Katika historia ya Tanzania, wachimbaji wadogo wadogo wa madini wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya madini, licha ya mchango wao kutotambuliwa ipasavyo. Katika kona ya milima ya Kwaga, mkoani Kigoma, kuna simulizi ya mchimbaji mmoja mdogo aitwaye Adam Petro Zungu.
Nilipokwenda mkoani Kigoma kumzika nikitokea masomoni, nilipata kutembelewa na ndugu yangu huyo, anayejiita ‘Mwafrika,’ akijitanabahisha na harakati za ukombozi za watu Weusi, huku akijumuisha neno la jumla la Mwanaharakati. Nilipomsikiliza, nikaahidi kuandika makala fupi kutokana na masimulizi aliyoniapa.
Hii ni simulizi ya maisha halisi ya mtu mmoja aliyeamua kukwepa minyororo ya unyonyaji na kujitosa katika mkondo wa ndoto zake na matumaini ya maisha bora kupitia uchimbaji mdogo wa madini.
Makala haya yanachambua maisha ya Masanja kama mchimbaji mdogo, mapambano yake, mafanikio, changamoto, ndoto na ushawishi wake katika muktadha mpana wa utafiti wa madini nchini Tanzania. Kupitia sauti yake, tunasikia kilio na matumaini ya maelfu ya wachimbaji wadogo wanaotafuta kutambuliwa, kupewa heshima, na kuungwa mkono katika juhudi zao.
Safari ya maisha
Adam Petro Zungu alizaliwa mwaka 1977 katika kijiji cha Kwaga, Kasulu, mkoani Kigoma. Alimaliza darasa la saba mwaka 1993, akiwa kijana mwenye ndoto kama vijana wengi wa wakati huo.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, Zungu alijikita katika shughuli mbalimbali za kutafuta riziki. Mwaka 1995, alijiunga na Chuo cha Ufundi cha Bukoba kujifunza ufundi wa magari. Hili lilikuwa ni jaribio la kwanza la kutafuta ujuzi wa kumwezesha kujitegemea.
Mnamo mwaka 1997, Zungu, kama vijana wengine wanaotafuta maisha waonavyo miji, alisafiri kwa mara ya kwanza hadi Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, na kuanza kuuza matunda.
Alifanya kazi hiyo kwa vipindi viwili tofauti, mwaka 1997 na kisha tena kuanzia 2004. Baada ya kipindi cha kuuza matunda, Zungu alihama tena mwaka huohuo kuelekea Mwanza ambako alijikita kwenye shughuli mbalimbali hadi mwaka 2006.
Kwa miaka hiyo michache, Zungu alipitia maisha ya kuhangaika, kuhama kutoka mji mmoja hadi mwingine, akijaribu kila awezalo kuikabili dunia. Katika juhudi hizo, mwaka 2008 alikwenda Unguja, Zanzibar, na kufanya kazi ya kung’arisha viatu, maarufu kama shoe shiner, kwa mwaka mmoja.
Haikuchukua muda kabla ya kujitosa kwenye kazi ya ulinzi katika kampuni ya Night Support huko Mwanza ambapo alihudumu hadi mwaka 2011.
Ndoto mpya
Akiwa mlinzi, Zungu alipelekwa kulinda maeneo ya machimbo ya madini yaliyokuwa chini ya uangalizi wa kampuni ya Major Drilling huko Mwanza. Hapa ndipo mbegu ya ndoto yake mpya ilipoanza kumea.
Zungu alijikuta anasimama karibu na mitambo ya mabilioni ya fedha, akiwa na bunduki au kirungu tu, na mshahara mdogo usiokidhi hata mahitaji ya msingi.
Alianza kutafakari kwa kina: Kwa nini alinde mali isiyo yake kwa mshahara mdogo, ilhali wanaomiliki mitambo hiyo walikuwa wakipata faida kubwa? Swali hilo lilimpelekea kujitafakari na hatimaye kuchukua hatua ya kuacha kazi hiyo mwaka 2014.
Alielekea Arusha, ambako alifanya vibarua vya ujenzi kwa muda mfupi kabla ya kufunga safari kuelekea Mpanda, mkoani Katavi kujifunza uchimbaji wa madini.
Safari ya kuelekea Mpanda ilikuwa na malengo mawili: kutafuta maarifa kuhusu madini na kutafuta madini yenyewe. Huko alikutana na ndugu Sostene Kalajwe, ambaye alimfundisha mbinu za kutambua madini, kuchunguza miamba, na kuelewa tabia ya ardhi yenye madini.
Zungu, maarufu kama Masanja, alilipa kiasi cha Shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya mafunzo hayo ya kipekee. Maswali yalikuwa mengi akiwa analipa kiasi hicho cha fedha, lakini imani ilikuwa kupambania ndoto na hivyo haikuwa na namna.
SOMA ZAIDI: Siku ya Wanawake Duniani: Kesho Yenye Usawa Inaanza na Leo Yenye Ujumuishi
Kupitia mafunzo hayo, Zungu alianza kuelewa aina za madini, utafiti wa miamba, na mbinu bora za uchimbaji. Alianza kujifunza tofauti kati ya madini ya mapambo, au ornamental kwa kimombo, na ya viwandani, au industrial, pamoja na utaratibu wa kuyatambua kwa kutumia vifaa na ujuzi.
Kwa kifupi, Zungu ameiva kisawasawa katika kazi yake ya madini na amejidhatiti kikamilifu katika kuitimiza ndoto yake ukiachilia mbali maswaibu madogomadogo.
Kwa sasa, Zungu ana uzoefu wa miaka zaidi ya nane katika uchimbaji wa madini kutoka mwaka 2017 hadi 2025. Licha ya changamoto nyingi, hakujuta kuingia kwenye sekta hii. Mafanikio yake ni kielelezo cha uvumilivu, maarifa na bidii zisizoyumba.
Nitakupitisha kwenye baadhi ya masimulizi ya nini alipata kutoka katika uchimbaji wake huo.
Mapambano katika jamii
Katika mazingira ya kawaida, wachimbaji wadogo hupata kipato kidogo sana kutokana na uchimbaji wa madini, hasa kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu thamani ya mawe wanayoyapata, kuwepo kwa watu wa kati, yaani madalali, wanaowanyonya, na ugumu wa maisha kwa ujumla.
Zungu maekuwa akihangaika kuwauzia mawe yake kwa bei ya hasara kutokana na kutokuwa na uwezo wa kuyapima, au kuyafikisha sokoni moja kwa moja. Hii imesababisha mapato yasiyo na tija, licha ya jitihada kubwa na muda mwingi anaowekeza.
Aidha, kuna ukosefu wa haki na ulinzi wa makubaliano, au mikataba, baina ya wachimbaji wadogo na wanunuzi. Wachimbaji kama Zungu mara nyingi hujikuta kwenye hali ya kupunjwa, kutapeliwa, au hata kutishiwa usalama wao pindi wanapopata madini ya thamani.
Kukosekana kwa mfumo rasmi wa mawe yote ya madini katika ngazi ya wilaya, na hasa changamoto za urasimu kwa watumishi wa Serikali, ni pengo linalopaswa kuzibwa na sera madhubuti.
SOMA ZAIDI: Nyaraka za Mahakama Zafichua Uhalifu Mkubwa Mgodi wa North Mara
Mwaka 2021 ulikuwa wa neema kwa Zungu. Alipata mawe ya thamani, akayapeleka kuyapima katika maabara za Arusha, Mwanza, na Dodoma. Hata hivyo, alipitia pia udanganyifu wa hali ya juu.
Alisimulia tukio alilopitia Mwanza: “Nilivuta vijana kunisaidia kupima jiwe, wao wakalivunja na kuniambia si madini kwa sababu halikutakiwa kuvunjika. Nikajiuliza: hivi dhahabu au almasi vinapaswa kuvunjwa ili vijulikane?”
Tukio hilo lilimuumiza, lakini halikumkatisha tamaa. Aliendelea kuchimba, na mwaka huo huo alipata Blue Diamond G-40, lakini aliibiwa na jamaa mmoja aliyemfahamu. Pia, alipata Black Diamond, ambayo pia ilichukuliwa na mtu aliyemtambua, aliyedai ataipeleka kupima lakini hakurudi tena.
Licha ya visa hivyo, Zungu aliendelea na kazi. Mwaka 2022 alipata Green Tourmaline kilo saba, akishirikiana na mwenzake mmoja. Mafanikio hayo yaliwasaidia wao na familia zao.
“Ni mambo mengi nimefanikiwa katika uchimbaji wangu, kifupi nimekueleza ila kilio changu ndio kikubwa zaidi ya mafanikio hivyo naomba nipaze sauti kuwa nahitaji msaada,” anasema Zungu.
Katika jamii nyingi, wachimbaji wadogo wanaonekana kama watu waliokata tamaa, au wanaojihusisha na kazi zisizo rasmi. Zungu anasimulia jinsi alivyowahi kudharauliwa Kijijini, akionekana kama mtu asiye na mwelekeo maishani.
