The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sheria Zinavyokiukwa Zanzibar kwa Kisingizio cha Kuvutia Wawekezaji: ‘Uholela Umetamalaki’

Zabuni kadhaa, zikiwemo za kuendesha bandari na viwanja vya ndege, zimetolewa kinyume na sheria ya manunuzi ya umma ya Zanzibar.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Wakati ni muhimu kwa Serikali kuachana na ukiritimba ili iweze kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi, utawala wa sheria haupaswi kukiukwa kwa kisingizio cha kuvutia wawekezaji, Mahakama ya Ushindani (FCT) ilisema kwenye uamuzi wake wa Oktoba 16, 2023.

FCT ilitoa kauli hiyo kwenye uamuzi wake uliolenga kuizuia kampuni ya saruji ya Twiga Cement kuinunua ile ya Tanga Cement kwa kigezo kwamba hatua hiyo itavunja sheria za nchi kwa kuipa Twiga sehemu kubwa ya soko la saruji nchini kuliko ile inayoruhusiwa kisheria.

Wakati haya yakitokea Tanzania Bara, hali inaonekana kuwa tofauti visiwani Zanzibar ambako Serikali inadaiwa kukiuka sheria za nchi, hususan Sheria ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma, Namba 11 ya mwaka 2016 kwenye kutoa zabuni mbalimbali za Serikali.

Tangu aingie madarakani hapo Novemba 2, 2020, Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akipigia chapuo uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za uchumi na huduma za Zanzibar, akiisifu sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya nchi hiyo yenye watu wapatao milioni 1.8.

Wawekezaji wamepewa jukumu la kuendesha shughuli kadhaa za kiuchumi visiwani hapa, kutoka kuendesha visiwa vidogo vidogo, uendeshaji wa Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume na hata uendeshaji wa Bandari ya Malindi, nyenzo kuu ya uchumi wa Zanzibar, kutaja miradi michache tu.

SOMA ZAIDI: Samahani Mheshimiwa Rais Mwinyi Lakini Kwenye Hili Umekosea

Wakati baadhi ya wananchi wanapongeza jitihada hizi, wengine, hata hivyo, wameonesha wasiwasi kwamba kwa kiwango kikubwa uwekezaji huu unafanywa katika mazingira yanayokiuka sheria za nchi, hali ambayo si tu inaweka hatarini ustawi wao bali pia msingi mzima wa utawala wa sheria.

Sheria za Zanzibar zinakataza Serikali kutoa zabuni kwa taasisi bila ya kuwepo kwa ushindani, utaratibu unaolenga kuiwezesha Serikali kupata mtu sahihi kwa ajili ya kazi fulani, lakini pia kupata thamani ya fedha kwa zabuni inazotangaza.

Matakwa ya wachache

Jabir Idrissa, mwandishi wa habari wa siku nyingi visiwani hapa na mfuatiliaji wa karibu wa mambo yanayoendelea humo, amesema ni lazima kwa mamlaka husika kujenga utamaduni wa kufuata sheria kwani madhara ya kufanya vinginevyo yanakuwa ni makubwa, hususan kwa wananchi wa kawaida.

“Athari ni kubwa kwa sababu gharama za maisha zimepanda sana, hali inayomuumiza zaidi Mzanzibari wa kawaida,” anasema Idrissa kwenye mahojiano yake na The Chanzo. “Hii ni kwa sababu kodi yake inatumika vibaya, ikielekezwa kukidhi matakwa ya watu wachache.”

Mchambuzi mmoja ambaye ametafiti sana masuala ya sera visiwani Zanzibar, na ambaye amekataa jina lake kutajwa kwa sababu ya unyeti wa suala lenyewe, amemuelezea Rais Mwinyi kama “Sultan anayechipukia,” ambaye angependa kuiongoza Zanzibar kama Masultan wa Oman walivyokuwa wakiongoza huko nyuma.

Utawala wa Kifalme Zanzibar ulikoma mwaka 1964 kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea Januari ya mwaka huo na kuweka msingi wa taifa la Jamhuri, huku nafasi ya Mfalme ikichukuliwa na Rais.

“Tatizo siyo neno sahihi kuelezea kinachoendelea Zanzibar hivi sasa,” mchambuzi huyo aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye. “Kuna ukiukwaji mkubwa wa sera na sheria za nchi kwa ajili ya watu wachache kujitajirisha. Watawala wameziteka taasisi za umma na wanazitumia kufanikisha malengo yao binafsi.”

