The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uwekezaji Duni, Mitazamo Hasi ya Kijamii Vikwazo Vikuu Maendeleo ya Soka la Wanawake Z’bar 

Mtazamo kwamba wachezaji soka la wanawake ni wahuni unazuia wengi kuingia kwenye mchezo huo, hali inayowafanya wadau wa soka kutokuupa mchezo huo kipaumbele.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Kidawa Kheri Hamad ni mchezaji na kapteni wa timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Green Queens, timu yenye jumla ya wachezaji 13. Kidawa, 32, alianza kucheza mchezo huo mwaka 2016 ambapo mpaka hivi sasa anacheza nafasi ya beki wa kati, mgongoni akiwa anavalia jezi namba 14.

Kabla hajajiunga na timu hiyo yenye maskani yake maeneo ya Kiembe Samaki mjini hapa, Kidawa alianza kucheza soka la mitaani, kisha akajiunga na timu hiyo ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Licha ya kuutumikia mchezo huo kwa muda wa miaka nane sasa, Kidawa anakiri kwamba kipato alichokitengeneza kwa muda wote huo hakimpi ari ya kuendelea kuutumikia mchezo wa soka, mchezo anaoupenda sana. 

“Natamani maisha yangeweza kunipatia nafasi nyingine ya kupata kipato,” Kidawa, mama wa watoto watatu, alisema wakati akizungumza na The Chanzo alipokuwa akifanya mazoezi kwenye uwanja wa Mao Zedong uliopo Kikwajuni. “Ikiwa nitapata kazi ya kufanya, yenye maslahi, itakayonisadia [kupata kipato kizuri zaidi], basi naweza kuacha mpira.”

Kidawa anawakilisha masaibu ya wanasoka wengi wanawake kutoka visiwani humu ambao vipaji vyao vimeshindwa kuwawezesha kuziishi ndoto zao kwa furaha na majivuno kutokana na uwepo wa uwekezaji hafifu kwenye soka la wanawake Zanzibar. 

Kukosekana kwa ligi

Mazungumzo na wanasoka hawa yanadhihirisha kwamba wengi wao wanandoto za kuwa wachezaji wakubwa, lakini mazingira waliyonayo, kubwa ikiwa ni ukosefu wa viwanja, kukosekana na mwendelezo wa ligi ya wanawake na kukosekana kwa wadhamini, yamekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwenye jitihada zao za kufanikiwa kwenye mchezo huo.

Kidawa Kheri Hamad, 32, mchezaji wa Green Queens, akiwa mazoezini kwenye kiwanja cha mpira wa miguu cha Mao Zedong, Zanzibar. PICHA | NAJJAT OMAR.

Hali ni tofauti na soka la wanaume visiwani hapa ambapo ligi inachezwa kila msimu, na mabingwa wakipewa zawadi. Pia, kumekuwepo na mashindano mengine kama vile Kombe la Mapinduzi, ambayo yote huchangia kuongezeka hamasa na hivyo kuvutia wadhamini wengi zaidi.

SOMA ZAIDI: Wanawake Zanzibar Wataka Uwakilishi Baraza la Maulamaa: ‘Hatuko Huru Kueleza Shida Zetu kwa Wanaume’

Mbali na changamoto hizo, uchunguzi wa The Chanzo umebaini pia kuwa wacheza soka wanawake wengi visiwani hapa hawana mikataba na timu zao, hulipwa kati ya Shilingi 50,000 na Shilingi 150,000 baada ya kucheza mechi, ambapo muda mwingine hupita miezi takribani sita bila ya kucheza mechi yoyote ya ushindani.

Wachezaji wengi waliozungumza na The Chanzo walisema kwamba wanalazimika kuugawa muda wao kati ya kufanya kitu wanachokipenda, yaani mpira wa miguu, na kufanya biashara ndogondogo zinazoweza kuwaingizia kipato na kuwawezesha kujikimu wao na familia zao.

Zuhura Soud Othman ni mchezaji wa timu ya Yellow Queens aliyeanza kucheza mpira wa miguu wakati akiwa mwanafunzi wa darasa la nne. 

Mwaka 2018, Zuhura alijiunga rasmi na wenzake katika klabu, akiwa anacheza nafasi ya beki wa kulia, mgongoni akivalia jezi namba 15. Zuhura ameiambia The Chanzo kwamba mpira haujaanza kuwalipa wachezaji kama yeye.

