Sikuwa mtandaoni siku ya Jumamosi ya Novemba 4, 2023. Nilipoingia huko Jumapili jioni, nilikutana na malalamiko mengi kutoka kwa wachangiaji kadhaa kwamba kuna video ya wimbo imetoka na haina maudhui mazuri. Si maneno, si picha.
Malalamiko mengi yalidai kuwa video ya wimbo huo inahalalisha utamaduni wa ubakaji. Wimbo huo uliopewa jina la Ameyatimba umeimbwa na wanamuziki watatu – Whozu kwa kushirikiana na Mbosso pamoja na Billnass.
Niliamua kuiangalia mwenyewe video ya wimbo huo ili kujiridhisha na madai hayo, nikianza na kipande kifupi kilichokuwa kimewekwa mtandaoni na kisha nikajongea kwenye mtandao wa YouTube kuiangalia video nzima.
Niseme tu hapa kwamba ilikuwa vigumu kwangu kuamini kuwa video hiyo ni kazi ambayo macho mengi yaliipitia kabla haijaifikia hadhira kubwa!
Neno hili kuyatimba nilikuwa nalisikia kwa mara ya kwanza. Baada ya kumuuliza kijana mmoja ambaye anajichanganya kitaa zaidi yangu, na pia ni kijana zaidi yangu, alinipa mifano miwili ili niweze kuelewa.
SOMA ZAIDI: BASATA na Kupatwa kwa Sanaa na Wasanii Tanzania
Mfano wa kwanza alionipa ni huu: Kama rafiki yako na rafiki yake wana ugomvi mkubwa, nawe bila kujua chanzo chake ukaenda kumsaidia rafiki yako, kisha na wewe ukajumlishwa humo kwenye ugomvi, hapo utakuwa umeyatimba.
Lakini mfano wa pili alionipa ni kwamba: Pale mwanaume anapompenda mdada ila mdada anamzungusha sana, siku akikubali kwenda kwa mwanaume, basi atakuwa ameyatimba. Yaani umejikoroga, na kuna hali fulani ya tafrani, vurugu na ubabe – kuyatimba.
Jinsi ilivyo
Kwenye wimbo huo wa Ameyatimba, picha inaanza na vijana wa kiume kama sita hivi wakiwa ukumbini wanacheza game kwenye video. Akiwa amevaa vesti nyeupe, Mbosso anaingia na binti mdogomdogo, kabana rasta zake ndefu.
Binti anaonekana akichekacheka kwa aibu. Wanapokelewa na Whozu akishangilia, pamoja na vijana hao wengine, ujio wa huyo binti ambaye anaelekea chumbani na Mbosso.
Hatuoneshwi nini kilitokea chumbani mpaka binti akabadilisha mawazo. Lakini tunajua kuwa alibadilisha mawazo kwani tunamwona akiwa amejiinamia katikati ya kitanda, Mbosso akiwa amekaa mbali naye.
SOMA ZAIDI: Waziri Pindi Chana, Wizara Wasitekwe na Umaarufu wa Soka
Binti ananyanyua uso na kurusha nywele zake nyuma. Halafu ghafla anatoka mbio, rasta zake ndefu zikipepea, huku nguo yake ikiwa wazi kwa nyuma na kuacha brazia nyeusi ikionekana.
Mbosso anatokeza kutoka chumbani na kumnyooshea binti huyo kidole, huku akiwaambia washikaji zake, Mshike huyo, ambapo nao wanamjibu, Hatoki mtu. Binti anapofika ukumbini, wanamdaka na Whozu anamrudisha chumbani alipo Mbosso.
Kwa sekunde hizo chache, inaonekana kuwa ni nyumba wanayokaa wapangaji wengi kwani kuna korido ndefu na vyumba vingi, muundo wa nyumba ambayo mara nyingi huwa sehemu za uswahilini, au uswazi kama vijana wa kitaa wanavyosema.
Mbosso anawaambia wenzake – nimeupaka mkongo // alinitia usongo, nao wanamjibu – hatoki mtu. Video ina mambo mengi, hapo ni mwanzo tu. lakini ndipo palipoleta hisia hasi.
Hali ya kubabaika
Kuna namna nilijisikia hali ya kubabaika ya kuwa hakuna pa kutokea. Umewahi kuota ndoto ambayo kila mlango unaoufungua haufunguki? Au unafunguka lakini hakuna jinsi ya kutoka nje? Ndivyo ilivyokuwa kwangu kama mwanamke.
SOMA ZAIDI: Waandishi Bunifu Tanzania Tukisahaulika Sasa, Tutakumbukwa Lini?
Kama haitoshi, Mbosso anaendelea kusema – Kashanipiga sana vizinga // leo kajichanganya, kayatimba – huku akiwa amemshikilia binti kwa nguvu kitandani. Binti anaonekana kwa juu akiweweseka na kujitahidi kujinasua bila mafanikio.
Kamera inachezacheza kuonesha jinsi vurugu hapo kitandani siyo ndogo. Kisha, tunaona kwa chini kama vile tumelala kitandani, kwa jicho la binti, kijana anachukua chupa inayoonekana kuwa ni ya mafuta na kujimiminia kwenye kiganja cha mkono wake wa kushoto.
Mbosso anaonekana akiongea na kamera kama vile kuongea na hadhira kuwa – Alitaka kunichukulia poa, kumbe mi mwenyewe ni mtoto wa town//Mara ooh nitakupa ukinioa, kashaniona boya kutwa kunipiga sound.
Video inaendelea kuonesha binti akiwa anatoa macho na kujikakamua hapo kitandani kama mtu anayeumia, na wakati mwingine unaonekana mkono ukimkaba. Huhitaji ufafanuzi zaidi ya hapo kuelewa kitendo kinachofanyika.
Halafu, mbele kidogo wanatukana matusi ya nguoni bila kuweka sauti yoyote ya kufanya yasisikike – beep au mute – kama ilivyo nchi za wenzetu ambapo maudhui yenye maneno makali hayaruhusiwi kurushwa redioni au kwa hadhira kubwa bila tahadhari, au bila kuwekewa mlio huo maalumu.
Hatua za mamlaka
Yawezekana malalamiko ya mtandaoni yalilishtua Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwani mnamo Novemba 5, 2023, iliwapa adhabu wasanii hao, likisema wimbo huo una maudhui yanayokiuka kanuni za maadili kutokana na kuwepo kwa ishara ya vitendo vinavyoashiria matusi kinyume na kanuni ya 25(6)(j) pamoja na vitendo vya unyanyasaji, ukatili na udhalilishaji wa utu wa mwanamke kinyume na kanuni ya 25(6)-(f).
SOMA ZAIDI: Kabumbu Itusaidie Kujenga Utambulisho, Ufahari Wetu Kama Taifa
Whozu aliagizwa aishushe video hiyo mara moja kwenye mitandao yote ya kijamii. Pia, wote walitozwa faini ya Shilingi milioni tatu kila mmoja na kufungiwa kujihusisha na kazi za sanaa kwa vipindi mbalimbali – Whozu kwa miezi sita na wenzake kwa miezi mitatu kila mmoja kuanzia Novemba 4, 2023.
BASATA ilisema kwamba hii haikuwa mara ya kwanza kwa Whozu kupewa adhabu kwa kukiuka taratibu za kuzingatia maadili katika kazi za sanaa lakini bado ameendelea kupuuza, likisema kwamba msanii huyo alishaonywa mara mbili na kutozwa faini mara moja huko nyuma.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa BASATA kumfungia msanii, au kumtaka alipe faini, kwa kigezo cha kutokufuata maadili. Mnamo Januari 2021, msanii Gigi Money alitakiwa kulipa faini ya Shilingi milioni moja na pia alifungiwa kutokujishughulisha na kazi za sanaa ndani ya nje ya nchi kwa miezi sita.
Hatua hiyo ilitokana na kitendo cha msanii huyo, wakati akiwa anatumbuiza huko Dodoma, “[Ku]panda jukwaani kwa ajili ya kutumbuiza na kuvua gauni –dera– na kubakia na vazi ambalo lilikuwa linaonyesha maungo yake ya mwili na hivyo kudhalilisha utu wake na kubugudhi hadhira ya wapenda sanaa ndani na nje ya Tanzania.”
Tukio hilo lilirushwa mubashara na chombo cha habari. Pia, Julai 2015, msanii Shilole alipata adhabu kwa kucheza uchi mbele ya hadhira, na matukio mengine kama hayo.
Uhuru wa wasanii
Rungu hili la kuingilia kazi za fasihi linaweza kutumika vibaya hasa pale msanii anapokemea au kuonya jambo fulani kuhusu Serikali. Pia, kuwafungia wasanii kwa sababu ya ‘maadili’ kumeleta maswali huko nyuma, kwamba haya ‘maadili ya Mtanzania’ ni yapi hasa?
Lakini, nafikiri kuwa suala la mavazi na staha ya mtu ni jambo moja. Kumvunjia mtu mwingine heshima, tena kuonesha kuwa unahalalisha kitendo hicho, ni jambo jingine kabisa lisiloweza kunyamaziwa. Na ningependa kuamini kuwa Watanzania watakubaliana na mimi kuwa ubakaji siyo sehemu ya maadili yetu.