The Chanzo iliitafuta Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambayo ndiyo mshauri mkuu wa masuala ya kisheria kwa Serikali, kufahamu kama imeshawahi kuishauri Serikali kwenye suala hili husika ambapo iligoma kujibu swali hilo, ikisema tayari Rais Mwinyi ameshalitolea maelezo.

SOMA ZAIDI: Serikali ya Mwinyi ni Muhimu Ikajibu Maswali Haya Muhimu

Mnamo Oktoba 23, 2023, wakati akizindua Hospitali ya Kivunge, iliyoko mkoa wa Kaskazini, Unguja, Rais Mwinyi aliukosoa mfumo wa manunuzi ya umma, akisema unachelewesha utolewaji wa haraka wa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi.

Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi akizungumza kwenye hafla mojawapo iliyofanyika Ikulu ya Zanzibar. PICHA | IKULU ZANZIBAR.

Rais Mwinyi alitoa kauli hiyo katika muktadha wa mpango tata wa Serikali yake wa kubinafsisha baadhi ya huduma za kiafya kwenye hospitali za Serikali ambapo, kama ilivyo kwa miradi mingi tu ya Serikali, wawekezaji hao hawakupatikana kwa utaratibu ulioanishwa kwenye Sheria ya Manunuzi ya Umma.

“Hakuna mgonjwa anayeweza kusubiri utaratibu wa manunuzi mpaka ukamilike,” alisema Dk Mwinyi baada ya kueleza mchakato mrefu ambao hospitali ya Serikali hupaswa kuufuata endapo kama kifaa chake kimeharibika. “Kwa hiyo, tukaona sasa tufanye kwa kushirikiana na sekta binafsi.”

Kwenye mpango huo, kampuni ya Lancet Laboratories Tanzania Limited imepewa jukumu la kuendesha huduma za maabara kwenye hospitali za Serikali, huku kampuni ya NSK Hospital Arusha ikipewa zabuni ya kuendesha huduma za picha.

Uchunguzi wa The Chanzo ulishindwa kubaini vigezo vilivyotumika kuzipata kampuni hizi mbili kuendesha huduma hizo nyeti kwani hakuna kumbukumbu zozote zinaoonesha kwamba Serikali ilitangaza zabuni hizo na kampuni hizo kupatikana kwenye mchakato wa ushindani ulio wazi kama sheria zinavyotaka. 

Kampuni zote mbili hazikuwa tayari kujibu zimewezaje kupata zabuni hizo.

Si mradi pekee

Huu, hata hivyo, si mradi pekee ambapo wawekezaji wamepatikana katika utaratibu ulioibua maswali mengi miongoni mwa wananchi. 

SOMA ZAIDI: Je, Rais Mwinyi Ni Abiy Wa Zanzibar?

Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Serikali ya Zanzibar iliibua malalamiko mengi miongoni mwa wadau wa usafiri wa anga nchini baada ya kuamua kuipa kampuni ya nchini Dubai ya Dnata kuendesha ‘Terminal 3’ ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume bila kuwepo kwa ushindani wowote.

Mnamo Septemba 21, 2023, pia, wadau wa usafiri wa baharini walipatwa na butwaa baada ya Serikali kutangaza kwamba kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) imeanza rasmi uendeshaji wa Bandari ya Malindi, ikisema imeingia mkataba wa miaka mitano na kampuni hiyo kuendesha bandari hiyo. 

Hakuna aliyefahamu lini zabuni hiyo ilitangazwa na ni vigezo gani vilitumika kuichagua AGL, hali iliyokiibua chama cha upinzani ACT-Wazalendo kuihoji Serikali, ikiitaka kuweka wazi vigezo vilivyotumika kuipata kampuni hiyo. Mpaka wakati wa kuandika habari hii, Serikali ilikuwa haijajibu maswali hayo.

Ukiukwaji huu wa sheria ya manunuzi ya umma haukukoma hata wakati wa matumizi ya fedha za mgao ambazo Tanzania ilipokea kama mkopo kukabiliana na athari zilizotokana na UVIKO-19, janga la kiafya ambalo kwa miaka mitatu sasa limekuwa likizitesa nchi kadhaa duniani na chumi zao.

Mradi huo uliopewa jina la Tanzania COVID-19 Social-Economic Response And Recovery Plan (TCRP) uligharimu Shilingi trilioni 3.62, huku Zanzibar ikitengewa Shilingi bilioni 230. 

SOMA ZAIDI: Ally Saleh: Usiku wa Dk Mwinyi Utakuwa Mrefu Sana

Lakini kwenye ripoti yake ya Machi 1, 2023, CAG alibainisha ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Zanzibar kwenye namna wawekezaji na wakandarasi wengine walipatikana kwenye miradi iliyokusudiwa kutumia fedha hizo.

The Chanzo ilimuuliza Msemaji wa Serikali ya Zanzibar, Charles Hillary, hadhani kwamba tabia hii ya Serikali ya kukiuka msingi wa utawala wa sheria inaweza kuwachochea wananchi kukiuka sheria kwenye maisha yao ya kila siku lakini aligoma kujibu swali hilo. 

Hillary pia hakujibu swali letu lililolenga kufahamu endapo kama Serikali ina mpango wa kupeleka Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kwenye Baraza la Wawakilishi ili irekebishwe kulingana na mwelekeo wa Serikali katika kuvutia wawekezaji wengi zaidi Zanzibar.

Inatisha

Ismail Jussa ni mwasiasa mwandamizi kutoka chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo ambaye amekuwa mstari wa mbele kwenye kuibua ukiukwaji huu wa sheria kwenye kuvutia wawekezaji Zanzibar.

Ismail Jussa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, akizungumzakwenye moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho cha upinzani. PICHA | SALIM BIMANI/X

Kwenye mahojiano na The Chanzo, Jussa, ambaye chama chake ni mshirika katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inayoongoza Zanzibar, alisema kwamba ukiukwaji wa sheria na kanuni unaofanywa na Serikali unamtisha, hali inayomsukuma kulizungumzia jambo hilo mara kwa mara.

“Nasema linanitisha kwa sababu jambo hili linaashiria jambo moja tu: kwamba watu walioko kwenye mamlaka wameamua kutumia nafasi zao kujinufaisha, ama wao wenyewe au jamaa zao na ndugu zao,” alisema Jussa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo.

SOMA ZAIDI: Profesa Mussa Assad: Ufisadi Umeshamiri Kwa Sababu Mafisadi Hawaadhibiwi

“Hilo ni suala ambalo linaleta athari kubwa sana katika nchi,” aliongeza mwanasiasa huyo. 

“Kwa sababu, kunapokuwa hakuna uwazi, kunapokuwa hakufatwi sheria katika masuala yanayohusu manunuzi, au upatikanaji wa huduma kwa Serikali, au kwa umma, maana yake gharama [za maisha] zinaweza zikawa kubwa zaidi.”

Lakini viongozi wa upinzani siyo watu pekee ambao wamekuwa wakipaza sauti dhidi ya utamaduni huo wa Serikali wa kukiuka sheria za nchi kwa kisingizio cha kuvutia wawekezaji visiwani Zanzibar.

Ukinzani CCM

Mnamo Julai 8, 2023, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilitangaza kumvua uanachama kada wa siku nyingi wa chama hicho tawala nchini, Balozi Ali Karume, kwa kile ilichodai ni hatua ya mtoto huyo wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, kukiuka maadili ya chama hicho.

Hatua hiyo ilitanguliwa na ukosoaji mkali wa Balozi Karume kwa Serikali ya Rais Mwinyi na namna inavyoendesha mambo yake, ikiwemo utolewaji huo wa zabuni kwa makampuni bila kuwepo kwa ushindani, hali aliyosema inakiuka sheria za nchi na kuifanya Zanzibar isiwe sehemu nzuri ya kufanyia biashara.

SOMA ZAIDI: Aidan Eyakuze: Ni Wajibu wa Wananchi Kusimamia Uwazi, Uwajibikaji Serikalini

“Lalamiko kubwa hapa Zanzibar ni kwamba zinatolewa zabuni hapa za mabilioni kwa mabilioni ya shilingi, lakini, unamuuliza mtu, ‘Hii zabuni ilitangazwa lini?’ Unaambiwa haikutangazwa,” alisema Balozi Karume kwenye moja ya mikutano yake na waandishi wa habari hapo Mei 18, 2023.

Balozi Ali Karume, aliyefukuzwa uanachama ndani ya CCM, akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari. PICHA | MICHUZI BLOG.

“Mazingira ya kisheria na kikanuni Zanzibar siyo mazuri kwa ajili ya kufanyia biashara,” aliongeza Balozi Karume ambaye amewahi kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Italia, na Ujerumani.

“Kwa sababu zabuni zinatolewa kwa upendeleo,” alifafanua mwanadiplomasia huyo. “Unakuta kampuni moja inapewa kila zabuni. Ukiuliza inakuwaje, unajibiwa kwamba Mkuu wa Nchi kaagiza.”

Balozi Karume hakua mtu wa kwanza kutoka CCM kukumbwa na zahama kutokana na ukosoaji wake wa namna Serikali ya Mwinyi inavyoongoza nchi. Kabla yake, kada wa CCM Baraka Mohamed Shamte alifukuzwa na chama hicho kwa sababu hiyohiyo ya kukiuka maadili ya chama.

Hatua hiyo ilifuatia uamuzi wa Shamte kuukosoa na kuupinga vikali uamuzi wa Serikali wa kuviuza kwa wawekezaji visiwa vidogo vilivyopo Zanzibar, akisema uamuzi huo unamuondolea sifa Rais Mwinyi kuchaguliwa kwenye uchaguzi wa 2025.

Mbali na kufukuzwa uanachama, kada huyo pia alifuatwa nyumbani kwake na kupigwa mpaka kufikishwa hospitali na watu ambao mpaka leo hawajajulikana, licha ya Serikali kuahidi kwamba ingewatafuta watu hao na kuhakikisha haki inatendeka. 

Mnamo Juni 15, 2022, Shamte alijitokeza hadharani akiiomba radhi CCM, akiisihi imrudishe kwenye chama hicho kwani maisha yake yote amekuwa akikitumikia chama hicho, na kwamba hawezi kujiunga na chama kingine chochote kile kwa sasa.

Vita dhidi ya ufisadi

Baadhi ya wadau walioongea na The Chanzo kuhusiana na suala hili wameeleza wasiwasi wao kwamba kama hali itaendelea kuwa hivi – zabuni kutolewa kinyume na sheria – dhamira na mipango ya Rais Mwinyi katika kukabiliana na rushwa na ufisadi visiwani Zanzibar inaweza isifanikiwe.

Mnamo Februari 13, 2023, Rais Mwinyi alizindua rasmi Mahakama Maalumu ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar, akitimiza ahadi yake aliyoitoa Februari 8, 2021, katika maadhimisho ya 10 ya Siku ya Sheria Zanzibar. Mahakama hiyo inalenga kuongeza mapambano dhidi ya adui huyo wa maendeleo visiwani humo.

SOMA ZAIDI: Ripoti ya CAG: Je, Ufisadi Unatokana na Udhaifu wa Serikali au ni Tatizo la Kijamii?

Lakini bila ya Serikali kukabiliana na “uholela” ambao kwa sasa unatajwa kutamalaki na kuzikalia juu taasisi nyingi za Serikali, mapambano dhidi ya rushwa na aina nyingine za ufisadi visiwani Zanzibar yapo hatarini kufeli.

Hii ni kwa mujibu wa tathmini iliyotolewa Septemba 14, 2023, na shirika lisilo la kiserikali la Center for Strategic Ligitigation (CSL), lenye makao makuu yake visiwani humo, linalojihusisha na uchambuzi wa masuala ya sera na sheria zinazoongoza utawala wa umma.

“Uwekezaji na manunuzi makubwa ya umma hayapo chini ya uangalizi wa umma au uchunguzi wa kiufundi,” inasema tathmini hiyo iliyopewa jina la ‘The Political Economy of Zanzibar: The Endless Struggle to Control Corruption.’ 

“Taasisi zinazokusudiwa kupambna na rushwa na kusimamia manunuzi sahihi ya umma haziko imara,” inaongeza tathmini hiyo. “Tathmini ya kina ya taasisi za uwajibikaji, sambamba na mjadala juu ya mfumo wa haki jinai kwenye ufisadi, vinahitajika kuongeza nguvu dhidi ya mapambano ya ufisadi Zanzibar.”

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts