The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kifo cha Job Ndugai: Wanawake Wenzangu, Hususan Wake wa Kwanza, Tusikubali Kuwa Vivuli

Kama wanawake, tunahitaji kufikiria na kutafakari upya taasisi ya ndoa, na ikiwezekana kuibadilisha kwa kuongozwa na uzoefu wa mama na bibi zetu.

subscribe to our newsletter!

Spika wa zamani wa Bunge, Job Ndugai, alifariki Agosti 6, 2025, huko Dodoma wakati akipatiwa matibabu. Vyanzo mbalimbali vimekua vikitoa idadi tofauti ya watoto ambao mwanasiasa huyo ameacha nyuma yake. Kiukweli, hata yeye mwenyewe Ndugai aliwahi kukiri hadharani kwamba hajui idadi ya watoto alionao. 

Hii, hata hivyo, ni hadithi ya siku nyingine. Leo ningependa nijielekeze kwenye kujadili, japo kwa uchache, kuhusu hii kauli ya “mke mmoja,” kwamba kiongozi huyo wa zamani wa Bunge alikuwa na mke mmoja tu, hali inayotofautiana na uhalisia uliopo, na hivyo kuwa fursa kwa sisi wanawake kujitafakarisha kidogo.

Kwanza, niwe mkweli, tangu kifo hiki kitokee,  akili yangu imekuwa ikienda mbio kutokana na taarifa zilizokuwa zikiripotiwa kuhusiana na kauli hiyo ya “mke mmoja” na matendo mengine yanayohusiana na kauli hiyo.

Kuna mahojiano ya vyombo vya habari na mke wa kwanza wa Ndugai, Stella Mmassy, kwa mfano, aliyedai kuwa yeye ndiye mke pekee, akisema walifunga ndoa mwaka 1988, na kwamba hawakuwahi kuachana, na hakuwahi kujua kuhusu ndoa nyingine. 

Wakati huohuo, viongozi wa ngazi za juu, wakiwemo wabunge, wamekuwa wakimtambua Dk Fatma Mganga, ambaye kwa sasa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, kama mke pekee wa hayati Ndugai. 

Kwenye kufanya hivyo, viongozi hawa wamekuwa wakigoma kabisa kumtambua Stella, wakijifanya kama vile hayupo na hakuwahi kuwepo.

Sasa, naomba nikumbushie hapa kidogo kwamba hayati Ndugai aliwahi kusema, mara nyingi, kuwa yeye ni Mkristo kwelikweli, na sio kama akina sie tunaohudhuria ibada wakati wa Pasaka,  Krismasi, au mazishi. Yeye Ndugai alijiita “Mzee wa Kanisa” kuonesha uzito wa imani yake kama Mkristo.

SOMA ZAIDI: Ukatili wa Wenza Kusambaza Picha na Video za Faragha Baada ya Kuachana Waliza Wanawake Zanzibar 

Kwa uelewa wangu wa kawaida, kama mtu ambaye haendi kanisani, Wakristo  wanatambua ndoa ya mke mmoja tu, ingawaje wengi wetu tunajua kwamba wanaume Wakristo, akina baba hawa, mara nyingi, wana wake zaidi ya mmoja, achilia mbali mipango ya pembeni, au mechi za mchangani kama tunavyosema mtaani. 

Lakini hii pia ni hadithi ya siku nyingine.

Stella hakusikika

Sasa, kwa waliofuatilia msiba na ibada ya mazishi ya hayati Ndugai, mbali na yale mahojiano ya awali Stella alifanya na vyombo vya habari, hakuna sehemu mama huyo wa watu kasikika tena na hajatajwa katika taratibu zote zilizofuata. 

Badala yake, watu tuliona picha za viongozi wa Serikali na Bunge wakiwa na Fatma, kama mke pekee wa marehemu, huku sala na salamu za pole zikielekezwa kwake yeye tu, huku familia nyingine ikiwa imepotea ghafla, na Stella akiwa kama aliandikwa kwa penseli, au chaki, na sasa ubao umefutwa!

Wakati wa mazishi ni Fatma pekee aliyekuwa na shada la maua lililoandikwa MUME, wakati Stella akijumuishwa na watoto wa Ndugai katika shada lililoandikwa BABA. Ilikuwa ni kana kwamba, kusema ule ukweli wa Mungu, Stella hakuwa sehemu ya familia, bali sehemu tu ya watoto wake. 

Mimi najiuliza, iliwezekanaje Ndugai amzae Stella, lakini pia awe aliwahi kuwa mke wake, ila mwenye umri ulio karibu na Ndugai na cha ajabu apate nae watoto?

Naomba nieleze hapa kidogo kwamba, binafsi, simlaumu Stella, hata kidogo, kwa kuendelea kuamini Ndugai ni mumewe, na hasa kama kwa maelezo yake walifunga ndoa ya Kikristo, na hakukuwahi kuwa na talaka, kwa macho ya mama na bibi zetu wengi, kwake Ndugai alikua bado ni mumewe. 

SOMA ZAIDI: Uwekezaji Duni, Mitazamo Hasi ya Kijamii Vikwazo Vikuu Maendeleo ya Soka la Wanawake Z’bar  

Najua wanawake wote tumeshawahi kusikia ile misemo, mwache aende zake ipo siku atarudi, kama siyo leo kesho, akizeeka, akiugua, na hata akifariki. Bahati mbaya, kwa kesi hii, Ndugai hakurudi, kapumzika zake Kongwa! Habari huku mtaani zinadai kwamba  Stella bado alikua mke bila mume, unajua, ile ya married but single?

Kwa hiyo, simlaumu Stella, hata kidogo, kwa sababu najua mama na bibi zetu wengi hawakupewa zana za kushughulikia mambo haya; hawakuandaliwa, au kupewa nyenzo za kuomba talaka, au kuendelea na maisha mengine. Nyenzo pekee wazazi wetu hawa walipewa ni uvumilivu na kusubiri. 

Ndiyo maana baba na babu zetu wanaweza kuondoka ujanani wakarudi uzeeni, na mama na bibi zetu wakitegemewa kuwapokea. Muhimu karudi nyumbani, hata kama hana matumizi. Ndiyo, nimesema akiwa hana matumizi, aliyeshika mawe nimekaa paleeee!

Baada ya kusema hayo, naomba niseme hivi, wanawake na wasichana, hasa  wale wanaofikiria kuolewa, au walioolewa tayari, na muhimu zaidi kama tayari ni mke wa kwanza, au utakua mke wa kwanza, sogea karibu tuongee, tung’atane sikio.

Tujipange

Shoga yangu, kuna haja ya kujipanga zaidi, na mapema sana, bila kupoteza muda. Kiufupi, ukishamaliza tu kuosha vipodozi vyako baada ya maharusi kutakiwa wakapumzike, chukua kalamu na karatasi, jipange.

Ni wakati sasa wanawake tutizame na kuichukulia ndoa kama jinsi wanaume wanavyoichukulia: chanzo cha usalama wa kiuchumi na afya ya akili, au, kama wanavyoiita wenyewe wanaume, “utulivu wa nafsi.” 

SOMA ZAIDI: Uhodari wa Mwanamke ni Zaidi ya Siku ya Wanawake Duniani

Tunafahamu kwamba wanaume wengi hawaoi kwa sababu wanakupenda kuliko kitu chochote, bali wanaoa mwanamke anayeweza kutunza familia, kuiendeleza, kudumisha nyumba, na kuhakikisha familia itasimama, hata likitokea jambo baya, ikiwemo kifo au maradhi. 

Wanaume, kusema ule ukweli, wanaoa “amani” ndani ya nyumba – ingawaje hii dhana ya “amani” na yenyewe inahitaji uchambuzi wa kina na wa kipekee. Kwa kifupi, wenzetu hawa wanaoa uhakika wa kiuchumi na usalama wa familia siku za usoni.

Kwa hiyo, sakata hili la dada yetu Stella liwaamshe wanawake na wasichana kuchangamka na kulinda nafasi zao kwenye ndoa, kuhakikisha watoto wao wanalelewa na kupata elimu itakayowapa nyenzo za kuweza kukulinda, kujilinda, kujisimamia, na kukufunika usibaki kivuli. 

Kamwe, usiruhusu kuwa kivuli na sauti yako kuminywa. Jiandae na andaa watoto watakaosimamia hili. Kama ni mke wa kwanza, uwezekano mkubwa ni kwamba umeolewa, au uliolewa, na mwanaume mwenye kipato cha chini, bado anajitafuta, si ajabu hakua hata na kazi.

Kama mlikutana chuo, ukute wote hamkua na kazi. Hakua na biashara, hakua na nafasi yoyote kijamii. Alikua tu mwanaume uliyeolewa nae ambaye harusi yenu, bila michango ya ndugu na jamaa, isingewezekana, ikiwemo hata kupata sehemu ya kulala baada ya harusi!

Inawezekana kabisa mlipitia kipindi cha uvumilivu wa kula kilichopo na siyo mnachotaka, na kama mmeanza kupata watoto, uwezekano mkubwa ni kwamba wewe mwanamke uliweka kando ndoto zako ili kulea na kujenga familia, ukileta ile “amani” iliyomruhusu mume wako kufanikisha ndoto zake ili familia yenu iishi vizuri baadae. 

Tunza kumbukumbu

Wakati huu wote, huenda ulisahau ndoto zako na thamani yako, bila kutambua mchango wako wote, ikiwemo “amani” uliyoleta. Ni muhimu kutunza kumbukumbu ya mchango wako. Hata kidogo, usiuchukulie poa. 

Vinginevyo, utajikuta umeshika shada la mtu uliyewahi kulala nae sasa limeandikwa BABA. Kataa katakata kugeuka kutoka aliyekua mke mpaka mmoja wa watoto wa marehemu!

SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’ 

Wanaume, ingawaje si wote, lakini wengi wao, hupitia hatua ya kuwa na mke anayehangaika naye ujanani, akijitafuta. Baadae, kuna mke sasa anayeefanana na hadhi yake – iwe  kipato,  cheo, au nafasi yake nyingine kwenye jamii. 

Huyu wa baada ya kuyapatia maisha mara nyingi anaweza kuwa msomi, ingawaje siyo mara zote, wa tabaka la kati au juu kama yeye, mwanamke wanayeongea lugha moja. Unajua ile misemo ya nataka mwanamke anayeni-chalenji kiakili? Ewaaaa, huyo sasa.

Yule anayejua kushika vyema glasi ya mvinyo na kutambulisha kwa marafiki zake wapya ili waongee yanayojiri duniani. Wewe, yaani yule wa ujanani, unabaki wa kusaidia kumwakilisha misibani, kwenye sehemu za ibada, mambo ya kifamilia – hiyo, hata hivyo, ni kama hajahama ndani na kuamua kuishi ugenini na nyumbani!

Kwa hiyo, wanawake wenzangu, tafadhali sana tujilinde tangu siku ya kwanza, na tujiandae ili itakapotokea akakuacha kimwili, kisaikolojia, kinafsi, au tu kaamua kuondoka na harudi tena nyumbani, uwe na uwezo wa kujibu maswali haya kwa jibu la ndiyo: 

Je, niko tayari? Je, nimewaandaa watoto wangu kujilinda? Je, nimejiandaa kwa yajayo? Mimi ni nani? Nilikuwa nani kabla sijakutana naye? Mimi ni nani tangu nikutane naye? Mimi ni nani kesho akiwa hayupo? 

Kuwa tayari kujiuliza maswali magumu hata kama ni ngumu kumeza.

Kamwe usitegemee viongozi wa dini, maana watakuacha na kwenda kupiga picha na wanasiasa, au watu mashuhuri, hasa ikiwa mume wako alikuwa na madaraka au pesa. Usiwategemee rafiki zake, wale waliokuwa wakikuita “mke wetu” wakati unawapikia na wanakula na hata hawasaidii kuosha vyombo wala kupeleka sahani zao jikoni.

SOMA ZAIDI: Dhuluma Baada ya Kuachika Inavyowasukuma Wanawake Zanzibar Kutaka Kumiliki Ardhi Kisheria 

Unajua wale wa mke wetu? Shem lake? Shemela? Haohao. Kuna mwingine wanamwita “mke wetu wa ukweli,” “huna baya na mtu,” “ukifa hauozi.” Kama mke, jifunze kuwa mbinafsi, ndiyo, nimesema kuwa mbinafsi, na kamwe usipoteze nafasi yako kama mke na msharika kwenye hayo mahusiano. 

Endelea na maisha

Pale mambo yanapokua magumu, akahama nyumba akaenda kwingine, endelea na maisha mengine, na ikibidi uwe na mahusiano kama ndicho ulichochagua. Nimesema mahusiano kwa sababu kina mama zetu, hata wakiachwa miaka, bado jamii inataka wasiwe na mahusiano, wakae walee watoto na kusali baba arudi.

Usisubiri, na kama ni kusali, ombea upate nguvu yako ya ndani na nje, uweze kuishi kama mtu aliye hai na aliyewahi kuwa na uhai wa ndani ya nafsi.

Mwisho wa siku, mwanamke ni lazima ukatae kuwa sehemu ya watoto wa mume wako baada ya yeye kuondoka. Kama wanawake, pia tunahitaji kufikiria na kutafakari upya taasisi ya ndoa, na ikiwezekana kuibadilisha kwa kuongozwa na uzoefu wa mama na bibi zetu. 

Tuifikirie upya taasisi ya ndoa kwa sababu tangu mwanzo haikuwekwa kuwafaidisha wanawake kiujumla, bali wao kuwa watumishi wa taasisi na kuifanya istawi na mzigo wote ukiwa mabegani kwao. Kama utaamua, au kuchagua kuolewa, hakikisha huo muungano unaleta manufaa kwako.  

Utajishukuru baadaye!

Mary Fadei ni mtaalamu na mwanaharakati wa masuala ya kijinsia. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia maryfadei05.mn@gmail.com au X @Mary_ndaro. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×