Hata hivyo, alipoanza kupata mafanikio, baadhi ya watu walianza kumuona kwa jicho la tamaa, wengine wakitaka kushirikiana naye, huku wakiwa na nia ya kujinufaisha binafsi. Zungu anaeleza kuwa uchimbaji wa madini si tofauti na kilimo, yote ni juhudi za mtu kutumia mazingira ya asili kwa manufaa.
“Kama mkulima haambiwi kwamba hana akili pindi anapokosa mavuno, kwa nini sisi wachimbaji tukose thamani pindi hatupati madini?” anauliza Zungu kwenye mazungumzo yetu. “Sisi wachimbaji tunasingiziwa kuwa tumechanganyikiwa. Sio nzuri hata kidogo.”
SOMA ZAIDI: Mawaziri Madini, Nishati na Viwanda Kikaangoni, Waelezea Miradi ya Kimkakati
Hayo ni baadhi ya maswali ambayo kifupi hayamkumbi mtu mmoja aitwaye Zungu, bali huwakuta wachimbaji wadogowadogo waliowengi katika jamii hapa Tanzania, hasa kabla ya kuyadaka madini yenyewe. Maswali hayo yanaonesha haja ya kubadili mtazamo katika jamii kuhusu kazi ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo.
Mapinduzi tarajiwa
Mwaka 2023, Zungu na rafiki yake, Musa Kilimba, ambaye sasa ni marehemu, walipata Scanner ya Gemstone. Walipima miamba kwa urefu wa futi 21 hadi mita 54 na kupata mawe ya thamani. Huu ulikuwa mwanzo wa mapinduzi binafsi ya uchimbaji kwa kutumia teknolojia.
Baada ya kifo cha Kilimba, Zungu alipumzika kwa muda na kujikita katika shughuli za kilimo, lakini ndoto ya madini haikumwacha. Mwaka 2024, alipata wadau wapya waliomsaidia kuwasiliana na Ofisi ya Madini, mkoa wa Kigoma, na kampuni ya SGS ili kufanya usajili wa maeneo ya uchimbaji kwa gharama ya Shilingi 200,000.
Anasisitiza kuwa maeneo ya Kwaga yana madini ya thamani kama Coltan, Cobalt, Platinum, Diamond, Sapphire na mengine mengi. Kwa msisitizo, anasema: “Miamba ya Kigoma inafanana kabisa na ile ya DRC. Ikiwa DRC wanapata Colbolt, nasi tunaweza.”
Swali la kujiuliza ni kwamba kwa nini amefikia kwenye huu msimamo? Akisimulia, anasema ana madini yanayofanana na coltan au cobolt ambayo ameyachimba na ameyahifadhi mkoani, hivyo kama unataka ushahidi fika kwake akuoneshe.
Nikiwa namhoji ndugu Zungu, alinionesha sampuli za mawe takribani 12 yakiwa tofauti tofauti, sasa huenda yakawa madini aliyoyataja, lakini mimi siyo mtaalamu, hivyo siwezi kusema kwa uhakika.
Changamoto
Uchimbaji mdogo wa madini, hasa ule usio wa vifaa vya kisasa, una madhara makubwa kwa afya ya wachimbaji. Zungu ni mfano hai: aliumizwa jicho lake la kushoto kutokana na jiwe lililomruka wakati wa kuchimba. Aidha, kwa sababu ya kutovaa mavazi ya usalama, au kutumia vifaa duni, ameshuhudia wenzake wakipata majeraha makubwa zaidi yake huko Mpanda au hata kupoteza maisha
Zaidi ya hapo, uchimbaji kwa ujumla una changamoto kadhaa, ikiwemo: kukosa vifaa vya kisasa vya uchimbaji; gharama kubwa za usajili wa maeneo na upimaji wake; kukosa fedha za kupeleka sampuli za mawe maabara; kukosa vifaa vya kuchoronga, au kuvunja, miamba migumu; na kukosa ulinzi wa mali na maisha wakati wa uchimbaji.
SOMA ZAIDI: Wanawake Wajitosa Kwenye Sekta ya Madini Licha ya Changamoto Wanazopitia
Ukiachana na changamoto za ndugu Zungu, niliweza pia kupata mawasiliano ya wachimbaji wengine kutoka Kalinzi na Uvinza. Pamoja na kwamba changamoto zinafanana, Yohana Festo, alilalamikia dharau wanayoipata ambayo muda mwingine hutweza hata thamani ya utu kwa kuwa tu mchimbaji hata kushindwa kujiamini.
“Tunadharauliwa mpaka tunakosa kujiamini,” aliniambia Festo. “Lakini sisi ndio tumefungua macho ya watu kuhusu madini ya Kigoma.”
Halikadhalika, kutoka Uvinza, Martha Paulo na Aisha Kechegwa wanasimulia jinsi watoto wanavyonufaika na uchimbaji wao na wanasomeshwa na kazi hizo za uchimbaji.
Ikumbukwe kuwa Uvinza ina madini chumvi, kiasi ambacho akina mama wanafanya shughuli za mnyororo kutoka uchimbaji hadi uuzaji wa chumvi kwa mlaji wa mwisho.
Wito kwa Serikali, jamii
Serikali ya Tanzania kupitia Sheria ya Madini ya mwaka 2010 (Marekebisho ya 2017) inawatambua wachimbaji wadogowadogo. Kuna kanuni za madini ikiwa ni msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogowadogo iliyopitishwa na kuanza kutumika April 25, 2025.
Kanuni hizi zinawapa msaada wa kiufundi wachimbaji wenye leseni za awali (PML), kuongeza usalama na ufanisi wa kiufundi, kuhakikisha utii wa sheria za kimazingira, na kuwezesha uchimbaji endelevu wa mda mrefu.
Hata hivyo, masharti ya kisheria na gharama kubwa za usajili, leseni, na uchunguzi wa madini yanazifanya fursa kuwa mbali kwa watu wa kipato cha chini kama masanja.
Utekelezaji wa sheria haujajikita kimalilifu katika kuwafikia wachimbaji vijijini kwao bali Serikali kujilinda kwamba tumewaandalia miongozo na sheria ya kuwatambua, bila hata kuwasaidia ipasavyo.
SOMA ZAIDI: Benki Kuu Yasaini Mikataba na Makampuni ya Madini Kuimarisha Mpango wa Ununuzi wa Dhahabu
Uchimbaji wa madini kwa mda mrefu umeonekana kuwa ni kazi ya wanaume, lakini hali hiyo imeanza kubadilika. Ingawa hakuna wanawake wanaojihusiha na uchimbaji pale Kwaga, hali ni tofauti maeneo ya Uvinza.
Kwa kweli, kuna wanawake wengi wanajihusisha na uchimbaji, uchakataji, na uuzaji wa chumvi hapo Uvinza. Hata hivyo, pamoja na kuonekana kuongezeka, changamoto katika kumiliki ardhi na vitalu, ama upatikanaji wake kwa akina mama huwa unagubikwa na changamoto nyingi za kimazingira na kitamaduni.
Kwa upande wa vijana, ni muhimu sana kujenga kituo cha mafunzo kwa wachimbaji chipukizi ili kuwajengea uelewa wa kisayansi ama kibiashara kuhusu madini. Vijana wengi wanapenda mafanikio yanayotokana na uchimbaji, hasa wanaposikia kumiliki alimasi, dhahabu, shaba, nakdhalika, lakini wanakosa mwongozo wa mifumo kuwaongoza kufika huko na kuikimbia kazi ya uchimbaji.
Zungu anatoa wito kwa Serikali, taasisi za elimu na utafiti, wawekezaji binafsi, na jamii kwa ujumla: Wamkumbatie mchimbaji mdogo kama mshirika halali wa sekta ya madini; wawekeze katika elimu, teknolojia, na vifaa vya kisasa kwa wachimbaji wadogo; watambue kuwa wachimbaji kama yeye wanatoa taarifa muhimu za kijiolojia; waandae mikopo maalum, mafunzo, na usajili wa maeneo kwa urahisi; na vyuo vya madini vijifunze kutoka kwa wachimbaji wadogo walioko kwenye ardhi yenyewe, yaani wachukue ujuzi mashinani.
Tunaelekea wapi
Kwa mujibu wa kifungu cha 8(2) cha sheria ya Madini, mmiliki wa leseni ya uchimbaji ya mwanzo ya PML anaweza kutoa msaada wa nje ya nchi ikiwa Tume ya Madini, kwa mapendekezo ya Afisa Mkazi wa Madini, itathibitisha kuwa ujuzi huo haupatikani nchini. Msaada wa kiufundi ni pamoja na maarifa, vifaa vya utafiti, uchimbaji, usindikaji, au uhamishaji wa maarifa.
Sheria ya madini na kanuni za uwekezaji wa ndani (GN No.3 ya mwaka 2018) zinawataka wamiliki wa leseni kununua bidhaa na huduma kutoka kampuni za Kitanzania, au kupitia ubia na kampuni za nje.
Hili nadhani linawalenga wawekezaji, kwa kigezo cha kwamba mtu awe anamiliki kampuni na awe bwenyenye, sasa sijui mchimbaji mdogo wa hapa Tanzania ambaye hana hata hiyo leseni kama anapata ubia au yeye asubiri usoda utakaopatikana.
Tatizo lingine ni katika kupata msaada, msaada uonekane katika maeneo kumi ya uchimbaji katika eneo moja. Wachimbaji wanaojitokeza ndio huvumbua maeneo haya, sasa tukisema tusubiri wapewe msaada ama waingie mkataba wa makubaliano na wadhamini katika maeneo kumi katika eneo moja tunawafinya watu kama Zungu ambao hawana nguvu zaidi za umiliki wa vitalu.
SOMA ZAIDI: Utata Leseni Ya Uchimbaji Madini Serengeti Kwenye Maeneo ya Wananchi. Afisa Adai Sio Lazima Kuwashirikisha
Pamoja na Serikali kuifanyia kazi sekta ya madini, bado kuna kazi kama za kuweka mfuko maalumu wa wachimbaji wadogowadogo, au Artisanal Mining Fund, ambao utawanufaisha watu wenye changamaoto za kimitaji wanaofanana na Zungu kutoka pale Kwaga, Kigoma, na maeneo mengineyo.
Kituo cha rasilimali cha mikoa, hasa mkoa wa Kigoma, kuwatembelea na kuwapa fursa ama elimu wachimbaji wadogowadogo waliopo katika maeneo anuai ya mkoa huo. Kazi ya idara isiwe tu kuwaona wachimbaji wadogo ni wakosefu na kwamba wako kinyume cha sheria, huku wakitafutiwa makosa ili wafungwe.
Fikra inatakiwa kubadilika na kuwatafutia fursa za kuwanufaisha na kuwakutanisha mara kwa mara katika vikao jenzi vya kutunga sharia ama bajeti ili watoe dukuduku zao kama sehemu zingine, na changamoto zitatuliwe.
Kuwezesha mafunzo mara kwa mara na vifaa vya kupima mawe, vitawarahisishia wachimbaji kushiriki kazi nyingi zaidi, ikiwa ni pamoja na kusaidia kuiboresha ramani ya madini ya mkoa wa Kigoma, ama eneo lolote la Tanzania, na kuachana na dhana za kikoloni za mnyororo wa unyonyaji unaoendelea mpaka leo.
Kuimarisha usajili wa leseni kwa wachimaji wadogo, kuwa za bei nafuu na zinazowafaa Watanzania na kuwafikia mahala walipo. Hali hii itasaidia kupunguza dharau zinazoendelea katika jamii juu ya wachimbaji wadogowadogo na dhana zinazorandana na imani potofu kwa sababu ya usajili kuwa kikwazo.
Hadithi ya maelfu
Maisha na hadithi ya Zungu haipaswi kuachwa kama simulizi ya mtu binafsi. Ni hadithi ya maelfu ya vijana wa Kitanzania wanaojaribu kujinasua na minyororo ya umasikini kupitia kazi ngumu ya kuchimba madini.
Simulizi hii ni taswira ya maelfu ya wachimbaji wadogo nchini Tanzania. Ni sauti ya watu walioko chini, wanaoishi pembezoni mwa mifumo ya kisheria, kifedha, na kitaalamu, lakini walio na maarifa ya kipekee yanayoweza kuibua fursa kubwa za kitaifa.
Wachimbaji wadogo ni zaidi ya wachimba mashimo; ni wachunguzi, wavumbuzi, walimu, waajiri, na walinzi wa fursa ambazo bado hazijachunguzwa kikamilifu na mfumo rasmi wa nchi.
SOMA ZAIDI: Nalilia Miradi ya Gesi Asilia Lindi na Chuma na Makaa ya Mawe Ludewa
Ni wakati sasa kwa Serikali, sekta binafsi, na taasisi za kitaaluma kutambua thamani ya kundi hili na kulifanyia kazi kwa dhati. Kwa kusikiliza watu kama Zungu, na kuchukua hatua mahususi, tunaweza kuibua enzi mpya ya ushiriki wa wananchi katika maenendeleo ya sekta ya madini chini Tanzania.
Zungu angependa kuendelea kuiishi ndoto zake za kufanikisha kupata madini zaidi katika milima ya Kwaga. Changamoto alizonazo yeye, pamoja na wachimbaji wenzake, zinawafanya warudi nyuma kidogo. Kama una mchango wa vifaa, elimu, ujuzi, na aina yoyote ya msaada kwao, tafadhali wafikie kwa barua pepe ya mkemia@gmail.com.
Ladislaus Tumbu ni mwandishi na mwanaharakati wa haki za kijamii. Kwa mrejesho, anapatikana ladislaustumbu@gmail.com.