SOMA ZAIDI: Wasanii, Chukueni Tahadhari Hii Katika Mikataba ya Matangazo
Ukiachilia mbali waliolalamikia video hii, wapo watu mtandaoni waliosema kuwa hawa wasanii wameonewa. Wengi walichekelea na kufurahia kile ambacho Mbosso alionekana anataka kufanya.
Kwa nini? Wanadai kuwa walichokionesha kwenye video yao ni jambo ambalo linaendelea kwenye jamii. Kwa nini sasa wazuiwe, na tena waadhibiwe?
Inawezekana kuwa wasanii wa Tanzania hawajui nguvu waliyonayo. Pengine, hawafahamu nguvu ya muziki, sauti na picha za video katika kuijengea jamii fikra na tamaduni.
Pengine imefika wakati kwa BASATA na wadau wengine kukaa tena chini na wasanii na kuwapa elimu juu ya mambo haya kwa kushirikiana na wadau wengine wanaofanya kazi kwenye jamii.
Kama kumekuwa na kuonywa mara nyingi, na faini za kutosha lakini bado tunaona hali ikizidi kuwa mbaya, pengine kunahitajika mwingiliano wa wasanii wa upande mmoja wa dunia kufanya majadiliano na wasanii wengine ili kupata uzoefu na kujifunza.
Uzoefu kwengineko
Mwaka 2016, Beyoncé aliachia video ya Formation iliyoakisi masuala ya kisiasa na kijamii waliyopitia Wamarekani Weusi katika vipindi mbalimbali kihistoria. Msanii wa Marekani, Childish Gambino, alipotoa video ya wimbo wa This is America mwaka 2018, hadhira ilishtuka. Magazeti yaliandika na uchambuzi ukafanyika.
SOMA ZAIDI: Ras Inno: Hatutungi Nyimbo Tukaziimbe Rumande
Video hiyo ilionesha madhila wanayopitia Wamarekani Weusi mikononi mwa polisi, na mambo mengine ya kijamii. Siyo tu maneno ya wimbo lakini pia video yenyewe inakuwa na ujumbe unaojisimamia. Yaani, ukizima sauti ukaangalia picha za video peke yake bado utapata ujumbe.
Video kama hizi sasa zinatumika vyuoni huko Marekani na kwengineko katika kujifunza mwingiliano wa sanaa na masuala ya jamii.
Lakini leo hii, ukipanda basi kutoka mkoa mmoja kwenda mwengine hapa nchini kwetu, na kuangalia video za muziki siku nzima, utajiuliza kama maamuzi yanayofanyika katika kuzitengeneza yana mantiki yoyote au yanafanyika tu kiholela.
Mara mtu amevaa kama cowboy, mara amevaa kama mtu kutoka Mexico. Ghafla, wako jangwani. Mara amevaa kama askari wa Kizulu na anakatika kama Mzaramo. Yaani, ni vurugu tupu!
Sanaa yetu inapaswa kuzingatia ubunifu na kuakisi upana wa fikra pia, kiasi kwamba mtu akitoka kuiangalia aweze kuandika utafiti, au thesis kwa kimombo, aone kwamba kuna utafiti ulifanyika. Je, ninasema kwamba kila wimbo uwe unazungumzia masuala mazito? Hapana.
SOMA ZAIDI: Tutapiga Marufuku Vitu Vingapi Kwa Kuwaletea ‘Ukakasi’ Watu Wengine?
Sanaa inafunza, lakini inastarehesha pia. Kila kitu kina sehemu yake. Ninachosema ni kwamba video kama hii ya Ameyatimba ilikuwa na lengo la kuonesha hali ya jamii, basi inabidi wanaotengeneza maudhui hayo wawe wabunifu zaidi.
Tusimpuuzie Afande Sele ambaye kwenye wimbo wake wa Darubini Kali anasema – Mimi ni msanii, kioo cha jamii. Mimi naona mbali, kwa darubini kali.
Na tena katika ubeti mmoja, msanii huyo anasema – Mwanamke kama hataki basi mwache aende zake, usimbake // Kulazimisha penzi ni hatari// Ni sawa na kulazimisha fani// Mwisho unaleta utani // Pumbavu! Hilo ni kosa kama padre kumbaka muumini eh // Au kama ticha mkuu kumbaka denti ofisini eh // Utafungwa!
Esther Karin Mngodo ni mwandishi na mhariri anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia mtandao wa X kama @Es_Taa. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.