The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Soma Hapa, Unaweza Kuwa na Uraibu wa ‘Energy Drinks’

Mtaalamu abainisha kwamba kama unatumia ‘energy drinks’ ili ujisikie vizuri, basi upo uwezekano wa wewe kuwa na uraibu wa vinywaji hivyo.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Mnamo Aprili 24, 2023, Serikali ilitangaza kwamba itafanya uchunguzi maalumu kugundua athari za kiafya zinazotokana na unywaji wa vinywaji vya nishati, maarufu kama enegy drinks kufuatia kesi iliyoripotiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyomuhusisha kijana mmoja na vinywaji hivyo.

Kwenye kesi hiyo, kijana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 28 alifikishwa kwenye taasisi hiyo akionesha dalili za kuwa hatarini kupata ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Wataalam walithibitisha kwamba dalili hizo, ikiwemo maumivu makali ya kifua, yalitokana na uamuzi wa kijana huyo kunywa chupa tano za energy drinks ndani ya masaa nane. 

Moja kati ya vitu vinavyotumika kutengeneza vinywaji hivi ni kafeini, ambayo pia kumekuwa na tahadhari nyingi kutoka kwa watalaam wa afya kuhusu matumizi yake sahihi, wakionywa kwamba matumizi yaliyopitiliza ya kafeini yanaweza kumletea mtumiaji shida kwenye afya yake.

Kufahamu haya na mengineyo, The Chanzo imefanya mahojiano maalum na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Ushauri katika Hospitali ya Bugando, Dk Gloria James Manyango, na hapa, Dk Manyango anaanza kwa kutueleza maana ya kafeini:

Gloria James Manyango: Kafeini ni kichocheo ambacho kinapatikana ndani ya kahawa [au] chai ya rangi. Inapatikana katika zao la kokoa; inaweza ikapatikana pia katika vinywaji vitamu kama cocacola. Lakini, vilevile, inapatikana katika dawa tunazotumia, hasa dawa za maumivu.

The Chanzo: Ni kwa namna gani kafeini inafanya kazi katika mwili wa binadamu?

Gloria James Manyango: Kafeini inaweza kufanya kazi katika mwili wa binadamu katika maeneo mbalimbali. Moja inasaidia kwenye namna mwili unavyopigana na magonjwa, ambapo kwa namna hiyo mtu akitumia kafeini anaweza akapata magonjwa ya moyo au ugonjwa wa kisukari.

Lakini, vilevile, kafeini inaweza kuongeza hali nzuri au kumfanya mtu ajisikie vizuri zaidi anapotumia kahawa. Kwa hiyo, mtu akitumia kahawa ndani ya nusu saa anaweza akapata hali fulani ya faraja, ama furaha, kushinda mtu ambaye hajatumia kahawa.

Vilevile, kafeini inaweza ikamsaidia mtu kumpatia nguvu, kwa mfano, wanaofanya mazoezi, kama ukitumia kahawa baada ya nusu saa mwili unakuwa na nguvu zaidi. Kwa hiyo, [kafeini] inaweza kukusaidia katika kukimbia au katika kufanya mazoezi yanayohitaji nguvu zaidi.

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Aonya Matumizi ya Njia za Kienyeji Kubana Uke: ‘Uke Una Ubano Wake wa Asili’

Lakini si hayo tu, kafeini inaweza ikasaidia kuongeza hali ya metaboliki, au kumeng’enywa kwa chakula kunaweza kuongezeka ambapo mwisho wa siku, kama mtu atakula na kutumia kahawa kidogo, inaweza ikasaidia katika kupunguza uzito ambao kwa sasa ni tatizo kubwa sana kwa vijana na hasa kina mama.

The Chanzo: Je, kafeini inapoingia mwilini inahusika, kwa namna yoyote, na mfumo wa fahamu?

Gloria James Manyango: Ni kweli, hii kafeini inaweza kuongeza kumbukumbu kwa maana inamsaidia mtu kumbukumbu zake ziwe za karibu. Lakini, vilevile, inaweza ikazuia magonjwa hasa yale magonjwa ambayo yanatokana na mishipa ya fahamu, kama vile

Alzheimer’s (kupoteza fahamu) au Parkinson’s disease (mwili kutetema mara kwa mara).

The Chanzo: Je, dhana ya kutumia kafeini kupunguza maumivu ina ukweli?

Gloria James Manyango: Utafiti unaonesha kwamba kafeini yenyewe inasaidia kupunguza uwezo wa mwili kujibu katika maumivu. Kwanza, kahawa yenyewe ukitumia mdomoni ni kama ina uchungu. Mtu anayekunywa kahawa [halafu] akala pilipili na wewe ambaye hutumii kahawa ukala pilipili yule anayetumia kahawa atahisi ule upilipili, au ule uchungu, katika hali ndogo kushinda yule ambaye hatumii kahawa.

Kwa hiyo, wale watu wanaotumia Panadol na kahawa hawafanyi makosa sana, japo sasa kujua kipimo gani cha kahawa ndiyo inayotakiwa, ndipo hapo inakuwa ni changamoto.

The Chanzo: Kuna dhana ya kutumia kafeini kuongeza kasi ya tendo la ndoa, je ni kweli?

Gloria James Manyango: Ni kweli inakuwa kama kichocheo na uchechemuzi ukitokea ile mishipa ya damu huwa inatanuka na kuongeza usambazaji wa damu katika eneo husika. Wanaume huwa wanatumia kafeini kwa kuongeza damu kufika eneo la tukio. Kwa hiyo, eneo la tukio likifikiwa na damu huwa linajaa, likijaa huwa raha inakuwa kubwa kushinda damu ikiwa haijajaa vizuri.

SOMA ZAIDI: Mtaalamu Aeleza Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Saratani ya Shingo ya Kizazi

The Chanzo: Kipi ni kiwango sahihi cha matumizi ya kafeini kwa mwili wa binadamu?

Gloria James Manyango: Mtu yoyote anaweza akatumia kafeini kwa sababu hii kafeini ambayo tunaizungumzia inatofautiana kati ya mtu na mtu. Lakini, vilevile, inatofautiana na ujazo, au ni ukubwa gani mtu anatumia, au tuseme kiwango gani mtu anatumia.

Kuna mtu akitumia kidogo inaweza ikaleta madhara fulani, akitumia nyingi inaweza ikaleta madhara fulani. Kwa hiyo, kwa wagonjwa kwa mfano wenye shinikizo, huwa haishauriwi sana kutumia kahawa kwa sababu kiwango kikiwa kikubwa kidogo mwili unaweza ukaenda zaidi ya inavyotakiwa na kufanya hali yake kuwa mbaya zaidi.

Katika viwango ambavyo vinashauriwa kutokana na tafiti ambazo zimefanyika, watoto angalau kwa siku wanahitaji miligramu 2.5 kwa uzito alionao kwa siku. Kwa hiyo, kama mtoto ana miaka 10, basi asizidi miligramu 25 kwa siku moja.

Kwa maana kama akinywa katika cocacola, kama akinywa katika chai ya rangi, au kama akiweka ile kahawa yenyewe imekorogwa, azingatie hivyo. Vijana tunashauri angalau miligramu 100 kwa siku katika aidha amekoroga au ametumia katika kitu ambacho kina kafeini ndani yake.

Kwa mtu mzima, angalau 400 miligramu kwa siku, lakini kuna tafiti nyingine zinaonesha hata 300 kuna wengine zinawaonesha madhara fulani wakati wastani 400 kushuka chini ndiyo inayotakiwa ikizidi hapo lazima kunakuwa na yale matokeo ambayo siyo mazuri.

SOMA ZAIDI: Ukosefu wa Vituo vya Upataji Nafuu Waacha Waraibu wa Dawa za Kulevya Njia Panda Mtwara

Lakini kuna watu wanatafuna kahawa kama kahawa, kwa hiyo, pale wanapata kafeini. Na watu hao, kwa sababu wanatafuna mara nyingi kama karanga, huwa wanakuwa katika hatari kubwa ya kupata shinikizo au kupata kisukari. 

[Hii ni] kwa sababu kile kipimo ambacho tunategemea kiwe kama kichocheo kinakuwa kimepitiliza, kile kipimo ambacho tunategemea kiwe kama uchechemuzi inakuwa ni kubwa kuliko ilivyotakiwa. Kwa hiyo, mwisho wa siku inakuwa tena siyo faida bali inaelekea kwenye hasara.

Lakini, vilevile, kuna jojo, au bubblegum, mbazo tunatafuna mara kwa mara lakini ndani yake unakuta zina kafeini. Kwa mfano, mtu anakuwa anaendesha gari anapenda kutafuna ili asisinzie. Lakini mwisho wa siku unakuta kama umetumia nyingi inaweza ikapitiliza na yenyewe ikaleta changamoto.

Lakini zipo hizo karanga za kola, au kola nuts, ambazo kama ni karanga zinaitwa kola. Lakini, vilevile, zipo kakao ambazo watu huwa wanatafuna kama matunda. Kwa pamoja ni chakula ambacho watu huwa wanakula lakini ndani yake kuna kafeini.

Kwa mfano, kwa jamii ya Kagera, na hasa Bukoba vijijini, [watu] wengi wana huo utamaduni wa kutafuna na ukifika maeneo hayo utaona hata ukienda kupima kwamba watu hawa wengi wanapata changamoto ya shinikizo na kisukari kwa sababu yale matokeo ya uchechemuzi kwao huwa ni makubwa sana kupita vile inavyotakiwa.

Kwa vijana ambao wamezoea kutumia vinywaji vya nishati, au energy drinks, vinywaji hivi vina kafeini ndani yake na sikumbuki kwa ukubwa gani ambayo ipo ndani ya kinywaji cha nishati lakini tunajua watu wengi wanatumia.

Lakini kwa kutumia vinywaji hivi, mara nyingi vijana wanajikuta kwamba wanakumbwa na msongo wa mawazo bila wao kujua; wanakumbwa na hali ya kuwa na mawazo, yaani bila kutumia kafeini hawawezi tena kuwa na furaha labda.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Wajawazito Wanakuwa na Tabia Zisizo za Kawaida?

Kwa hiyo, wakiamka asubuhi wanajihisi kama wamechoka mpaka wapate kinywaji cha nishati. Lakini, vilevile, wanajikuta kwamba wanategemea zaidi kinywaji cha nishati kushinda kawaida. 

Kwa hiyo, mwisho wa siku, wanaishia kwenye msongo wa mawazo na vilevile ili wawe imara mara nyingi wanaendelea kunywa vinywaji hivyo. Kwa hiyo, mzunguo unaendelea palepale: msongo wa mawazo, uraibu, kinywaji cha nishati. 

Kwa hiyo, wanaenda kwa kinywaji cha nishati siyo tena kwa ajili ya uchechemuzi bali kwa sababu hawawezi kuiacha na kama wakiiacha ule msongo wa mawazo unakuwa ni mkubwa zaidi. 

Kwa hiyo, wanakuwa wanaenda kutafuta tiba bila wao kujua, na ile tiba mwisho wa siku wanaendelea kuitafuta kila siku kwa sababu wako tayari na utegemezi [wa kafeini].

The Chanzo: Je, kafeini ina madhara gani kwa mwili wa binadaamu?

Gloria James Manyango: Madhara ya kafeini yapo lakini siyo ya moja kwa moja sana. Kama nilivyosema awali, wapo watu ambao tunawaita wanameng’enya taratibu na wale wanaomeng’enya kwa wepesi. Na vilevile wapo watu ambao matokeo yao yanatokea kwa upesi zaidi.

Labda kwa wastani tunasema mtu akitumia kafeini tunategemea ndani ya dakika 45 imeshanyonywa katika mfumo wa chakula na kuanzia nusu saa tunategemea tuanze kuona matokeo. 

Lakini kuna watu ndani ya nusu saa tunaanza kuona matokeo. Kwa hiyo, changamoto moja wapo, au madhara yanayotokana na kutumia kafeini moja wapo, ni kukosa usingizi kwa sababu mtu anaweza kuwa juu sana [baada ya kutumia kafeini] akakosa usingizi.

Na vilevile anaweza akapata maumivu ya kichwa kama ametumia nyingi. Kwa hiyo, tunashauri kile kiwango kidogo cha matumizi ni kizuri kuliko kiwango kikubwa, na kujua kiwango kikubwa na kidogo inatofautiana kati ya mtu na mtu.

SOMA ZAIDI: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?

Ushauri wangu kwa jamii yetu, hasa vijana, ni kwamba kama wanatumia hii kafeini au vyakula na vinywaji ambavyo vina kafeini ndani yake, basi wasitumie kwa wingi sana, wawe wanatumia kwa kiasi kidogo.

Mara moja labda kama anatumia jioni au asubuhi kuliko kutumia nyingi kwa wakati mmoja kwa sababu inaweza ikamsababisha aendelee kuwa anatumia bila kuwa na uwezo wa kuacha yeye mwenyewe. Nashauri pia kupima afya zetu mara kwa mara ili kujua mienendo ya miili yetu.

Rahma Salumu ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: salumurahma1@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts