Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu amesema kwamba kwa sasa wazalishaji hao wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti wanaendelea kufanya shughuli zao kwa busara za Serikali baada ya kutokidhi matakwa ya kikanuni kuhusu suala la umiliki, hali aliyosema inaathiri uhuru wao kama kampuni huru ya habari.
Kwa mujibu wa Kifungu nambari 4(1)(b) cha Kanuni za Huduma za Vyombo vya Habari, 2017, endapo kama mwekezaji kutoka nje ya Tanzania atataka kuanzisha gazeti nchini, mwekezaji huyo atatakiwa kuwasilisha serikalini orodha ya wanahisa wazawa ambao watakuwa wanamiliki asilimia 51 ya kampuni, huku mwekezaji huyo akibaki na asilimia 49.
Moja kati ya waathirika wakubwa sana wa kanuni hii inayokosolewa vikali ni MCL, kampuni tanzu ya Nation Media Group (NMG) ya nchini Kenya inayomilikiwa na Mfuko wa Aga Khan kwa Maendeleo ya Kiuchumi, wenye makao makuu yake nchini Uswizi pamoja na wanahisa wengine kama vile Alpine Investments Limited na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, zote kutoka Kenya.
SOMA ZAIDI: Utahitaji Kibali cha TCRA Kuweza Kuishitaki TCRA Mahakamani
Mpaka wakati wa mahojiano na The Chanzo hapo Julai 29, 2022, ilionekana ni kama vile bado MCL haijapata Mtanzania wa kumuuzia asilimia 51 za hisa zake, hali inayoifanya kwenda kinyume na matakwa ya kikanuni, na hivyo Machumu kuhitimisha kwamba kampuni hiyo inaendelea kuwepo kwa busara za Serikali.
“Ukiendelea kufanya kazi, na kanuni ipo, lakini ukategemea busara zaidi, [itafika muda] kanuni itatumika, na ikitumika huwezi kusema hapana, mbona tulikuwa tunaambiwa kuna busara hii?” alieleza Machumu wakati wa mahojiano hayo. “Cha msingi ni kwamba sheria zipitiwe, kanuni zipitiwe [na] zibadilishwe.”
Kuondokana na matakwa haya ya kikanuni ni kitu ambacho MCL inategemea sana kutoka kwenye mchakato unaoendelea hivi sasa wa kuzifanyia mapitio sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza tasnia ya habari Tanzania ulioanzishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.
“Tayari kuna mkutano unaandaliwa siku chache zijazo wa wadau ili kujadili masuala haya,” alidokeza Machumu. “Kwa hiyo, tunafikiri mchakato huu ukiharakishwa, na ukiweza kukamilika katika muda ambao aliuahidi [Waziri Nnauye], itakuwa ni jambo jema kwa tasnia na sisi hapa [MCL] tutakuwa tunaweza tukafanya kazi kwa nguvu kubwa zaidi.”
SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Wabainisha Changamoto Zinazoikabili Tasnia ya Habari Tanzania
The Chanzo ilimuuliza Nnauye, ambaye pia ni Mbunge wa Mtama (Chama cha Mapinduzi – CCM) kama kuna uwezekano kwa kanuni hii kufanyiwa mapitio na kubadilishwa ili kukuza uhuru wa habari Tanzania ambapo alisema tayari kamati ya kukusanya maoni ipo kazini na suala hilo linaweza likafikishwa huko.
“Bila shaka mnajua kuna mapitio ya sera, sheria na kanuni za tasnia ya habari [ambayo] yanaendelea,” alisema Nnauye kwenye mahojiano kwa njia ya simu. “Kama kuna malalamiko, yafikishwe kwenye mchakato huo na yatajadiliwa na kufikiwa muafaka.”
Mawazo mkanganyiko
Wadau wenyewe, hata hivyo, wana mawazo yanayokinzana kuhusiana na matakwa ya kanuni hiyo.
James Marenga ni Makamu Mwenyekiti wa MISA-TAN, asasi ya kiraia inayojishughulisha na kukuza uhuru wa kujieleza, ambaye ameiambia The Chanzo kuwa kanuni hiyo haitendi haki katika masuala ya uwekezaji kwani inamfanya mmiliki kutokuwa na sauti katika uwekezaji wake.
“Kitu ambacho kama wadau tunakisema, hiyo ni kanuni ambayo haitendi haki kwa sababu suala la uwekezaji ni suala la msingi sana,” anasema Marenga ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma.
“Ukimwambia mtu kwamba asimiliki asilimia mia ya hisa maana yake unataka kufanya biashara yake iwe tegemezi, yaani asipokuwa mmiliki kamili hata kuwa na sauti kwenye kwenye maamuzi ya kampuni na wawekezaji wakubwa hawataki hicho kitu,” aliongeza Marenga.
SOMA ZAIDI: Wadau Walaani Kushikiliwa Mwandishi wa Habari Zanzibar, Wataka Aachiwe Huru
Lakini kwa Dastan Kamanzi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), asasi ya kiraia inayolenga kujenga sekta ya habari huru, pana na inayojitegemea nchini Tanzania, hali ni tofauti, akisema “kwangu mimi hii [kanuni ya umiliki] haina tatizo.”
Kamanzi, ambaye ni mshauri mbobezi wa masuala ya uendeshaji wa vyombo vya habari Tanzania, anasema ni “hatari” kwa Serikali kuachia wageni kumiliki gazeti – au chombo kingine chochote kile cha habari – kwa asilimia mia moja.
“Huko nje wapo watu wenye nguvu, wenye utajiri, wanaweza kututeka, wakawekeza vitu vyao [humu nchini], halafu wananchi wa hapa wakawa kama wametawaliwa,” Kamanzi aliiambia The Chanzo.
“Wataleta tamaduni zao, hilo la kwanza,” aliongeza. “Lakini pia, Watanzania wetu watakosa fursa. Zaidi hawa [wawekezaji] ni kitu chao, na wakiamua kuondoka, wataondoka na kila kitu, na fedha watakazokuwa wanakusanya zitakuwa zinaenda kwao.”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.