‘Haulipi’

“Zanzibar mpira wa miguu kwa wanawake haulipi, tofauti na wanaume,” Zuhura, 18, anasema. “Pengine [nawaza], ningefanya kazi [nyingine ya] kupata kipato kwa sababu hapa Zanzibar hakuna mwendelezo wa ligi, hivyo hakuna fursa.

“Nilikaa nikafikiria faida ya kucheza mpira ndiyo hivyo tena hakuna, nikashauriwa na makocha wangu na wazee wangu wakaniambia nenda [kawe] mwamuzi utatoboa. Nishaamua michezo saba hadi sasa, ukiwa mwamuzi unakuwa unalipwa vizuri tofauti na mchezaji.” 

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Zanzibar, Yahya Khamis Ali, mpaka sasa kuna timu kumi za soka la wanawake kutoka Pemba na Unguja, huku idadi ya wachezaji ikiwa ni zaidi ya 150. 

SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria

Ali amekiri kuwa soka la wanawake visiwani hapa limezorota kwa kiasi kikubwa, hali anayoihusisha na kutokuwepo kwa ligi yenye mwendelezo pamoja na wadhamini.

“Changamoto kubwa ni wadhamini wa ligi za mpira wa miguu wa wanawake,” anasema Ali wakati akizungumza na The Chanzo kwa njia ya simu. “Sisi tunategemea ligi ikiwepo, pamoja na wadhamini, ndiyo vitawafanya wacheza soka wanawake visiwani hapa waonekane.” 

The Chanzo ilimuuliza Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Said Marine, ni hatua gani taasisi hiyo iliyo na dhamana ya kuratibu michezo visiwani hapa inachukua kulikuza soka la wanawake Zanzibar, ambapo alisema Serikali inaliona suala hilo na iko mbioni kulitafutia ufumbuzi.

“Serikali inajitahidi sana kukuza hili soka kwa kuweka ligi, mashindano mengine, na hata kutafuta wadhamini,” Marine aliiambia The Chanzo. “Lakini kwenye jamii pia bado kuna changamoto ya mashabiki kutojitokeza kwenye michezo ya wanawake, na hii inatokana na fikra kwamba mwanamke wa Kizanzibari hatakiwi kujihusisha na mchezo wa soka.”

Mitazamo hii hasi inazifanya changamoto zinazowakabili wanasoka wanawake Zanzibar kuwa kubwa maradufu, na hivyo kuwakatisha tamaa wanawake wengi kujiunga na soka hilo, hali inayozidi kuuzorotesha mchezo huo.

‘Hatupewi kipaumbele’

“Wanawake wa Zanzibar [tunaocheza soka] tunachukuliwa kama watu wahuni,” Mwajuma Abdallah Abdillah, anayeichezea Island Queens, alisema akizungumzia fikra hizo hasi. “Hatupewi kipaumbele.” 

Mwajuma, 29, alianza kucheza mpira rasmi mwaka 2016, akichezea timu kubwa za Tanzania Bara, kama vile JKT Queens, Yanga Princess, Tanzanite ya Arusha pamoja na timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars, kabla ya kurudi Zanzibar.

SOMA ZAIDI: ‘Siyo Uhuni’: Wanawake Jasiri wa Kizanzibar Walioingia Kwenye Sekta ya Uongozaji Watalii

“Jamii inatuangalia tofauti kwa sababu Zanzibar mpira wa wanawake ni kitu ambacho hakipewi kipaumbele kwa sababu asilimia kubwa ya watu wake wameshika sana dini [ya Kiislamu],” aliongeza mwanamichezo huyo. “Wanavyosema wao kwamba mtoto wa kike siyo mtu ambaye anatakiwa kucheza mpira.” 

“Kuna watu wengine wananiona mimi mhuni,” anasema mwanamichezo mwingine, Farida Khamis Kombo, ambaye amekuwa akiutumikia mchezo huo tangu mwaka 2018, akiichezea klabu ya Green Queens, akicheza nafasi ya beki na mgongoni akiwa anavalia jezi namba tano. 

“Mama yangu anasema mtoto mwenye uwezo wa kitu chochote namuendeleza hivyo hivyo, kwa hiyo yeye ndiyo kaniruhusu nijiendeleze,” aliongeza msichana huyo mwenye umri wa miaka 20. 

“Mtu unajua siku zote ukicheza mpira unajisitiri na bukta, vilemba, mikononi unavaa fulana, tofauti na wanariadha wanavyovaa, lakini wanariadha wanaonekana wale siyo wahuni kuliko wachezaji mpira,” anaendelea kusema Farida. “Wachezaji mpira [wanaonekana] wahuni zaidi wakati wanajisitiri.”

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake – Zanzibar (TAMWA-Z), ni mmoja wa wadau wanaojaribu kukabiliana na changamoto hii kwa kutekeleza programu zenye lengo la kuiwezesha jamii kuwa na mitazamo chanya kuhusu soka la wanawake na wanamichezo wenyewe.

Pamoja na jitihada zinginge, TAMWA-Z imekuwa ikiendesha mafunzo miongoni mwa waandishi wa habari yatakayowawezesha kuandika habari chanya kuhusu soka la wanawake, ikiamini kwamba vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwenye kubadili mitazamo hasi ya kijamii dhidi ya mchezo huo pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake. 

“Michezo ni kwa wote, na ikiwa timu za wanaume zinapewa kipaumbele na kukuzwa, basi Serikali ifanye hivyo hivyo kwa timu za wanawake ili kuleta usawa,” Khairat Haji, Afisa Miradi kutoka TAMWA-Z, ameiambia The Chanzo

SOMA ZAIDI: Shauku ya Kujitegemea Yawasukuma Wanawake wa Kizanzibari Masokoni

“Serikali itoe mchango wake, na sisi kama asasi za kiraia tunafanya nafasi yetu kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanashiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu, na wale ambao tayari wapo huko wanafaidika na mchezo huo,” aliongeza Khairat.

Bara yatoa mfano

Wanasoka wengi wanawake kutoka Zanzibar wanatamani kufikia angalau viwango vya wenzao kutoka Tanzania Bara, ambako soka la wanawake linaonekana kufanya vizuri. 

Mwaka 2016, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilianzisha ligi kuu ya wanawake ambayo imeendelea kufanyika na msimu wa mwisho wa 2023/2024 timu ya Simba Queens waliibuka mabingwa. 

Ligi hiyo imezalisha majina makubwa ambayo kwa sasa yamekuwa yakiendelea kutamba sehemu mbalimbali duniani, wakiwemo Opa Clement, anayechezea Henan Jianye FC ya ligi kuu wanawake nchini China, Aisha Masaka, anayechezea Brighton & Hove Albion ya ligi kuu ya Uingereza na Clara Luvanga, anayechezea Al Nassr FC inayoshiriki ligi kuu ya wanawake nchini Saudi Arabia.  

Riziki Aboubakar Islah, mwalimu wa soka la wanawake, anaamini kwamba mpira wa miguu unatoa fursa kubwa sana ya kumkomboa mwanamke kiuchumi, akitoa wito kwa wadau kusaidia kukuza soka la wanawake Zanzibar.

Riziki Aboubakar Islah, mwalimu wa mpira wa miguu, akitoa maelekezo kwa mchezaji wakati wa mazoezi. PICHA | NAJJAT OMAR.

“Sasa hivi mwandishi wa habari nikikwambia nenda kiwanja cha Mnazi Mmoja, kanitafutie sehemu ya vyumba vya kubadilisha nguo, huipati, lakini ni kiwanja,” anasema Riziki pembezoni ya uwanja huo. “Unaweza ukatimiza ndoto za wasichana wengi kwenye kile kiwanja, mazingira ndiyo yanasababisha zile ndoto zao zife.”

“Msichana anatoka nyumbani kwao amevaa vizuri, na baibui lake na kila kitu chake, akifika sehemu ya michezo abadilishe [nguo], aingie mchezoni, afanye shughuli ya michezo, amalize, avae tena vizuri, [mazingira ya kuwezesha] hicho kitu hakuna,” Riziki, 32, alilalama. “Ili soka liweze kuwatoa wasichana kimaendeleo, hilo, na mengineyo, yatapaswa kubadilika.”

Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar anapatikana kupitia najjatomar@gmail.com.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *