.
“Jambo lingine ni wazalishaji. Swali la msingi ni: je, wanachakata taka wanazozalisha, na wanazichakata kwa kiwango kinachoendana na kiasi wanachozalisha? Hapa ndipo ninapoona kuna udhaifu,” anasema Khalifa.
Wazalishaji wanasemaje?
Kwa upande wa wazalishaji, Joseph Ouma, Mratibu wa Mazingira wa Azam EPR Scheme, anasena kampuni ya Bakhresa Group imekuwa ikiendesha mpango wa majaribio wa kukusanya plastiki katika wilaya tano za mkoa wa Dar es Salaam, ambako ndiko pekee mpango huo unafanya kazi.
SOMA ZAIDI: Je, Tumefikiria Kulea Watoto Wanaojali Mazingira?
“Chupa ambazo tumeweza kukusanya kwa kipindi cha Septemba 2024 hadi Septemba 2025 zilikuwa tani 100. Na kwa kipindi cha kuanzia Septemba 2025 hadi sasa, tukielekea kwenye tathmini, tayari tunaona zimeongezeka na kufikia tani 130,” anasema Ouma.
Ouma anaeleza kuwa mpango huo umeanza na chupa za PET zenye rangi pekee, bila zile zisizo na rangi, hasa kutokana na msisitizo ambao mamlaka zimekuwa zikiutoa kuhusu chupa zenye rangi.
Ouma anaeleza kuwa mpango huo hauhusu bidhaa za kampuni yao pekee, kwani wanakusanya pia plastiki zinazozalishwa na wazalishaji wengine. Anasema kampuni hiyo inashirikiana na wanunuzi wa kati kununua plastiki hizo, na kwamba mpango ukionekana kuwa wa mafanikio, watajumuisha njia nyingine na kushirikiana na wadau wengine ili kufikia malengo yao.
“Lengo letu tukianza rasmi ni kuhakikisha ndani ya miaka mitatu tuna uwezo wa kukusanya angalau asilimia 40 ya kile tunachokizalisha,” anasema.
Kuhusu kiasi cha plastiki ambacho kampuni inazalisha kwa mwaka, Ouma alisema kwa sasa hawezi kutoa takwimu hizo kwa kuwa ni taarifa za ndani za kampuni. Aidha, alieleza kuwa lengo la asilimia 40 litategemea kiasi halisi cha bidhaa kinachowekwa sokoni, eneo ambalo mpango unafikia, na uwezo wa ukusanyaji utakaojengwa kupitia mpango huo wa majaribio.
Kwa maoni ya Ouma, zaidi ya tani 100 kwa mwaka ni kiwango kikubwa kwa hatua ya mwanzo, na lengo ni kujenga mfumo wa ukusanyaji, urejeshaji na ufuatiliaji unaoweza kupanuliwa baadaye.
Jambo Group ilitafutwa kwa simu kati ya Septemba 22 na Oktoba 5, na Watercom, mzalishaji wa maji ya chupa, kati ya Septemba 25 na Oktoba 12, kwa ajili ya maoni, lakini hazikujibu hadi makala hii inachapishwa.
Nini kinafuata?
Tanzania inaandaa mfumo wa lazima wa EPR, lakini mchakato bado uko katika hatua ya rasimu. Mwezi Julai 2026, NEMC na IUCN ziliomba maoni ya wadau kuhusu rasimu ya kanuni hizo kabla ya kukamilishwa.
NEMC ilisema mfumo unaopendekezwa utaweka wajibu kwa wazalishaji kusimamia taka zinazotokana na bidhaa zao. Hata hivyo, bado haijulikani kanuni hizo zitakuwa tayari lini.
Kwa waokota taka, chochote kitakachokuwa sheria hatimaye kitalazimika kuingia katika mfumo ambao tayari wanasaidia kuuendesha.
Katika mtaa wa Mshikamano, siku inayofuata Mazinge ataendelea kuchambua taka zilizo mbele yake. Chupa ambazo ana uhakika wa kuziuza ataziweka kwenye gunia lake. Nyingine ataziacha hapo hapo.
Mweha Msemo ni mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Dar es Salaam. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia mwehahamran@yahoo.com.